Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Singida Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa fursa hii muhimu sana kwa ajili ya kutoa mchango wangu katika sekta hii muhimu sana ambayo ndiyo chanzo cha uhai wa mwanadamu.
Mheshimiwa Spika, na mimi naomba nianze kwa kutoa pongezi nyingi sana kwa Mheshimiwa Waziri kwa utendaji wake mzuri, pamoja na Naibu wake na watendaji wake Wizarani, mikoani na mpaka wilayani.
Mheshimiwa Spika, sisi kule mkoani Singida katika maeneo ambayo tunajivunia kwamba kweli yana watendaji makini ambao kusema kweli wanatupa ushirikiano wa kutosha ni Meneja wa RUWASA wa Mkoa pamoja na kwangu wilayani. Kwa kweli nadhani ni labda wametengeneza hivyo wamekuwa trained kwa sababu MheshimiwaWaziri yuko hivyo basi hata kule chini pia tunapata hivi vionjo. Ninamuomba Mheshimiwa Waziri pamoja na watendaji hawa wasibadilike, waimarike, waendelee kuwa humble, waendelee kuwa imara katika utendaji na sisi tuko tayari kushirikiana nao.
Mheshimiwa Spika, mimi naomba kwanza nitoe shukrani nyingi sana pia kwa Mheshimiwa Rais, kwa ile mitambo aliyotuletea katika mikoa yetu ya kuchimba maji. Katika maeneo ambayo tunaona jambo hili ni la muhimu na kweli limetufaa ni Mkoa wa Singida hasa Jimbo la Singida Kaskazini.
Mheshimiwa Spika, katika kumbukumbu zangu hotuba yangu ya kwanza kwenye Wizara hii nilisema hapa wazi kabisa hapa kwamba, sisi Singida tunakunywa maji na fisi kwa sababu ya shida kubwa ya maji tuliyokuwa tunapata. Wananchi walikuwa wanakesha, usiku wa wa mane akina mama walikuwa hawalali, ndoa zilikuwa zinayumba kwa sababu mama ule muda anaotakiwa kuhudumia ndoa usiku yeye anaenda kusubiri maji kwenye mito. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini leo hii, kwa kupitia ule mtambo wa mama ule alilotuletea mkoani Singida, na kwa wilayani kwangu kwa Jimbo la Singida Kaskazini umeshatuchimbia visima vinavyopata vitano mpaka hivi sasa. Nimechimba maji katika Kijiji cha Nduhila ambapo huo mradi utakwenda kufanyiwa usambazaji wa zaidi ya Kijiji cha Nduhila. Kupitia mtambo huu tumepata katika Vijiji vya Makuro, Mkenge, Matumbo na bado kazi inaendelea kwenye maeneo mengine.
Mheshimiwa Spika, kwa mazingira kama haya siwezi kuacha kumshukuru na kumpongeza Rais wetu kwa kazi hii kubwa, kwa sababu sisi katika Imani tunasema ukichimba kisima unakuwa umetoa sadaka inayoendelea hata kama ukifa. Kwa hiyo hapa Mheshimiwa Rais ametenda wema na ametoa sadaka ambayo itaishi milele, haitamfuata hata kesho atakapokuwa hatupo hapa duniani.
Mheshimiwa Spika niishukuru sana pia kwa miradi 15 ya maji ambayo tutapata katika Jimbo langu la Singida Kaskazini, ambapo kupitia gari hili alilotuletea Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ninaamini tutapata visima katika Vijiji vya Ntondo, Nkwaye, Sekouture, Kinyamwenda, Msikii, Mwalala, Nongwa Mpoku, Igauli, Mwakiti, Itamka, Mkende kama nilivyoisema, Makuro, Nyisinko, Isimihi na Kijiji cha Mahandi.
Mheshimiwa Spika, haya ni maeneo ambayo kwa kweli wananchi walikuwa wana kiu ya maji ya muda mrefu lakini sasa watapata maji na hivyo watakata ile kiu. Jambo kubwa ninaloliomba hap ani kwamba, hii miradi itekelezeke kwa wakati ili wananchi nao waionje hii keki ndogo ya Taifa lao, waonje ule utamu wa maji ambao wamekuwa wakiukosa kwa muda mrefu.
Mheshimiwa Spika, vilevile niombe kuwasilisha changamoto chache zilizopo kwenye Jimbo langu la Singida Kaskazini ili Waziri atusaidie wananchi wetu nao waendelee kufurahia. Jambo la kwanza kuhusu usambazaji wa maji katika miji midogo; nikianza na mji wa Ilongero ambayo ni Makao Makuu ya Halmashauri. Huu mji hivi sasa ni populated, umeshakuwa na idadi kubwa ya watu na bado watu wanahamia. Una huduma muhimu za kijamii, una Hospitali ya Wilaya ambayo inahitaji maji muda wote.
Mheshimiwa Spika, tunacho kisima pale, lakini sio cha kudumu sana, tunahitaji maji kwenye miji midogo kama vile kuna masoko, kuna huduma nyingine. Katika huu mji kuna mradi pale unaitwa Uyanjo lakini umezidiwa. Naomba upanuzi kwenye huu mradi, ili uweze kuwafikia wananchi wengi ambao wanahamia kwenye ule mji, wanaojenga, sasa hivi kuna ujenzi wa hali ya juu unaendelea, kwa hiyo, niombe maji ya kutosha na ya kudumu, hivyo, upanuzi ufanyike, ili wananchi wengi wapate maji.
Mheshimiwa Spika, Mji Mdogo wa Mtinko. Ule mji una mradi wa maji, lakini mji ule maji yanayotoka pale ni ya chumvi. Kwa hiyo, niombe tupate teknolojia ya ku-purify yale maji ili yaweze kuwa matamu, kama haiwezekani basi tutoe maji kwenye miradi ya jirani, ili maji yale yawe matamu. Tunaumia, sasa hivi unaona meno yangu pamoja na kwamba, ni mazuri, lakini yanakuwa ya njano, tunakunywa maji ya chumvi, tunaharibiwa meno. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama walivyosema wazungumzaji wa kutoka Mkoa wa Arusha, kule watu wanaharibika viungo wanakuwa walemavu kwa sababu ya maji. Sasa shida yetu sisi Singida ni maji ya chumvi, kwa hiyo, niombe sana kuwe na teknolojia ya ku-purify maji, ili yaondoe kero hii, lakini hili niunganishe hapa katika Kitongoji cha Gairu kilichopo Kijiji cha Sagara; pale maji yapo, lakini ni ya chumvi mno, yaani ukinywa ni zaidi ya chumvi hiyo unayoifahamu.
Mheshimiwa Spika, niombe sana badala ya kuchimba kisima katika lile eneo, tutoe maji kwenye Kijiji cha Sagara, kipo chanzo cha kudumu, kizuri, kina maji ya kutosha. Tutoe maji kule juu tuyashushe, ni umbali wa kama kilometa mbili au almost two kilometers, nadhani haziwezi kuzidi hapo. Ni rahisi kusambaza maji kutoka kwenye chanzo cha Sagara kuliko kuchimba kisima kipya kwa sababu, tutakapochimba itakuwa ni chumvi tena. Nimeona kwenye bajeti kwamba, tunacho kisima pale, lakini nashauri badala ya kuchimba kisima tupeleke maji kutoka chanzo cha Kijiji cha Sagara ambacho maji yale ni matamu.
Mheshimiwa Spika, nilikuwa nazungumzia miji midogo, ukiwemo Mji wa Ngamu. Mji wa Ngamu una maji, lakini naomba usambazaji ufanyike ili wananchi wengi wapate huduma ile.
Mheshimiwa Spika, kuna eneo lingine na maeneo ambayo tumekuwa tukichimba maji, lakini hayatoki. Mfano Kijiji cha Mangida, alikisema pia Mheshimiwa Aysharose, Kijiji hiki tumechimba maji zaidi ya mara tatu, lakini maji hayatoki, lakini kuna vijiji jirani ambavyo vina maji na ni maji ya kutosha. Mathalani sasa hivi wanapata maji kutoka Mradi wa Kijiji jirani cha Sefunga.
Mheshimiwa Spika, niombe tufanye extension kwenye huu mradi, lakini pia hata Kijiji chenyewe cha Mangida kina maji, lakini yako mbali kidogo kama kilometa mbili. Tuyatoe maji pale, kuna mradi ambao ni wa muda mrefu umechakaa, ni wa tangu Nyerere wenyewe wanasema, kuna yale matanki yale wanasema ya Mjerumani, liko tanki kubwa sana pale, tuyavute maji kutika ule mradi, mengine tuyatoe pale Sefunga, wale wananchi waache kuteseka.
Mheshimiwa Spika, hakika wananchi wa Mangida wanateseka mno kwa shida ya maji. Niombe sana hii iwe ni mara yangu ya mwisho kuitaja Mangida kwa suala la maji, niombe sana Mheshimiwa Waziri alichukue hili kama ni special case atuletee maji pale kwenye kile Kijiji. Nimeona pia kuna mradi wa kisima pale, si sawa kuchimba pale maji kwa sababu, tumekuwa tukichimba hayatoki.
Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho ni Kijiji cha Mwokulu. Mheshimiwa Waziri aliwahi kufika pale wakati ule walivyokuja, akaahidi pale kwamba, atatusaidia kisima pale, niombe sana atuletee kisima pale, ili wale wananchi waweze kunufaika.
Mheshimiwa Spika, la mwisho kabisa ni gari. Halmashauri yangu ya…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Ahsante sana. Kengele ilishagonga Mheshimiwa.
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naunga mkono hoja, RUWASA Wilaya yangu hawana gari naomba wapatiwe gari, usafiri, wanateseka mno wamekuwa kama digidigi. Naomba kuwasilisha, ahsante sana. (Makofi)