Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya

Hon. Kwagilwa Reuben Nhamanilo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Handeni Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya

MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa na mimi niweze kuchangia bajeti hii ya Wizara yetu muhimu ya Afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja katika maeneo ambayo Serikali ya CCM imefanya mapinduzi makubwa ni eneo hili la afya. Mapinduzi haya yaliyofanyika ya kuleta miundombinu vikiwemo vituo vya afya, zahanati, Hospitali za Rufaa za Kanda, Mikoa yamesababisha tuwe na changamoto. Kwa hiyo, wajibu wetu sisi ni kuishauri Serikali hii namna ya kutatua changamoto hizi ili mafanikio haya ambayo tumeyapata yasigeuke kuwa laana.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo nitaongelea jambo moja tu ili kuishauri Serikali, jambo la dawa. Mwaka jana nilisimama hapa nikazungumzia kuhusu MSD, ninaipongeza sana Serikali kwamba ilichukua hatua thabiti na bado inaonesha dhamira ya kuleta mabadiliko kwenye Sheria ya Manunuzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa pale MSD nataka leo tupaangazie upande wa pili, tuuache ule wa MSD tuangazie upande wa pili wa mfumo wetu wa dawa. MSD pana miradi Minne ya kununua dawa. Mradi wa kwanza ni ununuzi wa vifaa na vifaatiba vya huduma za dharura, mradi wa pili ni ule wa mapambano dhidi ya Covid-19, mradi wa tatu ni utekelezaji wa mradi wa mfuko wa dunia na mradi wa Nne ambao ndiyo mimi leo nataka kuuzungumzia ni ule wa fedha zinazolipwa kutoka kwenye Halmashauri zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, iko hivi hospitali zetu kwa maana ya Madaktari wetu wa Wilaya, Halmashauri zetu zinapoweka oda kununua dawa MSD uzoefu unaonesha kwamba wakiweka oda ya dawa 10 MSD wanapata Nne, Sita hawazipati. Uzoefu unaonesha kwamba wakitoa oda ya dawa 100 pale MSD wanapata dawa 40, 60 hawazipati, huo ni uzoefu na ndiyo takwimu zilivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa upo mwongozo kwamba zile dawa ambazo Halmashauri zetu zikiweka oda MSD, dawa ikikosekana mwongozo unawataka wataalamu wetu na hospitali zetu zikanunue dawa kwa prime vendors (washitiri). Sasa hili la washitiri ndiyo mimi nataka tulijadili. Mimi hili la washitiri naliona ni tatizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni tatizo kwa sababu gani, kwanza nitoe takwimu Halmashauri ya Handeni Mjini mwaka 2021/2022 MSD tulinunua dawa za milioni 40 tu, lakini kwa washitiri tulipeleka milioni 60. Mwaka huu wa fedha mpaka as of 31st March MSD tumepeleka milioni 55 kununua dawa lakini kwa washitiri tumepeleka milioni 61.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ndiyo kusema nini? Fedha zetu nyingi za dawa kwenye Halmashauri zetu zinakwenda kwa washitiri. Kwa hiyo, tusipopaboresha hapa kwenye huu mfumo wa washitiri hili tatizo la ukosefu wa dawa tutaendelea kuwa nalo la ukosefu wa dawa.

MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini ni tatizo kwa washitiri?

NAIBU SPIKA: Taarifa.

TAARIFA

MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpe taarifa msemaji anaongea vizuri sana. Tatizo lililopo MSD hana fedha ya kununua dawa na kuzihifadhi ili anapopata oda kutoka kwenye Halmashauri aweze ku- deliver on time. Halmashauri wanapomkuta MSD hana dawa inawabidi waende wakanunue kwa mshitiri na ndiyo maana tumeomba katika taarifa MSD apewe mtaji awe na dawa ili huyu anapopata order apelike palepale. Ahsante sana. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Reuben uanipokea taarifa?

MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni mwanamapinduzi, lazima tufanye mapinduzi. Washitiri ni tatizo, na matatizo nayaeleza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza wakienda kununua dawa kwa mshitiri, bei wanayotuuzia washitiri ni kubwa kuliko ambavyo tungenunua MSD. Ni kubwa! Last time nilitaja figures hapa watu wakashangaa, kwa habari ya kidonge cha shilingi milioni nne kununuliwa kwa shilingi milioni 200 na kitu. Leo sitaji figures, nasema tu kwa ujumla, kwamba, tukienda kununua kwa washitiri, bei tunayonunua ni kubwa kuliko ambayo tungenunua MSD, la kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, tatizo kubwa ni kwamba, wale washitiri bei wanazotuuzia ni kubwa kuliko za wholesellers wetu wanaopatikana hapa nchini. Ni kana kwamba haitoshi, hata uki-order leo dawa, au kifaa tiba kinaweza kikamaliza mwaka hakijaletwa. Hii siyo sawa. Tuondokane na hii habari ya washitiri. Sasa wenzetu wa Wizara ya Afya wanayo mawazo, wanafikiri kwamba, badala ya kuweka mshitiri mmoja kwenye Mkoa mzima, waweke hata wanne. Hiyo haiwezi kuwa solution namna mlivyofikiria, kwa sababu nyie mnataka wawepo wanne, lakini wa- specialize kwamba huyu awe analeta hivi, huyu alete hivi, huyu alete hivi. Hapo hapatakuwa na ushindani. Kama bado mna idea ya kuwa na washitiri, ruhusuni wawepo washitiri washindanishe bei ili tusiwe tunalanguliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaongea hivi kwa sababu Mheshimiwa Rais anapeleka fedha nyingi sana. Sikilizeni niwaambie, bajeti ambayo MSD wanaihitaji ni kama shilingi bilioni 592 tu, lakini miezi sita tu iliyopita MSD wamefanya manunuzi ya zaidi ya shilingi bilioni 257. Hizi zinazonunuliwa na MSD zikiwa managed vizuri, na hizi tunazonunua Halmashauri, zikiwa managed vizuri, dawa zinatosha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kinachofanyika ni kwamba tunanunua bei mara tatu mara nne ya bei halisi. Haitakiwi kuwa hivi, kwa sababu tukifanya hivyo, wananchi wa wa Kwedizandu watapata lini dawa? Wananchi wa Kwalwala, Kwasindi, Kwabaya; haya majina ninayoyataja siyo ya Kongo, ni ya Handeni Mjini msiojua. Wananchi wa Kwedi, kule kwa Magono, hawawezi kupata dawa tukiwa na mpango huu. Kwa hiyo, twendeni tukafanye mapinduzi kwenye huu mfumo wa washitiri tuuangalie upya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, dada yangu Mheshimiwa Waziri namwamini sana, ni mchapa kazi mzuri, ana wasaidizi wazuri, ana wataalam wazuri wamemzunguka, twendeni tukakae chini, tufikirie namna ya kuisaidia MSD. Hii habari ya kukosa dawa wakati tuna fedha, kwa sababu dawa inapoagizwa, ikachelewa kuja kwa miezi tisa, kwa mwaka wakati fedha tunazo, huu ni umasikini mkubwa kabisa wa namna ya kuyatazama mambo. Hivi, huwa najiuliza kila siku, kama magari yanaweza yakaletwa Dar es Salaam, tukawa na bounded warehouse, yako hapo yamekaa, inashindikana nini kwa dawa tukawa na bounded warehouse za dawa?

Mheshimiwa Naibu Spika, asije mtu akachukulia kwamba habari ya bounded warehouse, naongelea godown, dawa zina utaratibu wake wa kutunza, ndiyo naongelea hivyo. Hayo maeneo ya kuhifadhi dawa, kwa nini tusiongee na wazalishaji, order tunazijua, maoteo ya vituo vyetu vya afya yote tunayajua. Tena katika eneo ambalo mnatakiwa mkaboreshe ni namna ya maoteo ya dawa yanavyofanyika, haya ndiyo yanayopelekea dawa zichomwe. Tunaagiza zaidi ya tunavyotumia, tuna-spend fedha nyingi zaidi ya tunavyotumia. Kwa ujumla kinachofanyika hapa ni mismanagement. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wataalam wetu msaidieni Waziri wetu, isije ikafika mahali tukisimama hapa ionekane tunaisema Serikali, tunawasema watu; tunawasema nyie wataalam, tunashindwaje kuji-organize? Fedha zinapoteapotea tu, tumelipa huku, tumelipa huku, nyingine zimechomwa, haiwezi kuwa nchi ya hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nahoji tena, kwa nini tusiwe na bounded warehouses za dawa na za vifaa tiba, kwamba mzalishaji akizalisha Urusi aje ahifadhi hapa Tanzania, mzalishaji akizalisha Ujerumani, aje ahifadhi hapa Tanzania ili MSD iki-place order saa mbili asubuhi, saa saba mchana dawa zimeshafika. Nini kinashindikana? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi. Naunga mkono hoja. (Makofi)