Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

Hon. Tecla Mohamedi Ungele

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi hii nami nichangie. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya uzima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, natoa pongezi kwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Naibu wake, Katibu Mkuu na timu yote ya Wizara hii ya Maendeleo ya Jamii na wote kutoka kule ngazi ya Mikoa na Halmashauri kwa kazi kubwa wanayoifanya usiku na mchana. Hakika wanafanya kazi nzuri, inabidi kuwapongeza.

Mheshimiwa Spika, pongezi za pekee nazipeleka pia kwa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa ya kujali jamii ya Tanzania na makundi maalum hasa wamachinga, ambao tunaona kabisa hata kwenye taarifa ya Mheshimiwa Waziri ameeleza kabisa kwamba Mheshimiwa Rais ametoa hizo shilingi bilioni 22.9 hivyo, ombi langu ni fedha hizi zitolewe kwa wakati sasa hivi ili zifanye kazi inayopaswa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, najikita kwenye eneo la ustawi wa jamii. Kazi ya ustawi wa jamii ni kubwa kwenye Wizara hii na tumeona kuanzia ngazi ya Taifa hadi kule kwenye Halmashauri. Kazi yake kubwa ni kuimarisha jamii zetu. Tumeona hata taarifa ya Kitaifa, imesema wimbi kubwa la watoto wa mitaani limepungua kwa asilimia 38. Pia hata migogoro ya ndoa imepungua kwa asilimia 27 hii ni jitihada kubwa kweli kwa Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata pia kwa Mkoa wa Lindi tunaona pamoja na maafisa ustawi wa jamii wachache, wako 19 tu lakini bado kumefanyika kazi kubwa na wamebaini ukatili wa kijinsia umepungua kwa kiasi kikubwa sana. Mashauri kama 1,105 yamefanyika kufuatilia changamoto ya ukatili wa kijinsia. Pia wamesimamia msamaha wa matibabu kwa walengwa zaidi ya 33,000 kwa Mkoa wa Lindi na mengine yote hayo ni mafanikio. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumeona mmomonyoko mkubwa kweli wa maadili na maadili haya yanaanzia ndani ya familia, familia ni kila kitu, naamini kabisa wote tulioko hapa tumetoka kwenye familia na tunazihudumia familia. Kwa hiyo, kila kitu katika maisha kinaanzia kwenye familia; maendeleo yoyote, familia, sasa tunaona familia zetu zimeendelea kuathirika na mmomonyoko wa maadili, hili jambo ni hatari sana. Tumeendelea kuhangaika na elimu, tumeendelea kuhangaika na afya, tumeendelea kuhangaika na REA hii ya umeme vijijini, vyote hivyo ni kwa ajili ya maendeleo lakini bado kama hatutazingatia maadili ndani ya familia zetu itakuwa ni bure kabisa, itakuwa ni shida kabisa, mwisho wa siku tutakuja kupata kizazi ambacho wala hata hiyo elimu yenyewe haitaonekana, wala hata afya yenyewe haitaonekana. Mimi naomba haya mambo yote yaendane sambamba, tuendelee kuyaboresha maadili ndani ya familia na miradi mingine tuendelee kuifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama tunavyoona taarifa ya utafiti wa Serikali na UNICEF, walibainisha kwamba asilimia 60 ya watoto walioathirika katika ukatili wa kijinsia imetokea majumbani, pia asilimia 40 imetokea shuleni, kwa hiyo bado naendelea kusisitiza katika mchango wangu huu, nakumbuka hata mwaka jana nilichangia, bado mtoto huyu hayuko salama, kila eneo analokwenda. Hata mchangiaji mwingine alisema, hata kwenye vyombo vya habari, hata kwenye makanisa, hata kwenye misikiti, bado huko kuna unyanyasaji wa kijinsia, mtoto huyu hayuko salama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia tunaona Wizara imekuja na mpango mkubwa huu wa malezi na makuzi ya mtoto huyu. Mimi naomba kwa kuwa vitendo hivi vya mmomonyoko wa maadili vimekithiri na mtoto huyu hana usalama wowote kila aendapo, ninaomba kwa unyenyekevu mkubwa ninaomba na Wabunge wenzangu tusaidiane, tuungane mkono katika hili kwa sababu vita hivi ni vyetu sote. Kuwepo kabisa na mkakati wa Kitaifa vituo hivi vijengwe kimkakati kabisa, viwe vituo vya kielelezo kwa nchi nzima. Vituo hivi ndivyo vile tulivyosikia hata Mheshimiwa Waziri alivyosema, kwamba vituo hivi ndiyo vitamlinda mtoto kiakili, kimwili, kiafya ili angalau kumlinda asogezesogeze umri ambao ataweza kujitetea mwenyewe. Kwa sababu tayari akiwa mdogo hana utetezi wowote, akiwa wapi hana utetezi wowote, wazazi wake wanakwenda kazini wanamwacha mtoto hana utetezi wowote. Tunaomba tafadhali jambo hili lizingatiwe ili angalau mtoto huyu afikie umri ambao ataweza kujitetea mwenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaomba wote tuungane katika vita hii ya kupingana na jambo hili ili angalau kwenye jamii yetu lipungue kwa namna fulani ili tuwe na Taifa lililo na maadili mazuri.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)