Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
House of Representatives
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. MWANTATU MBARAK KHAMIS: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Kwanza kabisa nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenijalia pumzi kwa wakati huu nikaweza kusimama mbele ya Bunge lako hili Tukufu. Aidha nikushukuru wewe binafsi kwa kunipa nafasi hii ya kuweza kuchangia bajeti hii ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Watoto. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitakuwa mkosefu wa shukrani kama sitamshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, mama mpambanaji ambaye anatupambania sisi Watanzania kwa jitihada zake za kuhakikisha huduma muhimu zinatufikia wananchi wa Tanzania popote tulipo. Aidha, niwapongeze Mheshimiwa Waziri wa Wizara hii pamoja na Naibu Waziri wake na watendaji wote kwa kusimamia vema majukumu yao na leo hii tukasikia Wizara hii imeanza kuonekana, hii yote ni jitihada yao wao kwa namna ambavyo wanaisimamia Wizara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niendelee kuipongeza Serikali kwa kupeleka miradi ya maendeleo 691, miradi ambayo ina lengo la kuhakikisha huduma muhimu zinapatikana kupitia Wizara hii. Huduma hizo ambazo zimeelezwa katika ukurasa wa 11 wa randama ni vituo vya huduma ya afya, madarasa ya shule za msingi, pamoja na shule za sekondari. Mpango huu ni mwema sana na unaleta matumaini katika kupatikana kwa huduma ambazo zinakwenda moja kwa moja kuimarisha maisha ya wananchi, lakini pia kuleta manufaa makubwa kwa wananchi wetu kupitia miradi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pamoja na kupongeza naomba nishauri. Kwa upande wa vituo vya afya; kuhakikisha wataalamu wanakuwepo, lakini pia na vifaa tiba vinapelekwa kwa lengo la kufikia malengo ya kujengwa vituo hivi, lakini kwa upande wa shule, pia, kuhakikisha Walimu na vifaa vya kufundishia vinakuwepo, lakini pamoja na kuwepo vizingatie mahitaji ya wanafunzi wote wakiwemo wanafunzi wenye ulemavu kwa sababu, wanafunzi wenye ulemavu wanapata changamoto kubwa katika kujifunza kwa kutokupatikana kwa uhakika kwa vifaa ambavyo vinaweza kuwasaidia kufikia malengo yao ya kujifunza kama walivyo watoto wengine wasio na ulemavu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niipongeze Wizara kwa kufuatilia na kubaini Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ambayo yanafanya shughuli zao kinyume na utaratibu uliowekwa. Kufuatiliwa kwa mashirika haya kumeleta picha ya kuona kwamba, kuna baadhi ya mashirika ambayo yanasajiliwa kwa nia nzuri, lakini matokeo yake vitendo vyake vinaleta athari kubwa katika jamii yetu. Niiombe Wizara kupitia hili kufuatilia zaidi kwa karibu mienendo ya jumuiya hizi ambazo zinasajiliwa ambazo zipo na zile ambazo zinaundwa sasa hivi, kufuatilia kwa karibu ili ihakikishe mashirika yanayosajiliwa yawe na malengo mazuri ambayo yataleta tija kwa jamii yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nasema haya natambua mchango mkubwa unaotolewa na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, yanasaidia sana Serikali, lakini kuna baadhi wanaunda mashirika haya kwa lengo la kupotosha utamaduni na silika zetu kama wengine walivyoanza kusema. Kwa hiyo, niwapongeze sana Serikali kwa hili, lakini waendelee kufuatilia kwa karibu zaidi na hayo ambayo wameyafuatilia wazidi kuyafuatilia na wawe karibu sana katika kusimamia utekelezaji wa mashirika haya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niendelee katika kipengele cha kulinda haki ya mtoto. Serikali imeeleza kwamba, imeunda madawati ya ulinzi na usalama yapatayo 1,393 kwa baadhi ya mikoa kwa shule za msingi na sekondari, lakini pia wameunda Mabaraza ya Watoto 560. Jambo hili ni jema sana kwa sababu, kuundwa kwa madawati haya na mabaraza haya yatakwenda kuwaweka watoto pamoja na kuweza kujadili changamoto zinazowakabili kwa pamoja na italeta picha ya kuwezesha kujua watoto wanakabiliwa na nini, kuliko hivi sasa hivi mpaka mtoto limfike, ndio uchunguzi unafanywa tunajua watoto wanapatwa na yapi, lakini katika mabaraza haya wataweza kutoa fikra zao na kila mmoja ataeleza changamoto.
Mheshimiwa Spika, nataka kujua mabaraza na madawati haya vipi yamemwangalia na kumshirikisha mwanafunzi mwenye ulemavu? Kwa sababu, miongoni mwa wanaopata changamoto kubwa ni wanafunzi wenye ulemavu katika familia zao, lakini pia katika jamii inayowazunguka, wanakumbana na changamoto ya kubakwa, lakini pia na kudhalilishwa kutokana na hali zao. Mheshimiwa Waziri atakapokuja atatueleza kwamba, watu wenye ulemavu au wanafunzi wenye ulemavu wameshirikishwa vipi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia niendelee kuishauri Serikali, mabaraza haya na madawati haya yana lengo zuri, lakini hayataweza kusimama na kuendelea bila kuyawekea bajeti ya kutosha. Mheshimiwa Waziri labda atwambie wamejipanga vipi katika kuhakikisha madawati na mabaraza haya yanafanya kazi zake vizuri na yanaendelea ili kufikia yale malengo ya kuundwa kwake? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niendelee na mchango wangu katika Program Jumuishi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto. Imeelezwa kuwa elimu ya uelewa imetolewa juu ya program hii, lakini elimu hiyo imetolewa kwa mikoa kumi na ndio iliyofaidika, mikoa yenyewe imetajwa katika randama. Nataka kujua tuna mikoa isiyopungua 32 kama sikosei, je, vipi Wizara imeangalia hii elimu kufikia katika mikoa mingine ambayo imebakia? Kwa sababu, maendeleo yanapokuja yaende kote na Wizara imechagua kwa mikoa kumi, hii mikoa iliyokuja hali itakuwaje, lakini vigezo gani ambavyo vinasababisha hii mikoa kumi ikachaguliwa kuanzishiwa program hii? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niendelee na mchango wangu kwa program ya usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake kiuchumi. Tumeelezwa kuwa kupitia randama hii Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake umeweza kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 663.4 kuanzia Julai mpaka Aprili, 2023. Fedha hizi zilitolewa kwa vikundi 11, lakini pia kwa wajasiriamali mmoja mmoja wapatao 14 na ikajumuisha wanufaika 104 kwa mikoa minne. Hapa pia nataka kufahamu je, kwa nini hiyo mikoa minne tu? Ni kigezo gani kilichotumika hata mikopo hii ikatolewa kwa hiyo mikoa minne? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimalizie mchango wangu…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Dakika moja Mheshimiwa, kengele ya pili ilishagonga.
MHE. MWANTATU MBARAK KHAMIS: Mheshimiwa Spika, ahsante. Mwisho, naomba nimalizie mchango wangu katika makusanyo na mapato ya Wizara hii. Kwa mwaka 2022/2023, Wizara ilikadiriwa kukusanya bilioni 8.5, lakini hadi kufikia Aprili, 23 imekusanya 3,025,562,821. Nataka kujua ni changamoto gani iliyosababisha Wizara kushindwa kufikia malengo hayo iliyojiwekea? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya mchango huo, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Naunga mkono hoja. (Makofi)