Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Korogwe Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. ALFRED J. KIMEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuchangia kwenye Wizara hii ya Elimu. Kwanza niwapongeze viongozi wa Wizara hii ya Elimu. Kwanza Ndugu yangu Mheshimiwa Profesa Mkenda, kaka yangu Mheshimiwa Omari Kipanga, Katibu Mkuu Profesa Nombo pamoja na Manaibu Katibu Mkuu kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya kuhakikisha wanasimamia sekta hii ya elimu kwenye nchi yetu ya Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, napenda kuishukuru Serikali ya Tanzania ambayo inaongozwa na Rais wetu, Jemadari kabisa, mama jembe, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo anaifanya kunyanyua sekta ya elimu kwenye nchi yetu. Mambo mengi yamefanyika, lakini nitazungumzia machache wala siwezi kuyaongea yote yaliyofanywa kwenye sekta ya elimu hasa kwenye Jimbo langu la Korogwe Mjini. Yamefanywa mambo mengi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikizungumzia vyoo, wanafunzi walikuwa wanapata shida lakini tumejengewa vyoo kwenye kila shule ya sekondari na shule ya msingi. Ukizungumzia maabara, kwenye shule zote za sekondari tumejengewa, ukizungumzia mabweni na miundombinu mingi kwenye sekta ya elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, vitu vikubwa ambavyo nataka kuvitaja wananchi wa Korogwe ambao wanatamani kuvisikia Mama Samia amevifanya; moja, katujengea sekondari mpya kabisa kwenye Kata ya Bagamoyo na sasa hivi sekondari nyingine inaendelea kujengwa kwenye Kata ya Mtonga kwenye Kijiji cha Msambiazi. Hayo ni mambo makubwa, lakini hivi tunavyoongea, tayari tumeletewa fedha kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya msingi na mambo mengine mengi yanafanyika kwenye sekta ya elimu. Kwa hiyo, hatuna budi kumshukuru na kumpongeza mama yetu, jembe kabisa, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo anaifanya. Kimsingi, baada ya miaka yake 10 ya uongozi, ataacha historia kubwa kwenye nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizo, pia nitumie fursa hii kwa ufupi kabisa kuwapongeza viongozi wangu wa Halmashauri ya Korogwe Mji, hasa viongozi kwenye sekta ya elimu, nikizungumzia Afisa Elimu, Walimu pamoja na wadau wengine wa elimu kwenye Jimbo langu la Korogwe Mji. Kwenye Halmashauri yetu tunaongoza kwenye ubora wa elimu kwenye Mkoa wa Tanga. Hivyo, nawapongeza lakini nataka niwatie moyo waendelee kufanya kazi kwa juhudi, tuko pamoja nao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuongea hayo, shukurani na pongezi hizi huwa zina tafsiri yake kwa nyuma kwamba bado tunahitaji vitu vingine. Tunajua vingi vimefanywa lakini bado tuna changamoto chache kwenye shule zetu. Bado tuna upungufu wa baadhi ya madarasa, vyoo na shule nyingine ni chakavu, lakini naamini kabisa kwa kasi hii ya Rais wetu, tutaletewa hivyo vitu na baada ya miaka yetu mitano ya uongozi na Mama Samia akiwa madarakani mambo mengi yatafanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa hilo. Hiyo ilikuwa sehemu yangu ya kwanza ya mchango wangu. Sehemu ya pili ni hoja yangu ya msingi kwenye siku ya leo, namwomba Mheshimiwa Prof. Mkenda apate kunisikiliza kwa umakini ili kama Taifa tuweze kufanya maamuzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo asubuihi alisimama ndugu yangu Mheshimiwa Maige kuzungumzia lugha ya kufundishwa kwenye shule zetu, lakini muda mchache amesimama ndugu yangu Mheshimiwa Erick Shigongo, nami pia nilikuwa na mchango kama huo huo. Sipingi kwamba lugha ya Kiswahili ni lugha yetu ya Taifa. Tunaipenda, tunajivunia lugha hii na kila mtu, sio mimi tu, nadhani kila Mtanzania anatamani lugha hii ikapate kuzungumzwa East Africa yote, ikapate kuzungumzwa Afrika nzima na hata dunia nzima. Ni lugha yetu, tunaipenda, nitaendelea kuipenda siku zote. Isipokuwa, sisi kama Taifa hatupaswi hata kidogo kupuuzia mchango wa lugha ya Kiingereza kwenye dunia hii na kwenye mchango wa uchumi wa nchi yetu. Sisi kama Taifa hatupaswi kupuuzia hata kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaeleza kwa uchache faida za lugha ta Kiingereza. Moja, nitaeleza faida kwa mtu binafsi, halafu baadaye nitaeleza faida kama Taifa. Kwenye dunia hii, watafiti wanasema, mtu mwenye uwezo mzuri wa kuweza kuongea vizuri lugha ya Kiingereza, akaweza kuiandika na kuisikia vizuri ana chance kubwa ya kuajirika kuliko mtu mwingine yeyote. Huo ndio utafiti unasema hivyo. Sisi kama Taifa hatutakiwi kupuuzia utafiti huo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia utaungana nami, kwenye nchi yetu, interview karibu zote zinafanyika kwenye lugha ya Kiingereza. Kwa hiyo, sisi kama Taifa pia tunafahamu umuhimu wa lugha ya Kiingereza. Pamoja na hilo, ili uajiriwe kwenye makampuni makubwa kwenye dunia hii, nenda Google, nenda Facebook, nenda Spacex na makampuni mengine yote, ni lazima uwe na uwezo mkubwa wa kuweza kuongea lugha ya Kiingereza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanafunzi wetu wakimaliza Form six wana option ya kwenda kusoma kwenye vyuo vikubwa kwenye dunia hii. Kama unataka mtoto kwenda kusoma vyuo vikubwa duniani, iwe Harvard, Oxford na vyuo vingine vikubwa kwenye dunia hii, bila ujuzi mzuri wa kuongea, kuandika na kusikia vizuri kugha ya Kiingereza, itakuwa ni historia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile, ili mtu aweze kufanya biashara za Kimataifa vizuri, lazima awe na uwezo wa kuongea lugha ya Kiingereza. Utakubaliana nami kwamba mikataba mingi ya kibiashara inaandikwa na inakuwa negotiated kwa lugha ya Kiingereza. Ili uwe consultant mzuri kwenye makampuni ya kitaifa na kimataifa, ni lazima uwe na uwezo wa kuongea lugha ya Kiingereza. Pamoja na hayo, hizo ni faida za mtu binafsi lakini nimeamua kufuatilia faida kama Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu kwenye Ilani ya CCM, tunasema tunataka kuleta ajira milioni moja kwenye miaka yetu hii mitano ya uongozi. Lugha ya Kiingereza ni sehemu ya ajira. Watu wetu wakiweza kuongea Kiingereza vizuri, watapata ajira nje ya nchi, kwa hiyo, tutapunguza kugombania ajira za ndani ya nchi. Kama tunataka ajira milioni moja, watu 500,000 wakienda nje ya nchi, 500,000 tutawaajiri ndani ya nchi. Ukiachana na ajira, kuna issue ya remittance kwa diaspora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimefuatilia, nika-compare remittance, fedha zinazotumwa na diaspora kutoka nje ya nchi kuja Tanzania, na nika-compare na zinazotoka nje ya nchi kwenda Kenya. Mtashangaa, kwenye nchi ya Tanzania kwa mwaka tunapokea dola milioni 500 kulinganisha na Dola bilioni nne kwenye nchi ya Kenya. Nikafuatilia sababu, nikaambiwa wananchi wa Kenya wana uwezo mzuri wa kujua Kiingereza, hivyo wanaajiriwa kwenye nchi mbalimbalia hasa Ulaya na Marekani. Hatutakiwi kupuuzia suala la uwezo wa Kiingereza kwenye Taifa hili. Kwenye nchi ya Kenya remittance kutoka kwa diaspora ndiyo inaongoza kwenye foreign currency kwenye nchi yao. Kama Tanzania, hatupaswi kupuuza hata kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnafahamu wote, nchi ya Kenya inavyotukimbiza na utalii. Watalii muda mwingine wanapenda kutembelea nchi ambayo hawatasumbuka kuongea lugha ya Kiingereza, ndiyo maana Kenya siku zote inatupiga gap. Tafiti zinasema, nchi ya India sasa hivi inaongoza kwa foreign direct investment kuajiri Wahindi wengi, kwani sasa hivi wana uwezo wa kuongea Kiingereza. Ukiacha India, nenda Kenya, nenda Ghana, nenda South Africa, huwezi kulinganisha na Tanzania. Wawekezaji wengi wanaenda nchi hizo kwa ajili ya uwezo wa kuongea Kiingereza na wananchi wao wanapata faida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuona faida hizo; moja, kwa mtu binafsi; na pili, kwa Taifa, nikaamua sasa kuchimba zaidi, ni wakati gani mtoto wa kitanzania, kwenye umri gani sahihi aweze kujifunza na kuweza kuelewa na kui- master lugha ya Kiingereza? Stadi zinatofautiana, lakini asilimia kubwa zinasema, mtoto anatakiwa kufundishwa lugha ya kigeni hasa Kiingereza akiwa na umri kuanzia miaka sita mpaka miaka 10. Baada ya hapo kweli tunaweza tukamfundisha, lakini hawezi kuongea vizuri kama native speaker. Hawezi kuongea vizuri kama lugha yake ya kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, mtoto asipofundishwa lugha hii ya kigeni hasa Kiingereza, kwenye miaka sita mpaka 10, baada ya hapo hawezi kuongea vizuri lugha ya Kiingereza na hawezi kupata hizi faida ambazo nimezielezea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kujiridhisha kwa hilo pasipo mashaka kabisa, kwamba huo ndiyo umri sahihi, nikaangalia sasa mfumo wetu wa elimu kwenye nchi yetu ya Tanzania.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa.
MHE. DKT. ALFRED J. KIMEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba dakika moja.
MWENYEKITI: Malizia sekunde 30.
MHE. DKT. ALFRED J. KIMEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo wetu wa kitanzania ni mfumo wa kibaguzi sana. Watoto wa kitajiri, watoto wa viongozi, watoto wa wafanyabiashara ndio wanapelekwa kwenye zile shule, wanasoma lugha ya Kiingereza tangu Darasa la Kwanza. Watoto wa kimasikini, watoto wa wapiga kura wa nchi hii wanapelekwa kwenye zile shule ya Kiswahili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kesho nitasimama na Shilingi ya Mheshimiwa Waziri. Kabla ya kumwachia Shilingi, aniambie watoto wake wako kwenye shule gani? Baada ya hapo tuchague mfumo gani tunataka kwenda nao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na ninaunga mkono hoja. Nakushukuru sana. (Makofi)