Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya

Hon. Dr. Christina Christopher Mnzava

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya

MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi na mimi kuweza kuchangia katika Wizara ya Afya. Kwanza nimshukuru sana Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa na uwekezaji mkubwa ambao ameufanya katika Wizara hii ya Afya kwa kujenga miundombinu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli usiopingika kwamba takriban Tanzania nzima, kila wilaya kuna kazi ambayo inaendelea kwa sasa hivi. Kama siyo jengo la OPD basi jengo la MD kama siyo wodi basi ni zahanati; yaani kila sehemu kuna kazi ambayo inaendelea. Kwa kweli nampongeza sana Mheshimiwa Rais, lakini nawapaongeza sana sana sana Wizara ya Afya chini ya Mama yetu Ummy Mwalimu pamoja Doctor Mollel nadhani Ummy pamoja na Mollel hawalali katika kuhakikisha kwamba Wizara ya Afya inasonga mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni shahidi watumishi wa Wizara ya Afya wanafanya kazi nzuri nzuri sana iliyotukuka; kwa nini nasema hivyo? Ukienda kwenye hospitali zetu kwa sasa, kwa mfano mimi nitatolea mfano wa Hospitali ya Benjamin Mkapa; wanafanya kazi nzuri wanahudumia vizuri, yaani wanatibu kwa weledi. Lakini tatizo liliopo kwa sisi Watanzania ambao hatuna bima ya afya ni changamoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nilikuwa si muumini sana wa ile bima kwa wote. Sasa hivi kutokana na gharama za matibabu, hasa kwa wagonjwa ambao wana matatizo makubwa kwa kweli bima kwa wote inahitajika. Usipokuwa na fedha ni ngumu sana mgonjwa wako akapata huduma inayostahili. Kweli atapokelewa na atahudumiwa, lakini kuna vipimo ambavyo vinahitajika kuna dawa ambazo zinahitajika, ni lazima uingie mfukoni.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa ninawaza je, yule mama wa kijijinim jem yule baba wa kijijini ambaye ni mkulima na hana kipato cha kutosha anapopata matatizo makubwa kwenye familia yake anafanya nini? Ninaomba sana suala la bima kwa wote mlilete mapema Bungeni ili tuweze kulijadili na kulipitisha kwa sababu ni Watanzania wengi ambao wanahitaji…

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

TAARIFA

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, nampa taarifa mzungumzaji kwamba suala la Bima ya Afya ni muhimu. Mimi kwa upande wa Ushetu wakulima wangu wote 800 walijiunga na ushirika wa afya, na wanasisitiza hili suala liletwe Bungeni lipitishwe haraka ili wakulima wa-enjoy na ushirika wa afya. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa taarifa hiyo.

MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea taarifa ya kaka yangu Cherehani, ni kweli tuna haja ya kuletewa huo mpango wa bima ya afya kwa wote kwa sababu ni Watanzania wengi sana ambao wanahitaji huduma ni Watanzania wengi sana ambao hawana uwezo wa kwenda hospitali na kulipia matibabu kwa pesa taslimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niishukuru tena Serikali kwa kutenga bajeti ya Wizara hii ya Afya na kuweza kuongeza bajeti kutoka bilioni 1.1 mwaka jana ya bajeti inayomalizika na mwaka huu wameweza kutengewa fedha bilioni 1.2 na kuendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli tuna haja sana ya kuipitisha Bajeti ya Wizara ya Afya, kwa sababu bila afya hatuwezi kukaa mahali hapa. Bila afya hatuwezi kufanya kitu chochote. Kwa hiyo afya ni msingi lakini kwenye taarifa ya Wizara ya Afya kuna upungufu mkubwa sana wa watumishi. Ukiangalia mahitaji ya watumishi katika zahanati zetu Tanzania nzima ni 100,646, waliopo ni 30,625 upungufu ni 70,000 sawa na asilimia 70, upungufu wa watumishi katika zahanati, lakini kwenye vituo vya afya mahitaji ni watumishi 68,204, waliopo ni 25,354, upungufu ni 42,850, sawa na asilimia 73. Kwenye hospitali za wilaya wanaohitajika ni 123,424, waliopo 29,409, upungufu ni asilimia 94,215, sawa na asilimia 76.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ina maana gani? Kama kuna upungufu mkubwa wa wafanyakazi kiuhalisia hata huduma hazitakuwa bora. Kwa sababu, kuna kiwango ambacho mtoa huduma za afya anatakiwa ahudumie, kuna viwango ambavyo vimewekwa na Wizara ya Afya. Sasa ukiangalia kwa upungufu huu wa asilimia 70, asilimia 63, asilimia 76 ni uhalisia kwamba watumishi hawa wanafanyakazi kupita kiasi na mtu anapofanyakazi kupita kiasi, matokeo yake atachoka, kwa sababu ni mwanadamu. Matokeo yake ataanza kutoa huduma ambayo sio bora, anaweza akaghafilika, ndio maana unakuta kuna sehemu zingine kuna watumishi ambao wanatoa lugha chafu, sio kwamba amedhamiria kutoa ile lugha chafu ni kwa sababu kazi zimemzidia amechoka, anajikuta anajibu kitu ambacho hakupanga kukijibu. Tunaiomba sana Serikali katika ajira ambazo zinatolewa na Serikali, waangalie sana sana sana Sekta ya Afya, kwa sababu ni sekta ambayo inahusu maisha ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Hospitali ya Wilaya ya Kahama, Hospitali ya Wilaya ya Kahama kwa siku inahudumia wagonjwa 450 mpaka 715 OPD na tuna watumishi 396. Pamoja na kwamba ni hospitali ya wilaya lakini inafanya kazi kama hospitali ya mkoa na tumekwenda mbali sana, Halmashauri ya Manispaa ya Kahama wameweza kujenga majengo kwa kutumia fedha za ndani. Wametumia bilioni za kutosha kujenga OPD, zaidi ya bilioni nne, wamejenga kwa fedha za ndani lakini haikutosha wamejenga jengo la uchunguzi wametumia zaidi ya milioni 803. Wamejenga Kituo cha Afya cha Kagongwa cha thamani ya milioni 800 kwa mapato ya ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba Serikali, halmashauri zinapokusanya mapato yake ya ndani zikajenga miundombinu ya afya, tunaomba kwa haraka mtupe support kuhakikisha kwamba vifaa tiba vinatolewa. Tuna jengo pale pale la uchunguzi lakini hatuna vifaa tiba, Serikali watusaidie tuweze kupata vifaa tiba ili wananchi wa Wilaya ya Kahama waweze kunufaika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Kahama haihudumii wakazi wa Kahama pekee yake inahudumia Geita, Kaliua, Urambo, Msalala, Nzega, inahudumia watu wanaopita kutoka Tanzania kwenda Burundi. Kwa maana hiyo basi, kwa sababu Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano alikwishatamka kwamba Hospitali ya Wilaya ya Kahama iwe na hadhi ya Hospitali ya Mkoa. Tunaomba Wizara ya Afya, huo mchakato ambao wamekwishauanza ukakamilike ili tuweze kupunguza uzito wa huduma ambayo wale wafanyakazi ambao wako katika ikama ya hospitali ya wilaya waweze kuwa katika ikama ya hospitali ya mkoa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli usiopingika Wizara ya Afya inafanya kazi kubwa sana…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante Dkt. Mnzava, kengele ya pili hiyo.

MHE. DKT. CHRISTINA P. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja, tunaomba watusikilize. (Makofi)