Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Buchosa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi ya kuwa miongoni mwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nimshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mema yote ambayo amelifanyia Jimbo la Buchosha kwa upande wa elimu. Ameleta fedha nyingi sana, tumejenga madarasa mengi, nina uhakika aliyoyafanya Wanabuchosha wote wanamshukuru wakiongozwa na mimi mwenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Elimu na najua anafahamu kabisa kwamba sina mashaka naye hata kidogo. Nimekwishazungumza naye mara nyingi kwamba uadilifu wake na uzalendo wake katika Taifa na namna anavyoipenda elimu, nina hakika kabisa elimu yetu iko kwenye mikono salama. Nimshukuru sana Naibu Waziri, rafiki yangu Kipanga ambaye mara kwa mara tunajadiliana kuhusu elimu ya nchi yetu, hakika anatumika vizuri sana kwa ajili ya Taifa lake, Katibu Mkuu na Manaibu Katibu Mkuu na Watumishi wote wa Wizara ya Elimu ambao wako hapa nyuma wananisikiliza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajadili suala la elimu, nimekuwa mshabiki mkubwa wa elimu na jambo moja ambalo nimekuwa nikilizingumza sana hapa Bungeni ni kuhusu elimu, kitu ambacho mwenyewe nikiwa kijana mdogo mtoto mdogo nilikikosa. Sikufanikiwa kupata elimu ya kutosha na kwa sababu nimefika kwenye hatua hii na najua umuhimu wa elimu kwa watu wa nchi yangu, nasimama imara siku zote kuhakikisha kwamba elimu ya nchi yangu inakuwa elimu bora. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Nelson Mandela aliwahi kusema na nitamnukuu alisema; “Education is the most powerful weapon you can use to change the world”. Kwamba elimu ni silaha yenye nguvu mtu yeyote anaweza kuitumia kuibadili dunia. Kwa hiyo tunapojadili elimu inatakiwa tuwe na umakini wa hali ya juu sana kwa sababu kuna uhusiano mkubwa sana kati ya maendeleo ya watu na elimu. Maendeleo ya watu yanategemeana sana na aina ya elimu ambayo nchi inatoa kwa watu wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi ya watu wenye akili sio wenye elimu pekee yake, haiwezi kuwa nyuma kimaendeleo. Ndio maana nasema na narudia kusema na nitaendelea kusema, tuna wajibu wa kuingiza maarifa kwenye akili za watoto wetu. Huo ni wajibu wa Serikali, Serikali ikitimiza wajibu wake sawasawa ika instill au kuingiza maarifa kwenye akili za watu wake, hatuna mashaka kuhusu maendeleo ya Taifa letu. Kwa hiyo Wizara ambayo Mheshimiwa Mkenda anaiongoza ni Wizara moja muhimu sana kwa ajili ya maendeleo ya Taifa letu. Kwa sababu kama hatutotimiza wajibu wetu tutakuwa na wananchi, tutakuwa na human capital ambayo haina elimu ya kutosha, haitoweza kusukuma maendeleo ya Taifa letu mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi zote zilizofanya vizuri katika ulimwengu huu watu wake wameelimika vya kutosha na aina ya elimu wanayopewa ndiyo jambo la muhimu zaidi. Sio tu kuwapeleka watoto shule wakasome, lakini aina ya elimu tunayotoa iwe ni elimu ambayo itasaidia kutatua changamoto zetu. Tunapeleka watoto shule tuwaelimishe ili watupe solution ya matatizo yetu, ndio lengo. Ninapopeleka mwanangu shule aweze kuja na solution kwa matatizo ya familia, solution kwa matatizo ya nchi na solution kwa matatizo ya dunia. Otherwise hapa hakuna sababu ya kupeleka mtoto shule kama tutapeleka watoto wetu shule wakasoma, lakini mwisho wa siku wasitupe solution ya matatizo yetu haina sababu ya kupeleka watoto shule. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo lengo letu tunasomesha watoto watupe solution ya matatizo yetu. Inaniuma sana, inaniuma sana mara nyingi, ninapokutana na kijana amesoma, amemaliza chuo kikuu, ana masters, yuko mtaani hatupi solution yoyote kwa Taifa letu. Anazunguka huku na kule akiwa na bahasha, hana mchango wowote kwa Taifa anageuka mzigo kwa Taifa, mzigo kwa familia yake, sio lengo la elimu yetu, lengo liwe ni kuwaelimisha watu wetu. Sasa tujiulize sisi wenyewe hapa tulipo ni matokeo ya aina ya elimu tuliyopata. Je, tunafurahia tulipo? Je, tungetamani tuwe mahali tofauti? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mawazo yangu mimi ni kwamba elimu iliyotufikisha hapa haiwezi kutupeleka tunapokwenda. Narudia, elimu iliyotuleta mpaka hapa tulipo, mimi sina furaha sana, nataka aina nyingine ya elimu itakayonitoa hapa kunipeleka kule ninapokwenda kwenye ulimwengu wa kidijitali. Internet of things, cloud computing mambo ya coding na namshukuru sana Mheshimiwa Waziri tulizungumza mambo ya coding hapa, nimeyakuta kwenye rasimu ya mtaala ambayo nimeisoma. Nimefurahi kwa sababu nina uhakika kwamba rasimu niliyoisoma, watoto tunaokwenda kuwatengeneza kwa rasimu hii watakuwa ni watoto ambao watatusaidia sana tunapokwenda. Kwa hiyo, ninao ushauri kwa Serikali, ushauri wangu kwa Serikali ni mambo yafuatayo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, wale wanaotoka kijijini kama mimi mnafahamu huwa tunafyatua matofali kwa kutumia kibao, kile kibao kinaitwa kifyatulio. Kwa hiyo kama kifyatulio ni cha duara matofali yatatoka ya duara, kama kifyatilio ni cha mstatili matofali yatatoka ya mstatili. Hauwezi ukawa na kifyatulio cha mstatili ukapata matofali ya duara. Maana yangu ni nini? Aina ya elimu tunayotoa tujiulize, tunatengeneza watoto wa aina gani huko mbele? Je, tunatengeneza watoto wanaofanya tushinde kwenye ulimwengu ujao? Hili ndilo swali langu la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nakuja kwenye mambo yafuatayo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, kwangu mimi ni mtaala, mtaala wetu ni lazima uwe ni mtaala ambao utamwandaa mtoto wetu kushindana kwenye ulimwengu ujao. Tusiwajaze watoto wetu content pekee yake kichwani isipokuwa tuwape elimu ambayo itawafanya waweze kuwa na solution za matatizo. Kwa hiyo, tuupitie mtaala wetu, nimeuona mtaala huu ni mzuri, una maboresho kidogo lakini watoto watakaosomeshwa kwenye mtaala huu wawe majibu ya matatizo kwenye ulimwengu tunaokwenda mbele, sio hapa tulipo hivi leo. Kwa hiyo, mtaala uboreshwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu Mheshimiwa Waziri ni kwamba tusichukue muda mrefu sana kutekeleza mambo. Tunapojadiliana kuhusu mtaala tufanye mambo yetu haraka. Dunia inaenda kwa kasi, unaweza kuwa mjadiliana, mnajadiliana, mnajadiliana kuhusu mtaala, dunia itabadilikia ukajikuta mtaala wako umekwenda obsolete kabla hujautekeleza. Kwa hiyo hayo nayo Mheshimiwa Waziri wameshayajadili, wadau wameongea, tuyafanyie utekelezaji kwenye mtaala tuanze kuufanyia kazi mara moja. Kwa hiyo mtaala wetu uboreshwe, uende na ulimwengu ujao, sio ulimwengu tuliotoka wala ulimwengu tuliopo hivi sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Walimu; Walimu wetu katika nchi hii wana matatizo sana. Walimu wetu wana shida; huwezi kuwa na elimu bora kwa Walimu wanaolalamika kila siku. Walimu wetu wamejaa mikopo, Walimu wetu wana kila aina ya dhiki, kama tumedhamiria kuboresha elimu ya nchi hii tuanze na Walimu wetu kuboresha maisha yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa kengele imelia niende katika jambo lingine la muhimu sana ambalo nataka kulisema, wazazi wa nchi hii watimize wajibu wao kwa watoto wao. Kuanzia kwa mama mjamzito, ahakikishe anakula chakula bora, mama mjamzito ajiepushe na matumizi ya dawa au vitu vinavyoathiri akili ya mtoto wake. Udumavu upigwe vita kwa sababu mtoto aliyedumaa hawezi kujifunza sawasawa tunakokwenda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu ya vitendo; tupunguze nadharia tuongeze vitendo kwenye elimu yetu. Medium of instruction, nilishasema huko nyuma, sikatai kufundisha kwa Kiswahili, lakini wasiwasi wangu ni kwamba mtoto utakayemfundisha Kiswahili kwenye ulimwengu ujao itakuwaje? Asubuhi ya leo wakati nafanya mazoezi, nimekutana na watoto wawili, mmoja amesoma English medium, mwingine anasoma shule ya kawaida ya Serikali wote wapo sekondari moja. Nikamuuliza yule aliyetoka shule ya msingi ya kawaida, akaniambia nahangaika sana form two kwa sababu nimesoma Kiswahili mpaka darasa la saba, form one Kiingereza. Yule mwingine akaniambia mimi sipati shida yoyote kwa sababu nimesoma Kiingereza mwanzo mpaka mwisho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ushauri wangu, tuamue kama ni Kiswahili, iwe ni Kiswahili, kama ni Kiingereza iwe ni Kiingereza na kama hilo hawalitaki, basi niwaombe wafundishe mpaka darasa la tatu au la nne Kiswahili, la tano mtu aanze Kiingereza kusudi wajiepushe na suala la mtoto form one, form two anajifunza Kiingereza hajakielewa vizuri form four umefika mtihani, anafeli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoteza watoto wengi sana. Naomba sana tuamue Wabunge sisi ndio wawakilishi wa wananchi, hebu tuchague tunataka nini, nani kati yetu hapa mtoto wake anasoma Mwananyamala Primary School? Nani? Napendekeza huko mbele ikiwezekana Waziri akiteuliwa tu iwe ni sharti kwamba mwanao asome shule ya kawaida. Tukifanya hivyo elimu yetu itabadilika. Sasa hivi tunawadanganya wananchi wetu kwamba tufundishe Kiswahili, watoto wetu hapa wote wanasoma international schools, that’s a lie, tusiendelee kuwadanganya wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie na cheti cha form four; kansa ya cheti cha form four katika nchi yangu. Nilizungumza mara ya mwisho hapa narudia tena. Hivi sasa nina stori ya watoto wamesoma China medicine, wamesoma miaka mitano medicine China, wamekuja hapa wamekataliwa kufanya internship kwa sababu hawana cheti cha form five na six. Waliondoka hapa kwenda kusoma medicine China kwa elimu ya form four, hapa wamelazimika kufanya QT ya form five na six ndio wafanye intership, what is wrong with this? Hebu tufike mahali tuache watu wapate elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme mapema, issue yangu ya RPL, Recognition of Para Learning ambayo ikanifanya mimi nikapata elimu ya chuo kikuu kutoka darasa la saba. Naomba sana Mheshimiwa Waziri anipe majibu ya suala hili, ni lini RPL itaanza?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Eric.
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)