Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya

Hon. Iddi Kassim Iddi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Msalala

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia fursa hii nami leo kuchangia. Kwanza kabisa, nampongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya, hasa kwenye sekta hii ya afya. Nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya, nampongeza pia Naibu Waziri Mheshimiwa Dkt. Mollel kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya. Niseme tu kwamba, kwa kweli Waziri ana Naibu Waziri ambaye ni mchapakazi sana. Mimi nitakuwa ni mfano wa Wabunge ambao nimeshuhudia kazi kubwa ambayo anaifanya Naibu Waziri. Hafanyi yeye, ni kwa sababu Waziri anamtuma. Kwa hiyo, ni mtiifu kwake, anatii maelekezo yake na anakuja kutusaidia kwenye maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimefanya kazi ya ziara na Mheshimiwa Dkt. Mollel kwenye Jimbo la Msalala tukizungukia vituo vya afya na zahanati mpaka saa nne za usiku, na wakati huo tunafanya ziara hiyo toka asubuhi mpaka jioni alikuwa hajala, anakula korosho na maji. Ni huyu anajali afya za Watanzania, na hata sisi Wabunge anatusikiliza na kutufanyia kazi kubwa kwenye maeneo yetu hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nampongeza sana Mheshimiwa Katibu Mkuu na Naibu wake, dada yangu Grace, naye pia anafanya kazi kubwa sana. Nimekuwa nikikutana naye mara kwa mara akihangaika kutembelea miundombinu ya afya katika maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa, nampongeza Mheshimiwa Daktari Mama Samia Suluhu Hassan kwa wema wake wa kututendea sisi Watanzania katika sekta hii ya afya. Katika Jimbo la Msalala mimi naweza nikawa ni Mbunge ambaye nimepata bahati sana ya kupata fedha nyingi ambazo zinaenda kwenye vituo vya afya, kwenye zahanati, na ununuzi wa vifaa tiba kwenye maeneo hayo. Mama Samia Suluhu Hassan ametoa fedha, tumejenga, tumemaliza kituo cha afya na Mheshimiwa Dkt. Mollel nafikiri alifika baada ya kutumwa na Waziri, akakitembelea Kituo cha Afya Isaka, kimekamilika, kimeanza kutoa huduma.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo hivyo, tumekamilisha Kituo cha Afya Mwalugulu kinatoa huduma, tumekamilisha Kituo cha Afya Bulige kinaendelea kwenye ukamilishaji, Segese na chenyewe kipo kwenye hatua ya mwisho, Mwalugulu tayari, kwa hiyo, utaona zaidi ya vituo vinne vya afya vyote vinakamilika. Niendelee kuwapongeza sana wadau wakubwa, Barrick ambao kimsingi wameunga jitihada za Mheshimiwa Rais katika kukamilisha zahanati mbalimbali. Wametupatia fedha, tumeweza kukamilisha zahanati 34 kwa mpigo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, katika Jimbo la Msalala tuna vijiji 92 na tunavyozungumza hivi, matarajio yetu mpaka sasa tumebakiza maboma zaidi ya kumi na kitu tukamilishe idadi ya kila Kijiji kuwa na zahanati; na vituo vya afya vinane. Hapa tunapozungumza Mheshimiwa Waziri tunapata fedha nyingine, mmetuletea tena, tunaenda kuanza ujenzi wa vituo vya afya Kata ya Mwanase na Kata ya Busangi. Kwa hiyo, utaona zaidi ya zahanati 92 kwenye vijiji hivyo, utaona vituo vya afya vinaenda kuwa zaidi ya kumi, na pia kuna hospitali ya Wilaya ambayo na yenyewe tayari imekamilika, na niwapongeze sana. Nampongeza Mama Samia Suluhu Hassan, tayari ametuletea fedha kiasi cha Shilingi milioni 700 tunaendelea kumalizia majengo ya mama na mtoto, mmetuletea fedha tumejenga ICU, na mmetuletea vifaa vya ICU kwenye maeneo hayo. Kimsingi, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan katika Jimbo la Msalala, tunamwahidi 2025 kura zake nyingi za kutosha kabisa tutampigia kwa sababu katika sekta ya afya ameonesha ni namna gani anatujali Wana-Msalala. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, haitoshi, kwa kuwa tumepata zahanati zote, tumepata Vituo vya Afya, lakini namshukuru pia Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan, ametupatia fedha za kununua vifaa tiba zaidi ya Shilingi milioni 600. Tayari kwenye maeneo haya, tumepeleka baadhi ya vifaa tiba, lakini bado havitoshi. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri katika bajeti hii, chonde chonde, tunazo zahanati zimekamilika na hivi sasa bahati mbaya nyingine zimeanza kuota nyasi baada ya kukosa vifaa tiba. Fedha mliyotupatia ni kidogo sana, tumejaribu kuweka kwenye zahanati zaidi ya nne tu, lakini bado kuna zahanati zaidi ya 24 hazina vifaa tiba. Siyo vifaa tiba tu, hata watumishi wenyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Jimbo la Msalala, kuna upungufu mkubwa sana wa watumishi kwenye kada ya afya. Utaona kwa sasa tuna watumishi Zaidi ya 264, lakini tuna upungufu wa watumishi zaidi ya 500. Sasa namwomba Mheshimiwa Waziri atusaidie ili tuweze kupata watumishi, kwa sababu tumekamilisha maboma ya zahanati kwenye kila Kijiji, lakini changamoto iliyopo sasa hivi ni vifaa tiba na watumishi ambao wataenda kutusaidia katika kuhakikisha kwamba tunazifungua zahanati hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, niliposema kwamba Mheshimiwa Naibu Waziri alifika na amezishuhudia zahanati hizo kwa macho yake zipo, na sasa kwa wananchi kila siku wanaenda kufanya kazi ya usafi kwenye maeneo yale wakisubiri vifaa tiba na watumishi. Mbali na hilo, nashukuru sana wadau wetu wa Barrick na Serikali, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuona umuhimu, na namna gani anaweza kukabiliana na upungufu wa watumishi, tayari ametupatia fedha, shilingi milioni 400, tumejenga Chuo cha Afya. Hicho Chuo cha Afya sasa kinaenda kukamilika. Namwomba Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Dkt. Mollel amefika alipomtuma, amekiona ni chuo cha kisasa, ni chuo kizuri. Sasa niwaomba waende kukifungua chuo hicho ili tuweze kusaidia upungufu wa watumishi kwenye maeneo yetu hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua nafasi hii kuwapongeza sana Mheshimiwa Waziri, wametujali mno. Mheshimiwa Naibu Waziri nakupongeza mno, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan nakupongeza mno kwenye sekta ya afya. Niseme tu kwamba kumekuwa na changamoto, na hii siyo kubwa sana lakini ichukulieni kwa uzito wake. Amezungumza hapa Mbunge mwenzangu, kwenye baadhi ya vituo vya afya, kuna maduka ambayo yameanzishwa mle ndani. Ninapozungumzia maduka haya, nahusisha suala zima la dawa. Kumekuwa na maduka kwenye vituo vya afya, lakini maduka haya bado hayajaunganishwa na huduma hii ya NHIF.

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto kubwa utakuta maduka haya bado usajili wake ni tofauti na zahanati ni tofauti. Mtu mwenye kadi ya NHIF anapoenda pale hapewi huduma kwenye duka lile kwa sababu bado halijaunganishwa. Hivyo hivyo maduka haya kwa sababu tumeyafungua kimkakati kuweza kuhakikisha dawa zinapatikana kwenye maeneo yale, tuwape uhuru wa kuweza kufanya biashara. Wanapouza, wanapata fedha zile kwenda kwa mshitiri kama alivyozungumza hapa Mbunge mwenzangu hapa Mheshimiwa Reuben, bado kuna changamoto kubwa sana ya hawa washitiri.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba mtoe vibali vya kwenye maduka haya yaweze kununua dawa kwa haraka zaidi kwa sababu fedha tunazo kwenye baadhi ya maeneo ya zahanati, lakini changamoto, wanapopeleka fedha zile aidha MSD au kwa mshitiri, dawa zinapokosekana, fedha zile zinabaki kule na wananchi wanaendelea kuumia. Toeni vibali, process hizi ni mpaka mtu atoke hapa aende mpaka kwa RAS Mkoani, wapate kibali ndiyo waje waanze kufanya utaratibu wa kununua dawa. Sasa naomba hebu toeni utaratibu wa namna gani maduka haya ambayo yamo kwenye vituo vya afya hivi, ili yanapotaka dawa yaweze kwenda kununua maeneo yoyote yanapohitaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, naomba tuweke mfumo mzuri kwenye vituo vyetu vya afya vya ukusanyaji mapato. Fedha nyingi zinapotea. Vile vile namwomba sana Mheshimiwa Waziri waone ni namna gani basi wanaweza kuviwezesha hivi vituo vya afya au zahanati viweze kuwa na vibali vya kuajiri kwa mkataba. Leo hii tunapozungumza hapa, ni kwamba ukiangalia Hospitali ya Bugarama kuna changamoto kubwa sana ya watumishi kwenye maeneo yale. Leo tumepatiwa fedha na Mgodi ya Bulyanhulu pale tumeweza kununua machine moja ya x-ray na utra-sound. Hata Mdhibiti Mkuu wa Serikali amezungumza, vifaa vile tumevinunua muda mrefu, tumevitunza pale, havina watumishi, havina wataalam wa kuviendesha, vimekaa pale. Naomba sana tuleteeni wataalam.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nampongeza sana Mheshimiwa Waziri, wametuletea fedha nyingine tumenunua digital x-ray kwenye Kituo cha Afya cha Isaka, lakini bado na penyewe hatuna mtumishi. Sasa vifaa vya kisasa tunavyovileta kule, kama hatutatua changamoto ya ungufu wa wataalam kwenye maeneo yale, maana yake vifaa hivi vitakaa kwa muda mrefu na vitaharibika. Kwa hiyo, nawaomba sana, tuleteeni wataalam kwenye maeneo yale ili wananchi wetu sasa waweze kupata huduma kwenye maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sitaki kuzungumzia habari ya ambulance kwa sababu mmeshatuahidi kwamba kila Jimbo tutapata ambulance. Kiu yetu ilikuwa ni ambulance. Kwa hiyo, ninaamini kabisa ambulance zikija, mimi Mbunge wa Msalala ndio nitapewa kipaumbele namba moja, ili nije nipokee ambulance hiyo ikafanye kazi kwenye maeneo yetu hayo ili kuhakikisha kazi kubwa kwenye huduma ya afya inafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia la mwisho mtusaidie. Tunapozungumza habari ya huduma zinazotolewa kwenye vituo vyetu vya afya na zahanati, bado huduma haziridhishi kwenye maeneo yale, Mheshimiwa Dkt. Mollel aliona.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante kengele ya pili.

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Ninaunga mkono hoja kwa asilimia mia moja, endeleeni kuchapa kazi, tunawaamini. (Makofi)