Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vwawa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipatia hii nafasi ili niweze kutoa mchango katika Wizara hii muhimu ambayo ndiyo imebeba maisha yetu. Kwanza nampongeza Mheshimiwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na viongozi wengine wote wa Serikali. Lakini nawapongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na timu nzima kwa kazi kubwa ambayo mnaifanya katika kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya elimu. Kwa kweli hongreni sana, sote tumeshuhudia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yeyote ili iweze kuendelea inategemea uwezo wa watu wake katika kufikili, inategemea uwezo wa watu wake katika kuwa na maarifa ya kutosha, inategemea uwezo wa watu wake katika kuwa na ujuzi wa kutosha lakini katika kuwa na umahiri wa kuweza kutenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ili hayo yaweze kutokea naomba ukisoma vitabu vitakatifu Hosea 4:6 unasema hivi “Watu wangu wana angamizwa kwa kukosa maarifa; kwa kuwa wewe umeyakataa maarifa, mimi nami nitakukataa wewe, usiwe kuhani kwangu mimi; kwa kuwa umeisahau sheria ya Mungu wako, mimi nami nitawasahau watoto wako”. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inatukumbusha kwamba bila maarifa nchi hii hatuwezi kuendelea, bila maarifa ya kutosha umasikini wetu hauwezi kupungua, hauwezi kuisha, ili tuweze kupambana na umasikini, ili tuondekane na maradhi yaliyoko, ili tujenge uchumi imara, ili tuhakikishe kwamba tunakuwa na sayansi na teknolojia za kutosha hapa nchini tunahitaji maarifa, tunahitaji ujuzi wa kutosha na hii Wizara wamebeba hii dhamana ya kutupeleka huko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri na timu yake yote na Makatibu Wakuu na wote tunawapongeza kwa mageuzi makubwa ambayo mmekuja nayo katika mwaka huu. Mmekuja na mageuzi makubwa kwanza bajeti imeongezeka na inazidi kuongezeka tumeona madarasa yanajengwa kila aina, vyuo vya ufundi vinajengwa hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mabadiliko ya mitaala ndiyo kitu muhimu sana, ambacho mmekibeba na hiki mtaacha legacy katika nchi hii. Mabadiliko haya ya mitaala, mitaala yeyote lazima iendane na mahitaji ya nchi na agenda ya kitaifa ya nchi. Ajenda ya kitaifa ya nchi yetu sasa hivi ni umasikini uliokithiri, nikujenga uchumi imara ili tuweze kushindana katika nchi yetu hasa haya yote yatawezekana tukifanya mabadiliko makubwa ya mitaala yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wizara imeanza mabadiliko makubwa na ninawapongeza, juzi tumeshiriki hapa wametufundisha lakini wameleta watu 1,500 kuchangia mawazo kwenye mitaala, haijawahi kutokea mmefanya vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka Lee Kuan Yew wakati ananza kuitawala nchi ya Singapore aliitisha watalam, akasema nataka mniambie kama watalam nifanyaje ili nchi hii iendelee? Na wewe Mheshimiwa Waziri umesema jamani sisi mawazo yetu ni haya, nyinyi mna mawazo gani? Ndiyo maana umeitisha kila aina ya semina na watu kuchangia na sisi hapa tunachangia nakupongeza sana sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimewasikia waliyochangia kuhusu kiswahili na waliyochangia kuhusu kingereza lakini mimi sitaki kuingia kwenye huo mjadala, nataka nikumbushe tu. Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Mwaka 1985 wakati anang’atuka, analihutubia Bunge hili nafikiri ulikuwa mwezi wa nane alisema hivi “kiswahili kimefanya kazi kubwa ya kuwaunganisha watanzania mpaka hapa tulipofika, akasema lakini kiswahili hakitatuwezesha kufika kule tunakotaka” sasa lazima tuzungumze kiswahili cha dunia, kiswahili kimetufikisha hapa sasa tuzungumze kiswahili cha dunia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda sitaweza kuyazungumza sana. Lakini kiswahili ni muhimu kimefanya kazi yake, kimetuunganisha watanzania sasa tutafute kiswahili cha dunia, ili tujifunze sayansi na teknolojia, iweze kutusaidi katika kujenga uchumi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mageuzi yanayoendelea Mheshimiwa Waziri ya Mitaala, tunataka tuone kuwe sasa na mageuzi ya namna ya kufundisha. Ufundishaji wetu uendane na mitaala yenyewe tunayoihitaja. Vifaa tunavyovitaka kama ni competence based, umahiri lazima tuwe na vifaa vya kuhakikisha kwamba tunawaandaa vijana wetu katika hawa, hawawezi kufikia huko bila kuwa na vifaa vya kufundishia vya kisasa. Tunahitaji kubadilisha fikra, kwa sababu ukiwa na maarifa, ukawa na ujuzi bila kubadilisha tabia bado hatutaweza kufika, tubadilishe tabia maarifa hii itusaidie tuwe na nidhamu tuweze kutekeleza mambo yetu, tuweze kufanya kazi yetu vizuri, naamini hili linawezekana na kila kitu kitawezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri kazi mnayoifanya nzuri, vyuo vya ufundi, vyuo vya sekondari mnabadilisha manakarabati vya zamani mnakuja na mitaala mipya, mnakuja na vitabu vipya, mmesema mnaanza kufundisha walimu katika ngazi mbalimbali ili wawe ni competent hongera. Kwa hiyo, na sisi tutakuunga mkono kwa hali mali ili kuijenga nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule Mkoa wa Songwe, Mkoa wa Songwe ni Mkoa wa Kilimo na unalima kweli kweli na tunachangia kwa kiwango kikubwa katika Taifa hili. Lakini tunazo shule za sekondari zaida ya 62 kwenye Wilaya ya Mbozi, Wilaya peke yake ya Mbozi yenye jimbo moja tunazo zaidi ya 62 shule za sekondari. Pamoja na kwamba sisi ni mkoa au ni wilaya ya kilimo lakini hatuna shule hata moja inayofundisha kilimo. Maana yake tunawaandaa wale watoto wasiende kwenye kilimo, kitu ambacho ni kizuri lakini je, kweli? Tuna uwezo wa kuwaondoa wote kwenye kilimo? Sasa hili Mheshimiwa Waziri naomba mliangalie, naomba hili mliangalie.

Mheshimiwa Mwenyekiti namshukuru pia katika Mkoa wa Songwe ametuletea Chuo cha VETA. Unajenga chuo cha VETA sasa na nimeambiwa fedha zimeanza kwenda za kujenga Chuo cha VETA, tunapongeza sana kwa hilo, tunafurahia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanasema hata wakifanya vizuri bado maombi ayaishi, tunaendelea kuomba mkoa wetu ni mchanga ndiyo mkoa wa mwisho kuanzishwa hapa nchini, bado unamapungufu mengi, baada ya VETA tunahitaji tawi la chuo kikuu angalau kimoja, sasa hiyo iwe ni kutoka sekta binafsi, iwe ni kutoka wapi, tunahitaji chuo kikuu katika Mkoa wa Songwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi ya hapo Mheshimiwa Waziri tumeona kazi ya kutoa elimu katika nchi hii ni kazi ya Serikali, lakini na wadau mbalimbali ambao wanachangia katika kutoa hiyo elimu ikiwemo sekta binafsi ambao kuna shule binafsi, kuna vyuo binafsi na kadhalika vyote vinachangia katika kutekeleza jukumu la kimsingi, la kikatiba, la Serikali yetu. Sasa basi vyuo hivi kusiwe na sera ya ubaguzi, hao watekelezaji wote waunganishwe, wanafanyakazi ileile ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi watoto waliyosoma kwenye vyuo, kwenye shule za sekondari za watu binafsi kwenye mikopo wanabaguliwa, wanaambiwa hawana uwezo hii siyo sahihi. Inatakiwa wale wasaidiwe, inatakiwa nao waungwe mkono ni watanzania, vyuo binafsi ni vyuo vya Tanzania. Kazi yetu sisi ni kuviimarisha, ni kuboresha mitaala vitoe maarifa mazuri, ili vivutie wasomaji na wanafunzi kutoka nchi za nje. Tupate watalii kutoka nchi za nje, waje kusoma Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa jitihada tulipofikia hapa, vyuo vyote vilivyoanzishwa hivi vinatakiwa vilindwe kwa sababu vinatoa ajira, vinatoa maarifa, vinachangia katika uchumi wa Taifa letu ili watu wengi kutoka nchi za SADC waje kusoma Tanzania, waje kuona Mlima Kilimanjaro, waje kuona bahari na maziwa waje kusoma hapa nchini kwa hiyo, ni muhimu tukaboresha katika hilo eneo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunahitaji vyuo vyetu sasa viwekeze kwenye kufanya utafiti na kutoa ushauri wa kitalamu. Sasa hivi kwenye vyuo vyetu mkazo uko kwenye kufundisha na kufundisha bado atujafikia kwenye level ya competence based, bado tunafundisha ya kinadharia zaidi. Sasa wakati tunatoka huko kwenda kwenye competence based lakini pia tusisitize kufanya utafi na tusisitize kutoa ushauri wa kitalamu na baada ya kufanya utafiti, tusisitize katika kuandaa machapisho ndiyo yatakayoisaidia nchi hii.

Mheshimiwa Mwwenyekiti, sasa hivi vijana wengi wanafanya project, vijana wengi wanafanya research nzuri sana unakuta anapata A lakini ukienda unakuta kwamba hiyo research aliyoifanya inaenda kuwekwa kwenye makabati badala ya kuichukua na kuona namna inavyoweza kuisaidia nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi, naunga mkono hoja, nasisitiza nawaunga kwakweli, tunawapongeza kwa kazi nzuri mnayofanya na nchi hii tunawategemea, maendeleo ya nchi hii yako mikononi mwenu Mungu awabariki, ahsante sana. (Makofi)