Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

Hon. Innocent Lugha Bashungwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Karagwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia bajeti ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora). Nianze kwa kuendelea kumpongeza Rais wetu Mheshimiwa Magufuli, Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Makamu wa Rais na Baraza la Mawaziri kwa kuendelea kufanya kazi nzuri ya kuwaletea matumaini Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuchangia kwangu bajeti ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora), ningependa kuchangia katika sehemu mbili; sehemu ya kwanza, ni changamoto za wananchi wangu wa Jimbo la Karagwe na sehemu ya pili ni ushauri kwa Serikali. Kwa sababu changamoto kwenye Jimbo langu la Karagwe ni nyingi, naomba kwanza nijikite kwenye hizi changamoto. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kwa kumshukuru kaka yangu Mheshimiwa Simbachawene kwa kazi nzuri na kuwa msikivu pale tunapomfuata kuwasilisha changamoto za wananchi wetu. Namshukuru Mheshimiwa Angellah Kairuki kwa kuwa msikivu na kwa kutupa ushirikiano mzuri katika kusikiliza changamoto za wananchi wetu na kaka yangu Naibu Waziri, Mheshimiwa Jafo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Karagwe ina changamoto nyingi, lakini kwanza nianze kwa kuwashukuru wananchi wa Karagwe kwa kuendelea kuniamini na kunituma hapa kuwa Mbunge wao. Wiki mbili zilizopita Karagwe tulipata janga kubwa, tumepata janga la moto pale Kayanga, maduka zaidi ya 117 yaliungua.
Mhesimiwa Mwenyekiti, kwa kweli, naomba nitumie nafasi hii kuwapa Wahanga wa moto, wananchi wa Karagwe pole sana na nitumie nafasi hii kwanza, nimshukuru Mheshimiwa Jenista Mhagama na Mheshimiwa Simbachawene kwa kuwapa pole Wana-Karagwe na kwa kuniahidi kwamba Serikali itaangalia namna ya kuwasaidia hawa wahanga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, juzi kulitokea tukio la ujambazi stesheni ya Nyakaiga, majambazi wakaua mwananchi mmoja pale na mwingine wakamjeruhi sana. Pale Nyakaiga ni stesheni kubwa, ina wananchi wengi lakini hatuna huduma ya kituo cha polisi. Napenda kuiomba Serikali itusaidie, pale Mji umekua, Serikali itusaidie kujenga kituo cha polisi ili wananchi waweze kuishi kwa amani na usalama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema, kuna changamoto nyingi Jimbo la Karagwe, lakini nitaje chache. Nianze na madeni viporo. Pamoja na jitihada ya Serikali kupeleka fedha za maendeleo, bado kuna changamoto ya kuchelewesha hizi fedha.
Katika Halmashauri ya Karagwe, bado tuna madeni makubwa ya wakandarasi, watumishi na wazabuni. Napenda kuiomba Serikali katika kipindi cha mwaka huu wa fedha wa 2015/2016 kabla hatujaenda mwaka wa fedha mpya, Serikali ijitahidi ituletee fedha ambazo tulitakiwa kupata katika kipindi cha mwaka wa fedha ili tuweze kupunguza haya madeni na fedha ambayo imetengwa kwa mwaka wa fedha unaokuja 2016/2017 iweze kwenda kufanya kazi za maendeleo ambazo tumezitarajia katika mwaka wa fedha unaofuata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna tatizo kubwa la upungufu wa watumishi katika Jimbo la Karagwe. Kwa upande wa walimu, sekta ya elimu kwa shule za msingi tu, tuna upungufu wa walimu 832. Kwa upande wa shule za sekondari tuna upungufu wa walimu 92.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sekta ya afya kwa upande wa upungufu wa watumishi tuna upungufu wa wauguzi 40 na madaktari watano na kwa upande wa kilimo Afisa Ugani tuna upungufu wa watumishi 15 na upande kwa maendeleo ya jamii tuna upungufu wa wataalam 27.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama takwimu zinavyoonesha, Halmashauri yangu ina upungufu mkubwa sana wa watumishi. Napenda kutumia nafasi hii kumwomba Mheshimiwa Waziri Angellah Kairuki, aione Karagwe. Tunakutegemea sana na tunaamini utatusaidia katika hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika suala la madeni ya Halmashauri, napenda kuishauri Serikali, kama fedha kutoka Hazina imekuwa ikichelewa kutolewa kwa miaka mingi, basi tuangalie ule utaratibu wa asilimia 70 ambazo zinatoka Halmashauri kwenda Hazina, tuigeuze ile; zile asilimia 70 zibaki kwenye Halmashauri halafu asilimia 30 ndiyo iende Hazina ili fedha za maendeleo siziwe zinachelewa kwa wananchi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna upungufu wa vitendea kazi hasa kwenye sekta ya afya kwenye Jimbo la Karagwe. Karagwe ina watu wasiopungua 350,000 na sisi tumezaa Jimbo jipya la Kyerwa ambalo bado tunaendelea kulihudumia katika huduma za afya kama Wilaya mama ya Karagwe ambayo imezaa Jimbo la Kyerwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukichukua Kyerwa na Karagwe, tuna jumla ya watu wasiopungua 800,000, lakini bado tuna ambulance moja tu ambayo inahudumia vituo vya afya 35 na jiografia ya Karagwe imesambaa sana. Kwa hiyo, naiomba TAMISEMI itusaidie angalau tupate ambulance mbili ili wananchi wa Karagwe wapate huduma ya ambulance pale tunapohitaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika upande wa afya, tuna hospitali ya Nyakahanga lakini imeelemewa. Kama nilivyosema, Kyerwa bado haijawa na Hospitali ya Wilaya, Karagwe Wilaya mama pia haina hospitali ya Wilaya. Tunategemea hiyo hospitali ya ELCT. Natumia nafasi hii kulishukuru kanisa la ELCT kwa kuendelea kusaidia wananchi wa Karagwe na hospitali ya Nyakahanga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia Karagwe tunakua kwa watu wasiopungua 10,000 kwa mwaka; hospitali imekuwepo miaka mingi sana, imefika mahali imeelemewa na inasaidiwa na kituo cha afya cha Kayanga ambacho hivi sasa hakina wodi ya akina mama na watoto. Kina wodi ya wanaume; na kituo hiki hakina wodi ya kulaza wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji. Kwa hiyo, napenda kumwomba kaka yangu, Mheshimiwa Simbachawene na Naibu Waziri Mheshimiwa Jafo, mtuangalie katika hili pia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna changamoto za barabara ambazo ziko chini ya TAMISEMI. Kuna barabara ya kuanzia Nyakasimbi kwenda Nyakakika, Kibondo, Nyabiyonza, Kiruruma mpaka kwenda kwenye Wilaya ya Kyerwa kupitia Rwabwere, hii ni barabara ambayo inaunganisha Wilaya mbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuiomba Serikali hii barabara ipandishwe kwenye kiwango wa TANROAD kwa sababu kwa kufanya hivi tutakuwa tumeondoa mzigo kwa Halmashauri, itatengenezwa katika kiwango kizuri na itasaidia kuinua uchumi wa wananchi wa Karagwe na Kyerwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mheshimiwa Rais Magufuli wakati alipokuja Karagwe kuomba wananchi ridhaa ya kuwa Rais wa Tanzania alituahidi barabara ya Nyakahanga kwenda Chamchuzi tuipandishe TANROAD na ijengwe kwa kiwango cha lami na tuweke kivuko pale Chamchuzi ili kusaidia kuimarisha biashara kati ya Karagwe na jirani zetu wa Rwanda. Kwa hiyo, napenda kuiomba Serikali itusaidie hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimefuatilia Wizara ya Ujenzi wakanielekeza kuwa kuna utaratibu wa kuingiza ahadi za Mheshimiwa Rais kwenye kitabu cha ahadi za Mheshimiwa Rais, lakini mimi ni mwakilishi wa wananchi wa Karagwe, Mheshimiwa Rais alitamka mwenyewe, Mheshimiwa Rais hawezi kusema uongo, na mimi hapa mwakilishi wa wananchi wa Karagwe siwezi kusema uongo. Napenda kuiomba Serikali itumie taarifa hii kama ni rasmi kwamba hili kweli lilitamkwa na watusaidie tupate hii barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na ninaunga mkono hoja.