Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya

Hon. Boniphace Mwita Getere

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bunda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara ya Afya. Cha kwanza niwashukuru tu Waziri wa Wizara ya Afya, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na viongozi wataalam wote wa Wizara ya afya. Kimsingi kwenye upande wetu wa afya kwa ngazi za juu wanajitahidi sana kufanya vizuri, wanafanya kazi nzuri na Mheshimiwa Ummy kwa kweli, ni zawadi tu ya kukupa mfanyakazi bora wa kufanya kazi za umma hatujakupa, lakini anafanya kazi vizuri sana. Hana mbambamba, yuko straight kwenye jambo hili. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mambo yananitatiza hapa naomba niyaseme tu. Hivi kweli toka tumepata uhuru tunashughulika na magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza. Hivi kweli toka tumepata uhuru wakati wa Nyerere, zahanati zilikuwa chache sana na vituo vya afya vichache sana na kwenye Wilaya tunapata hospitali chache, lakini huduma zilikuwa zinapatikana. Hivi kweli nchi yetu leo tunapeleka mabilioni ya hela kujenga zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya na mikoa, lakini hakuna huduma, hakuna huduma kwenye zahanati.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi kweli nchi yetu leo tunapeleka mabilioni ya hela kujenga zahanati, kujenga vituo vya afya, kujenga hospitali za Wilaya na Mikoa, hakuna huduma. Hakuna huduma kwenye zahanati, hakuna! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda pale Bunda, juzi nilikuwa natembelea hospitali moja ya Bukama mpya tumejenga ina Nesi mmoja. Huyo ndiyo alete dawa, atibu, afanye nini. Ni mwanadamu yule, anaweza kupata tatizo. Ukienda zahanati ya Matimero, kamejengwa kabanda watu wanazalia, wanazaa nje, ukienga Kambubu ni hivyo hivyo. Zahanati za Tanzania – sijui kuhusu maeneo mengine – lakini kwenye Jimbo langu hali ni mbaya kuliko kawaida.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunafanyaje, tunajenga majengo mpaka lini, yaani tunafanyaje kwa mfano? Kwa nini tusiamue hizi tulizonazo tukubaliane kupeleka wahudumu wa afya na wataalamu wa afya kwenye maeneo haya. Kwa nini tunajenga majengo makubwa? Nenda Hospitali ya Wilaya ya Bunda, jengo la kwangu, bilioni 35 iko pale, sijawahi kuona hospitali ya Wilaya rufaa inaenda kituo cha afya, sijawahi kuona ndiyo Bunda hiyo tunaiona.

Mheshimiwa Naibu Spika, yaani mtu akienda hospitali ya Wilaya hapati dawa anakwenda kituo cha afya Ikizu ndiyo anapata dawa. Ikizu hiyo ni hospitali ya zamani ya mwaka 1959, imechoka. Kwa nini tusikubali, kwani sisi ni wafungwa wa mfumo wa D by D? Devolution by Decentralization sisi ni wafungwa? kwamba lazima tufanye hivi? Hivi kweli TAMISEMI kweli, ishughulike na ajira tunalia hapa, ishughulike na majengo tunalia hapa, ishughulike na TARURA tunalia hapa, ishughulike na kila kitu TAMISEMI?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini tusikubali tusijaribu maisha ya Watanzania hiyo Wizara ya Afya ichukue mfumo wote kutoka juu mpaka chini, kwa nini? Kwa nini tunajaribu maisha ya Watanzania, kwa nini watu wanakufa tunaona hadharani. Kwa nini watoto wetu wanakufa mtaani? Tuwaache Watanzania tuwatibu wapate akili, waweze kujigharamia wenyewe kwenye umaskini wao na ujinga wao waweze kusoma vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mimi naomba kwa vyovyote vile itakavyokuwa Wabunge tukubali tuombe inavyowezekana, mbona tumeomba maji imewezekana, tumeomba kilimo imewezekana, kwa nini leo tunashindwa kuomba afya zetu?

Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunataka kutibu watu wetu kwa bima ya afya kwa wote, hivi kweli tutaipeleka bima ya afya kwa hali hiyo? Yaani Waziri anayeiamuri MSD atoe dawa ni mwingine na Waziri anayepokea dawa ni mwingine, haiwezekani. Madaktari wa zahanati, vituo vya afya na Wilaya wametuma hela kuja MSD kununua dawa, hela zinakuja MSD kununua dawa, dawa hazitoki, ni maneno tu. Nani atasema sasa huyu MSD atoe dawa? Tukubaliane kwamba jamani afya za Watanzania tusichezee, kama tumejenga zahanati zimefika mwisho tuongeze watumishi, hospitali na dawa watu watibiwe, shida sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna sera ya Taifa inalinda watoto, miaka mitano utakwenda utoe 54,000 utatibiwa, iko wapi? Watoto wanakufa nani anapokea? Hakuna kitu. Kwa hiyo, niombe kwenye hili jambo kwamba sasa tuna hali mbaya.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kituo cha Afya Mgeta cha kwangu pale tumejenga karibu milioni 500 lakini sasa nenda mortuary imejengwa 2018 haina jokofu mpaka leo, vifaa kuna ultrasound hakuna wataalam, tulijenga tulisema vile vituo vya afya vya zamani cha kwangu kilipewa milioni 400, tukaambiwa kwamba kuna milioni 700. Milioni 400 ya majengo, milioni 300 ya vifaatiba hakuna. Ni shida. Nani aamuru? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukubali kwamba sasa Wizara hii tusiweke afya za Watanzania kwenye mashaka, tuiweke iwe moja. Haya mambo ya D by D tuyaache, kwani nani anakufa, si dini tu, mradi ukubali mambo ya dini utaishi maisha yako marefu. Uwe Muislam utaishi, uwe Mkristo utaishi, hata ukiwa Mlokole, mradi tu uache dhambi. Sasa kwa nini tusikubali ili hospitali hizi zitoe matibabu, afya zetu ziende hii Wizara ichukue Wizara yote, ikope mikopo ya kutosha ilete kwetu hapa tufanye kazi. Kwa hiyo naomba hiyo inaweza kutusaidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Ummy, juzi nilikuwa India nikawa naongea na watu wa Apollo. Apollo ziko nyingi India. Sasa nikawauliza hivi ninyi mnafanyaje? Wakasema huku kwetu Waziri yeyote wa Serikali, hizi Apollo unazoziona ni za Serikali lakini ana uwezo wa kuja hapa akaangalia kinachofanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri wakati tumekaa pale tunasubiri Waziri anafika pale. Dawa ni cheap, bei ndogo sana India dawa. Sisi kwetu hapa kila mtu ana bei yake, wala Waziri husogei, wala husemi. Tuna bei elekezi ya maji, bei elekezi ya mafuta, bei elekezi ya dawa hakuna, wewe kunywa tu ufe, hakuna! Hakuna bei elekezi! Tuna bei elekezi ya kila kitu lakini siyo dawa. Wewe nenda unavyotaka fanya unavyotaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa wakaniambia bwana ninyi Watanzania afya zenu mnaweka siasa. Tusifiane hapa humu ndani lakini kwenye afya watu wanakufa, tusifiane nenda kwenye mstari utaendaje, utasemaje? Unakwenda kituo cha afya mtu mmoja utasema nini sasa, haiwezekani. Kwa hiyo ombi langu ni kwamba Wizara hii iwe moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Ummy nilipokuwa India niliuliza hivi mashine hizi za saratani ninyi mnafanyaje, wakatuambia iko mashine inaitwa PET-CT Scanner, ninyi watalaam akina Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla mnaijua, ambayo imefungwa Ocean Road toka 2021 mpaka leo haijafanya kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo ndiyo ukiiweka ikikamilika maana yake ukimwingiza mgonjwa yeyote mwenye saratani na magonjwa yoyote ya moyo inasoma moja kwa moja bila kuleta ujanja. Kwenye nchi zetu nasikia hapa Afrika Mashariki ni sisi tu tumenunua hapa ni bilioni 14. Sasa nikajiuliza bilioni 14 ndiyo nini? Kwa nini tusinunue ile mashine ikawepo Benjamin Mkapa, Wabunge tuko hapa ndiyo Bunge linaishi, ndiyo Mji Mkuu wa Serikali, ukimpeleka Mbunge pale mpaka umpeleke aende kupiga mionzi Dar es Salaam. Kwa nini tusinunue bilioni
14 ikakaa hapa, tukanunua Mwanza, tukanunua kwenye kanda, bilioni 14 PET- CT Scanner zikakaa pale zikatusaidia. Mionzi yenyewe mpaka uende kupigwa Ocean Road, hakuna Mwanza, tuna Hospitali ya Mkoa Mara imekaa pale Mheshimiwa Ummy, si uende uitembelee uione ina hali mbaya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unatibu tu wagonjwa, jamani hivi hospitali ya Mkoa wa Mara imekuwa tena kama clinic? Maneno gani haya, imekuwa kama zahanati! Sasa Mkoa wa Baba wa Taifa mmeufanyaje? Jamani, mbona hali mbaya. Mama Maria badala ya kutibiwa pale Mkoani analetwa mpaka Dar es Salaam, mambo gani haya? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mimi niombe hii PET- CT Scanner ifanye kazi lakini muilete Benjamin Mkapa, iende Mwanza, Mara, kila mahali iweze kufanya kazi, vinginevyo ndugu zangu mimi niwaombe hata ningeongea nini kama hii Waziri hatuwezi kuiunganisha tunapoteza muda. Ahsante. (Makofi)