Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya

Hon. Cecil David Mwambe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ndanda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi niungane na wengine wote kwanza kukushukuru wewe mwenyewe lakini kwa namna ya pekee kabisa kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa namna ambavyo ameamua kuipa nguvu sasa sekta ya afya. Niwapongeze sana pia Mawaziri, kwa maana ya Mheshimiwa Waziri Ummy pamoja na Naibu Waziri, watendaji wote wa Wizara ya Afya kuanzia wale wa juu kabisa mpaka wa chini ambao tuko nao kule vijijini kwa kazi kubwa wanazozifanya bila kuchoka usiku na mchana.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwapongeze kwa namna ya pekee Mawaziri hawa wanavyoshirikiana. Siku zote katika kazi zao ukimkosa Mheshimiwa Ummy ukimpata Mheshimiwa Mollel pale atatatua jambo lako kama ambavyo Mheshimiwa Ummy angeweza kulitatua, kwa hiyo niendelee kuwapongeza kwenye hili. Pamoja na hayo mimi ni mjumbe wa Kamati ya Afya na masuala ya UKIMWI. Tumeongea mengi sana kule ndani na nisingependa niyalete hapa kwa sababu tumeyaleta kwenye taarifa yetu na tulishakubaliana. lakini nina mchongo wangu wa ziada kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue pia nafasi hii kutoa pole sana kwa familia ya Mzee wetu Benard Membe kwa msiba mkubwa uliotokea huko. Wananchi wote wa Jimbo la Mtama, Mbunge wa Mtama pamoja na wananchi wa Chiponda kule Londo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mambo ambayo ningependa nishauri ili tuweze kuyafanya marekebisho ili Mheshimiwa Waziri waendee kutoa huduma zaidi kama ambavyo sasa hivi wanatoa huduma bora, lakini tunataka huduma bora zaidi kwenye Wizara yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza kabisa, hasa ukiangalia tone za Waheshimiwa Wabunge hapa ndani kuna haja kubwa sana kati ya wizara ya Elimu, Wizara ya Afya pamoja na TAMISEMI mkae na kuanza ku-define upya mipaka yenu ya kazi. Jambo hili limekuwa linatuchanganya sisi pamoja na wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana Waheshimiwa Wabunge wenzetu waliopata nafasi wanaongea Habari za zahanati ambazo ni huduma za afya za msingi chini kabisa, kitu ambacho naamini na nyinyi mna-level yenu. Kwa hiyo tunachanganya kati ya majukumu ya TAMISEMI, majukumu ya Wizara ya Afya lakini pamoja na majukumu ya Wizara ya Elimu. Kwa hiyo niombe kabisa tafuta nafasi mtusaidie ku-define hii, na ikiwezekana sasa tuweke mstari ulionyooka.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano ambao uko wazi kabisa, ninyi kwenu mnamiliki CMO, kwa maana Chief Medical Officer, lakini Chief Medical Officer hana mamlaka ya moja kwa moja kwa RMO. RMO naye hana mamlaka ya moja kwa moja kwa DMO. Nafikiri ananielewa Mheshimiwa Waziri; jambo ambalo linaleta mkanganyiko mkubwa, wakati ninyi Wizara ya afya mnatakiwa mfanye kazi kama Jeshi. Amri ikitoka juu kwa maana ya CMO iende mpaka chini kabisa kwa sababu ninyi ndio mnaoshughulikia masuala ya milipuko ya magonjwa pamoja na mengine. kwa hiyo niwaombe mkae na ku-define vizuri jambo hili ili CMO tumpe mamlaka lakini pia CMO awamiliki madaktari wenzie kwenye kada mbalimbali kushuka huko chini badala ya kuacha mfumo kama ambavyo uko sasa hivi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Tulikokuwa kwenye Kamati tulishauri suala la CCBRT pamoja na suala la Ndanda Hospitali; kwa maana ya wale madaktari wa CCBRT kuhakikisha wanapata mishahara yao kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kutoa huduma kwa watoto wenye mapungufu lakini pamoja na masuala ya ujumla ya ulemavu ikiwa ni pamoja na huduma za macho. Kwa hiyo wanastahili kupewa mishahara ili kuwapunguzia mzigo na kupunguza gharama kwenye eneo hili. Sawasawa na ilivyokuwa kwa Ndanda Hospitali, sasa hivi wameondolewa basket fund lakini wakati Hospitali yetu ya Kanda ya Mkoa wa Kusini inakua sehemu ambayo tunategemea sana kupata huduma ni Hospitali ya Ndanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tuone namna ambavyo tunaweza tukawarudishia basket fund au kutafuta namna yoyote ya kuwawezesha waweze kugharamia huduma waweze kutoa huduma ya mama na mtoto kwenye eneo hili kwa gharama nafuu kwa sababu sasa hvi yamekuwa malalamiko makubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Jambo jingine ni suala la Mfuko wa Bima ya Afya. Bima ya Afya sasa hivi inasuasua, lakini tukumbuke kwamba hawahawa Bima ya Afya ndio ambao walitoa fedha zao wakapeleka kuchangia kwenye ujenzi wa Hospitali ya Benjamini Mkapa pamoja na Muhimbili. Kwa hiyo tuone namna Serikali itakavyolipa madeni haya ili mfuko huu uweze kujiendesha wenyewe kwa sababu sasa hivi hawafanyi vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, Jambo jingine nakuomba sana Mheshimiwa Waziri ukaangalie taratibu au namna ya kufanya ili mifumo iwe inasomana. Sasa hivi kumekuwa na shida kubwa sana ya huduma za afya. Kwa mfano mgonjwa akitoka Hospitali ya Kanda ya Mtwara akatakiwa kuja kutibiwa Muhimbili Dar es salaam, atakapoleta kadi yake ya afya ikiwa ndani ya masaa 24 itaonekana kwamba imetumika; lakini hata vipimo alivyovifanya Mtwara, Hospitali ya Muhimbili Dar es salaam italazimika kuvirudia tena, kama ilivyo CT scan na vipimo vingine, kitu ambacho kinaongeza gharama kubwa sana. Ni bora hawa watu wenye kadi ya afya wanaweza kujigharamia, lakini watu wanaotumia cash ndani ya muda mfupi anarudia vipimo vilevile mara mbili ama mara tatu kutegemea na hospitali aliyokwenda.

Mheshimiwa Naibu Spika, Jambo jingine ambalo nataka kushauri, Tanzania sasa tumeendelea sana kwenye masuala ya afya; tuanzishe kitengo cha medical legal, kwa maana ya kutaka kusimamia taaluma ya madaktari. Siyo siri kwamba maslahi ya madaktari siyo mazuri sana, na ninaomba Wizara yako iboreshe. Kwa mfano sasa hivi wanapata asilimia 40 ya mgonjwa anayemhudumia akitokea kwenye Bima ya Afya, na ndiyo maana madaktari wanakuwa wanaamua wakati mwingine kufanya tiba ambayo si sahihi. Unaweza kukuta mama anauwezo wa ku-push mwenyewe lakini wanajua akiwa hospitalini akimchaji akimwambia kwamba inatakiwa afanyiwe scissor ya milioni moja na laki tano tuseme atapata pale pesa na yeye asilimia 40 ya hiyo pesa ili aweze kujikimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mbaya zaidi kuna madaktari wanaohamisha wagonjwa kutoka kwenye hospitali kubwa na kuwapeleka kwenye hospitali ndogo ambazo haziwezi kutoa huduma nzuri. Na Mheshimiwa Waziri mimi nitakuletea jina la daktari ambaye ninamfahamu amemuumiza ndugu yangu. Alimtoa Hospitali ya Regency akampeleka Hospitali ya Kinondoni, amefanyiwa operation na sasa hivi nakueleza ameridiwa kufanyiwa operation ya appendix kwa mara ya tatu kwa sababu daktari wa kwanza hakufanya majukumu yake sawasawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa watu kama hawa ambao wanaangalia zaidi kuhusu pesa badala ya kutoa huduma ndio ambao tunasema tuunde hii medical legal ili mwisho wa siku huyu naye awe na wajibu wa kushitakiwa kama alivyo mharifu mwingine yoyote.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua nia ya madaktari ni kutoa huduma, na nia yao hasa ni kuokoa maisha ya mgonjwa; lakini daktari anpofikia kwamba anataka sasa kuanza na kufanya biashara kwenye mwili wa mgonjwa kwa kumtoa hospitali kubwa anampeleka kichochoroni kwenda kumpa huduma ambayo haistahiki na baadaye mgonjwa yule anatolewa akiwa mahututi kwenye hospitali ya kichochoroni na kurudishwa tena kwenye hospitali kubwa, hili jambo halikubaliki. Tuyaangalie, tuwaongezee maslahi yao ili waweze kuacha kitu kingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo jingine, tunazo polyclinics nyingi sana zimezuka sasa hivi. Kunakuwa na emergency zinazotokea mitaani, tunaruhusu watu wa polyclinics waweze kusajiriwa na NHIF ili kuwaza kuzuia ajali kwa kupata huduma hapo wakati mwingine ama vifo vinavyotokea mitaani. Kwa hiyo tuyaone haya na tuone namna ya kuyasaidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kama ambavyo nimesema tangu mwanzo, kwamba mimi ni mjumbe wa Kamati ya Afya, kwa hiyo kwa vyovyote vile mchango wangu sehemu kubwa nilitoa nilipokuwa ndani ya Kamati. Nataka tu kuyasisitiza haya machache, tufanye definition upya ya kuona mstari mzima kutoka Wizara ya Afya, Wizara ya Elimu pamoja na Wizara ya TAMISEMI.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuangalie pia huo uwezekano wa kuwa na medical legal kwa ajili ya kuwasimamia madkatari ambo wanafanya vitu vya ovyo kwenye fani yao kama ilivyo kwa wengine; na ikiwezekana hata kabla ya kupata leseni nyingine madaktari hawa tukawapa record tracks zao za utendaji wao mzuri huko badala ya kufanya kwa uzoefu tunawapa leseni kila wanapofikia msimu wa ku- renew leseni wakati watu pengine wanayaacha.

Mheshimiwa Naibu Spika, jingine kubwa tuone namna ya kuhakikisha sasa Mfuko wa Bima ya Afya unawezeshwa kwa kulipa madeni yake; madeni yaliyoko Mhimbili, Benjamini Mkapa, na ninaamini pia madeni yaliyoko Bugando; tuhakiishe tunawalipa ili waweze kujiendesha wenyewe, kwa sabau mara nyingi mfuko wa afya tumekuwa tunaona wandaiwa na watu wengi tu huko chini wanashindwa kutoa huduma nzuri na kisingizio kinakuwa kwamba wao hawajapewa hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Nisisitize kuhusu kuwapa stahiki zao CCBRT, kama ambavyo tumeongea kwenye Kamati. Nirudie tena kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa kazi zake nzuri. Kama ambavyo nimesema, mimi ni mjumbe wa kamati kwa hiyo kwa vyovyote vile mchango wangu nilitoa kule ndani lakini nilitaka nikukumbushe hayo machache.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi kwenye majimbo yetu tunaona kuna vituo vya afya. Ukifika Jimbo la Ndanda sasa muda si mrefu tutapata huduma katika maeneo ya Lukuredi, Mpajani, Chilolo, Ndanda yenyewe na Ndanda na maeneo mengi. Kwa hiyo kwa vyovyote vile nikushukuru na kukupongeza, na ninakutakia kila la kheri kwenye utendaji wako. Na nikuhakikishie kwamba kwa sura ninazoziona za Waheshimiwa Wabunge hapa bajeti yako itapita tena kwa kishindo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi niliyopewa.