Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ubungo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. PROF. KITILA A. MKUMBO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi. Kwanza nianze kwa kumshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kuniahidi kunipatia Chuo cha VETA kwenye Jimbo la Ubungo kwa sababu huwezi kuwa na kiwanda cha pili kwa ukubwa cha kutengeneza nguo, kinaajiri zaidi ya watu 4,000, unayo pale EPZA kubwa kuliko zote Tanzania ipo pale na Naibu Waziri anayeshughulikia kazi anafahamu alishafika pale. Kwa hiyo kuna vijana wengi, hivyo, nashukuru sana kwa kuniahidi kwamba tutashirikiana tupate Chuo cha VETA kwenye Jimbo la Ubungo hususan Kata ya Makuburi ambapo ina high concentration ya viwanda hapa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la pili ambalo nataka niongeze sauti yangu ni kwenye suala ambalo Waheshimiwa Wabunge wamelichangia kwa hisia kubwa, suala la lugha ya kufundishia. Kwanza nianze kwa kuungana mkono kabisa na jinsi ambavyo sera imependekeza, nadhani iko sahihi kabisa kwamba lugha zetu mbili zitatumika kufundishia Kiswahili kwenye ngazi ya chini na Kiingereza kwenye ngazi inayofuata.
Mheshimiwa Spika, suala la mjadala hili huwa lina sehemu mbili tu. Unaweza ukajadili kwa kuzingatia uzalendo wa lugha na utamaduni, hiyo ni sawa pia, hawa wanaita cultural romanticism, lakini unaweza kujadili pia kwa kuangalia taaluma. Nadhani sisi hapa kwa maana ya sera tunaangalia taaluma na kuangalia tunazingatia kupanua wigo kwa vijana wetu lakini pia hali halisi. Hali halisi ni nini? Moja ni makosa, kudhani kwamba Kiingereza ni lugha ya wakoloni, ilishaisha siku nyingi.
Mheshimiwa Spika, Waingereza wapo milioni 67 tu tunavyozungumza, lakini duniani hapa kuna watu bilioni moja wanaotumia Kiingereza kama lugha ya kwanza. Kwa hiyo Kiingereza kuwa lugha ya wakoloni iliisha siku nyingi ndio maana kuna Kiingereza cha West Afrika, Kiingereza cha South Africa, Kiingereza cha Kenya, Kiingereza cha Scandinavian kuonyesha kwamba Kiingereza kwenye lugha ya ukoloni kilishaondoka lakini sikiliza takwimu zifuatazo: -
Mheshimiwa Spika, asilimia 53 ya tovuti kwa maana ya website zote duniani zinatumia lugha ya Kiingereza. Lugha ambazo zinafuata ni chini ya asilimia 10. Kwa mfano, Kichina hiki ambacho watu wanakizungumza sana hapa asilimia mbili tu, Kifaransa asilimia nne, Kirusi asilimia sita, Kijerumani asilimia sita, Kihispaniola asilimia tano, Kireno asilimia tatu. Asilimia 53 iko kwa lugha ya Kiingereza, hiyo nakwambia kwamba lugha ya Kiingereza imeendelea kuwa lugha ya taaluma na biashara duniani. Ndio maana Lufthansa ambalo ni shirika kubwa la ndege lipo Ujerumani na Ujerumani ni Taifa ambalo ni very conservative kwenye lugha, lakini waliamua kubadilisha policy yao mwaka 2010 kufanya kwamba lugha ya Lufthansa ni Kiingereza kwa sababu ndio lugha ya biashara. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hilo tuondoke kwenye uzalendo wa lugha, hii sio lugha tena ya wakoloni. La pili, katika nchi kumi zenye mfumo bora wa elimu Afrika, nazizungumzia Seychelles, Mauritius, Afrika ya Kusini, Botswana, Kenya, Cape Verde na Namibia. Nchi saba zinatumia Kiingereza kama lugha ya kufundishia na tatu zinatumia Kiarabu hizi ni Algeria, Tunisia na Misri. Pengine niwape mfano wa karibu hapa Afrika nchi ambazo zinasemekana kama ni bora kwa elimu ni Seychelles na Mauritius na zinafanana na sisi, kwa sababu wale wana lugha Yao, Seychelles na Mauritius lugha yao ni Krioli ndio lugha ya Taifa, lakini lugha yao ya kufundishia ni Kiingereza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ukiingia mtaani, mtaani hutosikia Kiingereza ni Krioli lakini kwa Seychelles wanaanza na Krioli mpaka primary kama sisi, wakifika sekondari all the way ni Kiingereza. Mauritius wenyewe tangu awali wanaanza na Kiingereza all the way lakini ndio nchi ambazo tunazungumza zipo bora katika suala la elimu. Nchi 47 duniani zinatumia Kiingereza kama lugha ya kufundishia, kwa hiyo usije ukadhani ni hapa tu na nchi 143 duniani Kiingereza ni somo la lazima.
Mheshimiwa Spika, tazama kwa hapa Tanzania, nikupe takwimu hii na unisikilize kwa makini sana hii. Ukichambua takwimu za matokeo ya darasa la saba ambayo tunatumia Kiswahili miaka mitatu iliyopita, ukiangalia shule pale, kwa mfano Dar es Salaam, ukichukua shule 50 za juu ambazo zimefanya vizuri, shule ya kwanza mpaka ya 50 zote zinatumia Kiingereza kama lugha ya kufundishia ikiwemo shule ya Msingi Olympio ya Serikali ambayo ni moja ya shule za Serikali ambazo zinatumia Kiingereza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hiyo maana yake nini? Hatuwezi kulaumu Kiingereza kama ndio chanzo ya wanafunzi kufeli, sio kweli, kwa sababu shule za msingi zinatumia Kiswahili, lakini tafuta shule 50 bora utakuta ni zile ambazo wanatumia Kiingereza.
MBUNGE FULANI: Aliongea bila kutumia kipaza sauti.
MHE. PROF. KITILA A. MKUMBO: Hilo sitaki kusema.
Mheshimiwa Spika, tunapoandaa mitaala tunaangalia factors nyingi. Moja ya msingi ambayo lazima uzingatie mtaala wowote lazima uzingatie matakwa ya wazazi, wazazi wanataka nini na tuna takwimu mbili hapa. Kabla shule za binafsi hazijapamba moto Tanzania, Watanzania middle class wengi wakiwepo Wabunge hapa walikuwa wanawapeleka watoto wao Uganda na Kenya, walikua hawafuati elimu, walikua wanafuata Kiingereza. Baada ya shule kuanzishwa hapa wamerudi.
Mheshimiwa Spika, takwimu ya pili tulishafanya utafiti kati ya mwaka 2015 mpaka 2017, tuliwauliza wazazi, mngetaka watoto wako wafundishwe kwa lugha gani, asilimia 63 yaani wazazi sita mpaka saba kati ya kumi walisema walitaka watoto wao wafundishe kwa Kiingereza kuanzia awali mpaka chuo kikuu na utafiti wa mwaka jana, wa karibuni unaonyesha kwamba ni asilimia 70. Kwa hivyo ukiwa Waziri wa Elimu unapotengeneza mtaala huwezi kutengeneza mtaala ambao upo mbali na matakwa ya wazazi, wazazi ni sehemu muhimu sana kwenye suala hili.
Mheshimiwa Spika, hapa nazungumza nini? Ninachosema hapa hakuna shaka kwamba lugha ni nyezo muhimu sana kwenye suala la elimu na ni muhimu watoto na Walimu watumie lugha ambayo wanaijua, lakini lugha huzaliwi nayo, lugha unaipata kwenye mazingira hili ni jambo la msingi ambalo tunatakiwa tulizingatie. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hivyo na hatusemi hakuna tatizo la lugha Tanzania, la Kiswahili na Kiingereza, lipo, ni kubwa, lakini jambo la msingi hutatui tatizo kwa kulikimbia, unalitatua kwa kulikabili. Hapa nataka nipendekeze kwamba, maadam sera imeshaelekeza hivyo, hatua mbili lazima zichukuliwe. Hatua ya kwanza lazima tukubali kwamba tuna changamoto kubwa sana ya Walimu kwenye somo la Kiingereza, kwa maana ya idadi na hata ubora wao. Sasa nchi zingine walifanyaje na mimi nilipitia pitia, walipoamua kwenda mfumo ambao tunataka kwenda nao, walikiri tatizo, lakini jambo la pili waliamua kufungulia milango.
Mheshimiwa Spika, nataka kushauri kwamba Serikali itumie nafasi ya uwepo wa protocol ya hii ambayo tunazungumzia ya free movement of labor tumeshafungua East Africa. Sisi tunauza Kiswahili, sisi ndio wababe wa Kiswahili katika Bara la Afrika lakini wapo wenzetu ambao wametutangulia kwenye Kiingereza, tufungulie mipaka, miaka mitano mpaka 10 waje Walimu hapa kutoka ndani ya Nchi za Afrika, waje Walimu hapa wa Kiingereza wale tunawapelekea Kiswahili tunakarabisha Walimu wa Kiingereza. Ndani ya miaka mitano mpaka kumi tatizo hili litakuwa limekwisha.
Mheshimiwa Spika, nadhani hili ni jambo la msingi, kwa hiyo tuombe Wizara ya Elimu, lakini pia Ofisi ya Waziri Mkuu pale kwenye Ofisi ya Kamishna wa Labor kwa sababu wako very rigid, pale kupata vibali vya kazi ni kazi ngumu sana. Kwenye suala la elimu lazima walipitie upya, tu-relax ili tupate Walimu wengi wa somo la Kiingereza kutoka Nchi zingine. Itakuwa ni hatari sana Mheshimiwa Waziri tukabadilisha sera, tukabaki na sera ambayo tunayo ya kutumia Kiingereza halafu tusiwe na wafundishaji wazuri wa Kiingereza, itakuwa ni hatari kwa nchi, tutakuwa tumetwanga maji kwenye kinu. Kwa hiyo suala moja muhimu tuwekeze sana kwenye suala hili la Walimu wa somo hili la Kiingereza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, la mwisho, nataka kusisitiza kwamba hakuna shaka, tunakipenda Kiswahili chetu. Tunachosema ni kwamba watoto wa Kitanzania hapa walipofika lazima wawe Kiingereza kizuri, Kiswahili kizuri na itafika mahali hata kitabu kitakuwa kwa lugha ya Kiswahili kwa lugha ya Kiingereza. Akisoma Archimedes Principle haielewi anafungua Kiswahili. Hata mtihani ukija hakuna tatizo lolote, anapewa mtihani upo kwa Kiingereza upo kwa Kiswahili. Akiona anaweza akajibu kwa Kiswahili vizuri anafanya kwa Kiswahili wala hatuna sababu, muhimu ni kwamba maarifa yapatikane kwa lugha mbili hizi, Kiswahili na Kiingereza na lugha isiwe kikwazo kwenye kupata elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja na niwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa jinsi ambavyo walirejea kwenye ripoti yetu kwenye suala hili. Ahsante sana. (Makofi)