Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Rombo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa fursa hii ya kuchangia na kutoa hoja.
Mheshimiwa Spika, naomba nianze kwa kutoa shukrani zangu za dhati kwa Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia kwa kuzungumza na kwa maandishi, rekodi inaonesha tumepata michango jumla ya 51 na shukrani za kipekee nazipeleka kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo chini ya Mwenyekiti Mheshimiwa Profesa Kitila Alexander Mkumbo na Makamu Mwenyekiti Mheshimiwa Husna Sekiboko. Michango yote ya Kamati tumeipokea mingi ni muhimu sana kwa asilimia kubwa tutayafanyia kazi na mahali tutakapohitaji kujadiliana tutajadiliana nao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa ujumla tunashukuru sana kwa kuungwa mkono kwa sehemu kubwa mno kwa hoja yetu hii tuliyoileta, kwa ushauri na maelekezo ambayo Waheshimiwa Wabunge wametupa, naomba niseme ahsanteni sana Waheshimiwa Wabunge na ahsante hizi ni kutoka kwangu na kutoka kwa wenzangu wote wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba sana mpitishe bajeti hii kama tulivyoomba. Kabla sijazungumza hoja na masuala mbalimbali ningependa kumshukuru sana kwanza Mheshimiwa Omari Kipanga, Naibu Waziri wa Wizara yetu na Katibu wetu Mkuu Profesa Nombo, Naibu Katibu Mkuu Profesa Mdoe, Naibu Katibu Mkuu Dkt. Rwezimula pamoja na Kamishna wa Elimu Dokta Mtahabwa na watumishi wote wa Wizara na taasisi zote kwa kufanya kazi pamoja nasi, kwa sehemu kubwa na chochote ambacho tutakuwa tumefanikiwa kwa kweli ni kazi imefanyika kama team work. Nashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba niitumie fursa hii vilevile kuwashukuru wananchi wetu wa Rombo kwanza kwa kumuunga Rais wetu mkono, wanaendelea kumuunga mkono kwa asilimia kubwa sana. Wanaiunga mkono Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Dokta Samia Suluhu Hassan na vile vile wanaendelea kuniunga mkono katika shughuli zangu za Ubunge na wanatambua kwamba muda mwingi nipo huku kwa shughuli za Kitaifa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee sana naomba nikushukuru wewe na uongozi wote wa Bunge letu. Naibu Spika na Wenyeviti kwa kutuongoza vizuri sana katika shughuli hizi. Natoa shukrani zangu za dhati sana kwa Walimu wote, Wakufunzi na Wahadhiri hapa nchini na nadhani tuliwaleta wale walimu wanaofundisha kwa namna ya ubunifu na hamasa sijui kama wapo humu ndani. Sasa hivi clip zao zilikuwa zinatembea, labda wangesimama sijui kama mimi naruhusiwa kutambulisha watu lakini walimu hawa katika mazingira hayo hayo wako Mikoani wanafundisha kwa namna ambayo kwa kweli inatia hamasa unatamani ungerudi kuwa mtoto ufundishwe na walimu kama hawa, wako wengi lakini tumewaalika wawili hapa kwa kuwapa heshima na wengine tutaendelea kukutana nao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunao wadau wengi wa elimu. Wadau wetu wa elimu kwa ujumla tunashukuru sana na wengine wako hapa, wengine ni local kwa mfano nadhani Meneja Mkazi Roselyn Marik wa ‘So they can Tanzania’ ambaye tunashirikiana nadhani yuko humu ndani vilevile tuko naye, na Rais wa Tanzania Academy of Sciences Profesa Yunus Mgaya ambaye nadhani yuko humu ndani. Wamiliki wa shule binafsi ambao kwa kweli kama alivyosema Mheshimiwa Mulugo na ninakushukuru sana kulisema hili, nakushukuru sana kwa dhati ya moyo wangu, kwamba tumefanya nao kazi kwa karibu sana sekta binafsi, tumeshirikiana nao sana kama nitakavyoeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hoja zilizotoka hapa nyingi kama nilivyosema tutazibeba. Zipo hoja nyingine ambazo zinagusa sekta ya elimu zote lakini nyingine za TAMISEMI, nyingine Utumishi na kadhalika lakini zote zinagusa sekta ya elimu, nitajaribu kuzieleza zote nyingine tutazifanyia kazi ndani ya Serikali.
Mheshimiwa Spika, kimsingi Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia wote kabisa wote kabisa wamempongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, wamempongeza sana kwa jinsi ambavyo ametoa kipaumbele kikubwa sana kwa ujasiri mkubwa sana kwa utashi mkubwa sana wa kisiasa kwa sekta yetu ya elimu kama ambavyo nitajaribu kueleza kidogo hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, utaona kama alivyosema Naibu Waziri hapa VETA sasa hivi katika Wilaya 64 pamoja na mikoa, kumaliza wilaya zote ambazo hazina VETA. Mradi wa HEET Mikoa 14 inanufaika kupata kampasi za vyuo vikuu ambavyo vilikuwa hamna. Hakuna Mheshimiwa Mbunge yeyote hapa ambaye kwake katika jimbo lake hakuna shule mpya, madarasa mapya, pengine kampasi ya chuo kikuu, kuna VETA inajengwa na kadhalika. Hakuna Mheshimiwa Mbunge yeyote ambaye hana suala la elimu ambalo analo la kujivunia na kulisemea kwa wananchi na kwa sababu kwa kweli haya ni maelekezo specific ya Rais wetu Mheshimiwa Dokta Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusu Walimu, Walimu ndiyo watumishi walio wengi zaidi Serikalini, kwa walimu ujasiri wa Rais wetu kusema kwamba tuende kwenye sensa, tutumie vishkwambi ili vishikwambi hivyo vianze sasa kutumika katika kufundisha na vimegawanywa kwa walimu wote kabisa wote Tanzania Bara na Visiwani pamoja na Maafisa Elimu na wakufunzi wa vyuo vyetu vya FDC, VETA pamoja na Wadhibiti Ubora hapa nchini, yalikuwa maamuzi ya Mheshimiwa Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusu wanafunzi wa vyuo vikuu, pamoja na kukutana uongozi wa wanafunzi wa vyuo vikuu kuwaongezea maslahi yao lakini ameendelea kuongeza fursa ya mikopo kubwa sana kwa wanafunzi wote. Kwa hiyo, kwa kweli ninaelewa kabisa ni kwa nini kila kila kila Mbunge aliyezungumza hapa bila kukosa na tumerekodi wote kila mmoja alianza kwa kusema tunampongeza na kumshukuru sana Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kubwa kuliko yote na ninadhani Mwenyekiti wetu wa Kamati Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo alilieleza vizuri sana. Kubwa kuliko yote ni maamuzi magumu ya Rais wetu kwamba tufanye mageuzi makubwa sana kwenye elimu, kwa kufanya mapitio ya sera na mabadiliko ya mitaala. Mageuzi haya yana gharama na mara nyingi ni rahisi sana kutafuta kitu ambacho matunda yake yanaonekana katika miaka miwili, mitatu, minne, mitano, lakini mageuzi haya ya elimu matunda yake halisi yataonekana kwa muda mrefu zaidi.
Mheshimiwa Spika, inahitaji utashi mkubwa sana wa kisiasa kuingiza Taifa katika maamuzi haya mazito, kufanya mabadiliko yatakuwa na gharama zake na matokeo yake makubwa yatakuja mbele ya safari. Kwa jambo hili kubwa hata mimi binafsi na yote aliyoyafanya Rais wetu, naungana na Waheshimiwa Wabunge wote kumpongeza na kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwa kweli mimi na wenzangu wote katika Wizara tunajisikia tuna bahati kubwa sana kupata fursa ya kuhudumu kipindi hiki ambacho Rais wetu ameelekeza jicho lake, ameelekeza maono yake katika sekta ya elimu.
Mheshimiwa Spika, chochote kitakachotokea hapa pengine wengine watatutaja mimi, wengine watamtaja Ndalichako kwa sababu tulikuwepo lakini yalikuwa ni maelekezo ya Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mheshimiwa Rais tunamshukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nawashukuru sana vilevile viongozi wetu Wakuu Mheshimiwa Dkt. Isdor Mpango, Mheshimiwa Dkt. ` Hussein Mwinyi kwa sababu suala la elimu kuna sehemu inaenda across the border na Rais wetu na kutupa miongozo mingi mizuri kutuwezesha kusonga mbele na Mawaziri wenzangu ambao tunafanya kazi vizuri kwa pamoja kumsaidia Rais wetu.
Mheshimiwa Spika, jambo moja ambalo limezungumzwa kubwa sana ni kuhusu muingiliano na mgongano wa majukumu kati ya sekta ya elimu na TAMISEMI. Kamati imezungumza, nadhani Mheshimiwa Mulugo ndiyo amelifafanua zaidi specific maeneo ambayo yanaumiza na mapendekezo yametoka kwamba kuwe na chombo maalum cha kusimamia elimu nchi nzima au pengine elimu yote iwe chini ya Wizara moja na kadhalika. Sasa kuna suala la ugatuaji na suala la kuendesha ugatuaji kwa ufanisi nadhani suala linahitaji mjadala.
Mheshimiwa Spika, suala la kuwa na chombo cha kusimamia elimu ni pendekezo ambalo nadhani limeletwa katika mapitio ya sera na ninajua tutapata fursa Waheshimiwa Wabunge wote kupitia mapitio hayo na kulizungumza, vilevile tukumbuke kwamba ugatuaji wa madaraka una sababu zake, msingi wake na umuhimu wake.
Mheshimiwa Spika, nitalizungumza suala moja ambalo lilizungumzwa hapa na Mheshimiwa Mulugo. Tunajua kwamba TAMISEMI inamiliki shule kama ambavyo BAKWATA inamiliki shule, Baraza la Maaskofu linamiliki shule, sekta binafsi zinamiliki shule. Wizara ya Elimu iko pale inasimamia sera, sheria na kadhalika. Kama ambavyo Waziri wa Kilimo anaweza asiwe na mashamba lakini kuna watu wana mashamba na kuna mashamba mengine ya Serikali mengine ya watu binafsi anamiliki pale.
Mheshimiwa Spika, sasa changamoto moja aliyoisema Mheshimiwa Mulugo na ninaitolea utatuzi hapa hapa ni kwa TAMISEMI kuchukua wakati mwingine jukumu la kutoa amri kwa shule binafsi kwamba sasa kuna mitihani wote lazima mfanye, lazima mfanye leo, keshokutwa mfanye na mlipie. Nimeongea na Kamishna wa Elimu kwa sababu na mimi naheshimu mamlaka yake japokuwa mimi ni Waziri na ameniambia atatoa tamko, maelekezo kuanzia sasa hivi, kuanzia leo shule binafsi hazitalazimishwa kufanya mitihani ambayo inapangwa na Halmashauri na kadhalika kwa amri na kuchangia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunahimiza zishiriki kwa hiari kufanya mitihani hiyo lakini hazitolazimishwa kufanya mitihani, taratibu za mitihani na kadhalika zinatolewa na Kamishna wa Elimu kwa mujibu wa Sheria yetu ya Elimu ambayo ipo, nadhani hilo tunaweza tukalimaliza. Yako mambo mengine chungu mzima ya ufanisi tu kati ya TAMISEMI na Wizara ya Elimu kwa sababu na tunafanya kazi vizuri sana kwa kweli na nadhani tutaendelea kufanya hivyo lakini suala la mitihani Kamishna ameniambia atalileta, tutaliona, tutalimaliza kwa namna hiyo. Mengine tutaendelea kuyajadili katika sera na sheria.
Mheshimiwa Spika, wengi wamezungumzia sana kuhusu mapitio ya sera na mitaala. Mmoja alisema kwanza tuanze kubadilisha sheria. Kimsingi sheria inatokana na sera. Ni vigumu sana kubadilisha sheria ya mwaka 1978 sasa hivi ya elimu kabla ya kubadilisha sera. Kwa mfano, sera ya mwaka 1978 ndiyo inasema elimu ya lazima ni miaka saba. Huwezi kwenda kubadilisha sheria kwanza ukasema kwamba sasa sheria iseme elimu ya lazima miaka 10 bila kuwa na sera inayosema elimu ya lazima ni miaka 10. Nawahakikishia na mtakumbuka mwaka jana wakati nilivyokuja hapa mbele yenu kwenye Bunge lako Tukufu, nilieleza kwamba kuna mambo saba ambayo tutakuwa tunayafanyia kazi.
Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza nilisema ni sera, nikasema mitaala, nikazungumzia sheria, nikazungumzia idadi ya walimu, nikazungumzia ubora wa walimu, nikazungumzia miundombinu, nikazungumzia vitendea kazi na kadhalika. Vitu saba tuliweka kwenye bajeti ambavyo bado tunavifanyia kazi. Kwa hiyo, suala la sheria litakuja tukishamaliza tu sera hii, kuna masuala chungu nzima ambayo itabidi tuende tukabadilishe kwenye Sheria ya Elimu ya Mwaka 1978, ama kuifumua yote upya au kufanya mabadiliko kulingana na jinsi ambavyo sera itakuwa imepita.
Mheshimiwa Spika, kadhalika mitaala, kwa kawaida mitaala mingi inapita Waheshimiwa Wabunge haiji Bungeni, haiji kujadiliwa hapa. Sasa hivi tumeileta hapa kwa sababu mitaala hii inaendana na structure mpya ya sera ambalo ni jambo kubwa sana, hatuwezi kulibeba wenyewe tu kama Wizara na kwenda nalo. Kwa hiyo, naona tumeleta tutakapopeleka hata cabinet paper itakuwa na mapitio ya sera na itakuwa addendum ya mitaala jambo ambalo mara nyingi linamalizwa kwenye taasisi ya elimu tu huko nyuma tulivyokuwa tunakwenda. Kwa hiyo, ndivyo ambavyo tutakuwa tunakwenda katika kufanya hilo.
Mheshimiwa Spika, sasa yako masuala chungu mzima yamezungumzwa hapa kuhusu mapitio ya sera. Pengine nisingependa niyajibu yote, kwa sababu gani? Tuliomba na ulitupa ruhusa tukafanya semina kwa Waheshimiwa Wabunge, tukawapitisha kwenye mapitio ya sera na mitaala, lakini tulifanya wakati wa break baada ya kukutana asubuhi halafu tulikuwa turudi mchana. Wabunge wengi wakasema; najua Mwenyekiti wa Kamati ambaye alikuwa ana-chair pale, akasema atakuona, kwamba ni vizuri tutafute siku ya weekend, tuwe na kutwa nzima ya kupitia mapitio ya mitaala tuliyoyafanya pamoja na sera hiyo ili tuweze kupata maoni kamili.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, baadhi ya maoni niliyokuwa nayasikia hapa kwa kweli, naamini kwa sababu kumekuwa hakuna muda wa kutosha kupitia, na tutaomba tupate kibali hicho hapa tunavyoendelea, na ninaomba sana tuweze kupata kabla ya tarehe 31 Mei, 2023.
Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge, pamoja na kwamba tutaomba tuwapitishe tupate maoni yenu, kwa sababu tunaamini sana nyie ni wawakilishi wa wananchi wote wa Tanzania, lakini hata mwenye maoni tutaendelea kuyapokea, kwa sababu baada ya kufanya kongamano lile kubwa tulitangaza hadharani makusudi ili kuchochea watu wengi zaidi walete maoni, na watu wengi sana walifuatilia na wengi wanaendelea kuleta maoni. Tunaendelea kupokea maoni. Tunatarajia kwamba tukifika tarehe 31 Mei, 2023, kwa kweli kila mtu atakuwa ameshaleta maoni yake, tutayachakata na kuandaa cabinet paper kwenda kupata approval kwa Mheshimiwa Rais kupitia washauri wake ambao ni Baraza la Mawaziri.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hata baada ya mambo tuliyoyazungumza hapa, japokuwa nitayazungumza tena kidogo, kwa mfano suala la lugha, bado kuna fursa ya kutoa maoni, kuyaleta na kuona namna ambavyo tunaweza tukayachakua. Nitafafanua kidogo kuhusu suala la lugha, lakini umuhimu wake ndiyo huo, bado safari ya kukusanya maoni ipo. Ilianza mapema wakati Mheshimiwa Profesa Joyce Ndalichako akiwa Waziri wa Elimu, tumeendelea nayo. Ndiyo maana nasema haya mageuzi ni makubwa sana, na hatufanyi kwa kukurupuka.
Mheshimiwa Spika, kuna suala limezungumzwa sana kuhusiana na sera na sheria, kwamba sasa hii sheria mkifanya, kuna uhaba wa walimu na uhaba wa miundombinu. Hatuwezi kukataa ukweli wa uhaba mahali ulipo, takwimu zenyewe zipo. Tuna kitabu kinaitwa Basic Education Statistics of Tanzania, kiko hadharani, kila mtu anaweza akaangalia. Pupil Teacher’s Ratio katika kila Halmashauri ni kiasi gani? Ni facts ambazo tunazo na sisi Wabunge tunafahamu maeneo yetu.
Mheshimiwa Spika, upo upungufu tunaweza tukaukiri, lakini shukrani zote tulizompa Mheshimiwa Rais hapa ni kwa sababu speed ya kuongeza miundombinu mashuleni sasa hivi wote tumeiona. Kwa kasi hii, tunatarajia kwamba tunaweza tukaendelea na safari hii ya mageuzi tunayoyafanya wakati tuna-catch up na miundombinu. Tunaona jitihada za Rais wetu sasa hivi za kuanza kuajiri. Ujue kwamba ajira ilikuwa frozen kwa muda fulani ambayo inaleta changamoto kidogo kwa sababu kuna watu wengi walimaliza shule hawajaweza kuajiriwa, lakini tunaona kwa kuangalia budgetary implication jitihada za kuajiri zinaendelea.
Mheshimiwa Spika, zaidi niseme vilevile kuna suala limezungumzwa hapa la mwongozo, Mheshimiwa mmoja alisema hapa, mwongozo wa walimu wa kujitolea. Wiki hii tunautoa na tumeanza kuzungumza na watu ambao wanaweza wakatusaidia kuhakikisha kwamba kweli, tunaweza kuhakikisha kwamba hawa wanaweza wakatusaidia kufundisha. Tutatumia teknolojia vilevile kuhakikisha kwamba tunapambana na uhaba huu wa walimu. Kuna mambo mengi sana tunaweza tukayafanya wakati ambapo Serikali inaangalia budgetary implication inaongeza ajira za walimu, nasi tutajitahidi kufanya hivyo hivyo. Hii ni pamoja kwa wakufunzi na Wahariri wa Vyuo Vikuu.
Mheshimiwa Spika, sasa hivi unaweza kuona kuna Mhadhiri wa Econometrics, yuko Dar es Salaam anafundisha darasa la UDOM. Tumefanya hivyo, najua nilivyokuwa nafundisha pale, watu wanafundisha kwa zoom, unafundisha watu wako Ghana, unafundisha kutokea Dar es Salaam. Nadhani tunaweza tukajitahidi hivyo kwenda mbele. Hata hivyo, Rais wetu kwa mwendo anaoenda nao, tunaamini kwamba tunaweza tukasogea mbele kuhakikisha kwamba tutapata hivyo.
Mheshimiwa Spika, suala lingine kubwa ambalo limezungumzwa sana ni tahadhari, kwamba mageuzi haya tumejiandaa vipi? Tunaendaje kutekeleza mageuzi haya? Yupo Mheshimiwa mmoja, nadhani ni Mheshimiwa Shigongo kama sikosei, alisema, tusijadili sana, dunia inaenda kwa kasi sana. Tutakuwa na mitaala, kabla haijatekelezwa utakuta tumeshapitwa na wakati. Wako wengine nadhani Mheshimiwa Tabasam alisema, tuwe tahadhari. Alitupa historia sana ya mageuzi ya mitaala tangu wakati wa Ujerumani mpaka sasa hivi. Kwa hiyo, haya yote ni muhimu, kwenda kwa kasi ili tusichelewe na kuchukua tahadhari ili tusiboronge. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa kalenda ile ya utekelezaji ambayo tuliileta kwenye semina kwenu, tulisema kwamba mwezi Januari mwakani tunaanza na pilot. Tunaishi kwa matumaini kwamba kwa kweli pendekezo letu litapita, rasimu hizi zitakubaliwa, iwe ni sera ya elimu na mafunzo 2014, Toleo la 2023 na mitaala yake itapita. Sisi tumeamua tunaanza kidogo kidogo mafunzo ya amali kwa sababu tunataka mafunzo ya amali tusiharibu. Hatutaki anayekwenda kwenye mafunzo ya amali ajisikie ni failure. Hatutaki kujenga mazingira ya mwanafunzi ambaye angependa kwenda upande wa mkondo wa mafunzo ya amali, aone kwamba kila mtu atamwona ni failure. Ndiyo maana tumeweka pathway ya mikondo yote miwili.
Mheshimiwa Spika, ukienda elimu jumla unaweza ukaenda mafunzo ya amali baadaye, ukienda mkondo wa mafunzo ya amali, utapunguza masomo, lakini bado kuna pathway ya kwenda high school na kwenda chuo kikuu kama kawaida. Tunataka tuhakikishe kwamba wote wanajisikia ni Watanzania bila kubaguliwa. Tutajenga mkakati baadaye wa namna ya kuwashauri wanafunzi kwamba wewe umefika Darasa la Sita, tunadhani itatusaidia sana, wewe unapenda sana michezo ukichukua masomo yako manne, matano halafu ukaenda Shule ya Michezo A-Level, utaenda mbali sana kwenye michezo, lakini unaweza ukaenda Chuo Kikuu kupitia yale masomo machache ambayo unachukua, halafu baadaye ukaenda ukafanya Diploma ukaendelea. Kadhalika mwingine anaweza kufanya hivyo.
Mheshimiwa Spika, sasa tulichofanya, tumechagua shule ambazo ni prestigious. Zamani kila mtu anajua tuliosoma enzi hizo, kwamba walikuwa wanaenda zile shule zilikuwa zinaitwa Tanga Tech., Ifunda Tech., Bwiru Boys Tech., Moshi Tech., ndio wale waliofanya vizuri sana darasani. Tena uwe mzuri sana kwenye hesabu, lakini yale mafunzo ya amali, ukisoma form one ukiingia form two unapata cheti. Hata ungeacha shule, unaweza ukaajiriwa kwa sababu una cheti. Ukifika form five unapata cheti cha level fulani unaondoka.
Mheshimiwa Spika, sasa tumeamua kwamba sisi tunaanza na vyuo vya ufundi vile tisa. Tumeweka bajeti hii ambayo tunaomba muipitishe sasa hivi, ili vyuo vifuatavyo tunaenda kuviwekea miundombinu. Tunavifahamu, tumevikagua ili mwezi Januari vichukue wanafunzi, waanze mwaka wa kwanza kwa mitaala mipya ambapo watakuwa na masomo machache ya elimu jumla. Watafanya shughuli nyingi zaidi ambazo ni mafunzo ya amali, wakimaliza pale, ni full technician, wako very qualified, wanaweza wakaajiriwa, lakini wakitaka, wanaweza kwenda kwenye diploma, wakitaka yale masomo machache wanaweza wakaenda high school. Shule hizo ni Bwiru, Chato, Ifunda, Iyunga, Moshi, Mtwara, Musoma, Mwadui na Tanga. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, napenda niseme, hapa yuko mdau, nilimtaja Rose Mariki makusudi kabisa ambaye alitusaidia sana kujenga chuo kule Babati, wamesema na wenyewe wanataka kuweka hela kuhakikisha kwamba tunaweza tukaanza shule ya mafunzo ya amali. Sekta binafsi pia, wengine wameshajitolea sasa hivi wanasema tuko tayari. Sijui kama naweza nikawataja, walisema tuko tayari, tupate maelekezo na mitaala hiyo na sisi tuhakikishe na sisi tuna shule zetu za mafunzo ya amali ambazo zinafuata mitaala yetu, halafu tunasonga mbele.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunaanza kwa pilot, lakini tunavyoenda kufanikiwa, tutasonga mbele. Zaidi ya hapo, tunaanza na walimu. Tumetenga bajeti. Kwenye bajeti hii ambayo tunaipitisha sasa hivi, tumetenga bajeti za kuandaa walimu wa kwenda kufundisha. Tunaangalia shule za ufundi, zina walimu, lakini hawatoshi, kwa hiyo, tunafanya juhudi za kuwafundisha lakini training, re-training, and re-orienting kwa walimu wetu itakuwa ni kazi kubwa sana mbele yetu kwa sababu baada ya document hizi kupita ambazo nadhani baadhi ya Wabunge walisema ni one of the best kwa kweli, tunaweza tukaharibu kama tusipokuwa na very good management ya process ya implementation. Kwa hiyo, tunakwenda hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nizungumzie kidogo suala la lugha kwa sababu limeleta mjadala hapa. Kwanza niseme, hatujafunga mjadala, hatujafunga maoni, kwa hiyo, siyo uala la kusema kwamba tumeshapitisha. Zile zinaitwa rasimu na tumesema maoni mpaka tarehe 31 Mei tutapokea maoni. Tuna semina ya Wabunge inayokuja na kuna nafasi ya kuzungumza sana.
Mheshimiwa Spika, kwenye lugha kuna vitu viwili ambavyo vimefanyika ambavyo ni vizuri sana tuvione. Kwanza, kwenye sera yenyewe imetoa fursa ambayo ipo sasa hivi, kwamba ukitaka kuanzisha shule yako hii iwe english medium ambayo ni primary, wakati huo itakuwa kuanzia elimu ya awali mpaka darasa la sita, unaomba kibali maalum, unakaguliwa, umejiandaaje, unaweza ukapata. Ukifika form one kwenda juu ni Kiingereza, ila ukitaka form one kwenda juu kufundisha Kiswahili, unaomba kibali maalum, ukaguliwe kama umejiandaaje. Kama umejiandaa vizuri unaweza kufundisha unaendelea.
Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo, hatuwezi sisi kama Taifa tukasema tumefungia Kiswahili, lakini najua mwendo wa kwenda kwenye Kiswahili utakwenda kwa tahadhari kubwa hata wazazi wengi, kama alivyosema Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo, kwa tahadhari kubwa kwa sababu tutapenda kuhakikisha kwamba kweli tunapokwenda kule hatutashusha kiwango cha elimu. Milango iko wazi, nasi kama Serikali tutajitahidi kuhakikisha kwamba hata watakaokwenda kule, kweli wakatoe elimu ya viwango. Kwa hiyo, hilo lipo.
Mheshimiwa Spika, la pili ambalo tumelifanya kubwa, na maoni yametolewa na Mheshimiwa Husna, na Mheshimiwa wakati unaongea nilijua ulisoma document thoroughly, kwa hiyo, nilikuwa very excited wakati unaongea. Kwa sababu ufundishaji wa lugha umebadilishwa kwenye mitaala, na ninaomba msome mitaala hiyo. Hatufundishi tena sijui syntax, sijui nini; rules nyingi sana, halafu unamaliza darasa la saba huongei Kiingereza. Unafundishwa Kiingereza cha kuongea, ukimaliza darasa la saba ni aibu uanze kusoma Kiingereza, unamaliza huwezi kuongea, darasa la saba. Kadhalika unamaliza darasa la saba, unaboronga Kiswahili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo, hata tunaposema kwamba vijana wetu wanamaliza darasa la saba sasa hivi hawaongei Kiingereza, ina maana ufundishaji wetu hauendi vizuri. Kwa hiyo, tumefanya mapitio, tutumie wataalam wa lugha, ufundishaji huu uache kukazia rules ambazo ni so boring, mwanafunzi hajui kama anajifunza lugha, ajifunze straight namna ya ku-communicate na kuongea, kwa sababu watu wanajifunza Kimasai, wanajifunza Kiusukuma, wanajifunza Kinyakyusa, wanaelewa ndani ya miaka mitatu. Utakaaje shuleni miaka minne unajifunza Kiingereza utoke huwezi kuongea Kiingereza chenyewe!
Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi ya hapo, sasa hivi somo la Kiingereza litaanzia darasa la kwanza. Litafundishwa kama somo moja na tutahakikisha kwamba ukimaliza Darasa la Sita, kweli uweze kuongea Kiingereza. Hizo rules zitakwenda tu kwa sababu huko mbele ya safari tutazungumza suala la communication na kadhalika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa alipokuwa anazungumza hapa, kwa kweli na mitaala iko huko. Nakuomba usome, kama kuna comments zaidi tutazipokea na comments nyingine kutoka kwa watu wote mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hata Kiswahili, kwa sababu tusije tukadhani kwamba watu wanaongea Kiswahili fasaha kwa Tanzania. Kwa sababu tunasema kwamba tuongee Kiingereza fasaha, Kiswahili chenyewe tunaboranga. Sikilizeni tu watu wanapoongea, hata tafsiri tu na lafudhi na kadhalika, ni vitu ambavyo lazima shuleni tujaribu kuviimarisha na kuvifanyia kazi.
Mheshimiwa Spika, sasa nizungumze suala lingine; je, Serikali inaona sekta binafsi ni washindani? Yaani shule binafsi ni washindani wa Serikali? Narudia tena, yaani Wizara inaona shule binafsi, vyuo binafsi ni washindani? Never, hapana, haijawahi kutokea, haitatokea na haiwezi kutokea chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, na haitatokea baadaye. Hii ni Serikali ya wananchi na hizi shule zinafundisha Watanzania.
Mheshimiwa Spika, mimi binafsi, bosi wangu alikuwa Mheshimiwa Charles Mwijage, alikuwa Waziri wangu, ndio aliniagiza tutengeneze blueprint ya kuimarisha sekta binafsi. Tulifanya kazi hiyo, siyo kwa sababu nilielekezwa na bosi wangu, we had passion ya kusimamia na kuendeleza sekta binafsi. Blueprint mpaka sasa hivi inazungumziwa. Haiwezekani leo, mimi binafsi kwa mfano, niko Wizara ya Elimu halafu nianze kufanya kazi dhidi ya sekta binafsi. Hapana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, shule binafsi pamoja na vyuo vikuu vimekuwa msaada mkubwa sana Tanzania, na nadhani Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo, sikumbuki nani alisema hili. Tulikuwa tunaona watoto wetu wadogo wanaondoka wanaenda kusoma Kenya na Uganda. Leo mabasi shule zikifunguliwa, huoni wanakwenda, shule zimetufuata nyumbani. Tunazifurahia, tutazilinda, tutazitetea. Narudia tena Mheshimiwa Mulugo kwa kusema ukweli hapa, kwamba tumekutana mara nyingi sana na kuongea. Kwa kweli ndiyo mwendo wetu, na tutakwenda kufanya kazi hivyo hivyo mbele ya safari. Tutakaa pamoja na tutaendelea.
Mheshimiwa Spika, niwaambieni ukweli maelekezo ya Rais wetu. Hivi vyuo binafsi, tumetenga hela kwa vyuo binafsi kuwasomeshea wahadhiri wao. Mara ya kwanza Serikali inatoa hela kwenda kusoma. Wataenda kusoma Wahadhiri binafsi South Africa. Unalipiwa na Serikali kwa sababu unafundisha chuo binafsi. Kwa hiyo, Serikali hii haioni kabisa sekta binafsi kama ni wapinzani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, juzi tulipokutana mara ya mwisho, alikuwa Mwenyekiti wa Wamiliki wa Shule, alisema kitu kimoja, na nitakirudia, kwamba na sisi sekta binafsi tusaidiane na Serikali, kwa mfano katika kupambana na wizi wa mitihani. Tusionekane sisi tunalalama kwamba Serikali kwa nini tunapambana na wizi wa mitihani, na sisi tusaidiane kupambana na wizi wa mitihani. Yeye mwenyewe ni owner wa shule akasema, mimi binafsi niligundua nilikuwa natoa motisha kwa walimu wanaofanya vizuri wakawa wana- organize wizi wa mitihani, nimechukua hatua. Hiyo ilitoka sekta binafsi yenyewe. Kwa sababu sisi tunapopambana na wizi wa mitihani, hatupambani na sekta binafsi wala sekta ya umma.
Mheshimiwa Spika, sisi tuliofanya mapitio ya mitaala katika mikutano yetu yote kabisa, tumekuwa tukiita sekta binafsi, wamiliki wa shule, walimu kutoka sekta binafsi, wote wameshiriki na ukweli wametoa mchango mkubwa sana hapa. Sasa vitu vingine ambavyo vimesemwa kwamba pengine ni dalili kwamba sisi tunapambana na sekta binafsi. Hili sikutarajia nitatoa tena maelezo. Ranking of schools, ooh mmeondoa kumi bora kwa sababu hamzipendi shule binafsi. Nilieleza vizuri hapa, lakini sasa niulize swali, kwamba ooh, mmeondoa ushindani, kwa hiyo, shule zetu zitaboronga. Ushindani gani tumeondoa?
Mheshimiwa Spika, bado tunatoa A, tunatoa B, tunatoa C, si ushindani huo! Tunatoa first class, second class na tunatangaza, si ushindani huo? Samia Scholarship, unapewa kulingana na performance yako na watu wanatangaza, si ushindani huo! Kwenye Samia scholarship wako wanafunzi wametoka private sector ambao wamepata Samia scholarship, si ushindani huo! (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunachosema sisi, ushindani lazima tutegemee kigezo kinachokubalika. Sisi tunashindanisha wanafunzi waliosoma masomo ya science na tumewapa full scholarship ambayo sisi Wizara ndio tumeamua iitwe Samia Scholarship. Tunaangalia wame-perform vipi na tunakutaja. Tumesema hivi kuhimiza watu washindane, kwa sababu wanafunzi wamekaa kwenye mtihani wa physics, wanafanya mtihani huo wa physics wote wanakwenda.
Mheshimiwa Spika, kushindanisha shule ni tofauti na kushindanisha wanafunzi. Kwani Kenya haipendi private sector! Mbona imefuta kutoa best school kwa kutegemea vigezo vya mitihani? Uganda je? UK je? Sasa sidhani kama nina haja ya kurudia tena maelezo tuliosema. Tunachosema, tutaangalia vigezo bora vya kushindanisha shule, siyo vigezo vya kusema kwamba wewe tu kwa sababu wanafunzi wanafanya vizuri sana, wewe ni shule bora.
Mheshimiwa Spika, nilitoa mfano mdogo sana hapa, na nirudie tena, hivi shule ambayo imechukua wanafunzi wenye C, C, D, halafu wale wanafunzi wakatoka wote A; na shule nyingine imechukua wanafunzi wote A, wakatoka wote A, wewe unadhani shule gani ni bora? Je, mnafahamu kuna shule zina matawi mawili; moja huku, anayefeli anahamishwa kwa nguvu, mzazi hapewi choice. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mtoto ameugua, tunatarajia shule sasa imlee, imsaidie, badala ya kumsaidia, inamtoa ili wabaki kupata A. Ushindani huo hauna afya sana, lakini wanaotaka kutangaza, matokeo yako hadharani. Serikali haiwezi yenyewe ikasema hii shule bora kwa vigezo ambavyo wanataaluma wamevikataa, na machapisho yako mengi, na nchi nyingi zimeacha.
Mheshimiwa Spika, ninachotaka kusema ni kwamba, Association of Private School Owners, wakitaka kusema haya, wasituweke sisi, matokeo tunatoa hadharani. Sidhani kama nina sababu ya kuelezea hili. Kwa nini watu wanadhani hii ni kupambana na private sector? Kwa hiyo, hizi nchi ambazo kwa kweli ndiyo private sector, zimekubuhu, wameacha. Sasa watu wanawahitaji. Sisi hatuwezi kupambana na private sector kwa sababu hiyo. Hata kidogo, na hatuna sababu ya kufanya vile.
Mheshimiwa Spika, tunafurahi wanapofanya vizuri, na ndiyo maana Samia Scholarship wapo watu walisema, angalia watu waliosoma private wasipate. No! Tumesema tunataka wanafunzi waliofanya vizuri waje wawe madaktari wazuri sana, waje wawe ma-engineer wazuri sana. Kwa hiyo, haijalishi wametoka wapi? Wametoka wengine Feza School, wametoka private schools, wameenda mpaka Samia Scholarship kwa mashindano hayo. Kwa hiyo, mashindano hatujayakataa, kabisa, naombeni dhana hiyo tuache.
Mheshimiwa Spika, lingine ni mitihani. Kwa nini Olympio kulikuwa na wizi wa mitihani hamkufungia shule kama kituo cha mitihani, lakini shule binafsi mnakuwa na haraka sana ya kufungia? Cha kwanza, wanafunzi wote wanaohusika na wizi na udanganyifu wa mitihani, tunafuta matokeo. Haijalishi anatoka shule ya umma au binafsi. Nyaraka zinaonesha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, shule inayofungiwa kuwa kituo cha mitihani, ni shule ambayo tumeona kulikuwa na organized effort ya ku-cheat ndani ya shule. Mfumo wa kitaasisi wa kufanya udanganyifu, sio mwanafunzi mmoja mmoja. Hata shule binafsi ambazo unakuta mwanafunzi mmoja mmoja ame-cheat hatuzifungii. Nitatoa mifano miwili, mmoja mnaufahamu. Iko shule moja mlisikia binti mmoja analalamika, mimi namba yangu ya mtihani nilibadilishiwa, nikawa nalalamika hawataki. Mtihani wa kwanza, wa pili, wa tatu, wa nne. Ule wa mwisho ndiyo wakatubadilishia namba, wakarudisha ile namba yangu ya mwanzo, halafu akaitwa na walimu wote wakaambiwa msiseme kilichotokea.
Mheshimiwa Spika, tusingejua kama yule binti asingetoa taarifa. Siyo jamani! Alivyotoa taarifa, tukachunguza, tukagundua ni ukweli. Hiyo shule ilikuwa one of ten best at some point. Shule hiyo nadhani iliongoza kwenye mkoa, ikawa one of the best.
Mheshimiwa Spika, siyo kwamba mwanafunzi ame- cheat, lakini walimu wameshirikiana, wamebadilisha namba za mitihani, wamempa huyu na huyu, for whatever reasons, halafu baadaye wanabadilisha, halafu wanaita wanafunzi wanaambiwa msiseme.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hata watumishi wa umma walikuwepo tumewachukulia hatua na wale wa nani tumewachukulia hatua alafu tumefunga kama kituo, sasa hiyo tumefunga kwa sababu ya kuchukia private sector.
Mheshimiwa Spika, mfano mwingine iko shule mwanafuzi kaingia na simu, hairusiwi lakini ame–manage kuingia na simu, ameingia kwenye mtihani akawa anapiga picha maswali halafu amemtumia mwenye shule halafu mwenye shule nje akapanga watu wa ku–solve matokeo. Sasa huyo tuna mtetea private sector mtakuwa mnafanya kazi nzuri sana, msitetee hiyo private sector msitetee hiyo, kwa sababu private sector inafanya kazi nzuri sana. Hawa wachache wanaweza waka tarnish image huo ni mfano lakini kwani private sector tu tunakwenda?
Mheshimiwa Spika, hapa navyozungumza wako watumishi Shinyanga wako ndani, alikuwa Afisa Elimu kwanza alihamishwa haraka haraka akakimbia nadhani akapelekwa Tukuyu tumemfuata, tumemdaka, tumemrudisha yupo mahabusu kwa reason tu organized. Wako polisi, wako ndani, kwani polisi ni private sector? Afisa Elimu ni private sector? Na sisi tuna deal zaidi kwa nguvu kubwa zaidi na Maafisa wetu ambao tunagundua wanaiba. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hao ambao tumewakuta, tuliwakutaje? Mtihani umeibiwa Serengeti, kwa kufungua mtihani mapema kwa kufanya mchezo kupiga picha, umetumwa kwenye simu Kahama. Sasa hamuwezi kujua system tuliyonayo sasa hivi ukiiba mtihani rahisi sana kukudaka, Kahama watu wamedakwa simu zimekamatwa, tumeangalia zimetoka wapi? Tumekwenda kule tumegundua, polisi aliyehusika kulinda mtihani hao wako ndani, Afisa Elimu yuko ndani na hili hawa ni Maafisa wa Serikali walikuwa wanafanya hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, isihusishe vita dhidi ya private sector nakuombeni sana. Kwa nini tufanye vita dhidi ya private sector? Kwa nini? Kwa hiyo, Olympio hatukupata mfumo wa kitaasisi wa wizi ni kweli, walikuwa wana–cheat wamepatikana, wamefutiwa matokeo kama ambavyo kuna shule za private ambazo tumekuta watu wame–cheat zikafutiwa matokeo. Shule moja ya Mwanza ilichukua muda kabla ya kuiondoa kama kituo cha mitihani kwa sababu tulikuwa tunafanya uchunguzi.
Mheshimiwa Spika, kwa hilo nilipenda nilizungumze sana, kwa sababu nisingependa private sector ione kama tuna pambana nayo ili iweje? Lakini wizi wa mitihani hakuna mtu atakae vumilia mahali popote kabisa. Tushikamane private sector na public sector tushikamane, tupambane na wizi wa mitihani. Then shule hizi za private ni nzuri sana, nyingine wala hazifanyi mtihani wa NECTA ndiyo wanachukua mtihani wa Cambridge wanafanya. Kwa hiyo, tushikamane jamani namna wanafanya kazi nzuri na mimi I can promise na Rais wetu, kwa sababu Rais wetu kwanza yuko hivyo hatuwezi kupambana na shule binafsi hata siku moja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lingine ambalo ningependa nilizungumze labda niseme tu mambo mengine ambayo kwa kweli ni operational nadhani alikuwa Mheshimiwa Tabasam alizungumza hapa kuhusu wananchi wamejiunga, wamejenga shule zao, wamemaliza karibu wamekamilisha wanaomba usajili halafu sisi hiyo lazima niseme sisi kwa sababu mimi nachukua jukumu. Tunakwenda pale tunasema haa hapa kimepunguka maabara kwa hiyo, hatutoi usajili.
Mheshimiwa Spika, tumeishakubaliana wale wananchi ambao wameishajipanga wamefanya kazi imebaki kitu kidogo sana baada ya sisi kukatalia usajili tunapeleka hela tunamalizia shule, shule isajiliwe ianze kufundisha wanafunzi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Tabasamu na wengine wote katika mazingira hayo na tukifanya hivyo tutaimiza wananchi maana yake hamuwezi kuwaambia wananchi hebu changieni tena, tukifika mahali Serikali itakuja itatushika mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hatuwezi kuacha kusajili shule kwa sababu haina maabara tu, haina kichomea taka na kadhalika lakini tuna Taasisi yetu ya Elimu na Mamlaka ya Elimu ambayo kwa kweli tunaweza tukai–direct bwana peleka kule kwa sababu wananchi wameisha pambana na tuone na tushafanya hivyo naomba hilo twende nalo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna suala jingine lilizungumzwa na baadhi ya Waheshimiwa nadhani suala la recognition power learning actually ukisoma Sera ndiyo utapenda zaidi. Ipo sasa hivi lakini, ipo ilikuwa inafanya chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, ipo vijana wapo mtaani wanafanya shughuli zao, VETA wana wa–trace, wanawafatilia, wanasimamia, wana–observe vizuri wanakuja wanawapa cheti kwamba kwakweli wewe uwe fundi magari ni mzuri sana cheti hiki ili uweze hata kufanya kazi hata za Serikali ipo sasa hivi.
Mheshimiwa Spika, kwenye Sera kuna utaratibu nyumbufu, mzuri zaidi wa kuwawezesha watu kupata kila kitu na hata ile nadhani alisema Mheshimiwa Kishimba, kuwafundisha vijana sijui house girl na kadhalika lakini iko kwenye hospitality ukarimu, ukarimu unafundishwa kutandika kitanda, kupiga pasi, kupika chakula na kadhalika, kufagia nyumba na vitu vyote vile ambavyo ni muhimu lakini tunachohitaji tumefanya tracer study kuangalia wanafunzi wetu waliyotoka kwenye vyuo vyetu wanakubalika vipi? Ili tuweze kubadilisha mitaala kazi yetu kubwa ni kuimarisha tunavyo fundisha kule ili kila mtu aone kweli hawa wanafaa kwa cheti kile waweze kuajiriwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jingine kubwa niliseme mabweni chini ya darasa la tano. Waraka wa kamshina unasemaje? Unasema kama mwongozo wa 2020 unavyosema yeyote haruhusiwi kuanzisha mabweni chini ya darasa la tano bila kibali maalum cha kamshina. Kama huna hicho kibali maalum, ulipewa deadline ambayo tu baada ya kukaa na private sector tumesogeza tunaongeza jitihada za kukagua.
Mheshimiwa Spika, kwa sababu mtoto elimu ya awali siyo kwamba anaenda shuleni tu, hata kwenda choo kujisaidia nini care yake ni kubwa zaidi ni more vulnerable. Kwa hiyo, lazima ukaguzi wake na vigezo vyake view vikubwa zaidi, tunatambua kwamba kuna mahitaji lakin vilevile tuna wajibu sasa sisi tukishatoa kibali kitakachotokea kule tutaulizwa sisi na sasa hivi tunafanya utafiti wa kuangalia ni namna gani ya kubana zaidi kuhakikisha kwamba kwakweli wale watoto wanalindwa lakini kwa kibali maalum. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tumekutana na private sector tukasema na wapo wenye vibali, tukasema mnaendelea lakini tutawakagua, tutawakagua kuhakikisha kwamba kweli hawa watoto wanakuwa well taken care of na tuna– encourage zaidi watoto wakae na familia lakini tunatambua wako yatima wamechukuliwa na vituo mbalimbali, wako wengine walikuwa nao hawana vibali wamekuja wametuletea document tumewapeleka kwa kamishna. Peleka timu kubwa ika kague kule kwa ajili ya kuhakikisha kwamba hawa yatima wanakuwa supported wataondoka wataenda wapi?
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hilo tunalijua lakini walioko huko very clear na maneno yako vilevile bila kibali maalumu cha kamishna haijasema hairuhusiwi. Kwa hiyo, kibali chake ni kigumu kuliko kuanzisha bweni tunaomba tu mtusapoti kwenye hilo na tutafanya kazi vigezo hivyo na private sector kuhakikisha kwamba ni vigezo ambavyo kweli vinaleta na. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lingine la mwisho, mwisho hapa kuna hoja nzuri sana ya vyuo vikuu imezungumzwa sana hapa Mheshimiwa Profesa Ndakidemi, Mheshimiwa Dkt. Chamuriho na Mheshimiwa Profesa Muhongo wamezungumza vizuri sana, vyuo vyetu kuhusu sasa hapo ndiyo rank ipo, unataka ku–rank vipi? Hatu–rank vyuo vikuu kwa matokeo ya darasani. Vyuo Vikuu vina heshimika kwa utafiti, namba moja na utafiti mzuri ni mwalimu mzuri.
Mheshimiwa Spika, nashukuru sana Bunge lako Tukufu lilipitisha fedha shilingi 50,000,000. Kwa muhadhiri yeyote, sasa hivi tunaanza na wahadhiri watakao fanya kazi kwenye natural science au medicine waka–publish kile alichosema Mheshimiwa Profesa Muhongo kwenye high impact factor journal na mwenyekiti wa kamati ya kuweka mwongozo ni Profesa Yunus Mgaya ambaye tuko nae hapa nae ni mtafiti.
Mheshimiwa Spika, akifanya akipata anaondoka na kitita cha milioni 50. Mwanzoni niliona watu wanasema kwa nini usi–support local journals Mheshimiwa Profesa Muhongo amezungumza vizuri sana namshukuru sana, sasa hilo linaeleweka. Hatuwezi kuleana hapa kuanzisha journal na kupandishana vyeo tutakuwa ni kichekesho, unaweza ukaitwa profesa hapa nchini ukienda nje ukikutana na watu wanavyoongea unawaambia msaidizi hebu usinite profesa hapa mpaka nirudi nyumbani, kwa sababu hapa nitahadhirika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunataka maprofesa wetu wapande na ushindani wa kimataifa na tunataka kama ambavyo tungependa wachezaji wetu wa mpira kama wale wa simba na wale wengine waweze kucheza kimataifa wakubalike. Tunataka wote Simba na Yanga, wote tunataka wahadhiri wetu wachapishe kwenye ma–journal hayo huko. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tuta ku–reward kwa kuchapisha huko na yako nje kwa sasa hivi, wenzetu wame catch up kwa kuanzia huko leo India wana journal nzuri sana lakini walianza kuchapisha huko. Kwa hiyo, siyo matumizi mabaya ya fedha, kwa hiyo, fedha mlipitisha Waheshimiwa Wabunge, nawashukuru sana, muongozo tunao nadhani tarehe Katibu Mkuu atatangaza na tutatangaza lini tutatoa tuzo hiyo kwa wale ambao wamechapisha kule na imehamasisha sana utafiti wetu kufanya vile.
Mheshimiwa Spika, nakadhalika tumefanya kitu kingine ambacho ni kikubwa kwenye Tuzo ya Mwalimu Nyerere ambapo na Waheshimiwa mlitoa hela. Tumefanya, tumeshangaa, Miswada iliyokuja mingi kweli kweli washapewa. Namba moja amepewa milioni 10 na Miswada ile inaenda sasa kwa wachapishaji itachapishwa na kuhamasisha publish industry hapa nchini unaweza kushangaa hata tuna vitabu vyetu, nexty tutaongeza na vitabu vya watoto tusiwe kama watu wa kubana tu, kubana tu vitabu lakini tunahimiza uandishi wa vitabu vile tulivyosoma wagaga gigi koku lakini tuwe na vitabu vya kisasa hivi vinavyo changasha watu.
Mheshimiwa Spika, lingine na hili litakuwa la mwisho kabla ya kengele ya pili. Kuhusu English Medium, yako mengine mengi lakini sikujipanga kuyajibu yote labda yaulizwe, English medium kamishna anaporuhusu kwamba umeenda halmashauri umeomba shule hii iwe English medium hasemi kwamba kachaji watu. Shule za Serikali hazichaji ni free, free ni elimu bila ada kuifanya English Medium hakukupi wewe kibali cha kuleta ada. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa hayo ya ada nimeuliza kidogo yanakuja kwenye Baraza la Madiwani ambapo sisi wote ni madiwani, hebu twende tukaangalie tunafanya hivyo kwa sababu gani? Kwa sababu kwakweli tunahitaji kwenda na mwongozo wa Serikali kwamba shule za Serikali zitoe elimu bila ada. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa muda wako, naomba kutoa hoja. (Makofi)
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naafiki.