Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya

Hon. Taska Restituta Mbogo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja ya Wizara ya Afya kwanza kabisa napenda kupongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi yake nzuri anayoijali kwa kujali Afya ya Watanzania. Mama mjali afya ya Tanzania hiki hakina ubishi kila mtu ameona nchini Tanzania jinsi gani Mheshimiwa Rais alivyoweka pesa nyingi kuhakikisha kwamba Watanzania wanakuwa na afya njema. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Afya, Mheshimiwa Ummy Mwalimu na Naibu wake Mheshimiwa Dkt. Molel wote kwa pamoja wanafanya kazi nzuri sana kuhakikisha kwamba Watanzania wanakuwa na afya nzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwakumbushe Watanzania kazi ambazo Mheshimiwa Rais amezifanya kwenye Wizara ya Afya. Mheshimiwa Rais amehakikisha kwamba Nchini Tanzania kumejengwa zahanati 1,066 kila sehemu katika kipindi cha miaka miwili Mheshimiwa Rais huyu amehakikisha kuna vituo vya afya vimejengwa 234 kwa kipindi tu hiki cha miaka miwili. Mheshimiwa Rais huyu amehakikisha kuna majengo ya ICU yamejengwa takribani 28 nchini Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais huyu amehakikisha kwamba kuna majengo ya dharula maana yake kuna magonjwa yale dharula yamejengwa takribani majengo 80 nchini Tanzania. Huyu Rais anayejali afya za watanzania, huyu Rais anaejali kizazi kinachokuja kwa sababu anataka watanzania wawe na afya njema ili waweze kufanya kazi vizuri na waweze kuendeleza nchi yetu ya Tanzania pongezi ngingi sana kwa Mheshimiwa Rais makofi kwake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, siyo hayo tu leo asubuhi Mheshimiwa Waziri wakati anawasilisha taarifa yake amekuja hapa na madaktari ambao watapita kwenye hospitali zetu kwenda kuwafundisha wale madakta kwenye kila wilaya hili ni jambo ambalo linatendeka kwa mara ya kwanza nchini kwetu Tanzania. Kwa hiyo, nakupongeza sana Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wako ni jambo jema wale watakapopita watakwenda kuboresha afya za watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nipongeze pia kwa jinsi hospitali yetu ya Benjamini Mkapa inavyofanyakazi wagonjwa wengi wanakuja pale wanatibiwa. Pia kwa lile jambo ambalo Mheshimiwa Ummy alituelezea hapa kuhusu kuweza kuwashughulikia wagonjwa wa Selemundo hilo ni tatizo kwa watanzania wengi. Watanzania wengi wanaumwa huu ugonjwa wa sickle cell na watoto wengi wameweza kupoteza maisha kwa ajili ya ugonjwa huu. Kwa hiyo, kuwepo kwa tiba hii nawapongeza sana sana Wizara ya Afya pamoja na watendaji wenu, lakini tunampongeza Mheshimiwa Rais kwa kuweza kuyatekeleza yote haya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona jinsi gani wilaya na mikoa zimepewa ambulance, hili halina ubishi. Katika kipindi cha miaka miwili ambulance nyingi zimepelekwa kwenye hospitali zetu, hata kwenye Mkoa wangu wa Katavi, ambulance zilipelekwa. Ninapenda kushukuru sana kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Katavi kwa ajili ya ambulance hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na pongezi hizi ninayo machache ya kuzungumzia kuhusu Mkoa wangu wa Katavi. Kwenye Mkoa wangu wa Katavi tunayo matatizo ya upungufu wa madaktari takribani 17 (MD). Tuna upungufu wa wauguzi 33, pia tuna upungufu wa wataalamu wa maabara takribani 13, tuna upungufu wa wataalamu wa meno. Vilevile tuna upungufu wa wataalamu wa dawa za usingizi. Katika hospitali zetu za wilaya pale tuna upungufu wa vifaa tiba ambavyo vinatakiwa viwepo pale kwenye hospitali yetu ya wilaya. Tuna upungufu mpaka wa vitanda na magodoro.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona niliseme hapa ili muweze kusaidia pale tuweze kupata magodoro pamoja na vitanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, Hospitali ya Mkoa wa Katavi ina madaktari bingwa sita tu, ambapo tuna matatizo katika magonjwa mengine kwenye Mkoa wetu wa Katavi; na mgonjwa anapokuwa na hilo tatizo inabidi apelekwe kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mbeya ambayo ni mbali. Kwa sababu kutoka Mkoani kwangu Katavi mpaka kufika Mbeya kule pana umbali. Kwa hiyo kama inapotokea kuna mgonjwa wa figo anatakiwa kuchujwa damu inabidi apelekwe Mbeya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naomba tuweze kupatiwa hivyo vifaa. Lakini kwenye Mkoa wangu pia wa Katavi tunayo matatizo ya Madaktari Bingwa. Mgonjwa anapoumia, kwa mfano anapovunjika mkono inabidi aende rufaa kama nilivyosema Mbeya au apelekwe Bugando. Lakini tatizo ambalo nimeliona kwenye Mkoa wangu wa Katavi kuna tatizo la kuchangia mafuta kwenye ambulance, lakini

kuna tatizo pia la kuchangia fedha ya yule nesi anayemsindikiza mgonjwa. Pia kunakuwa pia na tatizo la kumchangia pesa ya kujikimu…

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

TAARIFA

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kumuongezea taarifa mama yangu Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalumu kutoka kule Katavi. Jambo hili la kuwataka wagonjwa wachangie mafuta kwenye ambulance lipo pia na kwenye Mkoa wetu wa Songwe hususan kwenye Jimbo la Momba. Watu wakiumwa wanataka wachangie mafuta kwenye ambulance, sasa, watu wa vijijini wanapata wapi hela ya kuweka mafuta kwenye ambulance zaidi ya lita 50? Mheshimiwa Waziri jambo hili anapaswa kulitambua kwenye ngazi za zahanati na vituo vya afya.

NAIBU SPIKA: Taarifa hiyo unampa aliyezungumza.

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Nampa taarifa mama yangu wakati yeye anamwambia Mheshimiwa Waziri…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Taska.

MHE. TASKA R MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaipokea taarifa hiyo kwa sababu ndilo suala ambalo nilikuwa ninalizungumzia hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ukiangalia ule umbali wa kutoka pale kwetu Katavi mpaka kufika kule Mbeya kwenye hospitali ya rufaa unamwambia mgonjwa aweke mafuta hiyo ambulance. Kuna familia moja kule kwetu mkoani Katavi ilibidi wauze nyumba ili waweze kumpeleka hiyo mgonjwa kule rufaa Mbeya; lakini wameenda kule wameuza bill kubwa lakini pia mgonjwa yule alifariki.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nilikuwa ninaomba ufafanuzi; zile ambulance ni nani anatakiwa aweke mafuta kwenye ile ambulance? Lakini pia yule nesi anakuwa yuko kazini, dereva anakuwa yuko kazini kwa sababu anaendesha ile ambulance ambayo ni ya hospitali, sasa inakuwaje anatakiwa alipwe posho zake na mtu ambaye anamuuguza mgonjwa wake? Mheshimiwa Waziri Ummy na Naibu wako najua nyinyi ni wachapakazi wazuri ninaamini kwamba suala hili mmelisikia na mtalishughulikia kwa sababu linafanya mpaka wagonjwa wengine kutoka kwenye ule Mkoa wangu wa Katavi washindwe kwenda kwenye hospitali za rufaa kwa sababu wanakuwa hawana ule uwezo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema, tuna mapungufu ya madaktari bingwa, wagonjwa wa ndani, watoto, macho wagonjwa wa akili, mionzi pamoja na mapungufu ya vifaa tiba ni suala ambalo linaukabili Mkoa wetu wa Katavi kwenye vituo vya afya pamoja na zahanati…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana kwa mchango mzuri.

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru naunga mkono hoja.