Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

Hon. Tunza Issa Malapo

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nami pia naungana na Wabunge wenzangu wa UKAWA kuona kitu kinachofanywa kulizuia Bunge hili lisioneshwe live si sahihi. Kwa sababu sisi ni wawakilishi wa wananchi, tumetumwa na wananchi kuja hapa kuwatetea, kuwasimamia na wanatamani watuone. Sijui hata huyo aliyeanzisha huu mjadala Bunge lisioneshwe live alichukua maoni kutoka wapi. Ama aliamka asubuhi kwa matakwa yake binafsi akaamua Bunge lisionehswe live. Mjue kabisa hamuwatendei haki wananchi, kodi zao mnachukua lakini hamtaki kuwatendea haki. Wananchi wanajua si kwamba ni wajinga kama mnavyowafikiria, kwa hiyo, hilo mkae kabisa mnalijua.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakuja kuchangia…
TAARIFA...
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naipokea taarifa hiyo kwa mikono miwili.
TAARIFA...
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Malapo, naomba uendelee.
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa niende moja kwa moja kuchangia kwenye TAMISEMI na naanza na elimu. Kwa masikitiko makubwa sana, kama kila siku ninavyozidi kusema mimi ni Mwalimu lakini tunapozungumzia suala la elimu, tunakuja humu ndani tunajitutumua kusema kwamba tumedahili wanafunzi wengi, tumedahili lakini output yake itakuwaje? Hilo ni swali la msingi la kujiuliza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia kitu cha kusikitisha, Mkoa wa Mtwara, wakati mnazungumzia Walimu hawana nyumba, lakini nataka kuwaambia katika ripoti ya Mkuu wa Mkoa ametuambia shuleni kuna upungufu wa viti elfu moja mia mbili kwenda juu. Kwa hiyo, Mwalimu huyo amelala sehemu mbaya, akienda shuleni pia hana sehemu ya kukaa. Tunavyolalamikia watoto wanakaa chini pia kuna Walimu wanakaa chini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, afya. Tukienda kwenye suala la afya kwa Mkoa wa Mtwara ni majanga. Natoa mfano mkubwa wa kusikitisha, ukienda Mtwara Vijijini kwenye Kituo cha Afya cha Nanguruwe mganga wa pale anatamani afunge kile kituo kwa ukosefu wa maji. Maji hayo pesa yake ilishatolewa shilingi milioni tano kurekebisha hitilafu iliyotokea ila kuna wajanja wachache wamekula. Kwa bahati mbaya hata ukienda kwa Mkurugenzi, sijui anamwogopa nani, hataki kutoa ushirikiano wowote.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri alifuatilie suala la Kituo cha Afya Nanguruwe kwa sababu kituo kile kinahudumia watu wengi lakini mazingira yake ni mabovu, hakuna matundu ya vyoo ya kutosha, hakuna dawa, hakuna maji, wananchi wa pale kila siku wanalia. Naomba akifuatilie kituo kile ili tujue mwisho wake ni nini, watu wa pale wapate haki yao ya msingi kwa sababu na wao ni Watanzania wa kawaida.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakuja kwenye asilimia kumi kwa ajili ya akina mama na vijana, hili suala tunaomba lipewe kipaumbele. Ukienda Mtwara kwa tafiti zilizofanywa inaonesha asilimia 54 ya nyumba zinalelewa na akinamama kwa sababu labda waume zao wamefariki au matatizo ya ndoa yalitokea, kwa hiyo, wanahitaji wawezeshwe. Nami nasimama hapa kwa uhakika kabisa kusema kwamba wanawake na vijana wa Mtwara ni watu ambao wako tayari kutafuta maendeleo wanachokosa ni kuwezeshwa tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie Wenyeviti pamoja na Madiwani. Unamlipa posho Mwenyekiti wa Mtaa Sh. 20,000 kwa mwezi tena si guarantee, kuna mwezi anapata, kuna mwezi hapati. Hata hivyo, tukumbuke kukitokea matatizo yoyote katika mtaa, Mwenyekiti ndiye wa kwanza kufuatwa na wananchi wake kwenda kulalamikiwa, tujiulize Sh. 20,000 anafanyia kitu gani? Diwani kwenye kata ana majukumu mengi mazito, posho mnayompa inamsaidia?
Mheshimiwa Naibu Spika, tujiweke tungekuwa ni sisi, wewe Mheshimiwa Waziri sasa ndiyo ungekuwa Diwani unalipwa ile posho wanayolipwa ungeweza kuendesha maisha yako? Hii inaweza kuwapelekea wale watu kufanya mambo ya kupokea ama kutamani kupokea rushwa kwa sababu ni binadamu, wanahitaji kuishi vizuri. Naomba tuwaangalie kwa sababu Udiwani ndiyo kazi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tukija kwenye suala la masoko ambapo katika Halmashauri ya Mtwara Mikindani ni chanzo pia kikubwa cha mapato. Kwa masikitiko makubwa nimetembea kwenye masoko manne ya pale hakuna soko hata moja lenye choo cha uhakika. Wananchi pale wanatozwa ushuru, wafanyabiashara wale wanatozwa ushuru, wanalipa kila siku lakini hatuna choo cha uhakika kwenye soko lolote, naongea kwa uhakika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine, tuna vizimba vya takataka vimejengwa kwa masikitiko makubwa, sijui hata huyo injinia alikuwa anafikiria nini, kuna kizimba kipo mtaa wa Magomeni, chini yake limepita bomba la maji kubwa na maji yanamwagika pale, takataka zinaoza, funza wanatoka, wananchi wapo karibu lakini tunaambiwa Injinia wa Manispaa amekuja kujenga pale wakati anajua chini limepita bomba. Tunaomba vitu hivi mfuatilie kwa sababu sisi kila tukisema inaonekana tunaongea kisiasa, hatuongei kisiasa, tunawaongelea wananchi wale wanaoendelea kupata shida kila siku. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nazungumzia suala la maji katika Mkoa wangu wa Mtwara. Ukienda Jimbo la Nanyamba kuna shida kubwa ya maji. Sisi kule tunasema watu wanatumia maji ya kuokota. Ukisikia maji ya kuokota maana yake mtu anakuwa amechimba kisima cha chini halafu anaelekeza mifereji, yale maji ya mvua yanayotiririka barabarani yanaingia kwenye kisima. Mwisho wa siku huyu mwananchi anakuja kunywa yale maji, tutaepukaje kipindupindu, tutaepukaje magonjwa ya matumbo yanayosababisha dada zetu wasishike ujauzito kwa sababu vizazi vinaharibiwa? Hali hii hatuitaki na tunaomba irekebishwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa sababu ya muda, nataka niulize, Serikali ya Magufuli inafanya vizuri, kwa nini inaogopa kuwa transparency? Kwa nini haitaki kuonekana kama kweli inafanya vizuri, maana yake ina shida. Kama ingekuwa inajiamini Bunge lingeonekana live. Ninachosema, Serikali ya Magufuli haijiamini na ndiyo maana haitaki wananchi waone kinachoendelea. Hilo Bunge analosema linaoneshwa saa nne mimi jana nimeangalia, hakuna kitu, sasa mtu hapa anakuja kutuambia linaoneshwa, tuwe serious.