Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya

Hon. Regina Ndege Qwaray

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya

MHE. REGINA N. QWARAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia katika bajeti hii ya Wizara ya Afya. Awali ya yote napenda kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyoendelea kuboresha sekta hii ya afya ili afya ya wananchi wetu iendelee kuimarika. Nasema haya kwa sababu tumeona ni jinsi gani Mheshimiwa Rais ameendelea kuboresha afya ya wananchi hata kwa kusogeza huduma katika makazi ya wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, siyo hilo tu, Mheshimiwa Rais ameongeza jitihada ya pekee kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata huduma hapa nchini badala ya kusafiri kwenda nje ya nchi kuendelea kupata huduma za afya. Kwa namna ya pekee nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Ummy na Naibu Waziri wake, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na Wizara kwa ujumla, kwani wamekuwa washauri wazuri kwa Rais, lakini wameendelea kumsaidia kufanya kazi kwa bidii, kumsaidia Rais ili afya ya wananchi iendelee kuimarika zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nisipotoa shukrani kwa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan nitakuwa sijatenda haki. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kutuletea CT-Scan katika Hospitali yetu ya Mkoa wa Manyara. Kabla hatujaletewa CT-Scan katika hospitali yetu, wagonjwa walikuwa wakihangaika kwenda Hospitali ya Benjamin Mkapa, KCMC na wakati mwingine walikuwa wanaenda Muhimbili, lakini hivi sasa huduma inatolewa pale mkoani, wananchi wetu wanapata huduma kwa ukaribu na pia imewapunguzia gharama ya kusafiri umbali mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kutujengea jengo la OPD. Bahati nzuri alikuja Rais mwenyewe akalizindua jengo lile na sasa hivi linafanya kazi vizuri. Pia namshukuru Mheshimiwa Rais kwa kutujengea jengo la Radiology, na jengo la ICU pamoja na damu salama. Hapa naomba sasa, majengo haya ya ICU na Damu Salama hayajakamilika. Namwomba Mheshimiwa Waziri atupelekee pesa pale Mkoani Manyara ili jengo hili liweze kukamilika na liweze kufanya kazi kama ilivyopangwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kutupatia jengo la wagonjwa wa dharura na tayari limeanza kufanya kazi, wagonjwa wanapata huduma. Pia hospitali yetu ya mkoa kulingana na wingi wa watu katika mkoa, hatuna watumishi, waliopo ni wachache sana. Tuna watumishi 250, tunahitaji watumishi wafike 468 ili hospitali hii iweze kutoa huduma vizuri. Tunaposema huduma ya afya inalegea, ni pamoja na kutokuwa na watumishi wa kutosha katika hospitali. Kwa hiyo, mkituongezea watumishi, tunaamini huduma itatolewa vizuri na wagonjwa wataendelea kupata huduma, itawapunguzia wagonjwa kwenda kutafuta wataalam katika hospitali nyingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, naombe Wizara ituletee daktari bingwa wa magonjwa ya watoto, daktari bingwa wa magonjwa ya mifupa, madaktari bingwa wa macho, daktari bingwa wa usingizi na daktari bingwa wa mionzi. Mheshimiwa Waziri aone ni namna gani tuna upungufu mkubwa kwa sababu hatuna madaktari bingwa katika hospitali yetu. Kwa hiyo, akitupatia hao madaktari, tutakuwa na uhakika kwamba wagonjwa wetu watapata huduma kwa ukaribu na huduma sahihi kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, pamoja na kwamba hospitali yetu imeanza toka 2008, tunaishukuru Serikali imeendelea kuleta fedha siku hadi siku. Kila mwaka katika bajeti ya Serikali tumeendelea kuletewa fedha. Naomba, kuna upungufu mkubwa wa wodi. Hatuna wodi ya wanawake, wodi ya wanaume na wodi ya watoto. Ukiwa huna wodi hizo, moja kwa moja ujue kwamba hospitali yetu haijakamilika bado. Kwa hiyo, naiomba Serikali ituletee fedha kwa ajili ya kukamilisha au kujenga hizo wodi ili wagonjwa waweze kuhudumiwa pale na waweze kupata huduma ya malazi kama wagonjwa ambao wanatakiwa kulazwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, naomba gari kwa ajili ya uendeshaji katika hospitali yetu ya mkoa. Ili kuendelea kutoa huduma hizi katika maeneo mengine, basi ni vyema hospitali ikapata huduma hizi ili huduma za afya zitolewe kwa ukamilifu zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusemea hospitali yangu ya mkoa, niende moja kwa moja kwenye changamoto ambayo naiona siyo kwa mkoa wangu tu, bali katika maeneo mengi; suala zima la vifaa. Utakuta katika maeneo mengi vifaa tiba au vifaa vile vya vipimo vinaharibika, lakini vinachukua muda mrefu kutengenezwa. Mfano, unapoongelea X-Ray, inaharibika, na CT-Scan inaharibika, lakini haitengezwi. Wagonjwa wanaenda hospitalini hawapati huduma, hawapati vipimo kila akienda anaambiwa kifaa kimeharibika, anaenda wiki inayofuata, kifaa kimeharibika. Kwa hiyo, hii imeleta usumbufu katika maeneo mengi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe tu mifano hai. Kwa mfano, tuna hospitali yetu hapa ya afya ya akili ya Mirembe. Tunapozungumzia hospitali ya magonjwa ya akili, moja kwa moja kifaa kinachoitwa EEG ni kifaa muhimu sana katika hospitali, lakini jambo la kushangaza ni miezi karibia sita tunaelekea miezi saba hospitali ile haina kipimo hicho cha EEG. Sasa hebu fikiria, mgonjwa anatoka mkoani, analetwa hospitali, hapati kipimo, anatibiwaje? Zaidi tumesema ni hospitali special kwa ajili ya magonjwa ya akili. Kwa hiyo naombe Serikali iliangalie hili, kwa sababu tusipoliangalia wagonjwa watalundikwa pale hospitalini, hawapati matibabu na hawapati vipimo sahihi. Kwa hiyo, madaktari watapima kulingana na maelezo, badala ya kupima na kujua tatizo hasa ni nini? Kwa hiyo, naomba sana, vifaa tiba vinapoharibika, ni lazima Serikali ichukue jukumu la haraka sana ili vifaa vile vitengenezwe kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto kubwa tunayoiona ni kwamba, vifaa vile vinashindwa kutengenezwa kwa sababu hatuna wataalam wa kutengeneza vile vifaa katika vituo hivyo. Kwa hiyo, niombe wizara ijipange ni namna gani kuhakikisha wakipeleka vifaa tiba, pale pale kuwe na mtaalam wa kutengeneza vile vifaa pindi vinavyoharibika. Wapo vijana wetu waliomaliza vyuo wamemaliza mafunzo DIT wamekaa mtaani. Serikali kwa nini isiwatumie wale vijana wakawepo kwenye vituo au hospitali zetu za referral ili kifaa kinapoharibika tu, iwe rahisi kutengenezwa na huduma kuendelea kutolewa kwa wakati? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, kuna changamoto ya ukosefu wa madawa. Pamoja na kwamba Rais amefanya kazi kubwa sana kujenga vituo vingi vya afya, lakini bado madawa kule ni changamoto, hasa maeneo ya vijijini. Kwa hiyo, naomba Wizara ilichukue hili kuhakikisha kwamba wagonjwa wanapoenda katika vituo vyetu vya afya wanapata madawa muhimu yale ya binadamu ili watu wasipate tena usumbufu mwingi wa kutembea hapa na pale.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine nilizungumzie na nilishawahi kulizungumzia hapa Bungeni, ni suala zima la Sera ya Huduma Afya ya Mama na Mtoto. Wamama wajawazito bado wanapata changamoto wanapoenda kujifungua, kwa sababu mama anatakiwa abebe vifaa yenye mwenyewe kama gloves, pamba na vitu vingine ambavyo vinahitajika wakati wa kujifungua. katika vituo vyetu vya afya na maeneo mengine, hasa katika jamii zetu za kifugaji na umbali wa kwenda hospitali inawalazimu wale wamama kujinyima baadhi ya vyakula ili mtoto awe mdogo tumboni ili aweze kujifungulia nyumbani badala ya kwenda hospitali. Sasa matokeo yake watajifungua watoto ambao hawana afya na ambao hawajatimiza umri kwa kuwa amekosa virutubisho. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, haya yanachangiwa na gharama za hospitali. Hizi gharama kuna familia nyingine hawaziwezi kabisa. Kwa hiyo, naomba sera ya afya ikasimamiwe. Sera ya afya ni kwamba mama anapoenda kujifungua, basi apate zile huduma.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukija kwa mtoto mdogo wa umri chini ya miaka mitano, naomba sasa Wizara pia iliangalie hili, kwa sababu wapo watoto wadogo ambao familia zao ni duni pia, wanashindwa kugharamikia matibabu. Kwa hiyo, Serikali ione ni namna gani ya kuendelea kuwahudumia wale watoto kwa kuwapatia huduma ya afya ili waweze kuishi kama binadamu wengine ambavyo tunaishi kwa sasa. Kwa hiyo, naomba sana Wizara iweze kusimamia sera hii ili Watanzania waendelee kupata huduma hii na afya ya wananchi wetu iendelee kuimarika.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)