Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya

Hon. Festo Richard Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makete

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza kabisa niseme naunga mkono hoja, na nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake ambayo ameitoa leo; ni hotuba ya matumaini. Hata uteuzi wake alipokuwa anateuliwa kwenda Wizara ya Afya watumishi walitabasamu sana wakijua wamepata mtu ambaye walifanya naye kazi lakini kipindi chote amekuwa akionesha uwezo alionao wa hali ya juu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, cha kwanza, niseme wazi, kwa Watanzania wafahamu jambo moja, kwamba Mheshimiwa Rais kwenye Wizara ya Afya amefanya vitu vingi sana ambavyo havikuwepo kwa muda wa miaka mingi sana tangu nchi yetu ilipopata uhuru. Naenda tu kwa takwimu, kwamba, tulikuwa na Mheshimiwa Rais kwa kipindi chake tu kifupi ameongeza MRI sita ambazo hazikuwepo nchini, lakini Mheshimiwa Rais ameongeza CT-Scan 32, ambazo hazikuwepo kabisa nchini. Lakini wakati huo tayari sasa hivi ameshaanza kununua gari za ambulance 727, na tayari gari hizo zimeshaanza kuwasili nchini. Hii yote ni jitihada za Mheshimiwa Rais kwa ajili ya kuhakikisha kwamba sekta ya afya na Wizara ya Afya inaweza kutimiza malengo yake na inaweza kutimiza majukumu yake kama ambavyo Watanzania wamekuwa wakitegemea; ukiachana na ujenzi wa miundombinu kwa maana vituo vya afya na hospitali za mikoa. Mheshimiwa Rais kwa kweli anastahili kila heshima ambayo inatakiwa sisi kama Tanzania tumpe.

Mheshimiwa Naibu Spika, kati ya jambo kubwa kwenye taifa lolote lile ni suala la afya. Mtaji wa kwanza wa mwanadamu ni afya, si suala la fedha, si suala la nini, ni afya.

Unapoimarisha miundombinu ya afya kwenye taifa lolote umepigania maslahi ya taifa kwa kiwango kikubwa sana. Kwa hiyo mimi nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa sababu hata ukisoma takwimu na idadi ya vifo vya mama na mtoto vimepungua kwa kiwango kikubwa sana. Kwa hiyo tunampongeza Mheshimiwa Rais kwa haya yote ambayo anayafanya; na hata ununuzi wa digital x-ray ameshanunua digital x-ray 199 na hata Wilaya ya Makete tumepata digital x-ray ambayo kitu ambacho sisi Makete hatukuwahi kukitegemea kuwa na digital x-ray tungeweza kupata pale Makete.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pili, tumeona emergency ya hizi block, kwa maana EMD tayari hata Makete pia zimeshajengwa. Kwa hiyo, kwa niaba ya wananchi wa Makete, Mheshimiwa Waziri tunawashukuru sana kwa jinsi ambavyo mnafanya kazi, tunashukuru sana kwa maana ya kwamba Wakurugenzi na Wataalamu wa Wizara ya Afya, kwa kweli sisi kama Wabunge na mimi Mbunge wa Makete wanatupa ushirikiano.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo moja ambalo naliomba kwa ajili ya Makete, na wananchi wa Makete wanatusikiliza; ni suala la usambazaji wa dawa na vifaa tiba nchini. Hili ni lazima tuliangalie kwa ukaribu sana. Kwa mfano, mimi nina vituo vya afya takribani vinne vimekamilika, Kituo cha Afya Bulongwa, Kituo cha Afya Kitulo, Kituo cha Afya Mbalache kimeshakamilika, Kituo cha Afya Lukalilo kimeshakamilika, lakini hivi vyote vina changamoto ya kutokuwa na vifaa tiba ili vianze kutoa huduma. Tusingetamani sana vikae muda mrefu kwa sababu vitaanza kuleta taswira ya kwamba majengo yamejengwa lakini huduma haipatikani.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naongea na Mkurugenzi wa MSD sasa hivi, na ameniahidi, nimpongeze sana Mkurudenzi wa MSD, anafanya kazi kubwa sana, ametuahidi kwamba atatuletea vifaa tiba pale Makete. Kwa hiyo nikuombe sana Mheshimiwa Waziri kwenye hili jambo muweze kutusaidia. Jambo langu kubwa lingine Mheshimiwa Waziri kuna hili jambo la wanafunzi ambao wanasoma udaktari; na hapo Mheshimiwa Waziri naomba tusikilizane sana. Tuna wanafunzi ambao wanasomea utabibu, mambo ya utabibu; wanasoma kwa muda wa miaka mitano. Wakishasoma kwa miaka mitano mnawapeleka internship, kwa maana wanakuwepo na ile pre-internship exam.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kunakuwa na changamoto kubwa sana. Watoto hawa wengi ni watoto wa masikini. Amesoma kwa muda mika mitano ameenda kufanya field, ametoka kwenye field mnampa mtihani huu. Huu mtihani ambao kwa kweli kwenye syllabus haupo, ila ninyi miliweka kama sehemu ya kuchujia kama sikosei au mlikuwa mna lengo gani? Lakini hawa watoto wamesoma miaka mitano, na ukisoma kwa takwimu za mwaka 2021/2022 kuna madaktari 200 ambao wamemaliza miaka mitano au wamesomeshwa na Maprofesa wetu hapa nchini, lakini baada ya kufanya mtihani wa pili internship exam wamekwama, mmewaondoa kwenye mfumo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa issue ni moja. Miaka mitano daktari amewekeza kenye kusoma lakini mtihani huo ambao si tu wa chuoni ni mtihani kutoka kwenye Baraza la Madaktari mnaita MCT. Ninaomba sana Mheshimiwa Waziri kumbuka hawa ni watoto wa masikini, angalieni utaratibu upya jinsi gani ya kuweza kuwasaidia. Kwa sababu hata rufaa zao ukataji wa rufaa kwa mtu ambaye amefeli hii pre- internship exam, mwanafunzi huyu utaratibu wa ukataji rufaa haupo open. Ninaomba sana Mheshimiwa Waziri, tuna watoto madaktari zaidi ya 200 wamekuwa disqualified licha ya kusoma miaka mitano darasani na wamefundishwa na maprofesa wetu hawa, lakini pili wameenda field na wamefanya vizuri. Huu mtihani ambao hauna syllabus inawezekana ninyi mmeweka ndio mlango wenu wa kufungulia mtu aweze kupita, lakini sasa umekuwa ni kikwazo kikubwa sana kwa madaktari wetu nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati ambao Taifa linahangaika na upatikanaji wa madaktari kwenye vituo vyetu vya afya na hospitali zetu ninaomba Mheshimiwa Waziri uliangalie jinsi gani ya kuliangalia. Ninajua mlichokuwa mnakiangalia. Kwamba kuna sekta binafsi ambayo imekuwa ikipitisha madaktari ambao wako disqualified wanaenda kutusababishia matatizo, lakini tafuteni namna jinsi gani ya kuweza kuwasaidia wanafunzi ambao wamepita Chuo Kikuu cha Muhimbili na Maprofesa ambao tunawaamini waweze wakaende kulisaidia Taifa. Hawa watu 200 ni watu wengi sana, wamesomea miaka mitano, mama ameuza miti ameuza kuni amefanya nini…

MHE. DKT. HAMISI A. KIGWANGALLA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

TAARIFA

MHE. DKT. HAMISI A. KIGWANGALLA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumpa Taarifa mzungumzaji kwamba, ni muhimu sana tuka-standardize Madaktari ambao wametoka kwenye vyuo na sasa wanaenda kugusa mgonjwa kwa sababu, sasa inakuwa utaalam na huduma watakayoitoa inahusu kifo ama uzima wa mteja. Kwa hivyo, ni suala ambalo kama Taifa hatupaswi ku-compromise nalo kwa hivyo, pamoja na gharama mtu anayeweza kuingia kwenye training, lakini at the end of the day, daktari anaenda kugusa mtu na hujui atagusa nani; atakugusa wewe Mbunge, atagusa mkeo ama mtoto, usalama ni muhimu sana. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Haya ahsante. Taarifa hiyo Mheshimiwa Sanga.

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Namheshimu sana Mheshimiwa Kigwangalla kwa sababu, hii ni field yake na hata mimi mawazo yangu yalikuwa ni hayo kwamba…

NAIBU SPIKA: Sasa mwite basi Dkt. Kigwangalla.

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, sawa, Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla. Mawazo yangu nami yanaendana na hayo, kwa sababu huu mtihani ulikuwa una lengo fulani ambalo Waziri analifahamu, lakini umekuja ku- include hata vijana ambao wako qualified na wamesomeshwa na Madaktari wetu. Kwa hiyo, naomba kama ni mchakato uweze kuangaliwa ni jinsi gani ya kuweza kudhibiti.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli katika jambo ambalo hatuwezi ku-compromise ni suala la afya na uhai wa mwanadamu. Hili pia nipitie hapohapo, kati ya jambo ambalo Mheshimiwa Waziri anatakiwa aliangalie sana ni maslahi ya Madaktari kwenye Taifa letu. Namwomba sana kati ya watu ambao tunaweza tukawa tunazungumza sasa hivi kwa sababu, tuna afya njema, toka hapa nenda Benjamin Mkapa, Muhimbili, sijui hospitali gani ya Mkoa, Rufaa, Bugando, Madaktari wanafanya kazi katika mazingira magumu kwa 24 hours. Naomba sana Mheshimiwa Waziri aangalie maslahi ya Madaktari kwenye Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi hapa tumeshiba tunaona ni jambo rahisi, lakini ukienda kwenye mazingira ambayo wanafanya kazi ni mazingira magumu. Takwimu zinaonesha mwaka huu tu 2022/2023, wagonjwa milioni 35 wamepitia kwenye mikono ya Madaktari wetu. Kwa hiyo, hili ni jambo muhimu sana na siamini kama Serikali inaweza ku- compromise kwenye kuboresha maslahi ya Madaktari wetu kwenye Taifa letu kwa sababu, sisi wote jeuri yetu ni afya. Wabunge, Mawaziri na watu wengine kama wakulima jeuri yao yote ni afya. Kwa hiyo, naomba sana Waziri aangalie suala la maslahi ya Madaktari kwenye Taifa letu wanafanya kazi kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nenda kwenye vyumba vya watoto njiti na hili pia niweze kusaidia, Hospitali yetu ya Benjamin Mkapa ina changamoto ya mashine ya oxygen kwa ajili ya watoto njiti. Namuomba Mheshimiwa Waziri, hili waweze kulifanyia kazi, mashine za oxygen pale zimepungua na nimeshuhudia kwa macho yangu. Ni vyema sana wakiweza kusaidia Hospitali ya Benjamin Mkapa wakaongezewa mashine kwa ajili ya oxygen kwa ajili ya watoto wetu njiti. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii, lakini nasema wazi kabisa Mheshimiwa Waziri anafanya kazi nzuri, Mheshimiwa Mollel anafanya kazi nzuri, lakini the master of all these ni Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ameenda kuifanya Sekta ya Afya ionekane ni moja kati ya sekta muhimu kwenye Taifa letu na ameweza kutusaidia kwenye mambo mengi sana. Mungu ambariki sana Mheshimiwa Waziri, achape kazi, sisi wadogo zake tuko nyuma na Mungu amsaidie sana. (Makofi)