Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mpwapwa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kutoa mchango katika hotuba hii ya Wizara ya Afya. Kwanza kabisa naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Rais, kwa ajili ya kazi nyingi nzuri ambazo zinaendelea kufanyika katika nchi yetu. Sisi watu wa Mpwapwa Mheshimiwa Rais, amefanya mambo mengi makubwa na hasa ktika sekta hii ya afya.
Mheshimiwa Spika, tumeopata shilingi milioni 900 katika ukarabati wa hospitali yetu ya wilaya. Mtakumbuka huko nyuma nimezungumza sana habari ya uchakavu wa ile hospitali lakini nashukuru sana Wizara imepata tarifa na imesikia. Sasa hivi ukarabati unaendelea lakini tunajenga jengo jipya la huduma ya mama na mtoto. Kwa hiyo, nina mshukuru sana Rais, kwa ajili ya kutusaidia hilo.
Mheshimiwa Spika, sio hilo tu, tumejenga jengo la ICU kwa gharama ya shilingi milioni 250 na pia tumepata vifaa katika jengo hilo tayari vimefungwa vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 400 na huduma zinaendelea pale. Pia, kwa muda mrefu hospitali hii ya Mpwapwa haikuwa na x–ray lakini leo nina furaha kuwaambia Bunge lako Tukufu kwamba sasa tuna digital x–ray na wananchi wa Mpwapwa wanaendelea kufurahia huduma za Serikali yao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika mwaka huu wa fedha pia tumefanikiwa kujenga au kumalizia maboma ya zahanati nane na zingine kazi zinafanyika tayari zinaendelea kumaliziwa na nyingine tayari zinatoa huduma kwa wananchi. Pia, tumeopata vituo vya afya viwili, kituo cha Iwondo na kingine tumejenga Matomondo. Vituo hivi vimejengwa maeneo ya Kimkakati, maeneo ambayo yako mbali sana na mjini.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri amesema katika mwaka huu wa fedha wamepanga kununua ambulance zaidi ya 700. Niombe Mheshimiwa Waziri, utukumbuke na sisi wa Mpwapwa, tuna vituo vitatu kwa ujumla, kituo cha Mima, Iwondo na Matomondo vituo ambavyo viko kwenye maeneo ya kimkakati. Lakini pia tuna hospitali yetu ya wilaya haina gari ya kubebea wagonjwa, kwa hiyo, tukumbuke kwa ajili ya kupata magari ya kubebea wagonjwa.
Mheshimiwa Spika, pia Mheshimiwa Waziri nikushukuru wewe binafasi, umekuwa moja ya Mawaziri wanaofanya kazi zao kwa umakini sana. Nichukue fursa hii kukupongeza, na hata ukisoma ripoti yako unawea kuona umegusa kila eneo hata tunaposimama kuchangia tunasema kusema kweli tunataka kuweka mkazo tu lakini kwa kweli umejaribu kugusa kila eneo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nianze kuchangia katika eneo la matibabu ya wazee, Mheshimiwa Waziri, umezungumza katika ukurasa wa 55 habari ya kuongeza dawa kwa ajili ya wazee. Lakini kuboresha huduma zao, lakini nikwambie kwamba bado hatujawa na mkakati thabiti wa namna ya kuwahudumia wazee kwa sababu wiki mbili zilizopita nilimpeleka mpiga kura wangu mmoja mwenye umri wa miaka zaidi ya 70. Nilipofika pale hospitali nilikuta kuna mabango yameandikwa mpishe mzee asipange foleni, kuna msamaha wa wazee. Mheshimiwa Waziri, lakini kusema kweli hayo mambo yameandikwa lakini practically hakuna kitu kinachoendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wazee wanateseka sana kwa sababu ya umri na uchumi wao mdogo basi wanateseka na wengi wanafariki kwa sababu ya kuteseka na kuchelewa kupata matibabu. Mheshimiwa Waziri, ningekushauri jambo hili mliangalie upya ikiwezekana mje na mpango mahususi au sera mahususi ya kuwatibu wazee wetu.
Mheshimiwa Spika, wazee wetu ni wengi wamefanya kazi katika Taifa hili kwa uaminifu mkubwa lakini leo inaonekana kama hatuwajali kabisa. Kwa hiyo, mzee yule hata tulipofika issue nyingine ikawa ni dawa ile aliyotakiwa kupata hakuna. Nikupongeze nimeona mmeongeza dawa tano kwa ajili ya wazee labda hilo litatusaidia. Pia shida iko pale kwamba dawa hazipo. Mheshimiwa Waziri, uje na sera maalum kwa ajili ya wazee hawa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine, ambalo ningependa kukusisitiza pia ni uhaba wa dawa. Nimeona kwenye ripoti umezungumza mikakati ya kuongeza dawa hospitali lakini kwa kweli hospitalini bado kuna shida ya dawa. Kama nilivyosema watu wengi hawawezi kunua dawa nje ya maduka private. Kwa hiyo, mtu anakwenda hospitali na bima yake anaadikiwa dawa inakuwa hamna, akienda nje bima haiwezi kutumika, yako maduka ambayo hayakubali bima. Kwa hiyo, yule mtu anarudi nyumbani hana dawa kwa sababu tu hana hela ya kununua dawa.
Mheshimiwa Spika, ningeomba sana Mheshimiwa Waziri, yale maduka ambayo yako ndani ya hospitali yapate dawa zote ili wananchi wetu wakifika pale waweze kuhudumiwa vizuri. Shida ya dawa bado ni kubwa pamoja na juhudi nyingi ambazo Serikali inafanya na wewe Mheshimiwa Waziri lakini dawa bado ni chache.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni huduma zisizolirisha katika hospitali zetu. Kuna wafanyakazi wachache ambao bado hawana lugha nzuri kwa wagonjwa. Mfano, hospitali yangu ya Wilaya ya Mpwapwa bado kuna malalamiko mengi kuhusiana na uhafifu wa huduma zinazotolewa pale. Watu wanajibiwa vibaya, watu hawatibiwi kwa wakati, kuna vurugu nyingi. Mheshimiwa Waziri ningeomba jambo hili ikiwezekana watumishi hawa wa afya wapate semina za mara kwa mara ili kuwafundisha maadili ya kazi zao. Kazi ya kuwatibu watu ni kazi ya wito inahitaji upendo, inahitaji mtu anaejitambua vizuri.
Mheshimiwa Spika, pamekuwa na watu ambao ni wajeuri, mtu anakwenda anaumwa anajibiwa vibaya wakati mwingine wanadaiwa rushwa, wanadaiwa fedha kwa mambo ambayo hayatakiwi kulipiwa. Kwa hiyo, kuna fujo nyingi kwenye maeneo haya ya kutolea huduma na kelele hizi zinachafua mahusiano bora au mahusiano mazuri na Serikali na wananchi wao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo nirudie kumshukuru Mheshimiwa Waziri wetu wa Afya kwa kazi nzuri anayoendelea kuifanya na naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)