Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya

Hon. Dr. Florence George Samizi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Muhambwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya

MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ili niweze kuchangia hotuba hii ya Wizara ya Afya. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa jinsi ambavyo amejipambanua kuendelea kuboresha huduma za afya. Wenzangu wameshasema, tumeona jinsi ambavyo amekwenda kuboresha huduma za afya kwa kuongeza vituo vya kutolea afya. Tumepata hospitali nyingi, tumepata vituo vya afya, zote hizi ni jitihada za Mheshimiwa Rais kuhakikisha kwamba afya za Watanzania zinakwenda kuimarika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata sisi kule Muhambwe tumepata vituo vya afya viwili ambavyo vimeshakwisha kabisa katika Kata ya Kibondo Mjini na Kata ya Kunyambo na sasa hivi tunaendelea na ujenzi wa Kituo cha Afya katika Kata ya Rugongwe, ili kuendelea kuboresha afya za wananchi wa Muhambwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Afya na Naibu Waziri kwa jinsi ambavyo wanafanya kazi. Wamejituma na wamejipambanua kuhakikisha kwamba, wanafikisha huduma na hasa huduma bora ambazo ndio wananchi wanazitegemea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri amekuwa akisema kila siku kwamba, si bora huduma, hapana, anachotaka ni huduma bora. Tunampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa kujua kwamba, wananchi sasa wanahitaji huduma bora. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze Serikali kwa jinsi ambavyo imepeleka vifaa kila mahali. Wenzangu wameshasema, sasa ni jukumu letu sisi kuendelea kuvisimamia vile vifaa kule ambako tumeletewa ili viweze kutoa huduma inayostahiki kwa kuvitunza, ili viweze kutoa huduma hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimepitia lengo la Wizara na nikaona katika vipaumbele vyao wameweka kuimarisha huduma za afya ya mama na mtoto ya uzazi na mimi nitajielekeza hapo. Nimeona pia kwenye takwimu vifo vya mama na mtoto vimepungua kwa asilimia nne, niwapongeze sana Wizara kwa jitihada hizi za kupunguza vifo vya mama na mtoto kwa sababu, wote tunafahamu kwamba, afya ya jamii yoyote inapimwa kwa kupunguza vifo vya mama na mtoto. Kama kuna vifo vingi vya mama na mtoto, basi jamii hiyo haina afya iliyo bora. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee bado tuna mikoa ambayo haifanyi vizuri sana, ukiwemo Mkoa wangu wa Kigoma. Tumeona hapa kuna vifo 900. Katika hivi vifo 982 Mkoa wangu wa Kigoma una vifo 102, accumulative ni vifo vingi japo hatujazidi kwingine, lakini kwa vifo hivi bado akinamama wanakufa katika Mkoa wa Kigoma. Wilaya yangu ya Kibondo tumepata vifo 12 kwa mwaka huo 2023 kwa hiyo, ina maana tuna kifo cha mama mmoja kila mwezi. Bado hali hii haikubaliki kwa wananchi wa Muhambwe, bado tunahitaji jicho la pekee. Mheshimiwa Waziri Ummy anaweza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi Mkoa wa Kigoma tumejipambanua na tumekuja na Kauli Mbiu inasema Kigoma Safi ya Kijani Bila Vifo vya Mama na Mtoto Inawezekana. Sisi peke yetu hatutaweza, tunamwomba Mheshimiwa Waziri, atuangalie kwa jicho la pekee hasa kwa watumishi. Tunafahamu ziko changamoto nyingi zinazosababisha haya, Mheshimiwa Rais ameshaleta vifaa, ameleta majengo, sasa watumishi bado ni tatizo. Tuna uhaba, upungufu wa watumishi kwa asilimia sabini na kitu, ni ukweli usiopingika kwamba, hawawezi kukabiliana na vizazi hivi ambavyo viko vingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hawa watu 12 wamekufa katika vizazi hai 17 elfu kwa hiyo, unaweza ukaona ile burden tuliyonayo. Tuna burden ya wazazi wanaojifungua wengi kwa hiyo, tunaomba Mkoa wa Kigoma kipekee tupewe kipaumbele hasa kwa hawa watumishi ambao wanategemea kuajiriwa, ili waje kutia nguvu katika haya mapambano ambayo kipekee sisi wenyewe tumeyaanza. Nichukue nafasi hii kumpongeza RMO Jesca, kwa kweli ni mwanamama anajituma anafanya kazi. Tunaamini kabisa wakituwezesha watumishi basi, tutatoka huko tuliko. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli usiopinga kwamba, bado tumeona kwenye taarifa ya Wizara ukurasa wa 66 wameonesha ni jinsi gani halmashauri na zahanati, kliniki zina burden kubwa ya wagonjwa wa OPD. Amesema wameongezeka kutoka asilimia 16 hadi 22 na tukiangalia katika lile jedwali hospitali za rufaa zinachangia asilimia 5.5 ya wagonjwa wa nje, tunaita OPD. Hospitali za rufaa asilimia 6.6, lakini hospitali za halmashauri asilimia 22.8 na zahanati zinachangia asilimia 39, hii ina maana gani sasa?

Mheshimiwa Naibu Spika, bado tunahitaji kuelekeza huduma nyingi sana kule kwenye Halmashauri zetu kwa sababu, ndiko ambako wale wagonjwa wataweza kupatikana na wakipata huduma nzuri, basi tutapunguza hata wale wagonjwa wa kuwapeleka kwenye referral. Maana Dkt. Mzuri wa kwanza au nesi mzuri wa kwanza ni yule anayemwona mgonjwa mara ya kwanza na akaweza kutoa diagnosis iliyo sahihi na akaweza kutoa matibabu yaliyo sahihi. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri kwamba, halmashauri zetu, zahanati zetu na hivi vituo vya afya bado vinahitaji wahudumu wa afya na huduma bora kwa sababu ndiko wagonjwa wengi ambako wanaanzia.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii inawezekana kwa sababu, nimpongeze kwa hii program ya Samia Tuvushe Salama, ina maana wataalam hawa 100 wafike kule kwenye zahanati zetu, wafike kule kwenye kliniki zetu, wakafanye hizo mentorship na coaching ili tuweze kupata ujuzi ulio bora na weledi kwa watumishi wetu wa afya ili waweze kutoa huduma bora kwa wananchi wetu kule kwenye halmashauri zetu na kwenye zahanati zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimemwona Mheshimiwa Waziri kwenye hotuba yake ameeleza vizuri jinsi gani ya kuboresha maslahi ya watumishi wa afya, motisha itaenda kuchangia kuleta huduma bora kwa watumishi. Ni ukweli usiopingika kwamba, bado hakuna ulinganifu wa mishahara na motisha kwa watumishi wa afya kwenye hospitali za referral na hospitali za halmashauri. Kama tunaenda kupeleka watumishi kwenye halmashauri zetu na kwenye zahanati, lakini bado maslahi yao yako chini, basi tutashindwa kuwashikilia kule kwenye zahanati zetu kwa sababu, wote tumeshuhudia ajira zikitangazwa Muhimbili watu wanaomba kutoka kwenye halmashauri zetu wanakwenda Muhimbili. Ajira zikitangazwa huku kwenye hizi taasisi watumishi wanahama, wanahama kwa sababu Daktari Bingwa wa akinamama aliyepo kwenye Hospitali ya Kibondo na Daktari Bingwa yuleyule aliyeko kwenye Hospitali ya Muhimbili mishahara ni tofauti, motisha ni tofauti. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama hatutaleta ulinganifu wa hizi motisha za watumishi wa afya kwenye hospitali za referral na hospitali zetu za halmashauri, tutawapeleka hawa watumishi kwenye zahanati zetu na hawatakaa maana kila mtumishi anatafuta green pastures. Kama anatafuta green pastures, hawezi kukaa kusubiri mwongozo ambao kwa kweli mwongozo huu umeongelewa miaka mingi. Tuliambiwa unapitiwa ulinganifu, zile zahanati na dispensary na hospitali za referral, ni miaka mingi. Tunaiomba Serikali, sasa ni muda muafaka, kwa sababu Serikali imeshawekeza kwenye zahanati na vituo vya afya, basi na maslahi ya watumishi wa halmashauri yaboreshwe ili yaweze kulingana na hospitali nyingine humu nchini. Imewezekana kwenye taasisi nyingi, kilimo walikuwa na shida hiyo, I mean mifugo walikuwa na shida hiyo, lakini waliweza kuweka ulinganifu na watumishi wameweza kukaa mahali pale, kwa hiyo, hili linawezekana.

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kuishukuru Serikali kwa haya magari ya ambulance yaliyoletwa. Tumeona Serikali inavyopambana kupunguza vifo vya mama na mtoto na kwenye Taarifa ya Mheshimiwa Waziri amejipambanua kabisa akinamama sasa wameongezeka kwenda hospitalini. Tumeona akinamama walioenda hospitali mara moja asilimia 96, walioenda mara nne asilimia 86, ambao wameenda chini ya mimba ya wiki 12 ndio wchache asilimia 36. Hii ina maana gani?

Mheshimiwa Naibu Spika, ina maana akinamama wengi wanakwenda hospitali. Sasa akinamama tunawa-miss wapi? Tunawa-miss sana pale kwenye huduma ya kwenda kujifungua. Tumeona jinsi M-Mama imeanza juzi na inafanya vizuri sana. Sasa nimwombe Mheshimiwa Waziri, hawa watumishi wa afya ya jamii ambao tumeamua kuwasomesha na kuwawezesha tuwaweke kwenye mitaa yetu, hawa ndio waweze kujua mzazi yuko wapi na ambulance inaenda saa ngapi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeshuhudia ambulance zikikaa hospitali kusubiri referral. Kama tuna ambulance nne kila halmashauri, kwa nini zipaki hospitali zisiwahudumie hawa akinamama wajawazito ili waweze kuwahi hospitali? Kwa nini zipaki kusubiri mgonjwa mahututi na wakati mwingine hayupo? Ndio maana unakuta hizi ambulance saa nyingine zinafanya kazi ambazo hazikukusudiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe Mheshimiwa Waziri hawa watumishi wa ngazi ya jamii tuwatumie vizuri kwenye jamii zetu kupunguza vifo vya mama na mtoto kwa maana kwamba, waweze kuwa na coordination, huyu mama anapata uchungu saa ngapi, anategemea kujifungua saa ngapi, gari la ambulance liko wapi, ili limuwahishe hospitali ili aweze kupata huduma za afya. Hapa tutakwenda kupunguza vifo vya mama na mtoto kwa sababu, ambulance tunazo, ambulance haibebi mgonjwa kila wakati, tukifanya coordination nzuri hii inawezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee nimpongeze Waziri kwa jinsi alivyoona kwamba, sasa alete huduma ya ujuzi wa uongozi. Ni ukweli usiopingika kwamba, tunakuwa Madaktari hospitali na Manesi, tunajiongoza wenyewe hakuna kiongozi hospitalini. Kwa hiyo, naamini kabisa hii kozi ambayo ameamua kuileta ya leadership…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Dkt. Florence. Kengele ya pili.

MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)