Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja ya Wizara ya Elimu. Kwanza kabisa napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uhai leo hii tunachangia masuala ya elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi zangu za kwanza napenda nimpongeze Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri aliyoifanya kuboresha elimu nchini kwetu Tanzania, hususan kwa kujenga shule za sekondari kila Mkoa kwa ajili ya watoto wetu wa kike ili waweze kusoma masomo ya sayansi. Nampongeza pia, kwa kujenga shule za VETA 63 ambazo zitaenda kujengwa kwenye Wilaya ambazo hazina shule za VETA. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza pia kwa ujenzi wa shule za sekondari zinazoendelea nchini Tanzania na nampongeza Mheshimiwa Rais kwa ujenzi wa madarasa kwenye shule zetu za primary kwa kutumia mradi wa Boost. Baada ya pongezi hizo napenda nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Profesa Mkenda na Naibu wake kwa kazi nzuri wanayoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi nyingine ziende kwa watendaji wote wanaofanya kazi Wizara ya Elimu na walioandaa mabadiliko ya sera ambayo tutakwenda kuitumia nchini kwetu Tanzania ikiwa ni mwongozo wa nchi yetu kwa miaka inayokuja. Nawapongeza kwa kuja na hiyo sera, lakini ninayo mambo mawili ya kuzungumza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Elimu inaleta sera, mtekelezaji wa sera ni Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Sasa bado tunayo matatizo kwenye shule zetu, matatizo ya madawati, matatizo ya upungufu wa vyoo, lakini pia na matatizo ya madarasa. Tunaomba huyu mtekelezaji wa hii Sera ya elimu aweze kuwezeshwa, lakini asimamiwe katika kutekeleza hayo, hususan kwenye suala la madawati, lakini pia kwenye suala la ujenzi wa vyoo, lakini pia kwenye suala la kukarabati zile shule kongwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye shule zile kongwe utazionea huruma. Ziko shule kule Mpanda ambazo hususan kama mimi niliondoka pale miaka mingi, ile rangi niliyoiacha bado ipo mpaka leo, mfano Shule ya Kashaulili Mpanda. Pia zipo shule nilizitaja mara ya mwisho nilipokuwa nachangia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, watoto kutoka darasa la kwanza mpaka la nne wanakaa chini, Shule ya Msakila, Shule ya Shanwe, Shule ya Nyegere, Shule ya Mkapa. Shule hizo watoto kutoka darasa la kwanza mpaka la nne wanakaa chini, hawana madawati, ukienda kwenye shule hizo pia vyoo havitoshi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapokuja na haya mabadiliko ya sera, naomba Wizara inaposimamia hii sera ili ikatekelezwe ihakikishe kwamba, hivyo vitu vipo vinatekelezwa. Madawati yapo na watoto wanakaa kwenye madawati, sio kukaa chini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nichangie kwenye suala la Walimu. Hapo zamani miaka ya nyuma kwa wale tuliozaliwa mbele kidogo kulikuja mfumo kwamba, mtu akimaliza darasa la saba anaweza akafundisha shule za primary, elimu ikayumba. Naomba tunapokuja kutekeleza hii sera Wizara ya Elimu ihakikishe kwamba, inafundisha Walimu watakaoenda kutekeleza hii sera ambayo tunakwenda kuitekeleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona kutakuwa na program. Tuna matatizo ya watoto wetu kufeli, lakini tuna matatizo pia ya watoto wetu kutokuwa na competence. Hivyo basi, tunaomba hii competence ya watoto ipelekwe kwanza kwa Walimu wafundishwe ili waweze kwenda kufundisha vizuri. Haiwezekani wewe umepata division four ukaenda kumfundisha mtu apate division one, kama alivyosema Mheshimiwa Dkt. Chaya. Kwa hiyo, naomba hilo liwekewe mkazo. Walimu wapelekwe training ili waje wafundishe hizi shule ambazo Waziri ameziita amali, zamani tuliziita ufundi na sijui kwa nini amezibadilisha jina? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala ambalo ningependa kulichangia hapa, napenda niunge mkono hoja ya Kamati ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Mheshimiwa Waziri katika Wizara yake ameruhusu Halmashauri zijenge shule za english medium, ameruhusu Halmashauri zichukue walimu ambao wanalipwa na Serikali wakafundishe shule za english medium. Halmashauri inakusanya kodi kutoka kwa wananchi, ina maana mimi kama nauza nyanya, nauza mitumba, nauza ndizi, nina duka, unakusanya kodi kwangu, ukishakusanya zile kodi kwenye halmashauri yangu unakwenda unanijengea shule ya english medium, halafu unarudi unaniambia kama nataka mtoto wangu asome pale nikulipe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naliona hili ni tatizo na linaenda kugawa Watanzania. Sasa hivi kuna halmashauri ambazo zimejenga shule za english medium na hili ni tatizo nimeona niliseme hapa na liko ni hoja ya Kamati ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, iliwasilishwa hapa Bungeni, lakini nimeona nichangie kwenye Wizara kwa sababu nafahamu hawa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa hawawezi wakajenga hii shule kama hawajapata kibali kutoka kwenye Wizara ya Elimu ambayo Waziri ni msimamizi wa sera hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, anawezaje kumtumia Mwalimu ambaye analipwa na Serikali akafundishe shule ya english medium, halafu utatumia yale mapato ambayo wewe umekusanya kodi kwa wale wananchi walioko kwenye hilo eneo? Hii si sahihi, tunakwenda kujenga matabaka na hatutaki matabaka nchini Tanzania kwa sababu, watakaosoma hapa watakuwa ni wale watoto wenye uwezo na wale watoto wa wafanyakazi. Yule mtu ambaye ulichukua kodi yake ya shilingi 200, anayechoma mahindi, anayeuza mitumba, anayeendesha bodaboda, hawezi akamleta mtoto wake pale kwenye ile shule ya English Medium. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hoja nyingine nakaa nikijifikiria, kama Waziri alisema kwamba, anakuja na hoja humu Bungeni kwamba, Kiswahili si ndio lugha yetu, masomo yafundishwe kwa Kiswahili, kwa nini anaruhusu Halmashauri zijenge shule za english medium? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ni hivyo, basi Kiingereza kifundishwe kwenye shule zote za Serikali kutoka darasa la kwanza, ili twende na usawa na ili tusiwe na matabaka. Suala la halmashauri kuanzisha hizi shule si sahihi, tuachie shule binafsi kwa sababu, wanakwenda kutumia resources zilezile za Serikali, lakini wanakwenda kutengeneza mapato, lakini ukiangalia chanzo chake ni hicho nilichokisema. Naona siyo sawa, na sioni sababu. Kama ni hoja kufundisha english medium basi namwomba Mheshimiwa Waziri hii english ifundishwe kutoka darasa la kwanza kwenye shule zetu zote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, tumesema lugha ni biashara, lugha ni uchumi, kama wachangiaji wengine waliopita walivyosema, lakini pia tunakwenda kwenye teknolijia ya kisasa. Unaposema nchi yetu ya Tanzania iendelee kukikumbatia Kiswahili, tuendelee kuwafundisha watoto Kiswahili hayo mambo yalitakiwa yafanyike 1961 tulipopata Uhuru, siyo sasa hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, 1961 tulipopata Uhuru ungesema basi tunakwenda na mfumo wa kufundisha watoto Kiswahili kitupu, lakini Kiswahili pamoja na Kiingereza ni official languages, ni lugha za Taifa, Kiingereza ni Lugha ya Taifa na Kiswahili ni Lugha ya Taifa. Sasa unapokuja kutoa lugha moja unasema ifundishwe kwa mtindo huu, ili nyingine ifundishwe kwa mtindo mwingine, mimi ninaona siyo sahihi. Ninataka Kiingereza kifundhishwe kutoka darasa la kwanza kwa watoto wote, kwa shule zote ili kila mtoto awe na competence, anapokwenda ku-compete huko nje kwenye interview, mtoto unakuta anajua kitu lakini kwa sababu hakuandaliwa na hakusomeshwa ana-feel uncomfortable, kwa sababu anashindwa kujieleza. Na matokeo yetu tumekuwa tukidai nchi za jirani watu wake wanafanya kazi nje, wanafanya kazi nje kwa sababu wanajua lugha, wanaongea Kiingereza, wanaongea Kiswahili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, utaendaje kufundisha Kiswahili Marekani, Ujerumani, Sweden kama hujui Kiingereza? Ni lazima ujue Kiingereza ili ukafundishe kile Kiswahili, ili uweze kutafsiri. Mheshimiwa Waziri ninaomba hili ulichukulie uzito.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, mengine nitaandika. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Taska Restituta Mbogo.
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)