Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

Hon. Aysharose Ndogholi Mattembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

MHE. AYSHAROSE N. MATTEMBE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hoja iliyoko mezani. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenijalia uzima na kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu. Nikupongeze wewe kwa kazi nzuri unayoifanya kwa kuliongoza vyema Bunge letu.

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii pia kuwapongeza Mheshimiwa Waziri, Juma Aweso, Naibu wake Mheshimiwa Maryprisca na watendaji wote wa Wizara ya Maji kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuhakikisha maji yanapatikana katika maeneo yote. Nawapongeza sana, lakini pia nimpongeza sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi nzuri anayoifanya ya kumtua mama ndoo kichwani na kuhakikisha maji yanapatikana katika Mkoa wangu wa Singida. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya wanawake wa Mkoa wa Singida, nampongeza sana na namshukuru sana. Maji ni uhai, pamoja na pongezi hizo, Mkoa wangu wa Singida bado una changamoto kubwa sana ya upatikanaji wa maji safi na salama. Natambua jitihada kubwa za Serikali za kuhakikisha maeneo yote yanapata maji hususan ya vijijini lakini mkoa wangu bado una changamoto kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naishukuru sana Serikali kwa Wilaya yangu ya Manyoni kupata maji katika Vijiji vya Rift Valley, Kintinku, Lusilile, Makasuku, Sasilo na uchimbaji wa maji visima 10 lakini upo mradi ambao tumekuwa tukiupigia sana kelele, Mradi wa Maji Kintinku, Lusilile. Namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kutupatia fedha kiasi cha bilioni tano. Niiombe sana Serikali, basi fedha hizi zitoke kwa wakati ili sasa mradi huu uweze kukamilika, kwa kuwa umekuwa ni wa muda mrefu toka Awamu ya Nne, mradi huu hadi sasa haujakamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naishukuru pia Serikali kwa kupata miradi katika Wilaya yangu ya Mkalama ambapo ni Kijiji cha Singa, Tumuli, Mdilike, Matongo pamoja na uchimbaji wa visima 10, lakini yapo maeneo ambayo bado hayana maji kabisa katika Wilaya ya Mkalama. Maeneo haya ni Vijiji vya Mwangeza, Kisiluhida pamoja na Singa. Yana changamoto kubwa sana ya upatikanaji wa maji, niiombe Serikali iviangalie kwa jicho la kipekee vijiji hivi ili navyo viweze kuapata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru pia Serikali kuweka Mradi wa Maji Vijiji 28 na katika Mkoa wangu wa Singida tumeweza kupata Kiomboi, Manyoni pamoja na Singida Manispaa, lakini bado ipo miji ambayo inakuwa kwa kasi kama vile Ilongero, Ikungi, Mitundu na Nduguti. Niombe sana basi miji hii nayo iweze kupatiwa fedha kwa ajili ya upanuzi wa miradi ili wananchi wa maeneo hayo waweze kupata maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika Wilaya yangu ya Singida Vijijini, tumepata Mradi wa Semfuru, Ndugira, Ikiwu na Kinyamwenda, lakini kipo kijiji kimoja ambapo kupata chanzo cha maji ni changamoto kubwa sana. Kwa hiyo, niombe sana kijiji hiki cha Mangida nacho kiangalie kwa jicho la pekee. Yapo maeneo ya karibu ambayo yana ambapo maji hayo yanaweza kuvutwa hadi kupelekwa katika kijiji hicho cha Mangida. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika Mkoa wangu wa Singida kuna changamoto kubwa ya watumishi na niombe pia Serikali iangalie na tuweze kupata watumishi wa kutosha katika Mkoa wangu wa Singida ili utekelezaji wa miradi ya maji uweze kufanyika kwa ufanisi.

Mheshimiwa Spika, niwapongeze sana watendaji wa RUWASA katika Mkoa wangu wa Singida ambao wamekuwa wakifanya kazi nzuri sana ya kuhakikisha maji yanapatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa haya machache, naunga mkono hoja na nakushukuru sana kwa nafasi. (Makofi)