Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

Hon. Mariam Madalu Nyoka

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

MHE. MARIAM M. NYOKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kupata nafasi hii ya kuchangia Wizara muhimu ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum. Pia, nimpongeze Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuona umuhimu wa kipekee na kuamua kuiweka Wizara hii ijitegemee ili iweze kuwafikia Watanzania kwa ukaribu. Pili, nimpongeze Mheshimiwa Waziri na timu yake kwa namna wanavyofanya kazi kwa mshikamano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niende kuchangia kwenye maeneo kadhaa. Eneo la kwanza ni mafunzo ya mikopo ya asilimia kumi kwa wajasiriamali. Mafunzo haya muda unaotolewa ni mdogo, hautoshi. Namaanisha kwamba, Wizara hii kama ingeamua kujipanga vizuri ingeweza kutoa mafunzo haya ya kuanzia siku tatu mpaka tano na wakati huo wakiwa wanahakikisha bajeti ya mafunzo haya inakuwa imeshatengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye eneo hili wakati wa utolewaji mafunzo haya naomba pia wataalam wetu washirikiane na wataalam wa benki. Kwa kufanya hivyo, watakuwa wanaweza kufanya mambo yafuatayo: -

Kuandika andiko rahisi la kibiashara kulingana na mazingira yetu halisi; Kutoa mafunzo ya utunzaji kumbukumbu wa fedha; Kutoa mafunzo ya urejeshaji wa mikopo; na Kutoa mafunzo ya faida na mafunzo ya wajasiriamali kwa uhalisia kuendana na shughuli wanazozifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, mama lishe anatakiwa apate elimu ya umamalishe, ushonaji pia pamoja na makundi mengine kuliko ilivyo hivi sasa elimu inayotolewa inatolewa kwa ujumla wake. Elimu inatolewa kwa siku moja, muda huo hautoshelezi. Nilikuwa napendekeza kwamba, elimu hii itolewe kwa muda wa siku tatu mpaka tano, ili wajasiriamali hawa waweze kupata elimu ya kutosha na yenye uelewa, ili waweze kufanyia kazi mafunzo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilikuwa napendekeza pia, mikopo hii ingeweza kutolewa hata kwa mjasiriamali mmojammoja ambaye anaweza kuwa na dhamana isiyohamishika na ni mfanyabiashara ambayo inaendelea, ili aweze kuajiri na Watanzania wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sio hilo tu, napendekeza pia katika vikundi vinavyopewa mikopo waanzie watu wawili, watatu hadi watano, kuliko ilivyo hivi sasa mikopo inatolewa kuanzia watu watano na kuendelea. Watu hao mara nyingi wanakuwa hawaendani. Nasema hivi namaanisha kwamba, mikopo inapotolewa kwa watu watano ilimradi tu wanakuwa wamekidhi vigezo vya masharti yale, lakini wanapopewa mikopo ile wengi wao wanakuwa wanapotea, kati ya watu wawili au watatu kwa sababu, hawaendani na inakuwa vigumu baadaye kwenye marejesho, wanabakia wanaofanya biashara ile watu wawili au watatu. Kwenye urejeshaji wengine wamepotea, nani atarejesha mikopo ya wale wengine ambao hawapo? Kwa hiyo, tunaona mikopo mingi inakuwa chechefu kwa sababu hii, hawaendani kiuhalisia zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia, naomba niende kwenye upande wa waajiriwa hawa, wataalam wetu, Maafisa Maendeleo ya Jamii. Wataalam wetu wengi wanapoajiriwa wanakuwa hawapati mafunzo, wanakwenda moja kwa moja kazini kitu ambacho kinakuwa hawaendani na majukumu yao ambayo wanatakiwa waende wakayafanyie kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumeona Maafisa Maendeleo ya Jamii wengi wanapoajiriwa wanapenda kukaa ofisini. Hawa kazi zao sio za ofisini, inatakiwa waende vijijini na ndio maana tunaomba hata Maafisa Maendeleo ya Jamii hawa wapatikane kwenye kila kata. Utaona kule kwenye kata kazi ya maendeleo ya jamii anafanya Afisa Mtendaji wa Kata, sio sawa. Kwa kufanya hivi maana yake tunakuwa tunapunguza ufanisi wa kazi za maendeleo ya jamii kule vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho, naomba pia, wakati tunapoenda kutoa mikopo hii iendane sambamba na urejeshwaji wa marejesho ya mikopo hiyo. Kwa nini? Sheria yetu haiweki wazi namna ya urejeshaji wa mikopo hii. Naomba sheria yetu iseme, iwe na meno ili mikopo hii ipatikane na iweze kurejeshwa kwa wakati, izunguke waweze kupata na wajasiriamali wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hayo, naomba kuunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)