Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. PAULINA D. NAHATO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi ya kuchangia katika Wizara hii. Napenda kumshukuru Mungu kwa kunipa afya njema tena kusimama na kuchangia katika Wizara hii muhimu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia napenda kumshukuru Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa mara nyingine tena kwa kuona umuhimu wa kuwa na Wizara hii muhimu ambayo itashughulika na masuala ya maendeleo ya jamii yetu. Napenda kuwapongeza sana Mawaziri, Dkt. Gwajima pamoja na Naibu Waziri na watendaji wote pamoja na wafanyakazi wote wanaofanya katika Wizara hii ya Maendeleo ya Jamii.
Mheshimiwa Spika, leo naomba kuchangia katika jambo moja linalohusu wajane. Katika takwimu hapa duniani kuonesha kwamba, kuna wajane takribani milioni 259 na nusu ya wajane haw ani maskini na huishi katika mazingira ya unyanyapaa, ubaguzi sababu ya jinsia zao pamoja na umri.
Mheshimiwa Spika, katika nchi zinazoendelea, hususan Tanzania, wajane wengi wanapopoteza wenza wao huchanganyikiwa kwa sababu, wajane wengi wanapoishi na wenza wao hushirikiana katika mambo mbalimbali ya kimahusiano, ya kiuchumi na kadhalika. Kwa hiyo, kifo kinapotokea, hasa kwa mwanaume, wajane hulia mara mbili, hulia kwa kupoteza wenza wao, lakini hulia muda mrefu kwa kufikiria maisha baada ya kupoteza wenza wao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wajane wengi katika Nchi ya Tanzania wanapofiwa na waume zao, tafiti zinaonesha kwamba, hupoteza hadhi zao kwa sababu, katika jamii yetu, wanawake huonekana kama ni wenza wasaidizi. Kwa hiyo, pale anapoondoka mwanaume, basi wao hujiona au huoenakana kwamba, hadhi kidogo imepungua, hata utu pia huonekana umepungua, lakini zaidi ya yote kipato hupungua baada ya kufiwa kwa sababu katika jamii zetu wanaume wengi ndio ambao huleta kipato katika familia. Vile vile wajane hupelekwa mbali, huenguliwa kwenye mambo ya urithi wa mali za familia na katika baadhi ya jamii zetu wanawake hurithiwa kutokana na ile mila iliyoko katika jamii hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hivyo basi, wajane ni kundi muhimu sana ambalo Serikali na jamii kwa ujumla ni vyema tukawaangalia kwa jicho la tofauti kwa sababu, wajane hawa mwisho wa siku huishia kuchanganyikiwa. Ikumbukwe kwamba, wajane ndio wanaotunza familia, wanawake hawa ambao sasa ni wajane na wanaachwa na watoto ambao ni yatima. Yatima ni mtoto ambaye amepoteza aidha, mzazi mmoja au wazazi wote, kwa hiyo, ninapoongelea wajane nawaingiza na watoto yatima ambao hulelewa na hawa wajane na mwisho wa siku hawa wajane hushindwa kulea watoto na hushindwa kufanya shughuli zao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wajane mara nyingi wanapopoteza wenza wao wanakwenda Mahakamani kwenda kudai baadhi ya haki, ikiwepo mali. Hivyo, wajane hupoteza muda mwingi sana Mahakamani, wajane hupoteza muda mwingi sana katika mabaraza ya kifamilia, mabaraza yale ya usuluhishi na kadhalika na hivyo huathirika kisaikolojia na kushindwa kutekeleza kikamilifu majukumu yao katika jamii.
Mheshimiwa Spika, naongea kwa hisia kali kwa sababu, wajane ni wengi na ni kundi ambalo kwa kweli, wanahitaji sasa ifike mahali Wizara iwaangalie na waweze kuwa na nguvu kama wagane. Walie jambo moja kwamba, wamepoteza wenza tu na sio kupoteza vitu vingine na walee watoto kama wagane wanavyolea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninaiomba Wizara ya Maendeleo ya Jamii kuhusu hawa wajane, kwanza katika jamii yetu elimu ya kutosha itolewe kwa jamii kabla hata watu hawajawa ama wagane au wajane, kwamba kuwa mjane ni ile hali tu ya kupoteza mwenza na siyo kupoteza vitu vingine. Kwa sababu sasa hivi kuna vurugu nyingi ambapo wanawake wanajiandaa wanakuwa wakali na hivyo changamoto ni kubwa sana katika jamii zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hivyo basi, mimi naishauri tena Wizara hebu iunde kitengo maalum ambacho kitawaangalia wajane na kuwapa elimu ya kutosha ili waweze kuelewa haki zao na nini wafanye pale ambapo mtu atakuwa mjane kwa sababu kifo hakizuiliki. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la tatu, ninaomba Wizara iangalie kupata msaada wa kisheria jinsi ambavyo hao wajane wanapopata changamoto wanaweza kupata msaada wa kisheria wapi, sehemu gani waende ili waweze kupata msaada wa kisheria, pia waweze kupata msaada ili wasibaguliwe katika familia zao, vilevile wasipate ukatili wa aina yoyote.
Mheshimiwa Spika, naomba kuishauri Wizara sasa ifike mahali ambapo isomeshe wataalamu katika ngazi ya vijiji ambao watapata ujuzi wa kuwasaidia wajane kuzielewa haki zao, kuwafariji ili wasipate zile changamoto waweze kuendelea kulea familia zao, waweze kuchangia katika maendeleo ya jamii yetu na vilevile tusizalishe watoto ambao watakuwa wamechanganyikiwa au ambao watashindwa kusoma vizuri na mwisho wa siku hao watoto hubakia kuwa watoto wa mitaani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia, nami pia naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)