Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kupata fursa na mimi kuweka mchango wangu kwenye bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijatoa mchango wangu naomba nitumie fursa hii kuipongeza sana Serikali. Kuipongeza Serikali kwa sababu yapo mambo mengi ambayo tumekuwa tukisimama mbele ya Bunge lako Tukufu tunashauri Serikali namna ya kuboresha elimu ya Tanzania, tumeshuhudia kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri lakini tumeshuhudia kwenye mijadala mbalimbali ya Mheshimiwa Waziri na Kamati ya Kudumu ya Bunge, yameendelea kutekelezwa na yanaonesha kuleta tija kubwa katika mabadiliko ya elimu nchini, ninapongeza sana kwa jambo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sote ni mashahidi, binafsi tangu nimeingia kwenye Bunge hili pamekuwa na mjadala mkubwa wa uhitaji wa mabadiliko ya elimu Tanzania. Watu wamekuwa na kiu ya kuona elimu ya Tanzania inatolewa kwa kuleta mabadiliko ya mtu mmoja mmoja baada ya kuhitimu. Tumekuwa na uhitaji wa kushuhudia elimu ya Tanzania inamsaidia kijana wa Tanzania kujiajiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mkakati huu wa kutekeleza maombi na ushauri wa Waheshimiwa Wabunge ndani ya Bunge hili kwa kuamua kuleta mtaala mpya wa elimu, hii ni dhahiri kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi ni Serikali sikivu, ni dhahiri kwamba Wizara hii ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeamua kusikiliza mawazo na kutekeleza kadri ambavyo imeweza. Ninawapongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wazo hili la kubadilisha mitaala liliafikiwa na Rais wetu kipenzi, Mama Samia Suluhu Hassan na alilitolea maelekezo Madhubuti, na yeye kama Mama, kama Kiongozi alishagundua yapo maeneo ambayo yana mapungufu na yanahitaji kufanyiwa kazi ili elimu yetu iweze kuwa bora. Mimi nataka niseme pamoja na mambo mengi mazuri ambayo yamewekwa kwenye mitaala mipya, lakini jambo la kuweka internship kwa walimu, jambo la kuhakikisha kwamba mwalimu kabla hajaajiriwa anajitolea kwa mwaka mzima kwenda kufanya internship kazini kuimarisha ujuzi wake, ni jambo kubwa ni mabadiliko makubwa na ni jambo ambalo litaboresha sana elimu ya Tanzania. Niendelee kupongeza kwa jambo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba nianze kuchangia. Kama mtakumbuka vizuri kwenye mchango wangu juu ya Wizara, wakati nachangia Wizara ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI, niliishauri na niliiomba Serikali ije na mkakati wa maksudi wa kupunguza upungufu wa walimu kwenye mashule yetu. Nilikuja na takwimu, nilionyesha namna ambavyo kuna pengo kubwa kutoka kwa walimu wanaohitimu, walimu walioko mtaani na walimu ambao wanaajiriwa kila mwaka, nikashauri kwamba inawezekana kupunguza hili wimbi au pengo la upungufu wa walimu mashuleni kwa kutengeneza utaratibu wa kuajiri kwa mkataba au kuajiri kwa muda, kuleta ajira za muda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge litakuwa limerekodi kwenye Hansard. Majibu yaliyotolewa na Serikali ilikuwa ni kwamba Serikali haina mwongozo, hakuna utaratibu wa walimu kujitolea lakini walimu wengi wapo mashuleni wanajitolea, nataka niseme jambo moja, tunapozungumza sasa katika ngazi ya awali tunahitaji kuwa na walimu 61,487. Walimu waliopo mashuleni ni 8,619, upungufu wa walimu kwa ngazi ya awali pekeyake ni walimu 52,868. Huu upungufu ni mkubwa sana, upungufu ni mkubwa lakini walimu wapo mtaani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda sekondari vivyo hivyo, tuna uhitaji wa walimu laki tatu na zaidi lakini walimu walioko shuleni ni laki moja na kidogo. Kwa hiyo tuna upungufu wa zaidi ya walimu 100,000. Ukienda kwenye shule za msingi ni hivyo hivyo na inapelekea kama nchi sasa kuwa na zaidi ya upungufu wa walimu 300,000 kwenye mashule yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa nilizonazo Mama yetu, kipenzi chetu Mheshimiwa Rais ametangaza ajira za walimu hivi karibuni. Ajira ni kama 29,000 kama nakumbuka vizuri lakini walioomba ni zaidi ya walimu 300,000. Imagine tatizo ni kubwa namna gani? Tunawezaje kwenda kulitatua tatizo hili kwa kufikiria kwamba hatuwezi kuwa-consider wale ambao wanajitolea kwa sababu hatuna mwongozo. Hii siyo sawa na hii siyo sahihi. Niendelee kusisitiza na kuiomba Serikali tuleteeni mwongozo, walimu waliohitimu vyuo vya ualimu wapate nafasi ya kwenda kujitolea. Wanapojitolea mambo mawili yanatokea kwa wakati mmoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ni wao kuimarisha ujuzi wao na kujikumbushia yale material yasiweze kupotea, lakini jambo la pili wanatupunguzia upungufu gap ya walimu kwenye mashule yetu. Watoto watapata nafasi ya kusoma. Hili hatuwezi kuliacha pembeni kwa majibu kwamba hatuna mwongozo. Majibu hayo hayatoshi, hayatoshelezi. Kwa hiyo tunaiomba sana Serikali ifikirie namna nyingine ya kuleta mfumo au mwongozo ili tuweze kuajiri walimu wengi zaidi kwa mkataba kwa sababu sisi wote ni Watanzania, tunajua hali ya nchi yetu hatuna uwezo wa kutoa ajira kwa walimu 300,000 kwa pamoja lakini basi walau.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nafanya ujasiriamali. Huko kwenye m-pesa tumeajiri walimu wenye certificate, wenye diploma, wenye degree. Unamlipa mwalimu shilingi 100,000 kwa mwezi na anafanya hiyo kazi. Anafanya shughuli ambazo wala hajazisomea lakini yuko pale kwa ajili ya kutafuta angalau tonge la kila siku. Sasa kama Serikali itaamua kuajiri kwa mkataba au kutengeneza utaratibu wa walimu kujitolea maana yake ni kwamba bajeti inaweza kutumika ndogo lakini ikawa imetatua matatizo mawili kwa wakati mmoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kuhusu wadhibiti ubora elimu. Ukizungumzia ubora wa elimu hawa wadhibiti ni kama tunavyochukulia nafasi ya CAG kwenye Hesabu za Serikali. Wao ndiyo wanaangali utaratibu, utekelezaji na namna ambavyo elimu inaendelezwa katika maeneo yetu, katika shule zetu na kadhalika. Nilizungumza mwaka jana katika bajeti iliyopita nikaiomba Serikali, hawa kwa nia njema kabisa huko nyuma Serikali iliamua kuwabadilishia muundo kuwatoa kwenye watumishi wa kawaida kuwapeleka kweye watumishi viongozi ili walau maslahi yao yaweze kuongezeka na mwisho wa siku kazi zao ziweze kufanyika kwa ufanisi. Niiombe Serikali na nimuombe Mheshimiwa Mkenda, Mheshimiwa Mkenda wewe ni Mwalimu na tunafahamu uwezo wako na sasa hivi una mama mmoja jembe sana, Profesa Carolyne Nombo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge, Katibu Mkuu tuliye naye Wizara ya Elimu sasa ni Katibu Mkuu mwenye weledi mkubwa. Mimi nimefanya kazi katika Kamati hii na nimeshirikiana na Wizara hii ya Elimu tangu nimeingia hapa Bungeni, na nimeshapita na Makatibu Wakuu zaidi ya watatu lakini Katibu Mkuu tuliyenaye sasa ni Katibu Mkuu kweli kweli. Anatoa ushirikiano, anajibu hoja za Wabunge, anakerwa na yale ambayo sisi Wabunge tuna kerwa nayo. Hongera sana Mheshimiwa Waziri, hongera sana Mheshimiwa Nombo, lakini mwisho wa siku tunachoomba, yale ambayo tunayashauri kama wawakilishi wa wananchi basi yachukuliwe hatua ili wananchi ambao tunawawakilisha nao waone kwamba tumefanya kazi yetu vizuri. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Husna Sekiboko kengele ya pili imelia.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, naunga mkono hoja kwa asilimia 100. (Makofi)