Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kiukweli, kiroho safi, hata kama wengine hatupongezi hovyo hovyo, Mheshimiwa Aweso anafanya kazi na Naibu wake. Ni term yake ya kwanza humu Bungeni, lakini akikaa kwenye podium utadhani ni mzoefu zaidi. Pia nimpongeze Katibu Mkuu, nimpongeze na kaka yangu kijana wa Bunda, Naibu Katibu Mkuu, anatuwakilisha vyema wananchi wa Mkoa wa Mara. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Aweso sifa yake pekee ni unyenyekevu, hajavaa cheo. Mungu ambariki safari yake ya kumtua mwanamke ndoo kichwani itimie. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kuchangia na nashukuru Waziri wa Fedha yupo hapa anisikilize. Hivi kwa nini Serikali na taasisi zao hawataki kulipa madeni ya maji wakati wanatumia? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hapa aliwakumbusha Wabunge walipe madeni ya nyumba, leo tunawakumbusha wao wasitumie maji bure, walipe pesa za maji, ili mamlaka za maji kwenye maeneo yao hizi shida ndogondogo waweze kuzifanya. Hivi mbona hatuoni wakienda sheli nyie kukopa mafuta kwenda kufanya ziara? Au kwa sababu, Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri na watendaji wake hawawezi kusimama hapa kuwadai madeni? Yaani wanatakiwa wadaiwe na wafanyakazi, wadaiwe, hata kulipa maji wanayotumia kwenye taasisi zao? Aah, I see? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naanza hapa kwa kutoa mfano, Tanga, Mamlaka ya Maji Tanga inadai taasisi za Serikali bilioni 2 na milioni 477, wanatumia tu. Kwa nini hawaendi shell kukopa? Kwa nini huku wanatumia maji hawalipi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naendelea, Masasi inadai taasisi za Serikali milioni 307 na hii mpaka ilitokea aibu, mamlaka ikataka kwenda kukata maji Hospitali ya Wilaya, walipe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naendelea, haya, taasisi mbalimbali DAWASA, inadai bilioni 9.0 hee! Miaka mingapi hii hawajalipa bili ya maji? Wananchi wanalipa bili ya maji, private sector wanalipa bili ya maji, kwa nini wao hawalipi bili ya maji? Walipe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naendelea, Newala wanadai milioni 33.7, Mamlaka ya Maji Tabora milioni 126, Sumbawanga milioni 122, Kigoma milioni 534, Mtwara bilioni 1.3, Nzega milioni 22. Hapa namtetea Mheshimiwa Bashe. Naendelea, Korogwe milioni 21; Mamlaka ya Ludewa milioni 17. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hivi mnataka hizi mamlaka zijiendesheje? Kwa nini mnamchelewesha Waziri wa Maji Mheshimiwa Aweso safari ya kumtua mwanamke ndoo kichwani? Hivi wananchi hawa wanafanya biashara kwa kipato kidogokidogo wanalipa bili ya maji, ninyi hamtaki kulipa bili ya maji. Wanachi wasipolipa wanakatiwa, Mheshimiwa Aweso, kwa nini usikate? Waende siku moja ofisini wakose hata maji ya kuosha vikombe vya kunywea chai. (Makofi)
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, taarifa.
MHE. ESTER A. BULAYA: Unipe taarifa ya Yanga kushinda, mengine siyataki. (Kicheko)
SPIKA: Mheshimiwa Ester Bulaya, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, Waziri wa Fedha na Mipango.
TAARIFA
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge anayechangia, nimeona tangu mwanzo amesema na Waziri wa Fedha yuko hapo na kila anapochangia namuona ananiangalia.
Mheshimiwa Spika, ninataka nimpe taarifa kwamba nasi Wizara ya Fedha tunahimiza taasisi zote zinazotumia huduma zilipe. Zikishalipa wasitengeneze madeni mengine. Huu ndiyo msimamo wa Mheshimiwa Rais na ndicho ambacho tumekuwa tukisisitiza sisi tunaosimamia mafungu.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ninataka nimuunge mkono Mheshimiwa Mbunge na kwa kweli nitoe rai taasisi zinapotumia huduma wanatakiwa walipe na wasitengeneze madeni, hiyo ndiyo itakayochachua uchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nilitaka nimpe taarifa tu maana yake nimeona ananiangalia kwelikweli. Ninaomba kutoa taarifa. (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Ester Bulaya, badala ya kumuangalia Mheshimiwa Waziri kwa sababu unaongea na Spika mwangalie Spika ili usimtishe Mheshimiwa Waziri. Unaipokea taarifa hiyo?
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, mimi kwanza siipokei, lakini hapa nakuangalia wewe ambaye na wewe hutaki madeni.
Mheshimiwa Spika, hivi anaongea tu hela wamepeleka sasa, hao anaotaka walipe? Hela za bajeti tukipitisha hapa anapeleka zote kule? Lipeni madeni. Leo hapa tutataka mtuambie mtaanza kutenga shilingi ngapi ili mlipe madeni.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Kunti jana alisema, machache tu ni shilingi bilioni 33 sasa unganisha nilizozisema mimi. Mnatumia maji bure tu. Siku moja Mheshimiwa Aweso nakwambia Kata washindwe hata kuosha vikombe vya kunywea kahawa ofisini, uone kama hawatalipa madeni. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa mwanangu nisikilize mama yako nina ombi na andika kabisa. Nashukuru Mradi wa Maji wa Bunda wa kutoka Nyabehu umefika Mjini, umeanza kusambazwa baadhi ya maeneo. Nawe uliukuta ukiwa na asilimia 40, mimi na wewe tumefikisha asilimia 99 kufika pale Mjini, ninachotaka Kata zote 14 za Halmashauri ya Mji wa Bunda Mjini zipate maji. Tunahitaji shilingi bilioni saba tuweze kuhakikisha tumeweka miundombinu ya maji katika Kata zote 14. Hivi leo maji yanayozalishwa zaidi ya asilimia 45 hayatumiki kwa sababu gani; hakuna miundombinu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Aweso, sasa nisikilize, kuna ujenzi pale wa tenki ambalo litakuwa na ujazo wa milioni tano, hapa zinahitajika bilioni tatu. Naomba huu mradi ukamilike, wananchi wa Bunda waweze kupata maji safi na salama. Kwa mfano, kueneza mtandao wa maji Kata ya Guta, ili kata nzima iweze kupata maji zinahitajika milioni 876. Kata ya Wariku, milioni 786, Sazila milioni 564, kwenda Kiwasi milioni 687. Sasa huku ukitaka kwenda Nyamatoke – Bukole milioni 987, sasa na kusogea huku Bunda DC milioni 456. Tunahitaji tusiwe na mradi tu ambao umefanya maji yaje mjini, tunahitaji maji kwenye Kata zote 14. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, waliopo humu tangu 2010 wanajua huyu ni mtoto wangu niliyemlea, sasa amekua anataka kutembea kwenye Kata zote 14 wananchi wa Halmashauri ya Mji wa Bunda wapate maji safi na salama. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Aweso jambo lingine, Mamlaka ya Mji wa Bunda bado changa, hampeleki ruzuku. Unajua shida yake? Wanaongeza bili inakuwa kubwa kwa wananchi na wanalipa kwa sababu wanahitaji maji. Tuwapunguzie mzigo, tupeleke ruzuku waweze kujiendesha. Halafu ule mradi sasa usiwe laana, uwe una neema na bili ya maji iwe standard. Nimesema wananchi hapa wanalipa bili za maji, ambao hawataki kulipa ni huko Serikalini tu, tunaomba bili iwe fair, wananchi wameupokea mradi, mkikamilisha Kata 14 watalipa bili kwa wakati na hizo fedha wataweza ku-maintain maeneo mengine.
Mheshimiwa Spika, bomba kuu linalotoka katika ule mradi linamwaga maji, linavuja, kuna upotevu mkubwa wa maji, ukitoka huku Bunda Store mpaka kule Nyamakokoto maji yanamwagika sana. Tunaomba muangalie, hii inachangia upotevu mkubwa wa maji. Nendeni mkaangalie tatizo ni nini kwenye lile bomba. Naomba sana, ambalo pia linakwenda mpaka kule Kaswaka, naomba muangalie sana.
(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, jambo lingine…
SPIKA: Kengele ya pili imeshagonga Mheshimiwa.
MHE. ESTER A. BULAYA: Ahaa, ndiyo nilikuwa nashuka mambo ya Bunda. Ahsante sana. (Makofi)