Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya

Hon. Neema Gerald Mwandabila

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi jioni hii ili niweze kuchangia katika Wizara yetu hii muhimu sana ya Afya. Nitumie nafasi hii pia kuipongeza Serikali yangu, Serikali ya Chama cha Mapinduzi, Serikali inayoongozwa na mama yetu mpendwa, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, chini ya dada yetu Ummy pamoja na Mheshimiwa Mollel. Mimi binafsi niseme nina imani kubwa na hawa mawaziri wetu kwa namna ambavyo wamekuwa wakiendelea kutupa ushirikiano.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba nawapongeza kwa namna ambavyo nimeweza kuona wameelezea suala la lishe vizuri kwenye taarifa yao. Hii inaonesha kwamba Wizara kama hii wanaona umuhimu wa suala la lishe kwa nchi hii na kuangalia ni namna gani wanakwenda kuisaidia nchi kuweza kuondokana na changamoto za matatizo ya lishe yanayokuwa yanaendelea nchini. Kwa hiyo ninampongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yake kwa kuiona lishe kama ni kitu cha msingi. Nimependa zaidi sana pale walipoweza kuelezea kwamba wataanzisha viwanda vya utengenezaji wa vyakula dawa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, ilikuwa ni ajabu lakini iliyokweli kuona kwamba Tanzania tunaozalisha karanga, tuna maziwa mengi ya kutosha eti tunaenda kuagiza plant peanut, maziwa F100 na F75 kuitoka Ufaransa; kweli ilikuwa ni ajabu; lakini naona wameliona hilo na wanakwenda kulifanyia kazi. Na ninaamini hili litaweza kuleta ajira kwa wananchi wetu wa Tanzania kwa sababu karanga ni zetu na maziwa ni ya kwetu. Ninashukuru sana kwa hilo kwa Mheshimiwa Waziri kuweza kuliona.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nilikuwa na mambo machache, ninadhani yanaweza kuleta tija kwenye Serikali yetu. Wameendelea kutujengea miundombinu mingi sana. Sisi kama Watanzania hususani kutoka Mkoa wa Songwe tunawashukuru na tunajivunia sana yale majengo mazuri ambayo mmeweza kutujengea katika nchi yetu. Tunawashukuru. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia wameendela kutoa vifaa tiba vya kisasa vizuri na vingi sana. Kwa hiyo, na hili tunawapongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja yangu inakuja wapi? Hoja yangu inakuja, ni kwamba majengo na wataalamu waliopo kwenye majengo unakuta haviendani. Haviendani kwa ubora na wala haviendani kwa idadi ya watumishi wanaotakiwa kwenye yale majengo. Kwa hiyo nilikuwa natamani Mheshimiwa Waziri atakapokuja ku wind-up mwishoni atusaidie kutueleza kwamba, ana mpango gani angalau wa kufanya reshuffling ya kupeleka wataalamu waliobora kutoka kwenye hospitali zile kongwe ambazo zina wataalamu wazuri Kwenda kwenye hizo hospitali za rufaa mpya ambazo zimeanzishwa, ili majengo na wataalamu watoe huduma iliyobora?

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia kitu kingine ni kwamba wametusaidia sana kuleta vifaa vingi sana; na nimshukuru Naibu Waziri Mheshimiwa Mollel, mwaka jana mwezi wa pili alitupatia x-ray katika Wilaya ya Ileje. Lakini nitoe tu masikitiko yangu leo hii hapa kwamba x-ray ile katika Wilaya ya Ileje mpaka leo haifanyi kazi. Nashindwa kuelewa kwamba Serikali kweli Serikali hii inayopambana kutoa fedha nyingi kwa ajili ya vifaa tiba inashindwa kufanya ufuatiliaji na kuhakikisha mitambo hii iweze kufanya kazi kwa wakati? Ile dhamira ya mimi kupambana kuomba x-ray mashine katika Wilaya ya Ileje haijaweza kufanikiwa kwa mwaka mzima.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo unaweza ukaona kwamba kuna wataalamu kule chini ambao wapo na wanafanya kazi na supervision wanafanya, na hiyo supervision wanazozifanya ipo haja ya wale wataalamu huko chini waangalie kwamba supervision zao zinakuwa zina tija gani? Kwa sababu kama x-ray imekuja mwaka jana mwezi wa pili mpaka leo haifanyi kazi; yaani unashindwa kupata picha kwamba wale wataalamu walioko kule chini ina maana hawaoni shida yetu sisi kama Watanzania kwenye eneo lile kwamba tunahitaji x-ray? Na kila siku wanakwenda wanachukua posho za hizo supervision na x-ray bado haifanyi kazi?

Mheshimiwa Naibu Spika, hili tatizo si kwa Ileje tu, Ileje is just a sample, lakini nchi nzima yaani kuna maeneo mbalimbali ambayo vifaa vizuri vinapelekwa vya kisasa lakini havifanyi kazi kwa wakati. Lakini pia vifaa hivi vinavyokuwa vinaletwa wataalamu wale wahandisi wa vifaa tiba tunao wanagapi wa kutosha kuweza kutengeneza? Je, hawa wataalamu wa kuweza ku–operate hivi vifaa kama nchi tumetengeneza mkakakti gani wa kuwa na wataalamu ambao wataweza ku–operate hivi vifaa?

Mheshimiwa Naibu Spika,unashangaa x-ray imeletwa unaambiwa mtu wa radiology hayupo. Kifaa kimeletwa unaambiwa mtu wa anesthesia hayupo. Sasa you can imagine; mipango ya ununuzi wa vifaa unaokuwa unaendelea nchini na utengenezaji wa wataalamu ambao wataenda kusaidia vifaa hivyo kufanya kazi hauendi sambamba. Kwa hiyo nimuombe Mheshimiwa Waziri kupitia bajeti hii aje na mkakati ambao utaonesha uwiano wa ununuzi wa vifaa vya kisasa unaoendelea lakini na wale operators, wataalamu ambao wameandaliwa kwa ajili ya ununuzi wa hivyo vifaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kitu kingine, nilitamani kuongelea suala la misamaha. Tumeona hapa, alikuwa naelezea Mheshimiwa Alice kwamba kuna burden kubwa ya utoaji wa misamaha kwenye nchi yetu. Kiukweli ukienda kufanya assessment, critical assessment misamaha mingi unaweza ukakuta ni fake. Yaani watu wanajitengenezea utaratibu wao wa kujipatia kipato ambacho wanaikosesha Serikali mapato, anapata yeye mfukoni kidogo anaandika misamaha isiyokuwa na tija. Kwa hiyo mimi niombe tu Mheshimiwa Waziri awe na uataratibu wa kufanya analysis nzuri ya misamaha iliyotolewa, ukiacha ile ambayo wana mpango wa kuitoa ili tuende sawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu sawa tunatoa huduma za afya na watanzania wengi wazee wanakosa huduma kule kisa tu waliopewa misamaha mikubwa ni wengi. Kwa hiyo mimi niombe tu Mheshimiwa Waziri kwenye hili tusaidie, tusaidie sana Dada yetu Ummy kuhakikisha misamaha iwe ile ya kweli, kwa sababu tunaona burden iko kwenye NHIF, bima yetu ya afya inaelemewa lakini ukienda kufanya assessment unakuta na kwenyewe kuna utaratiubu ambao si mzuri ambao unafanyika wa watu kuwahudumia watu ambao hata hawako registered na bima, mtu anajipatia chochote kwenye mfuko wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nimuombe tu Mheshimiwa Waziri, sisi tunapenda kazi yake anayioifanya, lakini suala la bima ni lazima atusaidie, suala la misamaha ni lazima atusaidie, kwa sababu haiwezekaniki bima mpaka leo eti tunakuwa tunaongelea bima kushindwa kuwahudumia wateja kwamba inaweza ika-collapse au ikafanya nini, wakati tuna uhakika waliojiandikisha na bima si wengi kiwango hicho.

Mheshimiwa Naibu spika, baada ya kusema hayo, I am sorry. Kuna suala la Tuduma. Tunduma iko mpakani, mpaka ule you can imagine tunapokea tu simu kila siku eti X-Ray hawana, Tunduma Mpakani, tena ni Halmashauri ya Mji ambayo sasa hivi mmetujengea Hospital nzuri haina X-Ray mpaka sasa hivi. Kwa hiyo nikuombe Waziri suala la Tunduma lichukulie kama emergency na ukatusaidie tuweze kupata X- Ray eneo lile.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Baada ya kusea hayo naunga mkono hoja, nakushukuru sana.