Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

Hon Munira Mustafa Khatib

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

MHE. MUNIRA MUSTAFA KHATIBU: Mheshimiwa Spika, awali ya yote namshukuru Mungu kwa kunijalia afya njema. Aidha, nampogeza Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake katika kushughulikia tatizo la maji nchini.

Mheshimiwa Spika, juhudi za Mheshimiwa Rais zinaonesha wazi dhamira yake ya kutua ndoo kichwani wanawake ambao ni waathirika wakubwa wa tatizo la maji. Hatua hizi za Mheshimiwa Rais zinaonekana kupitia namna alivyotoa fedha za miradi ya maendeleo ya maji.

Mheshimiwa Spika, miradi ya maendeleo; katika mwaka 2022/2023 Wizara ya Maji - Fungu 49 ilitengewa shilingi 657,899,338,000; kiasi hicho kinajumuisha shilingi 407,064,860,000 fedha za ndani na shilingi 250,834,478,000 fedha za nje.

Mheshimiwa Spika, hadi mwezi Aprili, 2023 Wizara imepokea jumla ya shilingi 623,753,326,424.64 sawa na asilimia 94.81 ya bajeti iliyoidhinishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa mwaka 2022/2023; kati ya fedha zilizopokelewa shilingi 374,794,312,195.31 sawa na asilimia 92.07 ni fedha za ndani na fedha za nje ni shilingi 248,959,014,229.33 sawa na asilimia 99.25.

Mheshimiwa Spika, kwa namna fedha zilivyotolewa na Mheshimiwa Rais ni wazi kuwa amelenga kuondoa changamoto ya maji nchini.

Mheshimiwa Spika, pamoja na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kutoa fedha za kutosha katika Wizara hii, bado kuna changamoto kadhaa ambazo zinaathiri malengo yaliyokusudiwa. Changamoto hizo ni kama ifuatavyo; upatikanaji wa maji katika Jiji la Dodoma.

Mheshimiwa Spika, pamoja na juhudi za Serikali, tatizo la maji Dodoma limeendelea kuumiza wananchi kutokana na uhitaji wa maji. Mahitaji hayo yanatokana na ongezeko la wananchi waliohamia Dodoma na kuanzisha makazi. Hali ilivyo sasa maji yanatolewa kwa mgao wa mara tatu kwa wiki hali ambayo inarudisha nyuma maendeleo hasa kwa wale wananchi wanaojishughulisha na biashara ya maji na sekta ya maji.

Mheshimiwa Spika, pamoja na juhudi za Serikali za kuondoa changamoto hizo kwa kuanza mpango wa kuleta maji kutoka Bwawa la Mtera na kujenga bwawa jipya la Farkwa, hatua hiyo haijaonesha dhamira ya muda mfupi ya kuondoa tatizo hilo. Nashauri Wizara kuharakisha mchakato wa kukamilisha hatua za ujenzi wa miradi hiyo.

Mheshimiwa Spika, kuhusu changamoto ya wakandarasi kuchelewa kulipwa; kumekuwepo na changamoto ya wakandarasi kutekeleza miradi bila kulipwa fedha zao kwa wakati hali ambayo imesabisha miradi kuchelewa kukamilika na nyingine kukwama na kuongeza gharama za utekelezaji wa miradi hiyo.

Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali kulipa madeni ya wakandarasi kwa wakati ili miradi ya maji iweze kukamilika kwa wakati.

Kuhusu changamoto ya wakandarasi kupewa mradi zaidi ya mmoja; taarifa zinaonesha kuwa moja ya changamoto kubwa ya kutokukamilika kwa miradi ya maji nchini ni pamoja na mkandarasi mmoja kupewa mradi zaidi ya mmoja. Hali hiyo imesababisha wakandarasi wengi kushindwa kukamilisha miradi hiyo kwa wakati kwa kuwa wamekuwa wakihamisha mashine na nguvu kazi kutoka mradi mmoja kwenda mradi mwingine.

Mheshimiwa Spika, tatizo hili linasababisha hasara kubwa kwa Serikali kutokana na miradi kuchelewa kukamilika na kusababisha ongezeko la gharama za vifaa. Hivyo ni rai yangu kuwa Wizara itaangalia suala hili kwa kina katika mipango ijayo ya miradi ya maji nchini.

Mheshimiwa Spika, mwisho nampongeza Waziri wa Maji Mheshimiwa Jumaa Aweso na Naibu wake Mheshimiwa Maryprisca Mahundi kwa kazi nzuri wanayoendelea kufanya katika Wizara hii.

Mheshimiwa Spika,naunga mkono hoja.