Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya

Hon. Vita Rashid Kawawa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Namtumbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya

MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara hii muhimu kwetu kwa afya zetu na kwa wananchi wetu wa Tanzania. Naomba nianze kwa kuwapongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa kazi nzuri wanayoifanya katika Wizara hii. Tumeshuhudia wakiwa mstari wa mbele katika mambo mbalimbali na magonjwa mbalimbali ya mlipuko yanapotokea na wanajitahidi chini ya uongozi wao kuzima magonjwa hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Rais katika kipindi hiki cha mwaka 2022/2023, tumeweza kupata zaidi ya bilioni tano na milioni 318 katika kujenga miundombinu ya hospitali zetu katika Wilaya ya Namtumbo. Hospitali ya Wilaya tulipata bilioni mbili na milioni mia tatu, tumejenga majengo, wodi ya akinamama na akinababa, tumejenga Hospitali ya meno na macho, lakini tumejenga jengo la mama ngojea, tumejenga na mortuary pia.

Mheshimiwa Naibu Spika, mama ngojea ni muhimu sana sisi kwetu kwa sababu, jiografia ya Namtumbo, Kijiji cha mwisho kinafika kilometa 254, kwa hiyo, kuna akinamama wanaopata complications kutoka katika hospitali wanapata rufaa kuja pale wengine kwa ajili ya kungojea kusubiri kujifungua, basi Serikali imewajengea jengo la mama ngojea, wanasubiri wakiwa palepale. Kwa hiyo, hii ni kazi nzuri sana waliyoifanya na inawasaidia sana mama zetu wale ambao wakifika pale wanakuwa bado hawajawa-admitted, lakini wanakuwa katika jengo lile la mama ngojea. Kwa hiyo, dharura yoyote inapotokea wanatibiwa, kwa hiyo, tunashukuru sana Wizara na Serikali kwa eneo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili Serikali wametujengea vituo vya afya vilivyokamilika. Kilichokamilika kimoja cha Mtakanini, lakini tuna vituo vya afya viwili viko mwishoni tulipata bilioni moja, Kituo cha Afya cha Ligela milioni 500 na Kituo cha Afya cha Magazini milioni 500 ambayo tuko katika hatua za mwisho kabisa. Pia Serikali ilitugawia fedha za kukamilisha zahanati nane, tulipata milioni 400; kila zahanati milioni 50 na tumekamilisha Zahanati ya Namali, Uramboni nayo iko mbioni kukamilika, Nahimba pia iko mwishoni, Kilangalanga iko mwishoni kukamilika, Misufini iko tayari na inatoa huduma, lakini Kumbara iko mwishoni kukamilika, Nahoro nayo ipo mwishoni, Luhangano nayo iko mwishoni kukamilika na Muhangazi iko mwishoni kukamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mafanikio hayo ila tuna mapungufu ambayo pia, naomba niiombe Wizara kwamba, Kituo chetu cha Afya cha Mtakanini kina upungufu bado wa wodi mbili, wodi ya akinamama na wodi ya akinababa ya kulaza wagonjwa, lakini pia tuna upungufu wa wataalam wa usingizi, hatuna mtaalamu wa usingizi pale, alkini pia hata Hospitali ya Wilaya pia ina upungufu wa mtaalam wa usingizi, lakini ikama ya watumishi katika Hospitali ya Wilaya haijatimia.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunashukuru Kituo cha Afya cha Mtakanini walitupatia watumishi 11 na walifika wameripoti na wanaendelea na kazi, lakini bado tuna upungufu wa mtumishi wa usingizi. Hospitali ya Wilaya nayo ina upungufu wa vitendeakazi vingine kama standby generator kwa ajili ya mtu akiwa anafanyiwa operation na dawa zile ambazo zinahitaji kuwekwa kwenye majokofu umeme unapokatika, hatuna standby generator katika Hospitali ya Wilaya na vituo vyetu pia havina standby generator.

Mheshimiwa Naibu Spika, Hospitali ya Wilaya pia ina upungufu wa vitanda, baada ya majengo mengi kujengwa bado tuna upungufu wa vitanda. Kwa hiyo, tunaomba sana Wizara ituangalie kwenye hili, watumishi, lakini pia baadhi ya vifaa tiba.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine, tunaambiwa hela zimepelekwa MSD, lakini kuna kuchelewa kufika kwa vifaa tiba na dawa pamoja na kwamba, tulipata vifaa tiba vya milioni 758, tunaishukuru sana Serikali, vifaa tiba vya milioni 758 tumeshavipokea, lakini kuchelewa kwa vifaa tiba vingine nayo inatuchosha, lakini tunawashukuru sana. Nawashukuru sana Waziri wakati wote na Naibu Waziri nikiwafikia, basi huwa wananisikiliza na wananitatulia tatizo langu, kwa hiyo, nawashukuru sana, waendelee hivyohivyo na kwa kusema kweli wameiweza Wizara yetu hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna upungufu pia wa wataalam wa meno na vifaa vyake. Kwa sababu, tuna jengo jipya la huduma hii ya meno kwa hiyo, hatuna vifaa vyake, lakini tuna upungufu pia wa ultra sound katika Kituo cha Afya cha Mtakanini kwa hiyo, tunaomba sana. Hivi vituo vya afya vingine viwili vilivyobakia ambavyo viko mwishoni tunaamini kabisa wakati wowote vitakamilika na watatupatia vifaa tiba. Tunaomba sana ili majengo yasikae muda mrefu, tungeweza kuanza kupata vifaa tiba sasa hivi yanapokamilika kwa sababu, yameshaisha, wako kwenye final touches, kwa hiyo, vile vifaa tiba vingeanza kupelekwa sasa hivi, ili wakimaliza kabisa, basi huduma inapatikana. Tunawashukuru sana kwa yote ambayo wanatutendea sisi Namtumbo katika kipindi hiki, asanteni sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naunga mkono hoja.