Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Maswa Mashariki
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. STANSALAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kwanza kabisa ya kuchangia katika hotuba hii ya Wizara hii ya Afya. Kabla sijachangia nichukue fursa hii kwanza kumpongeza Mwenyekiti wa Wabunge wa Afrika Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson, Spika wetu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jinsi alivyoaminiwa kuwa Mwenyekiti wa Wabunge wa Kanda ya Afrika kule IPU. Basi tumtakie kila la kheri katika safari yake ya kugombea Urais wa Bunge au moja ya Mabunge ya Duniani (IPU). (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa makofi haya Waheshimiwa Wabunge wote wanamuombea uende ukashinde uwe Rais wa wa Wabunge wote duniani, na Inshaalah Mwenyezi Mungu atakubariki na utakuwa Rais wa IPU. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpongeze sana Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan kwa kipaumbele chake cha kutoa fedha katika sekta ya afya, na kwa kweli tunaona uwekezaji mkubwa ambao anaufanya Rais wetu katika kuwekeza katika sekta hii ya afya na kupeleka huduma kwa wananchi, tunakushukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi hii kubwa unayoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kama Kamati ya Afya tumefanya kazi kubwa, tumechambua kwa kina, tumeangalia kuona ni namna gani Serikali inafanya kazi kwa niaba ya Bunge lako. Tunatambua maadui wakubwa, hatujawasahau; wa kwanza ni maradhi umaskini na ujinga hawa ndio maadui zetu wakubwa katika nchi yetu. Lakini si hivyo tu maadui hawa ni maadui wa Afrika nzima; maradhi ujinga na umaskini ndio maadui wetu wakubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, miaka ya nyuma viongozi wetu walikaa kule Abuja, walikaa chini wakatafakari wakasema kwamba kila nchi inapoandaa bajeti basi itengwe walau asilimia 15 ya bajeti ya nchi iende ikahudumie masuala ya afya. Mpaka sasa hivi tunavyozungumza tuna asilimia 2.8 tu ya bajeti yetu tunatenga kwa ajili ya huduma ya afya. Bado tuna kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha kwamba tunapeleka huduma za afya kwa Mtanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna mambo mengi ya kufanya, hakuana anayekataa, lakini mtaji wa kwanza ni afya yako. Kabla hujaenda kutafuta kitumbua au kwenda kutafuta chakula kwa ajili ya watoto wako ni lazima afya yako iwe imara. Ni lazima tuwe na mikakati ya pamoja kuhakikisha kwamba afya za Watanzania zinakuwa ni jambo la kipaumbele; kwa maana ya kwamba kila Mtanzania asiwe na wasiwasi pale anapopata shida ya maradhi yoyote basi aende akapate tiba, tiba ya uhakika na tiba ambayo ni ya hali ya juu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Afya yeye na timu yake, Naibu Waziri viongozi alionao katika Wizara ya Afya, Katibu Mkuu wataalamu wetu wakuu wote wa taasisi, hiki kidogo ambacho wanapewa wanakitendea haki kwa kufanya kazi kubwa kwa kuona ni namna gani tupeleke hiki mwanzo na hiki kiwe kipaumbele cha pili. Keki hii ndogo tunayoipata ya taifa wao wanalala hawalali wanapanga ni namna gani Watanzania wapate huduma bora za afya, hongera sana Mheshimiwa Waziri Ummy kwa kazi unayoifanya.
Nakupongeza wewe kwa sababu wakati mwingine umekuwa huogopi kuchukua maamuzi kwa ajili ya Watanzania. Kuna wakati tunakuwa kama hatumuelewi, lakini tuna kuelewa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu maradhi ni adui mkubwa ni lazima tuwe na mkakati wa kutenga fedha kwa ajili ya kuwahudumia wananchi. Majuzi tulikuja na mkakati wa kuwa na bima kwa watu wote. Serikali imefanya kazi kubwa kupitia mikataba ya kimataifa, kuna kitu kinaitwa Universal Health Coverage, kwamba kila nchi lazima ipeleke Huduma ya Afya kwa wananchi wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania imefanya kazi kubwa kupitia Serikali yetu. Tumejenga vituo vya afya tumejenga zahanati, hospitali za kanda na hospitali za rufaa. Tumefanya kazi kubwa na sasa hivi ninyi Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi, kwamba kila Mbunge katika eneo lake kuna vituo vimejengwa, kuna zahanati imejengwa, vituo vya afya vimejengwa na hospitali za wilaya zimejengwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni moja ya sehemu ya universal health coverage kwa sababu lazima tupeleke matibabu, lazima tupeleke huduma za kinga lazima tupeleke huduma za chanjo, pawe na parental care pawe na dedication; hizi zote zinaletwa. Changamoto kubwa iliyopo ni kwamba huduma imeshasogezwa kijijini huyu mwananchi anakwenda kulipia vipi huduma katika kituo ambacho ameletewa; na ndio maana tunapiga debe kwamba tuwe na universal health insurance kwamba kila mwananchi awe na bima ya afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hali iliyopo mfuko wa bima iliyopo ina-suffocate kwa upungufu wa fedha. Toto Afya Card Mheshimiwa Waziri juzi umeifuta, mimi nilishangaa, lakini tumekuja kukaa Waheshimiwa Wabunge kuona hali halisi hapakuwa na njia, njia iliyopo ni kutafua namna nyingine mbadala ya kuhakikisha watoto hawa wanapata huduma kwa kupitia huduma za bima; na bima iwe ni kuhakikisha kwamba watoto wanaingia katika package za wazazi na shule zetu zihakikishe kwamba watoto wote wawe na bima ya afya. Sasa, tunahakikisha kwa namna gani, lazima tuwe na ushirikiano kati ya wananchi wenyewe na Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi naishauri Serikali, kwa upande wa Serikali tuanzishe mfuko maalumu kwa ajili ya kuwahudumia wananchi kupitia bima zao. Tuna asilimia 28 ya Watanzania ni masikini, ni lazima Serikali iwahudumie kwa kuwapatia bima. Lakini Serikali inaingia gharama kubwa ya kuwasafirisha wananchi kwenda nje kwa ajili ya matibabu ya kibingwa. Kuna gharama nyingine kwa ajili ya ubingwa bobezi ndani ya nchi. Lakini bado tuneona hospitali zetu za mikoa na kanda zinatoa misamaha kwa wananchi zaidi ya bilioni 600 wanatoa msamaha kwa mwaka mmoja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lazima tuwe na mkakati wa kuhakikisha kwamba tunatoa fedha kwa ajili ya bima kwa wananchi. Suala jingine nataka kutoa ushauri, na kwenye Kamati yetu tumeeleza na Mheshimiwa aliyesoma amesoma vizuri; MSD amekuwa ni mtu anayepokea fedha kwenda kununua dawa. Tunaomba tuipatie MSD mtataji iliyoomba, inataka bilioni 592 kwa ajili ya kununua dawa. kuna kununua dawa kwenda kujenga maghala pamoja na kuanzisha viwanda vya dawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, wanahitaji bilioni 92 kwa ajili ya kuwawezesha watu binafsi kujenga viwanda ili waweze kuzalisha dawa kwa matumizi ya Watanzania; na si hivyo tu watazalisha dawa hadi kwenda kuuza nje ya nchi. Tunaomba na naomba sana, Wizara ya Fedha mnatusikia, wasikilizeni MSD. Msipo wasikiliza tatizo la upungufu wa dawa ambao tunauona kwa wananchi wetu litaendelea kujitokeza. Leo tunaona kabisa kwamba MSD anafika sehemu akisema leo apelike dawa atumie fedha zote anakuwa na upungufu wa zaidi ya bilini 133.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lazima tufanye jambo tuihakikishie kwamba MSD anapata mtaji aweze kufanya kazi zake ambazo amepangiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kusema, kwamba huduma za afya, Wizara ya Afya inafanya vizuri tunaona hospitali za kanda za mikoa zinafanya vizuri, kule chini kwenye hospitali za wilaya, zahanati na vituo vya afya bado tunaona kuna tatizo. Nadhani inafika wakati sasa, aliyeshikilia Sera ya Afya, Mheshimiwa Ummy unafanya kazi vizuri, ushikilie hivyohivyo kutoka hospitali za rufaa tukupe power ya kushikiria huduma hii ya afya mpaka kwenye zahanati na Vituo vya Afya uisimamie wewe ili…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Mwenyekiti, kengele ya pili hiyo.
MHE. STANSALAUS H. NYONGO: ...wananchi waweze kupata huduma bure bora na safi. Baada ya kusema hayo nami naunga mkono ahsante sana.