Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya

Hon. Seif Khamis Said Gulamali

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manonga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii ya kuweza kuchangia kwenye Wizara hii ya Afya.

Kwanza nipende kutumia nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa fedha nyingi ambazo amekua akizitoa hasa katika upande wa afya na Wizara zingine, lakini hasa kwenye Wizara hii ya Afya, ameleta mapinduzi makubwa sana. Tunaweza kuona kwa muda mfupi, tumeweza kununua mashine za MRI na zimeweza kusambazwa baadhi ya hospitali na hospitali zingine zitapatiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, haya ni mapinduzi makubwa ambapo hapo awali mashine hizi za MRI ulikuwa ukizipata katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na ilikuwa inabidi upate ratiba ya hospitali, kwamba kama Mgonjwa atatoka Igunga Choma Chankola anaenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, atafika pale hatoenda kupata moja kwa moja kipimo cha MRI, itabidi apangiwe muda, inawezekana baada ya mwezi mmoja au miezi miwili ndio aweze kupata kipimo hicho. Wakati akisubiria maana yake huyu mgonjwa amesafiri, amepanga guest, lakini pia hata hiyo huduma kuja kuipata inategemea kama Mwenyezi Mungu amemjalia kupata huo uhai wa kufika huo mwezi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwepo kwa mashine za MRI kuongezeka katika kanda mbalimbali inapunguza kufanya watu wetu kusafiri kwenda katika Jiji la Dar es Salaam lakini inapunguza usumbufu wa kulipa katika hotels, lakini pia inapunguza usumbufu wa kusubiri kwa muda mrefu. Tunapongeza sana juu ya jitahada hizi kubwa ambazo Serikali imezifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe tu kwamba Mheshimiwa Waziri Ummy anafanya kazi nzuri pamoja na Naibu wake, kazi zao ni nzuri sana na ndio maana unaweza kuona karibu Wabunge wote wanawapongeza kwa sababu ya namna ambavyo wanaweza kufanya kazi zao. Niwaombe tu na kuwakumbusha kwamba Mkoa wa Tabora ni mkoa mkubwa sana kijiografia, lakini sio tu mkoa mkubwa kijiografia, idadi ya watu pia ni mkoa wa tatu baada ya Dar es Salaam, Mwanza inafuata Tabora.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika taarifa ya Mheshimiwa Waziri sijaona mashine ya MRI akitupa pale katika Hospitali ya Tabora. Napenda kumwomba Mheshimiwa Waziri katika wind up yake ahakikishe basi anatupa matumaini kwamba ni lini Hospitali ya Tabora tutapata mashine ya MRI na ukitambua Tabora iko katika Ukanda wa Magharibi. Inategemewa na Mikoa ya Katavi, Kigoma na wakati fulani Singida. Kwa hiyo nimwombe Mheshimiwa Waziri azingatie Hospitali yetu ya Kitete pale kuweza kuipatia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nawapongeza kwa maboresho ambayo wamendelea kuyafanya kwenye hospitali za wilaya. Kupeleka fedha hospitali mbalimbali hata sisi pale Igunga wametuletea fedha kwa ajili ya Jengo la ICU, lakini na fedha ambazo wametupatia milioni 900 kwa ajili ya kuboresha hospitali yetu. Tunawapongeza sana na ambalo napenda kuzungumza ni kwamba nawapongeza kwa fedha walizotupa za vituo vya afya, tulipokea sisi milioni 500 kwa Kituo kipya cha Afya cha Ziba na milioni 150 kwa ajili ya ununuzi wa madawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo, niombe hii inawezekana wanashikirikiana na watafutaji wa fedha, wanashirikiana pamoja na watu wa TAMISEMI. Waendelee kutafuta fedha tuendelee kujenga vituo vya afya, mahitaji ni makubwa, Mkoa wa Tabora ni mkubwa, Jimbo letu pia la Manonga ni kubwa. Tunahitaji tupate hizo fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho napenda kusema vituo, zahanati, hawa wagonjwa wanaokwenda kwenye hospitali kubwa hizi wanasababishwa na kutokupata huduma kwa wakati katika zahanati au vituo vya afya. Kwa hiyo wanatumia madawa ya kienyeji, wanapokuja kujua wana tatizo ugonjwa umekua mkubwa inawasababisha kwenda kwenye hospitali kubwa za Muhimbili. Waboreshe au tumalizie maboma yaliyopo kwenye zahanati itasaidia kupunguza idadi ya wagonjwa kuja kwenye hospitali kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo ningependa kuzungumza ni masuala mazima ya upungufu wa watumishi. Tumekuwa na upungufu mkubwa wa watumishi na hii inasababishwa ni kwamba wanaomaliza wengi wametoka vyuo vikuu, hawa wa kwenye kwenda kwenye hizi zahanati wakati mwingine ni changamoto kwa sababu ya level ambayo wamefikia. Tunahitaji tuwekeze katika vyuo vya kati, kwanza vyuo vya kati ada zao ni ndogo, lakini pia hata kama tukiwakopesha ni rahisi kulipika. Kwa hiyo niombe sana Serikali iangalie suala hili la kuwekeza katika hawa watu wa rural medical officers, tupewe fedha nyingi sana kwa kuwakopesha na hawa wote tuwachukue twende kuwaajiri kwenye zahanati zetu. Tutaondoa tatizo la watumishi katika level za chini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine, Mheshimiwa Waziri kuna huu ugonjwa UTI ni changamoto sana. Kila ukienda hospitalini ukipimwa unaambiwa una UTI yaani hapo hapo UTI, hivi hii haina kuotesha kwamba nikae siku moja angalau niweze kujua na kama iko hivo je, hakuna chanjo? Tuweze kupata chanjo ya huu ugonjwa wa UTI, athari kubwa ziko kwa watoto wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda sasa kuzungumzia maboma yaliyojengwa kwa muda mrefu. Tutafute fedha tuyakamilishe. Majengo ya maboma haya yamekaa zaidi ya miaka saba au miaka naneā€¦

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Gulamali.

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, lakini mwisho niwapongeze wananchi Yanga kwa kazi nzuri wanayofanya. Ahsante sana. (Makofi)