Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya

Hon. Hawa Mchafu Chakoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya

MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Ningependa kuanza kuwapongeza Dkt. Ummy na Dkt. Mollel kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya na nikope maneno yake kwamba Mawaziri hawa wako very loyal na very committed nawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa nianze kwa kumpongeza Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya. Rais Samia anaendelea kuboresha na kuimarisha Sekta hii ya Afya Nchini. Hivi tunavyozungumza tayari takribani bilioni 290 zimeshatumika kwa ajili ya kukarabati ama kuboresha hospitali za kanda, hospitali za mikoa na hospitali ya Taifa. Sambamba na hilo Mheshimiwa Rais Samia ameweza kusaidia kupunguza rufaa takribani kwa asilimia 97 za kwenda kutibwa nje ya nchi. Tunampongeza sana Dkt. Samia Suluhu Hassan. Pia tunaona nchi za jirani sasa ni zamu yao kuja Tanzania kufuata matibabu kama ambavyo zamani ilikuwa sisi tunatoka kwenda kufuata matibabu Kenya, India na nchi zingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, juzi nimeona Madaktari saba wa Tanzania wakienda Malawi kwa ajili ya kwenda kutoa tiba, lakini pia kufanya uchunguzi pamoja na ukaguzi kwa wagonjwa ambao kimsingi walitakiwa waje kutibiwa Tanzania. Madaktari wetu hawa wakaenda kuwatibia kule kule Malawi. Hongera sana kwa Mama yetu kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya kwa wananchi wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, nitapenda kumpongeza sana Waziri Ummy na timu yake kwa kuja na wazo la kufikiria sasa Hospitali ya Taifa ya Mirembe kuipandisha hadhi kuwa Taasisi ya Taifa ya Afya ya Akili. Napenda sana kuwapongeza kwa hili, kwani hapo awali hospitali hii ya Mirembe imepewa majina mengi ikiwemo hospitali ya vichaa, jambo ambalo mtu kama unahitaji huduma kwa hospitali ile inakuwa ni changamoto kwa namna vile ilivyokuwa ikiitwa. Kwa hiyo hongera sana kwa Wizara kwa namna ambavyo wameipandisha hadhi na kuweza kuiita Taasisi ya Taifa ya Afya ya Akili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi tunaambiwa karibu Watanzania wengi tunazo dalili za magonjwa ya afya ya akili, kucheka kupitiliza tunaambiwa ni dalili ya afya ya akili, kukasirika kupita kiasi, tunaambiwa hizi ni dalili za magonjwa ya afya ya akili, wivu uliokithiri na uliopitiliza tunaambiwa ni dalili ya magonjwa ya afya ya akili, lakini pia uwoga uliopitiliza, zote hizi tunaambiwa ni dalili za magonjwa ya afya ya akili. Kama hivyo ndivyo, mimi nitapenda kuuliza Serikali haya maswali yafuatayo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la kwanza, je, Serikali inaifahamu changamoto hii kwa ukubwa gani? Swali la pili ambalo ningependa Waziri Ummy aje atujibu sasa, je, Serikali wamejiandaa vipi sasa kukabiliana na tatizo hili, maana inaonekana karibia kila Mtanzania anayo dalili ya ugonjwa huu wa afya ya akili? Kwa hiyo ningependa kujua mipango na mikakati ambayo wamejipanga nayo na kama wana takwimu sahihi kabisa za wagonjwa hawa na hawa walionyesha dalili za magonjwa ya afya ya akili.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala langu la pili, lilikuwa ni kuhusiana na Toto Afya Card, kwa sababu ya muda ningependa Mheshimiwa Waziri achukue ushauri na maoni yaliyotolewa na Kamati hii ya Afya pamoja na Masuala ya UKIMWI, wamelichambua vizuri na wameshauri vyema. Kwa hiyo kwa kutunza muda ningependekeza wachukue ushauri huo uliotolewa na Kamati.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na MSD; amesema vizuri Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati hii. Niliwahi kuuliza swali hapa ama niliwahi kuchangia hapa kwamba MSD sasa hivi kazi yake imekuwa inachukua ama inapokea hela ya Kituo cha Afya Mlandizi, inaenda inanunua dawa ya kituo kingine. MSD inapokea hela za Hospitali ya Wilaya ya Kibiti inaenda inanua dawa za Hospitali za Wilaya ya Mkuranga. Kwa maana hiyo imekuwa inachukua hela huku inaenda inanunua dawa kule, wamesema kwamba tuwaongezee mtaji, ifike mahali wapewe mtaji ili waweze kufanya kazi iliyokusudiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la MSD ni Bohari ya Madawa, tunatakiwa tuwe na stoo ya madawa pindi zahanati, hospitali ya wilaya ama hospitali ya mkoa inapopeleka mapendekezo ama inapopeleka fedha kwa ajili ya kupatiwa dawa, basi dawa ziwepo stand by pamoja na vifaa tiba, lakini tusikuchue hela za dawa za huku na kwenda kununua dawa kule. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo nililokuwa nataka kulizungumzia ni kuhusiana na suala zima la bima ya afya kwa wote. Hili nilishalizungumza na leo narudia tena, Watanzania tumefika mahali tunahitaji bima ya afya kwa wote na hususan kwa upande wa magonjwa yasiyoambukiza. Magonjwa haya yamekuwa yanachukua kiasi kikubwa sana cha bajeti ya Serikali. Kwa hiyo muda umefika, kama suala tunaambiwa 360,000 kwa mwaka ni kubwa, basi tuiangalie tena na tena lakini kwa mwendo huu tunaoenda nao tutawapoteza Watanzania wengi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi, naunga mkono hoja. (Makofi)