Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Magdalena Hamis Sakaya

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Kaliua

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia kidogo kwenye Mpango uliopo mbele yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue fursa hii pia kuendelea kuwashukuru wananchi wa Jimbo la Kaliua kuendelea kuniamini kuwa mtumishi wao na kunipa tena fursa ya kuweza kuwepo ndani ya chombo hiki cha uwakilishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitabu hiki nimekipenda sana kwa kuwa kina Mipango mizuri kweli kweli, tena sana. Nina imani kabisa kama itakwenda kutekelezwa vizuri nchi yetu itapiga hatua kubwa sana. Wasiwasi wangu ni wale wanaokwenda kutekeleza, juzi nilichangia kwa ufupi, tuna shida kubwa ya watendaji wa nchi yetu. Tumekuwa na gap kubwa, watu hawafanyi kazi kwa kuwajibika, hii Mipango yote haiendi kufanywa na robbot, inakwenda kutekelezwa na watu kwa kutumia brain zao, mikono yao na akili Mungu alizowapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma kwenye kitabu, kwenye mradi mmojawapo mkubwa ni kusomesha vijana wengi kwa mkupuo katika fani mbalimbali. Sijaona Mpango gani wa kwenda kubadili mindset za watendaji wa nchi hii na vijana wetu wakasome, wakielewa wanakwenda kusoma kwa ajili ya kwenda kufanya nini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna shida kubwa kama Serikali haitaangalia hili, Mipango yote hii iliyopo huku haina watekelezaji. Kwa hiyo, shida kubwa namna gani kwenye mipango yao ya kawaida ya Serikali lazima waliopo kazini, wanaoingia, waliopo mashuleni wakajengewe uwezo namna gani ya kujituma, namna gani ya kuwajibika, namna gani ya kujipima na kwenda kutekeleza miradi ya Kitaifa ambayo ipo kwenye mipango hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze suala kubwa tulilonalo ni suala la maji, tena niseme kwa uchungu mkubwa. Nchi yetu ina shida kubwa sana ya tatizo la maji na ni tatizo ambalo linawatesa watu, nina maumivu makubwa na zaidi kabisa kwa kina mama na watoto. Kina mama wengi wanakosa hata fursa za kuhudumia familia kwa sababu ya maji, lakini watoto wengi na hasa wa kike wanakwenda kufuata maji wanakosa hata muda wa vipindi kwenye madarasa wanachelewa shuleni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa miradi ya maji, nimesoma mingi huku, ninavyosikia Serikali inasema kwamba tutaendelea na utaratibu wa maji vijijini, ndiyo hadithi miaka yote. Nimekaa ndani ya Bunge hili miaka 10 tunaambiwa miradi ya maji, miradi ya World Bank, kwenye Wilaya yangu ya Kaliua, kati ya vijiji vyote vijiji vitatu tu vilipatikana na maji na yale maji hayakusambazwa popote, yameishia pale pale. Kwa hiyo, unavyosema kwamba tutaendelea na utaratibu wa kumalizia au kutekeleza Miradi ya Maji ya Vijiji 10 ya World Bank almost 70% ili-fail.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba lazima tunapokwenda kuangalia miradi ya maji tuone kweli inafanikiwa. Nimeangalia kwenye Mpango hapa, Mkoa wetu wa Tabora tulipata faraja baada ya kuambiwa kwamba kuna mpango wa kutoa maji Ziwa Victoria kuleta Wilaya zote za Mkoa wa Tabora, kuanzia Nzega kwenda Igunga kwenda Bukene mpaka Sikonge, Tabora Mjini mpaka Urambo, Kaliua haikuwepo. Nimeangalia hapa tena haipo kwenye Mpango wa mwaka huu, haipo kabisa, kwamba ule Mpango umeishia wapi? Ni miaka mitatu uchambuzi yakinifu unafanyika, miaka mitatu upembuzi unafanyika, miaka mitatu utafiti unafanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hotuba ya Mheshimiwa Rais hapa alisema ule uchambuzi na upembuzi yakinifu utakuwa haupo tena kwenye Serikali hii, mbona huu upembuzi unaendelea miaka mingi. Naomba sana kwenye mpango wa mwaka huu mradi wa kutoa maji Ziwa Victoria kuleta Mkoa wa Tabora na Wilaya zake utimie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Wilaya yangu ya Kaliua Mpango wa Victoria haupo na mpango uliokuwepo kwenye Wilaya ya Urambo kuanzia mwaka 2013 ni kutoa maji kutoka Ziwa Ugala. Ni jambo la kusikitisha juzi nimesikia Mheshimiwa Waziri anasema hapa, mchakato bado unaendelea 2014 zilitengwa milioni 450 kufanya uchambuzi yakinifu na upembuzi, leo ni mwaka wa tatu bado uchambuzi unaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini bado Serikali ikaja na mpango wa kwenda kutoa maji Malagarasi, bado tunaambiwa uchambuzi yakinifu unaendelea. Naiomba Serikali, kwenye Mpango huu uwepo mradi wa maji katika Wilaya ya Kaliua wa kuondoa machungu na mateso kwa akinamama wa Kaliua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kuendelea kushuka kwa shilingi ya Tanzania. Nilikuwa nazungumza, nitaendelea kuzungumza, ndiyo wajibu wangu kama mwakilishi. Tumekosa udhibiti wa shilingi yetu ya Tanzania kabisa kwa miaka yote na nimekuwa namlaumu hata Benno, Gavana Mkuu, ameshindwa kusimamia, kusimama kwa shilingi ya Tanzania. Ni Tanzania pekee, dola inatumika kununua vitu madukani, ni nchi gani utakayokwenda ukatumia Tanzania shillings kununua vitu madukani kwao. Tanzania tunatumia fedha ya nje kununua vitu, kutoa huduma kwenye maduka yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ni Tanzania pekee kuna utitiri wa bureau de change kila kona unakuta viduka vya kubadilisha fedha. Leo ukienda Kariakoo watu wana dola mikononi, mikononi tena Wamachinga watu wadogo, wanashika dola wanauza nchi gani hii! Kuendelea kushuka kwa shilingi ya Tanzania kumeendelea kushusha uchumi wetu, hili hatulifahamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda nchi nyingine kubadilisha fedha unaingia gharama kubwa unateseka kweli na wana centers Tanzania tunaongea hapa halifanyiwi kazi. Kwenye Mpango wa mwaka huu tunataka tujue mpango wa kudhibiti matumizi ya dola ndani ya nchi yetu, mpango wa kudhibiti maduka holela ya fedha hapa nchini na mpango wa kuimarisha fedha yetu ya Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatusafirishi chochote Tanzania, sisi ndiyo tumekuwa masoko ya wenzetu, tunauza kila kitu, ni masoko tu, masuala mengine hayajaleta viwanda vikubwa vya ajabu. Hivi kweli, tunahitaji kiwanda cha aina gani kutengeneza pamba stick, tunaagiza kutoka nje. Tunahitaji kiwanda cha aina gani kutengeneza toothpick ya kuchokonolea meno, tunaagiza kutoka nje, tunahitaji kiwanda gani kule kuleta ndani ya nchi yetu vibiriti, vitu vingine ni vidogo vinatutia aibu, ni Taifa kubwa, lakini hebu aibu hii iondoke. Vile vitu ambavyo tuna uwezo navyo ndani ya nchi yetu tusiagize, tumezidi kuwa masoko ya wenzetu, tunatoa ajira kwa wenzetu, sisi tunaendelea kunyanyasika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimefurahi kusikia kwenye hotuba hapa, kwamba, kuna viwanda kuendana na jiografia ya nchi yetu. Tuna bahati kweli Watanzania, maeneo mengi almost karibu kila kanda ina vitu ambavyo Mungu ameweka. Mkoa wa Tabora tuna misitu, tunasafirisha mbao, kuna magogo, jambo la ajabu vijana wanadhurura, hawana ajira, lakini mbao zinapelekwa China zinakwenda kutengeneza furniture tunarudishiwa makapi, tunanunua. Tunaomba kwenye Mpango wa mwaka huu kuwepo kiwanda kikubwa Mkoa wa Tabora cha kutumia rasilimali ya mbao na magogo ya Tabora, badala ya kusafirisha yaende nje, vijana wapate ajira, lakini pia tuweze kuzalisha ndani ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilisema hapa Bungeni, itahakikisha samani zote za ofisi zinanunuliwa ndani ya nchi. Huu ni mwaka wa nne, Serikali wameshindwa wanaagiza, leo ukienda ofisi zote za Serikali ni samani za Kichina, wakati tunao vijana, tunazo mbao, tunayo magogo, miti ya thamani, mininga, mikongo mnapeleka China, tunaletewa makapi, tunanunua vitu ambavyo ni very low quality, this is shame! Naomba sana Serikali kwenye Mpango ihakikishe sasa ile mipango ya miaka mitatu, minne iliyopita hakuna kutoa kitu nje, tuwezeshe vijana wetu, tuwezeshe Magereza, tuwezeshe Jeshi ili tununue vifaa ndani ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la kilimo. Hili ni muhimu kwa hiyo, lazima tuligusie, lazima tuwe na kilimo cha uhakika, lakini pia lazima tuhakikishe kilimo chetu kinaendana na hali halisi. Leo kilimo chetu kimekuwa cha jembe la mkono kwa asilimia kubwa. Lakini pia utaratibu unaotumika kupata pembejeo sio mzuri, ni wizi unafanyika, Serikali kila mpango unaokuja nao hautekelezeki. Sasa tunaomba, tunapokwenda kwenye uchumi wa viwanda uende sambamba na uchumi na kilimo chenye tija. Umwagiliaji, pembejeo, mechanization, wawezeshaji wale watumishi wawe wa kutosha lakini pia wawe na ujuzi wa kutosha kuweza kutoa elimu kwa ajili ya kilimo chetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, ni suala la elimu. Nashukuru kwamba Mheshimiwa Rais ameamua kutoa elimu bure kwa Watanzania, ni jambo jema. Naomba suala la elimu bure liendane na miundombinu ya watoto, ukiwapa leo watoto elimu bure, wengi wanakaa chini, kwangu Kaliua kule watoto wanasomea chini ya mti. Mtoto anasomea chini ya gogo, kwanza hajui kama kuna elimu bure kwa sababu ananyeshewa na mvua, anapigwa na jua, lakini pia tuhakikishe watoto wetu wanakaa kwenye madawati yote.
Kwa hiyo, naomba kwenye Mpango huu, mwaka huu Serikali ihakikishe ndani ya mwaka mmoja, watoto wote wa Tanzania vijijini na mijini wanakaa madarasani, lakini pia wanakaa kwenye madawati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo, angalau kila mtoto atajua kwamba Serikali yake inamjali, atathamini sana elimu ambayo anapewa, lakini pia itamjengea uwezo. Leo tumekuwa tunapata kwenye taarifa zetu kwamba mtoto anamaliza shule hajui kusoma wala kuandika. Kwa sisi ambao tunatoka vijijini hushangai, kama mtoto anakaa chini ya mti, mvua inamnyeshea miaka miwili, mitatu, hajui kusoma…
MWENYEKITI: Mheshimiwa Sakaya muda wako tayari.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA:Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)