Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya

Hon. Hawa Subira Mwaifunga

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na mimi kwa kunipa nafasi niweze kuchangia Wizara hii ya Afya. Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kunijalia afya ya kuweza kusimama tena kwenye Bunge hili nikichangia katika Wizara hii ya Afya.

Mheshimiwa Spika, naomba nitoe ushauri kwa Serikali kupitia Wizara hii ya Afya. Kumekuwa na ujenzi wa hospitali za Wilaya, kumekuwa na ujenzi wa vituo vya afya, kumekuwa na ujenzi wa zahanati nyingi sana ambazo ukipita kwenye Halmashauri mbalimbali hospitali hizi za Wilaya hazifanyi kazi, vituo vingi vya afya havifanyi kazi, zahanati nyingi hazifanyi kazi kwa sababu hazina vifaatiba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo mimi niombe sana, nafikiri kwamba hii kasi ya Mheshimiwa Rais anayoenda nayo ya kuweka miundombinu ya afya muende nayo na nyinyi sasa Wizara ya Afya kwa kupeleka vifaatiba pamoja na Madaktari na Wauguzi katika hospitali zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa hivi ukizunugumza kwamba kuna hospitali za Wilaya, kuna vituo vingi vya afya kama havifanyi kazi, wananchi hawa hawawezi kuona tija ya hivyo vituo vya afya na hizo hospitali za Wilaya ambazo zinajengwa. Kwa hiyo, niombe sana kupitia Bunge lako Tukufu, Wizara hii sasa ijikite zaidi katika kupeleka vifaatiba, kupeleka Madaktari pamoja na Wauguzi ili majengo haya yaweze kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, majengo ni mengi mno tumeyaona na tumeshuhudia lakini hayana vifaatiba wala hayana Madaktari, maeneo mengine yanavyo vifaatiba lakini hayana wataalam. Unafika unakuta mitambo imefungwa hapo, iko vizuri imekaa sawa sawa hakuna wataalam. Unauliza huu mtambo umefungwa lini? Una mwaka mzima hakuna mtaalam, huu mtambo umefungwa lini? Una miezi sita hakuna mtaalam.

Mheshimiwa Spika, tumekwenda Halmashauri ya Sumbawanga Mjini kuna kifaa kipo zaidi ya miaka miwili sasa hakijawahi kufanyakazi wala kufunguliwa kule kwenye makaratasi. Sasa hii ni kitu gani? Mimi naomba tuwe tunaangalia zaidi vipaumbele vyetu hasa kwenye afya ni kitu gani ili tuweze kusaidia wananchi wetu, tuendane sawa na kasi ambayo anakwenda nayo Mama ya kuhakikisha kwamba watu wanapata huduma za afya, basi huduma za afya zipatikane kwa tija inayohitajika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nizungumzie suala zima la dawa. Mheshimiwa Waziri amekuwa mara nyingi sana hapa akizungumzia suala la dawa, kwamba sasa hivi hakuna shida ya dawa. Inawezekana hakuna shida ya dawa lakini dawa zinazotakiwa katika maeneo yale ndiyo zinazokosekana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, unakuta kuna hospitali haina panadol, unashangaa mbona Waziri kasema pale kuna madawa, hata panadol kweli hakuna? Lakini utakuta kuna dawa zinawekwa kwenye hospitali husika hazina hata watumiaji mpaka zina expire. Kwa nini tusiangalie uhitaji wa dawa zinazohitajika kwenye hospitali zetu na kwenye maeneo yetu ili tupeleke zile dawa zinazohitajika, wananchi waweze kupata huduma ya dawa kuliko ilivyo hivi sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumetembea kwenye hospitali mbalimbali tumekuta dawa zime-expire ziko pembeni zinatakiwa zitupwe lakini ukiwauliza naomba paracetamol hakuna, naomba cetirizine hakuna. Sasa tunaomba sana muangalie ni dawa gani ambazo zinahitajika kuchukuliwa ili wananchi wetu waweze kupata huduma inayostahiki kuliko ilivyo hivi sasa kupeleka tu dawa bora mmepeleka dawa mwisho wa siku dawa zile hazifanyi kazi na matokeo yake zinaharibika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kuzungumzia kuhusiana na suala zima la maradhi haya ya kansa. Hili jambo limekuwa ni janga tena ni janga kubwa sana hasa kwetu sisi wakina mama. Kansa hasa za shingo ya kizazi zimekuwa ni nyingi mno, kiasi kwamba mwanamke mpaka uje ujigundue kwamba una kansa ya kizazi hasa wanawake wetu wa maeneo yetu ya vijijini kupima ni kwa nadra. Unakuta imeshafika stage ambayo haiwezekani tena. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi natokea Mkoa wa Tabora. Katika Mkoa wetu wakina mama wengi sana wanapata matatizo hayo, mwisho wa siku anapopata tatizo hili hana pa kwenda kukimbilia, anaambiwa aende Bugando ama aje hapa Benjamini Mkapa. Ni wangapi ambao wanao uwezo wa kufika kwenye maeneo hayo? Kwa hiyo, unakuta mama huyo mpaka tayari stage yake imefika mbaya anaelekea kufa unaweza ukamsaidia lakini unamsaidia wakati tayari hali imeshakuwa mbaya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo niombe sana, kwanza elimu inahitajika sana hasa kwa wanawake wetu maeneo ya vijijini kuhusiana na hili janga. Sisi wa mjini angalau tunajua kama nitakwenda hospitalini naomba mni-check, mni-check matiti, mni-check na kizazi nitaangaliwa na nitakutwa labda niko salama ama nina dalili za huo ugonjwa lakini wenzetu kule ni ngumu sana. Kwa hiyo, niombe sana Wizara ya Afya mfanye kazi ya ziada tusaidie wanawake hawa wanakufa sana, pamoja na hizo tezi dume zinazosemwa lakini kwa kweli kansa za wakina mama zimekithiri sana maeneo mbalimbali katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo niombe sana tupelekewe na sisi basi hivi vifaatiba vya kansa pale katika Hospitali yetu ya Kitete katika bajeti hii, tunawaomba jamani mtusaidie. Hawa wanawake tuweze kuwaponya ili angalau na wao sasa waweze kupata nafuu na kujua kwamba wanapata huduma ile maeneo yale.

Mheshimiwa Spika, Tabora imefunguka, barabara sasa hivi zimefunguka, kila sehemu magari yanapita yanaingia. Tusaidieni basi ili angalau watu wa kutoka hata kwenye Wilaya za karibu waweze kufika pale kwenye hospitali yetu ya Kitete waweze kupata huduma hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nifahamu kuhusiana na suala la Bima ya Afya hasa kwa Watoto, imekuwa kero kubwa sana. Hatuelewi, hatujui tushike wapi. Ukiwauliza wanakwambia, kuna siku nilimuuliza Naibu Waziri akaniambia inabidi mzazi amsajili na mtoto wake kwenye bima yake. Mimi mtoto wangu ameshakuwa mkubwa lakini kuna watu ambao wana watoto wana miaka mitano. Huyu mtoto analipa wapi na bima yake imesha-expire? Hebu tunaomba Mheshimiwa Waziri unapokuja hapa, utoe majibu yatakayowaridhisha wananchi huko waweze kujua, mtoto wa kuanzia mwaka mmoja mpaka mitano ambaye bima yake imesha-expire anatakiwa afanye nini ili aweze kupata bima ya afya? Kwa sababu ukisema ni shule, shule gani anasoma mtoto huyu, kwamba labda ataenda kusajiliwa shuleni? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tunaomba mtoe maelezo basi yatakayowasaidia huko wazazi wengi, au kama ni kulipa hiyo shilingi 190,000 semeni. Mzazi lipa shilingi 190,000 mtoto wako aweze kupata huduma ya afya vieleweke kuliko kuwa mnafumba fumba na kusema kwamba watu wote wasajilini watoto kwenye mashule yao. Shule gani wengine watoto wadogo bado hawaja anza hata hizo shule? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tunaomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja ku-wind up hapa, atupe majibu ya kuhusiana na hili suala la bima ya afya hasa kwa hawa watoto wadogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na madeni pia makubwa sana katika Wizara hii ambapo hospitali nyingi sana za Kanda na hospitali za Mikoa zina madeni yaliyokithiri. Niombe sana Wizara ya Fedha pelekeni fedha wenzenu waweze kulipa madeni haya. Saa zingine kuna huduma nyingine zinakwama kwa sababu ya madeni makubwa ambayo wanayo katika hospitali zetu za Kanda na hospitali zetu za Mikoa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa ya CAG ya Hesabu za Serikali Kuu ya mwezi Machi, 2023, Wizara ya Afya ina madai ya zaidi ya shilingi bilioni 9.21. Madai hayo yanadaiwa katika hospitali ya Rufaa ya Apollo. Inaonekana kwamba kuna baadhi ya wenzetu Serikalini wanatibiwa huko, kwa hiyo kuna madeni hayo ambayo yanadaiwa kwa mujibu wa Taarifa ya CAG ya Machi, 2023 muende mkaipitie muione. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika hospitali zetu 33 za Rufaa na za Mikoa kuna madeni ya jumla ya zaidi ya shilingi bilioni 34.02. Hizi fedha ni nyingi sana na hapa hata ukizitoa, haya ni madeni ya muda mrefu zaidi ya miezi 12 madeni haya wala hayana mpango wa kulipika.

Mheshimiwa Spika, nitoe tu mfano wa hospitali chache hata hii hospitali yetu mnasema Mirembe mimi najua bado Mirembe sijajua kama tayari imeshabadilishwa lakini ina deni la zaidi ya shilingi bilioni tatu. Kuna Hospitali ya Kanda ya Mbeya ina zaidi ya deni la shilingi bilioni tatu. Dodoma hapo hospitali ya General zaidi ya shilingi bilioni 2.8. Hata hospitali ya Mkoa wa Tabora Kitete ina zaidi ya deni la shilingi milioni 948. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaiomba Wizara ya Fedha iweze kusaidia haya madeni kuondoka ili watu waweze kupata huduma zinazostahili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimeona umeshika mic naona muda wangu umeisha. Nakushukuru sana, ahsante sana. (Makofi)