Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya

Hon. Neema Kichiki Lugangira

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuchangia katika hoja hii muhimu ya hotuba ya bajeti ya Wizara ya Afya. Niungane na Wabunge wenzangu kuipongeza sana Wizara inayoongozwa na dada yangu mahiri kabisa Mheshimiwa Waziri Odo Ummy Mwalimu, lakini pia na Naibu Waziri Dkt. Mollel na viongozi wote wa Wizara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee kabisa naendelea kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo anaendelea kusisitiza kwamba kwenye Wizara hii ya Afya pamoja na kufanya tiba, lazima tuwekeze jitihada za maksudi kabisa kwenye kinga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na pongezi za Wizara nikiri wazi nimesikitika kwamba katika hotuba nzima ya Mheshimiwa Waziri na baada ya kusikiliza hotuba pia nimeipitia, sijasikia akigusia jambo lolote linalohusiana na suala zima la usalama wa chakula. Nasema usalama wa chakula kwa maana ya food safety. Mara kadhaa ndani ya hili Bunge tumekuwa tukisisitiza suala la usalama wa chakula ni dhamana ya uhai na maisha na afya ya Watanzania. Hatuwezi kuendelea kuweka maisha ya Watanzania rehani kwa kuruhusu suala la kudhibiti usalama wa chakula kwa maana ya food safety iendelee kuwa chini ya TBS kwa maana ya Wizara ya Viwanda na Biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni dhahiri TBS ina conflict of interest. Huwezi ukawa wewe ndio unatoa vibali kwa wafanyabiashara, halafu wewe ndio unaangalia udhibiti wa usalama wa chakula kwa maana ya food safety. Mheshimiwa Waziri ni shahidi pamoja na Naibu Waziri, hili jambo nimelisemea mara nyingi hata nikiwa kwenye Kamati ya Huduma ya Maendeleo ya Jamii iliyokuwa Huduma ya Maendeleo ya jamii na hata ndani ya Bunge lako Tukufu. Tukifanya rejea kwenye hansard tutakuta kuna kauli ya Serikali kupitia Wizara ya Afya ambayo iliahidi kwamba Serikali inafanyia kazi jambo la kuhamisha mamlaka ya masuala ya usalama wa chakula, kutoka kwenye TBS na kuja kwenye Wizara ya Afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa, pamoja na pongezi na jitihada kubwa za Sekta hii ya Afya kumekuwa na ongezeko kubwa la magonjwa ya kansa, kumekuwa na ongezeko kubwa na magonjwa yasiombukiza ambayo hayaeleweki, ambayo mengi yao yanachangiwa kwa kiasi kikubwa na ulaji wa vyakula ambavyo havina ubora wa usalama wa chakula. Ikiwa tunaweza kukidhi vigezo vya usalama wa chakula ili tupate soko la nje. Kwa mfano soko la EU, tunashindwa vipi kulinda na kukidhi na kuweka vigezo vya kulinda uhai wa soko la ndani ambalo ni zaidi ya wananchi milioni 60. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hili suala naongea kwa uchungu mkubwa kwa sababu tunaendelea kuweka maisha ya Watanzania rehani, wakati tunaweza kudhibiti ikiwa tu tutarudisha mamlaka ya udhibiti ya usalama wa chakula yarudi chini ya Wizara ya Afya, ambao kimsingi ndiyo awna dhamana ya kuhakikisha uhai wetu unaendelea kuwa salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawapongeza sana viongozi wa Hospitali zetu za KCMC, Bugando, Muhimbili, JKCI, Ocean Road, hapa Benjamini Mkapa, lakini naamini hata na wao watakubaliana nami, suala la usalama wa chakula limekuwa likiendelea kutotiliwa mkazo na maanani wakati linaendelea kutuwekea Watanzania hatarani. Haiwezekani tukaendelea kuruhusu suala la usalama wa chakula kwa maana ya food safety libaki chini ya TBS ambao kimsingi mimi binafsi ninao ushahidi dhahiri na nimeshasema hapa Bungeni. Kuna ndugu yangu aliwahi kuagiza bajaji, bajaji zile zilikwenda kufanyiwa ukaguzi na wahitimu wa food science, kwa nini? Kwa sababu pale TBS hawana kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri anafanya kazi kubwa sana, nimwombe sana atulinde Watanzania, tunaingiza vyakula hapa nchini, nani anaangalia usalama wa vyakula vinavyoingia. Tunazalisha chakula hapa nchini, nani anaangalia usalama wa chakula tunachokula? Nani anaangalia machinjioni usalama wa chakula, nani anaangalia mbogamboga na vyakula vinavyokuja sokoni iwapo chemical residue yake ipo vipi, lakini tunafanya hivyo kwa soko la nje, kwa nini tunashindwa kufanya hivyo kwa soko la ndani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ina maana wale wananchi wa nje wana haki zaidi kuliko sisi Watanzania zaidi ya milioni 60.

Pamoja na kwamba dada yangu nampenda sana, niweke wazi nisipopata kauli ya Serikali inayoridhisha kuhusu nini Serikali inakwenda kufanya kuhusu suala zima la kuhakikisha usalama wa chakula kwa maana ya food safety linarudishwa kwenye Wizara ya Afya, naondoka na shilingi ya mshahara wa Waziri mpaka kieleweke.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nashukuru sana kwa fursa hii. (Makofi)