Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naomba nimshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kupeleka fedha kujenga VETA Tarime, shilingi bilioni 1.4. Pia nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kulipa baadhi ya madai ya watumishi wakiwemo walimu wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kupeleka vishikwambi ambavyo vimesaidia pia kupeleka teknolojia na kurahisisha mawasiliano. Nampongeza Mheshimiwa Rais kwa jambo kubwa hili ambalo ameruhusu tufanye mjadala wa kupitia mitaala ya elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu katika eneo hili, hili ni jambo muhimu sana, tunazungumzia Watanzania wa leo na kesho na vizazi vijavyo, tujipe muda wa kutosha wa kutafakari jambo hili. Tunahitaji kupata muda wa kujadiliana. Yako maswali yanahitaji kuwa na majibu. Kwa mfano, Mheshimiwa Waziri amesema, Januari mwakani 2024 wanaweza wakaanza utekelezaji. Tungependa Mheshimiwa Adolf Mkenda atuambie mkakati wa utekelezaji huu ukoje? Zile shule za zamani za ufundi wamekarabati lini? Vitendea kazi vya kisasa umepeleka lini, kwa maana ya ukarabati wa karakana na kadhalika? Vyuo vya ufundi vimesimama kwa muda mrefu. Walimu wabobevu wenye taaluma hiyo wameandaliwa lini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, haya mambo ni muhimu. Unaona watu wanauliza, Zanzibar kule Darasa la Kwanza mpaka la Saba hapa mnapendekeza Tanzania Bara, Darasa la Kwanza mpaka la Sita. Tumetajiwa mifano ya nchi nyingine ambazo zimefanikiwa, mnafanya reference wapi? Mambo haya yote yanapaswa kujadiliwa kwa kina ili tupate kitu cha maana sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wamependekeza hapa pia, ni vizuri tukapitia Sheria ya Elimu, twende kwenye sera, twende kwenye mitaala na tutengeneze kitu ambacho kitadumu kwa miaka 100 ijayo, tutengeneze Tanzania ambayo inaonekana kwa macho tuchore roadmap ya nchi yetu kwa upande wa taaluma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile watu wanahoji hata lugha ya mawasiliano. Hili ni muhimu pia tutakubaliana kama Taifa, tunatoka hapa tunaenda wapi? Kila mtu aweze kuridhika na tuweze kwenda mbele. Pia maeneo yetu kwa mfano, mimi maeneo yetu watu ni wakulima kule, mitaala ambayo inatengenezwa, tungetarajia kuwe na fani ya uchimbaji, kuanzia level ya chini kabisa. Mahali ambapo kuna kilimo, kuwe na fani ya kilimo proper na vifaa viende vya kisasa. Mahali ambapo kuna uvuvi, kwenye maziwa na Bahari, lazima mitaala ya kisasa ya kuvua iwepo ili tukimaliza jambo hili, tuwe tumefanya once and for all na watu waweze kunufaika tupunguze shida kubwa ya ajira katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, ni ubora wa elimu. Nimeangalia matokeo ya Kidato cha Nne, ni kwa miaka mitatu. Kwa mfano, 2020 waliopata Division One mpaka Division Three walikuwa 152,909. Division Four mpaka Zero ni 318,148. Hao waliofeli ni asilimia 65. Mwaka 2021 waliofanya Form Four, waliopata Division One mpaka Three ni 173,422; Division Four mpaka Zero 310,398. Asilimia 62 hawa walifeli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2022 waliofanya mitihani darasa la kwanza mpaka la tatu ni 192,348, lakini daraja la nne na zero 328,000, kwa ujumla wake, kwa miaka mitatu hii. Maana yake waliopata Division One mpaka Four ni asilimia 34, zilizobaki walifeli kwa lugha nyingine. Hawa wako mtaani. Hii nime-sight miaka mitatu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna sura moja nimeona hapa, mwaka huu wa 2022 kwa mfano, division one walipata wawili, division two wakapata sijui sita, wengine wote katika watoto 200 walipata four na zero. Hii maana yake ni dalili mbaya kwenye ubora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nini kinachangia hapo? Mimi nazungumza kama mwalimu na Mbunge wa Vijijini. Tusijifiche ukaweka kichwa chini kwenye katani, halafu huku nje ukasema umejificha, lazima tuambiane ukweli. Tuna upungufu mkubwa kwa mahitaji ya elimu kwa walimu wenyewe. Ukiacha upungufu kwa maana ya idadi, hawa walimu wanaweza kufundisha? Unaposema anafundisha hesabu, anaijua? Kiingereza anafundisha anakijua? Kiswahili hicho anakijua? Kifaransa anakijua? Au ni walimu ambao wanafundisha Kiswa-Kinge shuleni! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kuna shida, Mheshimiwa Profesa Mkenda kuna kazi ya kufanya ya ziada. Hawa walimu wetu, hii performance ndiyo maana unakuta kuna ukinzani kati ya shule za watu binafsi na shule za Serikali. Hawa watu binafsi wana walimu wa kutosha kila somo. Shule za Serikali hakuna walimu wa kutosha. Shule za private kuna wanafunzi idadi ndogo darasani, shule zetu kuna 100,000 mpaka 200,000 kwenye darasa moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa private wana motisha A moja kwa shilingi 100,000, hawa wa Serikali hawana motisha. Hawa wa private wana usafiri, wana chakula shuleni, wa Serikali hatuna. Hawa walimu wetu vijijini hawana nyumba. Leo tunazungumza matundu ya vyoo hayatoshi, lazima tukae kama Wabunge tuzungumze hali halisi. Hii imesababisha Profesa kwa kweli katika sehemu ambayo mimi mlinikwaza sana Wizara ya Elimu ni kitendo cha kundoa ranking. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani shule tunajua kabisa kwamba kama mwalimu analipwa vizuri, kama mwalimu ana usafiri, maeneo mengine wana ratiba ya chakula, halafu ana wanafunzi wachache, anaweza akamfuatilia mwanafunzi mmoja mmoja, obvious performance ya huyu wa wanafunzi wachache itatofautina na performance ya mwalimu ambaye ana wanafunzi wengi na hana sehemu ya kufikia na ana madeni na mshahara ni mdogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo lazima tulizungumze. Unapotaja shule imefanya vizuri, hivyo ni vigezo. Tunazo maabara ambazo ni mbovu hazijakamilika. Wenzetu wana maabara na vifaa. Tuna walimu wachache wa hesabu. Hivi kama una shule ambayo ni form one mpaka form four, hakuna mwalimu wa hesabu, mnatarajia apate A kwenye mtihani? Hiyo miujiza inatokea wapi? Sasa Profesa ungetuonesha mpango wa Serikali kupata walimu wa hesabu wa kutosha nchi hii, mpango wa Serikali wa kuleta walimu wa sayansi wa kutosha, mpango wa kuajiri walimu wa Tanzania ambao wako mtaani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa taarifa yako, Profesa sasa hivi vijana wetu wamekata tamaa kwenda kusoma masomo ya ualimu. Wanaona kama ni fani ambayo hawapati ajira huko mitaani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa taarifa yako Profesa sasa hivi vijana wetu wamekata tamaa kwenda kusoma masomo ya ualimu, wanaona kama ni fani ambayo hawapati ajira huko mitaani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe jambo hili pia liangaliwe upya, tupeleke walimu, tuboreshe mazingira ya kazi watoto wetu wasome vinginevyo kuzuia ranking eti wanafanyabiashara unajidanganya tu. Walimu wana magrupu, wanafunzi wana magrupu, wazazi wana magrupu, wanafunzi tunawasiliana na ukweli hata mimi watoto wangu wanasoma private.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtoto wangu wa form two anaweza akamshinda mwanafunzi wa kawaida wa form four mimi naangalia mimi ni mwalimu naangalia hata wanacho kifundisha, mazingira ya kufundishia na kujifunzia lazima yaboreshwe. Kwa hiyo, hilo lifanyike vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano mimi ni Mbunge wa Tarime Vijijini jirani na Kenya. Kenya walimu wa Serikali ndiyo wanalipwa vizuri zaidi kuliko private, nenda ufanye research. Kwa hiyo, inamaana Kenya unapoenda kuomba kazi walikosa kazi za Serikalini ndiyo wanaenda private, kwanini? Wanalipwa vizuri zaidi na motisha ni kubwa. Tunaweza kuiga jambo zuri si vibaya tukaiga na kwa maana ya kuanza kuboresha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, muingiliano na usimamizi wa elimu ni kweli kuna mapungufu kwenye private, wana michango mingi, wana masharti mengi lakini tuwe na chombo huru cha kuwasimamia. Hivi nimeamua kupeleka mtoto wangu private kwa kipato changu alafu unakuja kuniwekea masharti, tuboreshe shule za Serikali ambazo wananchi wengi masikini wanapeleka watoto wao. Watu walipeka Kenya, walipeleka Uganda, walikuwa wamerudisha, kwa mtindo wa sasa hivi tena watu wameanza kwenda Kenya na Uganda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuboreshe shule za Serikali, tuajiri walimu, tujenge maabara, tuboreshe huduma motisha alafu tushindane. Ila kwenye level ile ya chuo kikuu mimi natofautiana na wenzangu, kwamba mtoto wa waziri akope sawa sawa na mkulima kule Kangeliani, kule Nyabitucho, mimi nadhani tuliangalie. Vigezo vya mikopo ya elimu ya juu vinaweza kuangaliwa visiwe fixed. Mtu alikuwa ni mtumishi angeweza kusomesha mtoto, sasa amestaafu awe anaumwa, au mtu siyo Mbunge tuangalie vigezo hali halisi ya maisha ikoje? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tusikalili mambo, maombi yangu Mheshimiwa Waziri nina shule zangu sita nguvu za wananchi, shule ya Kubiterere, Kimusi, Nyagisya, Barata halafu Inchugu, Nyanungu hizi shule mpeleke wakaguzi kule zifunguliwe. Wananchi wangu wamechanga pesa wenyewe, wamejenga shule, wanataka watoto wao wasome ili tushindane na watu, kwetu tulichelewa sana kwenda shule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaomba hiyo Mheshimiwa Waziri hilo lifanyiwe kazi lakini wale wakaguzi wa udhibiti ubora wale hawana hata magari, posho zenyewe wanaenda kukagua huku awajalipwa wamekopwa, wanatangulia kazini halafu unataka akakague shule nzuri aridhike. Unakuta wanaficha ficha hata wamepokelewa wakapewa tu chakula, akapewa sehemu ya kulala, akahifadhiwa wanakaguaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, equip hiyo department ya udhibiti ubora watu wawe fame wawe sawa sawa wakague na vigezo tuvijue na kusiwe na meanders. Hata mkifungia shule kwenye matokeo, watoto wanaumia sana. Watoto wametoa hela mamilioni unafuta matokeo, unaadhibu watoto na wazazi, adhibu shule, adhibu wale wataalamu wetu msiumize wazazi wanaumia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho niunge mkono hoja ya Mheshimiwa Profesa Palamagamba Kabudi, mwalimu wangu nilitaka niwaombe Waheshimiwa Wabunge. Mkiangalia kwenye uchaguzi ukitaka kujua anachozungumza Mheshimiwa Profesa Palamagamba ni kwamba wakati wa uchaguzi hivi ni wananchi wangapi ambao walishindwa kupiga kura? wanaandikiwa ni wazi kwamba ni wengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tupeleke mfumo elimu ya watu wazima kwa kila kijiji wale ambao wapo tayari kusoma, wasome kuna wengine hawasomi kwa sababu hawana nafasi, kuna wengine wamesoma hakusoma sana malezi, tutoe fursa kwa wote kama ambavyo tumetoa fursa kwa wale ambao wamepata ujauzito na changamoto mbalimbali ya kurudi shuleni basi na hawa ambao hawakusoma vijijini wasome kwa hiyari na walimu wapo na vijana wetu wawepo. Pendekezo muhimu la mwisho kwenye ualimu… (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwita, ahsante sana. Kengele yako imelia.

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hii hoja ni muhimu niunge mkono kwa nguvu zote tupate mjadala wa kutosha kwenye mitaala ya elimu. (Makofi)