Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema kwa kuendelea kutupa uhai na afya njema, na leo amenipa kibali cha kusimama mbele ya Bunge lako tukufu.
Mheshimiwa Spika, naishukuru sana Serikali ya Awamu ya Sita ya mama yetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo inafanyika katika Wizara hii ya Maji. Nawashukuru sana Waziri na Naibu Waziri pamoja na Watendaji wote. Kwa kweli mnafanya kazi kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mradi wa Ziwa Victoria ulianza katika Mkoa wa Shinyanga, ukijumuisha Mkoa wa Shinyanga Mjini pamoja na Manispaa ya Kahama. Kwa kweli sisi wakazi wa Shinyanga ambao tulizaliwa miaka ya 1970 tukakulia pale Shinyanga, tunajua adha ambayo tulikuwa tunaipata. Ilikuwa kabla hujaenda shule, ni lazima uhakikishe umechota maji, na unayachota saa nane usiku, ndiyo unaweza ukayapata yakitoka kwenye Bwawa la Lilwa; lakini sasa hivi maji katika Mkoa wa Shinyanga hasa Shinyanga Mjini na Kahama ni historia. Tunaishukuru sana Serikali yetu kwa juhudi kubwa ambazo imezifanya.
Mheshimiwa Spika, Shinyanga ina majimbo sita. Jimbo la Ushetu lipo katika Wilaya ya Kahama, lakini ni Jimbo pekee ambalo maji ya Ziwa Victoria hayajafika. Ukitoka Kahama kwenda Tabora ni kilomita nyingi, lakini kutoka Kahama Mjini kwenda Ushetu, Kijiji cha mwisho cha Manispaa ya Kahama kwenda Ushetu ni kilomita tano; kutoka Nyandekwa kwenda Ukune ni kilomita tano; kutoka Nyandekwa kwenda Igunda ni kilomita saba; lakini watu wao hawana maji. Mheshimiwa Aweso mmefanya kazi kubwa sana, na tunashukuru katika bajeti hii mmeweza kusema kwamba mmetenga Shilingi bilioni 47 kwa ajili ya maji ya Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu. Tunaomba tutakapopitisha bajeti hii, masuala ya upembuzi yakinifu, usanifu, yafanyike kwa haraka ili wananchi wa Ushetu nao waweze kuepukana na hii adha ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukiangalia maji yamefika Tabora. Kutoka Ushetu kwenda Kaliua, ni kilometa kama 40. Kule Tabora wenzetu wanapata maji, huku Ushetu hawapati maji. Wale wananchi wanakuwa wanyonge, wanaanza kuwaza vibaya kwamba kwa nini sisi tumetengwa? Mheshimiwa Waziri kwa sababu kwenye bajeti hii mmetenga fedha shilingi bilioni 47 kwa ajili ya Halmashauri ya Ushetu, tunaomba basi mweze kutekeleza suala hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunashukuru sana kwa Halmashauri ya Msalala, maji ya Ziwa Victoria katika baadhi ya Kata yapo, hasa katika ule mradi wa upanuzi wa maji ya Kagongwa – Isaka. Tunashukuru sana, matenki matatu yenye ujazo mkubwa wa lita 470,000, yameshajengwa, na utekelezaji umefikia asilimia 80. Kuna vijiji ambavyo vinafaidika kama Jana, Mwalugulu na Itogwamholo, tunaomba basi, katika Halmashauri ya Msalala, kata ambazo hazijafikiwa na haya maji, waweze kupata maji. Ukiangalia Ikinda kule, maji hayajafika; ukiangalia Lunguya, maji hayajafika. Tunaomba kuwe na usawa ili kila mtu aweze kufaidi haya maji ya Ziwa Victoria. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hata katika Jimbo la Kishapu, Wilaya yetu ya Kishapu kuna miradi ambayo inaendelea. Kuna utekelezaji wa mradi ambao unatokea Kishapu – Mwataga, Mkandarasi tayari yuko kazini. Tunaomba huyo Mkandarasi aanze kazi mara moja. Speed aliyonayo Mheshimiwa Waziri, tunaomba na kwa watendaji speed hiyo hiyo iendelee.
Mheshimiwa Spika, pia tumepata mradi wa Shilingi bilioni 6.5 wa Igaga - Mwamashele - Ngofia – Lagana, na Mkandarasi yuko site. Tuseme nini sisi watu wa Shinyanga? Kwa kweli tunashukuru. Kwa sababu upungufu ni kidogo kuliko mafanikio na maendeleo ambayo tumeyapata kwenye sekta hii ya maji. Tunaomba basi sehemu ambapo kuna upungufu, Serikali iongeze msukumo. Watu wa SHUWASA, DUWASA na RUWASA, wanafanya kazi kubwa sana, wanatusikiliza Wawakilishi wa Wananchi, wanafanya mambo makubwa sana, na Waheshimiwa Waheshimiwa wa Majimbo wanapambana sana kuhakikisha kwamba wananchi wao wanapata maji safi na salama. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimalizie na Jimbo la Solwa, Wilaya ya Shinyanga. Kwa kweli katika Wilaya hii, nafikiri kama kuna Wilaya ambazo zimependelewa, na Mheshimiwa Mbunge ame-fight sana kuhakikisha kwamba wananchi wake wanapata maji, basi ni katika Jimbo la Solwa. Kwa kweli kuna miradi mikubwa ambayo inaendelea; mradi wa Tinde – Shelui, zaidi ya vijiji 34 vinapata maji, vikiwemo 22 vya Jimbo la Solwa.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri, tunaomba basi utekelezaji wa sehemu ambazo maji hayajafika hasa katika miradi ambayo inaendelea na fedha zimekwisha tengwa basi maji yaweze kufika kwa wakati na wananchi wa Mkoa wa Shinyanga hususani Jimbo la Solwa, waendelee kupata maji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninaomba nitoe ushauri, Serikali yetu imetenga fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya maji, wakandarasi wako site, wengine wanakaribia kumaliza kazi zao, wengine wamekwisha maliza. Tunaomba muwalipe fedha kwa wakati kusiwe na ucheleweshaji wa aina yoyote. Kwa sababu unapomchelewesha mkandarasi kuna masuala mazima ya kupigwa faini.
SPIKA: Mheshimiwa Christina, kengele ya pili imeshagonga ahsante sana.
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi ninaunga mkono hoja kwa asilimia 100. (Makofi)