Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

Hon. George Natany Malima

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpwapwa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi kuchangia Hotuba hii ya Waziri wa Maji. Kwanza naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Rais, kwa jinsi ambavyo sisi watu wa Mpwampwa ametugusa kwa upande wa maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunalo bwawa kubwa linajengwa pale Msagali lenye thamani zaidi ya shilingi bilioni 27 lakini tunayo madarasa zaidi ya 80 tumejenga katika kipindi hiki lakini pia barabara upande wa TARURA tumefungua barabara karibu zote za vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivi karibuni pia tumepewa fedha kwa ajili ya kujenga mabweni katika shule yetu ya Sekondari ya Mpwawa high school ili iweze kuchukua wanafunzi wengi. Kwa hiyo, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa sababu ni mara ya kwanza Mpwapwa kupata miradi mingi hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nimshukuru sana Waziri Maji ndugu yangu Aweso. Aweso anasifa moja ni msikuvu sana, Mpwapwa tuna miradi mingi ya maji, tuna mradi wa Kisokwe – Biro – Mazae lakini tuna mradi wa Mpwapwa Mjini ambao utahudumia Ving’hawe mpaka Mang’angu lakini tuna mradi mwingine ambao unatekelezwa pale katika Kata yetu ya Lupeta ambayo utaudumia vijiiji viwili Lupeta Namakutupa. Tuna mradi katika shule yetu ya Sekondari ya Berege unaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, concern yangu kubwa nikwamba miradi hii haitekelezeki, haikamiliki dhamira njema ya Serikali ni kumtua ndoo kichwani mama wa kitanzania lakini jambo hili linaenda linachukua muda mrefu sana. Katika miradi hii niliyoitaja katika Wilaya ya Mpwapwa ina miaka zaidi ya miwili sasa. Mheshimiwa Waziri utakubaliana na mimi kwamba kuna siku moja nilikupeleka katika Shule ya Sekondari ya Berege ukaona shida ya watoto wale, watoto wako wengi zaidi ya 1,000 hawana maji ya kunywa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukatoa maelekezo kwamba, kisima kichimbwe mara moja na kwamba kilichimbwa mara moja lakini baada ya pale watoto wale wamekuwa wakishuhudia mtambo ule. Hakuna pampu imewekwa, na shida ya maji inaendelea katika Shule ya Sekondari ya Berege. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilikuwa naomba sana Mheshimiwa Waziri utoe maelekezo ya haraka kama ulivyotoa mara ya kwanza kuchimba, utoe maelekezo kisima kile kiwekwe pampu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, iko miradi ya kuchimba visima virefu katika jimbo langu la Mpwapwa iko katika vijiji vya namba thelathini Kata ya Mlembule kule, Nana, Ngaramiro, Katechitemo kuna Igojirani kuna mradi wa kusambaza maji unaendelea. Mheshimiwa Waziri miradi hii kila mwaka naiona kwenye bajeti inakuja bajeti inapita vijiji hivi maji hayachimbwi, na nilikuwa nategeamea kwamba miradi ya kuchimba visima ni miradi yenye gharama ndogo sana, lakini watu wanateseka sana kwa sababu ya miradi midogo kama ile. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nikuwa nakuomba sana Mheshimiwa unapo wind up hotuba yako ningependa kusikia miradi hii ya Mpwapwa itatekelezwa lini? Naamini Mheshimiwa Rais angetaka kuona kweli wakinamama wakitanzania wametuliwa ndoo kichwani. Lakini naona kama tunasubiri mpaka wachoke sana ndiyo tutue hizo ndoo kichwani. Kwanini mpaka wachoke? Dhamira hii nadhani hii slogan ingekamilika haraka ili tutafute nyingine, tumekuwa kila mwaka tunazungumzia kumtua ndoo kichwani mama wa kitanzania lakini matokeo yake bado utekelezaji haupo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nilikuwa nashauri tuwaongezee bajeti. Najua labda tatizo ni fedha ndiyo maana miradi hii aikamiliki tuongeze bajeti ili miradi hii ikamilike Waheshimiwa Wabunge siasa ya kwenye majimbo yetu ni maji piga uwa ni maji, maji lazima yapatikane. Sasa kama maji hayapatikani watu wanashuhudia mkandarasi yupo anazunguka tu hakamilishi mradi siasa ya kule kwenye majimbo inakaa vibaya. Kwa hiyo, nilikuwa naomba sana Mheshimiwa Waziri uliangalie sana jambo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo ningependa kulizunguzia ni utaratibu wa kutoa bili za maji, kumekuwa na malalamiko sana kwa wananchi kwamba wanabambikiwa bili maana yake nini? Maana yake bili inayokwenda, inayomkuta mraji wa maji inakuwa kubwa kuliko maji ambayo ameyatumia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nadhani hii inatokana na ukweli kwamba wafanyakazi wa mamlaka zetu wengi hawafiki kwenye maeneo ambako wananchi wanatumia maji. Badala ya kusoma zile mita wanafanya hesabu za makadirio sasa katika kukadiria kuna impact mbili moja ni hasi kwamba Taasisi yetu ya Maji itapata hasara kwa sababu unaweza uka-under bill ukamuwekea bili ndogo kuliko maji anayotumia. Lakini nyingine ni kwamba mnunuaji unaweza ukamzishia bili akatakiwa kulima hela nyingi kuliko kiasi cha maji anachotumia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nilikuwa nashauri kwanini msi–shift kutoka kwenye current billing system mwende kama wanavyofanya watu wa TANESCO. Tufanye pre-paid system ili mtu akinunua unit ya maji anatumia ikiisha maji yanakatika, hili aweze kupata hiyo huduma tena lazima anunue kama tunavyonunua umeme na tunavyonunua simu hii itawasaidia kuondoa hizi lawama na kelele kwa ajili ya watumiaji wa maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo ningependa kuchangia kuna hizi taasisi za watumiaji wa maji wanaita COWSOS, ideally it was good lakini utekelezaji wake nimeona kama umekuwa na matatizo makubwa ni changamoto kubwa sana.

Mheshimiwa Spika, mfumo ni kwamba kunakuwa na kamati za maji kwenye vijiji lakini wale watendaji ambao wanafanya kazi technical wanaletwa na uongozi wa Wilaya wa Maji RUWASA. Sasa wakishwa letwa pale kinachotokea ni kwamba wale watendaji wanapo ajiriwa pale kamati ile ya wanakijiji inampa mkataba, lakini utakapompa maelekezo anapofanya vibaya hawezi kuwasilikiliza hawa anasikiliza wale waliyomleta.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kumekuwa na vurugu miradi haiendelei, matumizi mabaya ya fedha lakini wale wameletwa na mtu wa wilaya. Kwa hiyo, hawawezi kusikiliza Kamati, Kamati haiwezi kutoa ushauri kwa huyo mtu. Baadae kamati ya kijiji ambayo ndiyo wenye maji wanageuka kuwa watumwa wa mtendaji wa maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sana jambo hili Mheshimiwa Waziri walipitie upya ili waone kama kuna namna nyingine ya kubadilisha.

Mheshimiwa Spika, wameharibu mambo mengi, mahali pengine niliona Mtendaji Mhasibu wa maji ana–paralyze mpaka system ya kijiji. Wakitaka kuitisha mkutano waulize mapato na matumizi ya mradi wa maji, anahonga wenyeviti wa vitongoji ili wasiitishe mkutano asije akaulizwa hayo maswali. Kwa hiyo unakuta hata Serikali ya Kijiji haiwezi kufanya functions zake kwa sababu anawa–paralyze kwa visenti (cent) vilevile vya mradi wao…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Kengele ya pili imeshagonga Mheshimiwa.

MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ningeomba sana Mheshimiwa Waziri anaposimama basi atueleze kwa nini miradi haikamiliki, na ikiwezekana aniambie Mpwapwa miradi itakamilika lini?

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)