Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya

Hon. Noah Lemburis Saputi Mollel

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Arumeru-Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya

MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Wizara hii ya Afya lakini nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema aliyetupa uzima kuwepo katika Bunge hili.

Nikushukuru na wewe kwa jinsi ambavyo unaendelea kuendesha Bunge lako kwa umakini na umahiri mkubwa sana. Niendelee kutoa shukurani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo anaongoza Taifa letu, lakini kuhakikisha kwamba wananchi wake wanaendelea kupata afya njema kwa kutoa vifaa tiba, kujenga majengo, zahanati, vituo vya afya na hospitali za wilaya na hata za mikoa na kuleta vifaa tiba mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kweli Mheshimiwa Rais katika kipindi hiki ametuheshimisha sana sisi Wabunge, kwa sababu ametuletea miradi mikubwa mpaka ukiwa jimboni unakosa uelekee upande upi katika kukagua miradi. Kwa kweli tunampongeza sana Mheshimiwa Rais. Pamoja na pongezi zote nilizozitoa kwa Wizara ya Afya kwa maana ya Waziri wetu Ummy Mwalimu pamoja na Naibu Waziri wake pamoja, Katibu MKuu na Naibu Makatibu Wakuu na Wizara nzima kwa ujumla na Madaktari wote hapa nchini lakini bado tunasema barabara ndefu haikosi kona. Kwa hiyo, katika yale ambayo tunayo kama Wabunge na hasa mimi kama Mbunge wa Jimbo la Arumeru Magharibi, kuna mambo ambayo pia napenda tujaribu kushauri ili basi mwisho wa siku hili gurudumu liweze kusonga mbele sisi kwa pamoja kwa maana ya kuwahudumia wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa Serikali katika Jimbo langu la Arumeru Magharibi tumejengewa vituo vya afya karibu vitatu. Tumejengewa zahanati nyingi kumalizia nguvu za wananchi, bado zingine hazijaisha, lakini kwa kweli hizo ni shukrani ambazo naweza kusimama katika Bunge hili na kujivunia kwamba natoa shukurani nyingi sana sana kwa Serikali yetu chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema barabara ndefu haikosi kona. Kwenye Jimbo la Arumeru Magharibi kulikuwa na hospitali ambayo naiongelea kila siku katika Bunge hili ya wilaya. Imepandishwa hadhi toka 2012 na Rais wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Jakaya Kikwete. Hospitali hii ilipandishwa hadhi, Rais aliahidi pia kwamba lami kilometa 2.8 iwekwe lakini pia majengo yaongezwe, hospitali hiyo haina jengo la wagonjwa wa nje kwa maana ya OPD, hospitali hiyo haina X- Ray, hospitali hiyo haina jengo la mochwari. Hospitali hiyo haina chochote na tangu Serikali ianze kuboresha hospitali za wilaya, kwa kweli sisi hasa katika Jimbo langu la Arumeru Magharibi hatukuweza kubahatika kupata hizo fedha za kwa ajili ya kuhakikisha hospitali hiyo inakaa katika mkao sasa wa kuitwa hospitali ya wilaya.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa suala hili liko katika Wizara mbili kwa maana ya TAMISEMI na vile vile katika Wizara ya Afya kwa maana ya upande wa vifaa tiba. Nalizungumzia kwa ujumla wake ili Mheshimiwa Waziri wetu wa Afya aweze kuona namna gani atahakikisha tunapata x-ray, lakini pia tunapata na vifaa tiba vingine vyote ambavyo vinatakiwa katika hospitali hiyo. Upande wa majengo, TAMISEMI nao wataona jinsi ambavyo wataboresha hospitali ile kwa sababu sasa umefika wakati muafaka hata katika bajeti nimeona wameiangalia hospitali hiyo na nashukuru sana.

Mheshimiwa Spika, kuna suala la kutoa huduma kwa wazee na watoto; suala hili la kuhudumia wazee wetu halijakaa vizuri kabisa. Kwa bahati nzuri Mheshimiwa Ummy na Dkt. Mollel, ni Wabunge wenzetu, hiki kilio nadhani na wao wanakipata mara kwa mara. Wazee wetu wanakwenda pale hospitalini, wanaandikiwa barua wanakuwa labda na hiyo sijui ndio vitambulisho wanapewa halmashauri, lakini wanapoenda pale wanaambiwa dawa zenu hazipo.

Mheshimiwa Spika, wale wazee wanateseka, kwa kweli wazee wetu wanateseka. Kwa hiyo, naomba kuishauri Serikali kama itawezekana na naomba iwezekane kwa sababu wale wazee wametumika Taifa hili kwa umri wao wote huo ambao mmeuona na sisi sote siku moja tutakuwa wazee na hapa tunaelekea kuwa wazee sasa. Kwa hiyo tunahitajika kuhakikisha kwamba tunaanzisha msingi wa kuendelea kuwatunza wazee wetu.

Mheshimiwa Spika, niombe Wizara iangalie namna ya kuwasaidia wazee. Aidha, wawape kabisa CHF moja kwa moja ili ijulikane kwamba wakienda pale, basi Serikali ndio inatoa hiyo ruzuku kwa wazee. Hebu tulione hili kwa kweli kwa sababu linaumiza na linatesa sana wazee wetu.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni suala la upungufu wa watumishi. Kuna upungufu wa watumishi katika zahanati zetu, hospitali zetu za wilaya na na kadhalika. Kwa hiyo, naomba waliendelee kuliangalia suala hili pamoja na kuishukuru Serikali kwamba imetangaza ajira hizi za juzi, lakini bado upungufu ni mkubwa sana katika hospitali zetu.

Mheshimiwa Spika, lingine ni suala la ununuzi wa madawa na vifaa tiba. Katika sehemu hii inatakiwa sana Mheshimiwa Waziri wakae waangalie namna ya kuhakikisha kwamba watakuja na strategy mpya kwa sababu, kwa mfano, juzi katika Jimbo langu la Arumeru Magharibi, Halmashauri ya Arusha DC, Serikali imetoa fedha kwa ajili ya kununua vifaa tiba tangu Mwezi wa Tisa mwaka jana. Mshitiri anasema kila siku hakuna vifaa, hakuna vifaa mpaka juzi mwezi Machi ndio vifaa vimekuja kupatikana, can you imagine? Ina maana hiyo variation lazima bei zinapanda, kuna vitu ambavyo vitakuwa havijanunuliwa na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili eneo la Mshitiri na kuimarisha MSD, hebu wakae vizuri waangalie kwa umakini na umahiri zaidi, kwa sababu kwa kweli tutatesa wananchi wetu na hata ukizingatia Ilani ya Chama cha Mapinduzi katika ukurasa wa 138 imeeleza kinaga ubaga na dhahiri shahiri kwamba, naomba kunukuu; “Kuimarisha Mfumo wa Mshitiri ili kuhakikisha kuwa bidhaa za afya zinapatikana kwa uhakika na kwa gharama nafuu katika ngazi zote za huduma”. Hiyo ni Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya 2020-2025.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa katika suala la upungufu wa magari katika Halmashauri yetu ya Arusha DC, Jimbo la Arumeru Magharibi. Tunaomba Serikali itakapokuwa imekamilisha ugawaji wa ambulance, Jimbo la Arumeru Magharibi tuna zahanati nyingi, tuna vituo vya afya vingi, jiografia yake imekaa katika mazingira ambayo kwa kweli ni changamoto sana. Kwa hiyo naomba sana watukumbuke katika kupata gari la wagonjwa. Hasa gari mbili tukipata angalau itakuwa imetusaidia sana na imetufaa sana kuwaokoa wale wananchi katika kuhakikisha wanapata huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho; suala la maadili kwa Madaktari wetu, lakini kabla sijasema maadili, niombe Wizara pia muangalie namna ya kuwawezesha Madaktari na Wauguzi katika mishahara yao, posho zao na mambo yote yanayowahusu. Naomba sana waangalie hili kwa sababu yawezekana pia katika changamoto tunazozisema inawezekana na yenyewe ikawa ni changamoto kubwa. Kwa sababu mtu anapochoka hata hapati overtime, hapati chochote anajitoa, ana-toil lakini mwisho wa siku hapati stahiki yake ambayo anastahili. Kwa hiyo naomba sana tuangalie Madaktari wetu, wanaoshika roho zetu, wanaoshika afya ya Taifa hili, ili waweze kupata stahiki zao kwa kiwango kinachotakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa muda naunga mkono hoja. (Makofi)