Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya

Hon. Esther Lukago Midimu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya

MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuongea, kwanza kabisa nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anazozifanya anaboresha miundombinu ya afya.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais amejenga zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya na hospitali za mkoa. Mheshimiwa Rais amefanya kazi nzuri, Mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hassan hayuko tayari watu wake wafe kwa kukosa matibabu. Mama yupo vizuri tunampongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, cha kwanza hapa duniani ni afya, bila afya hata ukiwa na mamilioni ya pesa haisaidii. Tunampongeza Mheshimiwa Rais kwa kuboresha afya ndio maana vifo vya mama na watoto vimepungua.

Nampongeza Mheshimiwa Waziri Ummy na Naibu wake kwa nzuri wanazozifanya. Mheshimiwa Waziri anafanya kazi nzuri, hotuba yake ni nzuri, namjua yeye ni mchapakazi, nina imani atasimamia hotuba yake ambayo imesheheni matumaini ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naendelea na pongezi kwa Mheshimiwa Rais kwa kuboresha Hospitali ya Muhimbili. Hospitali ya Muhimbili, sasa hivi inafanya operesheni ya kichwa, inapandikiza figo, inafanya operesheni ya moyo. Hata wagonjwa kutoka nchi za nje wanakuja kutibiwa. Hiyo ni kazi ya Mheshimiwa Samia Suluhu, Mama yetu ametuheshimisha, tuko vizuri Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuboresha huduma ya matibabu ya kansa Bungando. Mwaka juzi tulisimama hapa Wabunge wa Kanda ya Ziwa tukaomba matibabu ya kansa yasogezwe Bugando kwa sababu wagonjwa wengi wa kansa wanatoka Kanda ya Ziwa. Mheshimiwa Rais alisikia kilio chetu sasa hivi matibabu yanatolewa hapo karibu, hawawezi kuhangaika tena kwenda Dar es Salaam kutibiwa. naishukuru Serikali kwa kuanzisha utafiti wa kuweza kujua ugonjwa wa kansa unasababishwa na nini Kanda ya Ziwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naendelea na pongezi kwa Serikali imetujengea hospitali ya mkoa, lakini pia tuna jengo la mama na mtoto, Mheshimiwa Ummy analifahamu yeye ni mwanzilishi. Bajeti yake ni bilioni 5.7, jengo hilo limefikia asilimia 85. Tunamwomba Mheshimiwa Ummy akija kutoa majibu hapa, atupatie bilioni 1.7 ili tuweze kukamilisha hilo jengo la ghorofa na ni zuri la kisasa. Hiyo ni kazi ya Mama Samia Suluhu, hongera sana Mama yangu kwa kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naendelea na pongezi kwa majengo yafuatayo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imetujengea jengo la kutakasia vifaa, ufuaji wa nguo, nyumba mbili za watumishi, nyingine ni three in one, lakini pia katika hospitali yetu hiyo tumeletewa CT scan. Tulikuwa tunahangaika na kipimo hicho, watu wa Mkoa wa Simiyu walikuwa wanaenda kupata hicho kipimo Mwanza, lakini sasa hivi wanapata Mkoani Simiyu, hiyo ni kazi ya Mama Samia Suluhu, Mama yuko kazini. Ahsante sana Mama kwa kazi nzuri kwa kujalia afya za watu wako. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ombi, hospitali yetu ya mkoa haina uzio kabisa na mwaka jana nilisimama nikasema hospitali haina uzio. Upande wa kushoto tumepakana na mlima, upande wa kulia tumepakana na barabara ya lami. Mlimani kuna vichaka vichaka, hospitali ikikosa uzio, utoroshwaji wa vifaa tiba na madawa ni rahisi sana. Mtu anaweza akasomba akaenda kuficha mlimani, halafu baadaye usiku anavisafirisha. Pia na hospitalini wanaenda wagonjwa wa aina mbalimbali. Kuna mwingine anaweza akaenda amechanganyikiwa wa afya ya akili akakimbilia barabara akagongwa gari. Naomba Serikali itujengee uzio, Mheshimiwa Ummy mtani wangu ameinisikia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia hospitali hiyo hiyo haina wodi za kulaza wagonjwa. Hatuna wodi ya wanaume, hatuna wodi ya wanawake na hatuna wodi ya watoto. Naiomba Serikali iweze kutujengea halafu na jengo la bima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la hospitali ya mkoa halijapimwa, halina hati. Naiomba Serikali iweze kupima eneo hilo halafu iweze kutupatia hati miliki. Katika hospitali yetu ya mkoa tuna upungufu wa watumishi. Watumishi walipo ni 231, upungufu wa watumishi 437, specialist wa nne, specialist wanaohitajika 21, Wauguzi waliopo 102 upungufu 97, upungufu wa Madaktari 27, upungufu wa Wafamasia 12. Tunaomba Serikali ituletee watumishi wa kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niendelee kumpongeza Rais wetu katika hospitali zetu za wilaya ametuletea X-Ray. Kama unakumbuka nilisimama hapa mwaka jana nikaomba X-Ray kila wilaya. Sasa hivi Serikali yetu ni sikivu imeshaleta X-Ray, hata kama mtu akipata ajali sasa hivi hawezi akakimbia kwa waganga wa kienyeji, atatibiwa hapo hapo, matatizo yatagundulika mapema. Ila naomba sasa wataalam wa mionzi hatuna. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, tuna Hospitali ya Somanda wakati hospitali ya mkoa hawajaanza kujenga ile hospitali ilipandishwa hadhi ikawa hospitali teule ya mkoa. Hiyo hospitali ni ya muda mrefu, majengo yamechakaa, tunaomba pesa ili yale majengo yaweze kukarabatiwa.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo nakushukuru sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)