Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

Hon. Abdallah Ally Mtolea

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Temeke

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kukupa uwezo wa kunisimamisha mahali hapa ili na mimi kidogo niweze kusema machache juu ya Serikali hii. Of course ina-bore kumshauri mtu au unapojiandaa kumshauri mtu ambaye unaamini hashauriki. Inafika tu wakati huna jinsi unahitaji kufanya hivyo hata kama hashauriki ni wajibu wetu kuendelea kuiambia Serikali labda kunaweza kutokea muujiza mwaka huu au miaka michache hii ambayo mnamalizia muda wenu wa kuwa madarakani kwani miaka michache ijayo sisi ndiyo tutakuwa madarakani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wenzetu waliotangulia katika Mabunge haya wamesema sana, wameishauri sana Serikali, lakini hakuna hata moja wanaloweza kulichukua. Muda wote wao wanajenga ile defensive mechanism kwa kupinga kila kitu na kila ushauri mzuri ambao Kambi hii imekuwa ikiwashauri. Jana hapa tumesikiliza hotuba nzuri kutoka Kambi hii ikiishauri Serikali lakini bado wanazibeza, wanazifumbia macho ili waendelee kujikita katika ile misingi mibovu na mambo mabovu ambayo mara nyingi wamekuwa wakiyashughulikia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kitendo cha ajabu kwa Serikali hii toka imeingia madarakani yaani jambo kubwa la ubunifu ambalo wao wamelifikiria ni kuhakikisha tu kwamba wanazima matangazo ya moja kwa moja ili wananchi wasiweze kuliangalia Bunge. Ni aibu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati tulipokuwa tukisikiliza Baraza Jipya la Mawaziri likitangazwa tunaona kina Nape wanachaguliwa tulikuwa na matumaini makubwa sana kwamba sasa tutaona Serikali ikiendeshwa kisasa zaidi, lakini kwa ajabu leo namwona Ndugu yangu Nape mishipa ya shingo ikimtoka hapa kutetea eti ni sahihi kutoonyeshwa live kwa Bunge, ni ajabu kweli kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, si kwamba Serikali hii haitambui mchango wa waandishi wa habari au mchango wa waandishi kuonyesha vitu hivi live kwa sababu wao wakati wanaenda kwenye zile ziara zao wanazoita za mishtukizo, za kutumbua majipu ambazo of course wanakwenda tu kukuna vipele na siyo kutumbua majipu kwa sababu majipu hayajatumbuliwa, wanaongozana na makundi makubwa ya waandishi wa habari.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiwakuta utafikiri pengine wasanii wanakwenda location ku-shoot movie kumbe wanatambua kwamba unapofanya jambo lolote unahitaji wananchi walione, unahitaji kusikika, unahitaji kuonekana wananchi waone unafanya kitu gani, leo hapa mnalifunga Bunge hili wananchi wasione. Hili ni tatizo kubwa lakini ukweli utaendelea kubaki palepale kwamba huwezi kupambana kuirudisha nyuma teknolojia ya mawasiliano. Teknolojia inazidi kwenda mbele, inazidi kuendelea na huwezi kutumia mikono kuizuia. Kwa hiyo, itafika mahali haya mnayoyaficha wananchi watayaona tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali hii inaongea sana, lakini yale wanayoyaongea ukitaka kuyaweka katika utekelezaji unaona kwamba hizi ni ndoto na hivi vitu vitaendelea kubaki ndoto haviwezi kutekelezeka. Tunaimba hapa suala la afya, wananchi wanategemea waone mabadiliko makubwa katika sekta ya afya, wananchi wapate huduma za afya katika maeneo ya karibu, wahudumiwe kwa uwiano unaostahili lakini bado Serikali hii haijaonesha dhahiri ni kwa kiasi gani itakwenda kutuwekea vituo vya afya kwenye kila kata.
Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti zinazoletwa hapa ni bajeti za kujenga vyoo siyo za kwenda kutuwekea vituo vya afya kwenye kata zetu. Ni bajeti ndogo ambayo itaweza tu kujenga vyoo au kujenga uzio na mwisho wake mtatumia fedha nyingi kuupeleka mwenge ili uende ukazindue vyoo hivyo.)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, unakuta tuna Serikali ambayo iko tayari kutumia nguvu nyingi kwenye vitu vidogovidogo lakini haiwezi kutumia nguvu nyingi kwenye mambo makubwa. Ukiwaambia kwenda kuzindua choo wataidhinisha mabilioni ya fedha uende Mwenge kule ukamulike uzindue ujenzi wa choo. Choo kinajengwa kwa shilingi milioni tano unapeleka mwenge ambao unatumia zaidi ya bilioni 120. Wakati mwingine unafikiria kwamba inawezekana hii Serikali inaamini kwenye nguvu za giza!
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa akili ya kawaida unawezaje kuuthamini moto ndiyo uutembeze nchi nzima kwa fedha nyingi, lakini unaacha kuyafanya yale mambo ya msingi? Nishauri tu kwamba Serikali hii ya Chama cha Mapinduzi iko madarakani si kwa sababu mmewaloga Watanzania kwa kuwapitishia Mwenge wa Uhuru. Mko madarakani kwa sababu ninyi ni wazuri sana wa kuiba kura wakati wa uchaguzi. Itoshe mkajiamini na mkajikita katika sifa hiyo ya kuiba kura. Huu mwenge uwekeni mahali, uwekeni makumbusho uendelee kubaki pale kama alama nyingine za kawaida, lakini tusitoe fedha kwa ajili ya kuutembeza moto ambao unaharibu vipindi vya wanafunzi mashuleni, wanakaa kuusubiria mwenge lakini pia moshi wa mwenge unachafua mazingira na unaathiri afya za wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hotuba ya Waziri jana inajaribu kuwatia moyo wananchi kwamba kuna fedha, vikundi sijui vitaboreshwa, mikopo na vitu vya namna hiyo. Wakati unakwenda kwenye kuahidi kwanza angalia yale ambayo yanaendelea kufanyika katika jamii unayasimamia kwa kiasi gani?
Mheshimiwa Naibu Spika, wajasiriamali wamekuwepo kabla ya Wizara hizi hazijaanza kutenga hizo fedha, wananchi kwa jitihada zao wenyewe wamejikita katika ujasiriamali. Nichukulie mfano tu watu ambao wameamua kujikita na kujiajiri katika shughuli za bodaboda ambazo zimetoa ajira kwa kiasi kikubwa sana kwa vijana pale Dar es Salaam. Cha ajabu Serikali badala ya kuwawekea miundombinu mizuri ili waweze kuzifanya shughuli zao kwa tija sasa hivi Serikali inatumia Jeshi la Polisi kuwatesa vijana wa bodaboda utafikiri ni majambazi, wezi au siyo watu ambao wanastahili kutunzwa na kuhudumia katika Taifa hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, vijana hawa wa bodaboda wanavamiwa katika vituo vyao, polisi wanawachukulia bodaboda zao wanazipakiza kwenye magari wanazipeleka kituoni, eti wanataka kwenda kuwauliza tu kama wana leseniā€¦
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa hiyo, tunaitaka Serikali na ndani ya bajeti hii mlishauri Jeshi la Polisi likome mara moja tena likome kwelikweli na likome hasa kuwanyanyasa hawa watu wa bodaboda. Wawaache wajasiriamali hawa ambao wamekopa fedha na kujiajiri waweze kufanya shughuli zao na zilete tija kwao na kwa familia zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati wa majumuisho ya Waziri nitapenda pia atuambie ni kwa nini wale pensioners toka wamepandishiwa malipo yao mapya Sh. 100,000/= kwenye bajeti ya mwaka jana wale ambao hawalipwi moja kwa moja kupitia Hazina hawajawahi kulipwa hayo malipo yao mapya mpaka leo. Hii fedha iko wapi? Kwa nini hawalipwi?
Mheshimiwa Naibu Spika, pia Walimu waliosimamia mitihani katika Halmashauri ya Wilaya ya Temeke mwaka 2015 mpaka leo hawajalipwa fedha zao, fedha hiyo iko wapi? Tunahitaji hayo majibu kutoka kwa Mheshimiwa Waziri atakapokuja kufanya majumuisho yake tuone hizo fedha zimekwenda wapi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali hii ya Chama cha Mapinduzi wananchi kwa kweli wameichoka na ninyi wenyewe mnafahamu. Kumbukeni jitihada kubwa mlizofanya kutengeneza matokeo ya Bara na hata kulazimisha matokeo ya Zanzibar, kulazimisha uchaguzi ambao haukuwa na sababu ya kuwa uchaguzi kwa sababu uchaguzi ulishafanyika. Sasa mtatumia mabavu ya kubaki madarakani mpaka lini, wananchi hawa wanajitambua na wanafahamu nani wanataka awaongoze. Hata ninyi wenyewe hamuoneshi dalili kama kweli mnahitaji kubaki madarakani kwa sababu mahitaji ya wananchi mnayajua, kwa nini basi kama mnapenda kubaki madarakani msifanye kazi kwa bidii wananchi wakaona kwamba ninyi mnafaa?
Mheshimiwa Naibu Spika, mna bahati nzuri sisi hatufichi mbona tunasema mambo mazuri ni haya, ni haya, ni haya, mmekaa madarakani chukueni haya mazuri tunayoyasema muyatekeleze kule. Sisi tunapambana kwa sababu tunajua hii nchi ni yetu sote. Mambo yakiwa mazuri kwa wananchi ni kwa ajili ya Tanzania, acheni ubinafsi, acheni ubinafsi Serikali ya CCM.
Mheshimiwa Naibu Spika, siiungi mkono hoja hii hata kidogo.