Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Monduli
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nitumie nafasi hii kukushukuru, kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Wizara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kujielekeza katika elimu. Ni kweli kwamba tumeanzisha programu ya elimu bure; na kimsingi katika hili tunajua kabisa na ndiyo ilikuwa Sera ya CHADEMA kwamba inaenda kuwaondolea wananchi adha mbalimbali. Kuna maeneo ambayo tunataka kushauri na mkubaliane na sisi kama kweli tunataka kuboresha elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ubaguzi uliopo katika mfumo wenyewe. Waraka uliotolewa ulionesha kwamba shule za day hawaruhusiwi kupata fedha za chakula kwa sababu wanafunzi wanakuja na kurudi nyumbani. Vilevile tufahamu kwamba ni mfumo ndiyo unabagua wanafunzi. Hakuna mwanafunzi anayependa kukaa day, wenzake walale boarding wasome usiku na watoto wa kike waende nyumbani wakaokote kuni. Ni mfumo! Sasa anapata hasara ya kukaa day, lakini bado anaenda shuleni mchana, hapati fedha ya chakula, lakini shule za bweni mnawapa fedha za chakula.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo langu la Monduli, ni kweli shule zetu zote ni bweni, lakini ziko shule ambazo ni za day katika mazingira magumu. Tuache ubaguzi katika suala hilo, kama tunatoa hela za chakula, tutoe pia kwa wanafunzi wa day wakiwa shuleni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, tatizo la Shule za Sekondari za Serikali, siyo ada. Siyo shilingi 20,000, naamini wote tunafahamu hata Waziri wa elimu anafahamu. Tatizo siyo shilingi 20,000 kila mzazi angaweza kutoa shilingi 20,000. Tatizo ni mzingira hasa majengo, madarasa, madawati, vitabu, maabara na vitu vingine vinavyosaidia kuboresha elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama sisi tuanenda kujificha kwenye kivuli cha shilingi 20,000 hatujawasaidia watoto wetu. Tutakuwa tunazalisha, kwamba tumeingiza watoto 2,000 darasani watatoka 2,000 lakini empty. Kwa sababu tunataka kuboresha kweli, tuache kwenda kujificha kwenye shilingi 20,000, twende katika kuboresha miundombinu ya wanafunzi, maabara na mazingira mengine yanayosaidia mtoto aweze kufanya vizuri, pamoja na vitabu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, tunafahamu kabisa kada ya Walimu ina mazingira magumu sana ya kufanyia kazi. Shule nyingi za kijijini na Wabunge wengi wanatoka kijijini watakubaliana nami katika hili. Walimu wanatembea kilometa nne mpaka tano kwenda shuleni, halafu wanatumia nauli shilingi 2,000, shilingi 3,000 kila siku kwenda shuleni. Wakati huo huo anapanga mjini kwa sababu kule vijijini hata nyumba ya kupanga hakuna.
Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu tunasema atumie mshahara wake kulipa nauli, atumie na kupanga nyumba, halafu unategemea wakati huo huo afanye vizuri, haiwezekani! Kama kweli tunataka kuboresha elimu yetu ni vizuri tukajali mazingira ya walimu kwa kujenga nyumba za Walimu katika shule zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata wakati Waziri wa Elimu anawasilisha hapa, alisema kwamba ni kwa namna gani mwalimu anaweza akakaa kilometa tano au kumi kutoka shuleni akaondoka asubuhi nyumbani halafu akafanya vizuri na watoto wakafaulu. Tusiangalie watoto tu, lakini tuangalie mazingira ya watumishi wetu wanaofanya kazi katika maeneo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nataka tukubaliane kama Bunge. Kama tunasema tunawapima watumishi wa umma kwa OPRAS, tuwapime Mawaziri nao kwa mfumo huo huo. Kabla hatujajadili bajeti yoyote katika miaka inayokuja, ni lazima Mawaziri na kila Wizara iwasilishe imetelekeleza kwa kiwango gani bajeti tuliyoipitisha kwa mwaka uliopita. Hii itatusaidia sisi Wabunge kuacha kupiga kelele hapa, kama tunapitisha bajeti ya bilioni tano, halafu Serikali haipeleki fedha, halafu tunakuja kumsulubu Mheshimiwa Waziri hapa, hakuna sababu ya kukaa kupitisha bajeti ambayo hatuwezi kuitekeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tatizo kubwa kwenye nchi yetu ni mfumo wa upelekaji wa fedha katika miradi ya maendeleo ya wananchi, ndiyo hiyo tu! Sasa kama tunapitisha bajeti lakini hatupeleki fedha, ni kila siku tunasigana hapa maswali, miongozo kwa sababu kile ambacho tumetarajia kupata kwenye Majimbo yetu, hatuyapati. Ni lazima tupige kelele kwa sababu hatujapata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kama Serikali itapeleka fedha kwa wakati kwa kiwango kile hata kama ni kidogo, hakuna sababu ya Bunge kupoteza muda. Tungekuwa tunasema hapa tunashukuru kwa sababu tumetekelezewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hamjatekeleza, tutasema hamjatekeleza. Hii ni kwa sababu Serikali haipeleki fedha. Kwa hiyo, nashauri kila Wizara, wakati mwingine inavyopelekewa fedha kuwe na mgawanyo sawa wa kupeleka fedha wakati fedha zinapokusanywa. Siyo Wizara nyingine zinapewa, nyingine hazipewi. Bila hivyo, miradi yetu itaendelea kuwa haifanyi kazi vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni wanyapori katika maeneo yanayopakana na Hifadhi za Taifa. Hili niseme kwa masikitiko makubwa. Katika Jimbo langu mpaka sasa, tembo wanavamia kila siku zaidi ya heka kumi ya mazao ya wananchi, lakini haturuhusiwi kuwapiga wale wanyama. Baadaye nataka Waziri wa TAMISEMI kwa sababu tunasema tunahitaji kuwa na chakula, lakini wanyama wale wanaharibu sana mazao na wakati mwingine tunasema Serikali ishiriki basi kufanya patrol ya kuwarudisha wale wanyama kwenye park ili wananchi wetu waendelee kufanya kazi zao kwa amani, lakini haifanyiki hivyo!
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine nitahamasisha kwamba ni bora Wabunge wanaotoka katika maeneo hayo tuungane kuwakataa wale wanyama, kama ninyi Serikali hamwezi kutusaidia kuwarudisha katika park hizo, badala ya kuwaacha waharibu mazao ya wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna magari; hakuna askari, kila siku iendayo kwa Mungu kuanzia mwezi wa tatu katika Jimbo langu, heka kumi zinaliwa na wanyama. Tembo wanavuruga, wanavunja. Ukienda Halmashauri hakuna gari. Kwa hiyo, tunaomba katika hilo mtusaidie ili wananchi wetu, jasho lao lisiende bure.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maji. Mimi katika hili kwa kweli nimshukuru sana Waziri wa Maji kwa kufika Monduli. Baada ya kuingia kwenye Wizara hiyo, tumepata angalau shilingi milioni 700 kwa ajili ya kupunguza madeni ya wakandarasi na sasa kuna maeneo mengine wameanza kupata maji. Nakushukuru katika hilo kwa sababu kwa kweli miradi hiyo imesimama zaidi ya miaka miwili. Mwaka 2015 hatujaletewa hata shilingi ya maji. Umeonesha nia, basi naendelea kukusitiza kwamba bado tunahitaji wanachi wetu wapate maji kwa wakati ambao bajeti yao imeshapitishwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili katika hilo la maji, naomba nishauri Serikali ifanye kama inavyofanya Road Fund. Ukiangalia Wizara ya Maji yenyewe ni centralized, kwamba wanapanga Wizarani bajeti, halafu wanapeleka kwenye Halmashauri. Kwa nini isipangwe kama inavyopangwa miradi mingine fedha zikaanzia kule chini halafu zikaenda zikafanya hivyo? Kwa sababu inaonekana wakati mwingine hata Halmashauri hatujui tunapangiwa nini katika Wizara ya Maji kwa sababu imefanyika centralization.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la miundombinu. Tunaona hili ni tatizo kwamba kila mtu analalamika miundombinu, lakini ni kweli barabara zetu zimeharibika, hazipitiki. Sasa unakuta katika Halmashauri barabara za vijijini hazipitiki; zahanati hazipo, akina mama wanajifungulia njiani, wengine wanakufa kwa sababu hakuna miundombinu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama dispensary zetu tunasema katika vijiji 12,500; vijiji 4,000 tu ndiyo vina dispensary, halafu barabara hazipitiki, kwa nini watu wasife njiani? Watakufa tu! Kwa hiyo, tunaomba tuzingatie kabisa na ili tusaidie wananchi wetu ni lazima angalau miundombinu hiyo iwe imeboreshwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye suala la utawala bora. Ni kweli mnasema na sijamwona kaka yangu Mheshimiwa Lusinde, nataka nimwambie, Watanzania wote wanalipa kodi bila kujali vyama vyao na kinachopeleka maendeleo ni kodi ya wananchi na siyo kodi ya mtu mmoja mmoja wala Serikali iliyoko madarakani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine mnazungumza habari ya utawala bora, na mimi niseme, mnasema sisi tunataka tuuze sura kwenye tv, siyo kweli! Serikali ilikuja hapa ikasema sababu mbili, kwa nini hawataki kurusha live.
Moja, wakasema gharama. TV za private wakasema tutaonesha sisi kwa gharama zetu. Jambo lingine mkasema watu hawafanyi kazi; lakini niwaulize, hivi wakati wa kufanya kazi ni wa asubuhi wakati wa Bunge au saa hizi wakati kila mtumishi ametoka kwenye Ofisi yake amekwenda nyumbani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kweli hamna nia ya kudhulumu Bunge hili na kuzuia Watanzania wasijue tunachojadili, badilisheni kipindi cha Maswali na Majibu kiwe giza, halafu kipindi hiki cha mjadala ambao wananchi wanataka kuona kiwe live, kama kweli hamna nia mbaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mmeamua kujificha kwenye Kipindi cha Maswali na Majibu, kwa sababu kila mtu anauliza swali. Tunataka mijadala hii Watanzania wajue Bunge lao linajadili nini kuhusu maslahi ya maisha yao na mustakabali wa Taifa lao. Kwa nini tunaficha? Leo tumeeleza bajeti nzuri ya viwanda hapa, tunataka Watanzania waone Bunge linasema nini kuhusu habari ya viwanda. Tunaficha nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli hakuna empire yoyote inayotakiwa misingi yake itikiswe. Serikali ya CCM imetikiswa kwa kutumia Bunge hili. Hawako tayari kuendelea kuona likitikiswa. Tusema hivyo! Huo ndio ukweli! Mnaficha ili wakati fulani msionekane kwamba mmeendelea kuonesha udhaifu kama ambavyo Wabunge wanaendela kusema hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa mambo makubwa ambayo amefanya na kwa kipindi kifupi tu. Miaka zaidi ya 30, ameturudishia ekari zaidi ya 12,000 kwa wananchi wa Monduli. Tunakushukuru na tunakuomba uendelee kuyamalizia yale, tunajua kuna figisufigisu zinafanyika lakini tutahakikisha kwamba mashamba yale yote yanarudishwa.
MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, siungi mkono hoja.