Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya

Hon. Mussa Ramadhani Sima

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya

MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema. Pia nampongeze Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa aliyoifanya. Sisi Wana-Singida Mjini tumekuwa na kero kubwa ya hospitali ya wilaya, sasa tumepatiwa hospitali ya wilaya. Tunamshukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na timu nzima ya Wizara ya Afya, walikuwa tayari kutuachia majengo ya hospitali ya mkoa ili yaweze kuwa hospitali ya wilaya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba mchango wangu nianze kwa rejea ya Mwanafalsafa nguli na mpigania uhuru wa India, Mahatma Gandhi. Aliwahi kusema “it is health that is real wealth and not pieces of gold or silver.” Alimanisha nini? Kwa tafsiri isiyo rasmi, afya ndiyo utajiri halisia kuliko kuwa na vipande vya dhahabu ama fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mahatma Gandhi alikuwa anamaanisha nini hapa? Unaweza kuwa na kila kitu; na Serikali leo tumewekeza miundombinu ya kutosha kwenye elimu, kwenye afya, na maeneo yote tumewekeza na tumeweka fedha nyingi, lakini tunawahitaji Watanzania wenye afya bora ili waweze kutumia hiyo miundombinu iliyopo hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa rejea hii ya Mahatma Gandhi, nataka niangalie maeneo mawili. Moja ni la Mfuko wa Bima ya Afya. Mfuko wa Bima ya Afya siyo siyo taasisi ya kibiashara (business entity), mfuko huu unatoa huduma, na kama unatoa huduma, nilitarajia kuiona Serikali inauwekea ruzuku ili uweze kufanya kazi yake vizuri. Leo Watanzania wengi wanasubiri Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote. Ukiwa na bima, maana yake una security ya kuweza kupata huduma ya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nitoe mifano michache. Kwenye Toto Afya Kadi kwenye taarifa ya Bajeti ya Mheshimiwa Waziri hapa, imeeleza vizuri kwamba katika katika watoto 205,000 waliosajiliwa, wamechangia shilingi bilioni 5.99, wametumia, shilingi bilioni 40. Mfuko huu unaenda kufa. Pia wamesema hapa kwamba kuna huduma za vipimo zinatolewa. Huduma hizi zimekuwa ni za gharama kubwa, hakuna Mtanzania anayeweza ku-afford. Anayeumia kwenye hizi huduma, mfuko ndiyo unaenda kuumia kwa sababu ndiyo utakaolipa fidia au utakaolipa hiyo fedha ambayo mtu anahudumiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hatuwezi kuchukua vipimo vya India labda shilingi milioni 30, sisi tukaweka Shilingi milioni 15, badala kuangalia uhalisia wa mazingira yetu ili tuweke kiwango ambacho kitamsaidia Mtanzania kupata huduma, na kitausaidia pia huu mfuko uweze kulipwa kwa gharama ambayo inaendana na mazingira yetu tuliojiwekea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine muhimu sana ni eneo la dawa. Taarifa ya Kamati imesema vizuri hapa kuhusu MSD kwamba wanapaswa kuwekewa fedha ama kukopeshwa fedha zaidi ya shilingi bilioni 500, nakubaliana nao; lakini jambo hapa la kuangalia, kama kuanzia bajeti ya mwaka 2021 tulitenga shilingi bilioni 200, mwaka 2022 shilingi bilioni 200, mwaka huu shilingi bilioni 205, projection ya
kutenga hizi fedha za dawa tunaipata wapi? Maoteo ya dawa tunayatoa wapi?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye zahanati zetu huku chini, mtu anayeuza dawa ni medical attendant. Ni mhudumu aliyeajiriwa kwa ajili ya kupanga ma-file labda kufanya usafi, ndiyo anayetufanyia kazi hii. Nataka nitumie fursa hii kuwapongeza sana medical attendants wote, wamefanya kazi kubwa, na wamelibeba Taifa hili, lakini huyu hana taaluma, hawezi kufanya inventory, hawezi kutupa data halisi za mahitaji ya dawa. Huyu mhudumu anasimamiwa na DMO.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inapaswa kuajiri wafamasia na wafamasia wasaidizi huku chini ili tupate data halisi, tunataka dawa za kiwango gani na dawa gani? Kama leo unatenga shilingi bilioni 200, mahitaji yetu inawezekana ni shilingi bilioni 400. Sasa kama ni shilingi bilioni 400, ceiling inatuambia shilingi bilioni 200, kwa nini Serikali kila mwaka tunaweka shilingi bilioni 200? Tuweke walau shilingi bilioni 300 ili matatizo ya uhaba wa dawa yasiwepo tena. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo hili lina changamoto moja kubwa sana ambayo mimi nadhani mara nyingi nimekuwa nikizungumza, na nilizungumza wakati wa Wizara ya TAMISEMI, wasimamizi wakuu wa eneo hili ni Wizara ya TAMISEMI. Msemaji wa sekta ya afya ni Wizara ya Afya. Unafanya projection ya dawa kutoka huku chini, unaenda kumkabishi Wizara ya Afya ili aweze kuleta dawa. Hapo kuna changamoto. Kama upungufu unaendelea, maana yake hapa kuna changamoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto hii kuiondoa ni nyepesi sana. Tunaye CMO, Mganga Mkuu wa Serikali; huku chini kuna RMO, kuna DMO. Hawa watu wawili; RMO na DMO, wako chini ya TAMISEMI. CMO akitoka kule, lazima aripoti kwa Katibu Tawala wa Mkoa, amekuja na jambo gani? Apokelewe, maana yake atapokea taarifa ambayo wao wameiandaa. Taarifa hii inaweza isiwe halisi, naye hawezi kujiridhisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kushauri hapa, naiomba Serikali, DMO hawa ni wataalam; RMO, huyu ni mtaalam, hawa sio watawala. Kazi wanazozifanya kule ni za kiutawala zaidi badala ya kufanya kazi za kiutaalam, kwa sababu wao wako chini ya Wizara ya TAMISEMI. Kama tunataka kweli kujali afya za Watanzania na tuondokane na upungufu huu ninaoueleza, maana yake RMO, DMO wawe chini ya Wizara ya Afya. Wakiwa chini ya Wizara ya Afya, watatusaidia sisi kwenye projection yoyote ya dawa na vitu vingine vyote kwenye tiba. Hapa kuna changamoto kubwa sana. Tukishindwa kufanya hivi, basi tutachoweza kufanya CMO aanzishe ofisi zake kwenye mkoa ili awe na authority ya kuweza kusimamia eneo la tiba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe mfano mwingine mzuri sana. Walifanya vizuri Mheshimiwa Mzee Lukuvi hapa na dada yangu Mheshimiwa Angeline Mabula kwenye Wizara ya Ardhi walipoamua kuwapeleka Makamishna wasaidizi kwenye kila mkoa. Tumepunguza tatizo kubwa la migogoro ya ardhi, na kila mkoa leo unao Kamishna Msaidizi. Bado hata CAG tunayemtuma sisi, kule ukienda kuna National Audit Office, ziko kule. Kwa nini CAG hajafanya kazi na internal auditor? Kwa sababu internal auditor mwajiri wake anayemsimia ni Mkurugenzi, hawezi kupata data halisi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama huku tumeweza kufanya hivi, kwa nini kwenye afya tusiweze kufanya? Kama coordination hii imeshindikana kutupatia taarifa halisi, basi ni vyema tukahakikisha kwamba Mganga Mkuu wa Serikali naye aanzishe ofisi zake kwenye mkoa. Huko kwenye mikoa, anaweza akasimamia vizuri eneo hili la afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumzia afya ya Watanzania, tunazungumzia jambo la muhimu na jambo la msingi sana. Fedha inayotengwa kwa ajili ya uendeshaji wa Wizara hii, haitoshi; na kwa kuwa haitoshi, haiwezi kutekeleza majukumu yake kwa pamoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tuna hospitali ya wilaya sasa, tumepewa na wenzetu wa Wizara ya Afya. Kwa kweli tunawashukuru sana.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Kengele ya pili hiyo Mheshimiwa.

MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie kidogo kwa sababu ni mchangiaji wa mwisho na Mungu atakubariki sana, kwa kuwa najua kazi hii umeifanya vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunahitaji fedha za ukarabati wa jengo la hospitali ya wilaya Shilingi bilioni moja, na pia tunahitaji fedha nyingine kwa ajili ya kuweka miundombinu mingine yote.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuitakie pia Yanga tarehe 17 waweze kufuzu wacheze vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)