Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

Hon. Sophia Hebron Mwakagenda

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kupata nafasi na mimi kuchangia katika Wizara hii.

Mheshimiwa Spika, ninampongeza Waziri kama wenzangu walivyosema, pamoja na Naibu wake kwa kazi nzuri ambayo wameweza kuchangamsha Idara na Wizara ya wanawake kuonekana sasa tupo na tunaweza tukapiga kelele kwa sauti kubwa.

Mheshimiwa Spika, bado tuna changamoto nyingi sana, leo nitazungumza chache nikianza na suala la mauaji kwa kutumia mapenzi. Tumeona kwa siku za hivi karibuni kumekuwa kuna mauaji makubwa sana kisa wivu wa mapeni. Mheshimiwa Waziri, kuna haja kubwa sana sasa ya kupiga kelele. Na suala hili haliko Tanzania peke yake, watafiti wa haki za binadamu wamefanya utafiti, mwaka 2021 na 2022 kwa dunia nzima takribani wanawake 45,000 wamekufa kwa wivu wa mapenzi, kwa Afrika Mashariki peke yake, asilimia 43 wanawake wanapigwa, wasichana wanapigwa na vijana kisa wivu wa mapenzi, na wakati mwingine hawana uhakika, ni wivu tu umewatokea anaamua kutoa roho ya mtu kwa sababu ya kumuonea wivu. Mheshimiwa Waziri, kuna haja ya kupiga kelele katika eneo hili.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, wanafunzi wa vyuo, wanandoa, wanapigana wanauana na kuacha watoto mitaani wakizunguka kisa tu baba aliona simu au mama aliangalia simu ya mumewe na kuingia kwenye matatzizo. Labda niseme tu hili pia kwamba tuna haja sasa ya kujijenga tabia njema katika familia kwa sababu mwisho wa siku wivu umeondoa roho za wanawake wengi katika Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri, ukatili wa kisaikolojia. Kuna Mbunge mwingine amezungumza hapa, leo hii takribani ndoa zaidi ya 700 zimeripotiwa katika kuwaumiza wanawake kwa kuwaacha. Mwanaume anamwacha mwanamke na watoto watano, watoto 10 anakwenda kuoa nyumba ndogo na kumwacha mke wake na kusababisha yule mwanamke kupata msongo wa mawazo.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri, kuna namna nafikiri watu wanaohusika na afya za akili na ustawi wa wanawake wanasimamia suala hili. Kwa sababu Mheshimiwa Waziri, leo hii tunataka kujenga Taifa la kesho, unalijengaje Taifa ambalo mtoto anaona mama yake anapigwa mbele yake? Mtoto anaona baba mtu anaingia usiku na matusi kwa sababu tu kalewa anatamka maneno yasiyofaa katika familia. Kuna haja ya kujenga Taifa bora, kuna haja ya kusema na kukaripia pale mambo mabaya kama haya yanapotokea, kuna haja ya kujenga Taifa jipya.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo hii tunazungumzia mmomonyoko wa maadili. Mheshimiwa Waziri tukiwepo sisi viongozi, unatoka nyumbani asubihi unakwenda kazini, unarudi jioni kwa sababu ya foleni, hujui mtoto ameshinda na nani siku nzima, akiwa shuleni walimu wana msongamano wa wanafunzi wengi, mwalimu hawezi kuangalia tabia ya mtoto mmoja mmoja darasa lina watoto zaidi ya 50 au 60. Kwa hiyo, tunataka turudi nyuma sisi kama familia tuhakikishe tunafuatilia haki za watoto na makuzi yao ili tupate kuwa na Taifa bora. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri, leo hii msichana wa kazi ndiyo anakuwa mlinzi wa mtoto nyumbani, Mama umerudi umechoka, baba amerudi na frustrations zake naye amechoka, huyu mtoto anajilea mwenyewe, anajifunza mwenyewe, wanaanglia pornographic pictures kwa sababu hakuna uangalizi nyumbani. Kisasa ambacho tumekuwa nacho, kizungu, tunaiga mambo ya magharibi, unamnunulia mtoto ma-toys ya kuangalia na wanajifunza mambo yasiyofaa.

Wakati mwingine tunaona sifa tunawanunulia watoto simu, unampa simu anakuwa na uhuru nayo, anakwenda ana- google anaanglia picha zisizofaa na wewe mzazi unafikiri ndiyo uzungu, unafikiri labda ndiyo maendeleo, mwisho wa siku tunaharibu watoto wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunahitaji kujenga Taifa bora ambalo litafundisha watoto wetu umakini, kama inabidi, turudi zamani zile ambazo mtoto ni wa kijiji, mtoto ni wa mtaa, mtoto ni wa Taifa, anapokosea mtoto achapwe na jirani, aonywe na jirani, wala mzazi asiende kumgombeza mwalimu kwa nini umenichapia mwanangu ukome, huyu mtoto siyo wa kwako. Mtoto kwa sasa tunahitaji awe mtoto wa jamii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri, rushwa ya ngono vyuoni. Tumeona mabinti wengi wakilalamikia suala la rushwa ya ngono vyuoni, wasichana wanaona bora basi kama ni hivyo hata kusoma wanashindwa wanajua mwalimu fulani ananihitaji basi nitatembea naye, naye atanipa GPA ya kutosha. Tunaomba Mheshimiwa Waziri kwa sababu wewe unahusika na Wizara hii, simamia nidhamu ya walimu wa vyuo.

Mheshimiwa Spika, kuna Mbunge hapa anayewakilisha vyuo vikuu amesema, mwalimu ni mdhamini mkuu wa mwanafunzi, lakini kama anataka ngono ili ampatie maksi anakuwa hatendei haki kazi yake na taaluma aliyosomea. Leo hii rushwa ya ngono imekuwa kilio kikubwa sana kwa wasichana na wanawake vyuoni, ninaomba wewe kama Waziri uweze kulisimamia hilo nasi tutakusaidia kupiga kelele katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, ukatili wa watoto wengi wameshausema. Mtoto mdogo ukatili unaanzia nyumbani. Leo hii nyumbani watoto wanaharibika tunazungumza suala la ushoga na mambo kama hayo, lakini asilimia kubwa inaanzia nyumbani. Leo hii tunaogopa kukaribisha mashemeji nyumbani, kaka zetu tunaogopa kuwakaribisha nyumbani kwa sababu utasema lala na uncle kule ndiyo uharibifu unakotokea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna namna kama Wizara inabidi tuzungumze, leo hii unajua unao majirani, majirani zako ni watu sahihi, lakini huyohuyo jirani yako unashangaa anatongoza binti yako na wewe uko palepale. Tunahitaji kupiga kelele kama Taifa. Ukatili wa kijinsia umekua mkubwa sana kwa sababu hata takwimu za 2022 ambazo zimezungumzwa na haki za binadamu, zaidi ya matukio 350 yamewakuta watoto wadogo. Leo tuna madawati lakini vijijini mpaka kufikia kwenye dawati la kijinsia ushahidi unakuwa umekwisha kupotea. Kuna haja ya kujitahidi sana kama Taifa kuweka ulinzi kwa watoto wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kingine ninachoweza kushauri ni kwamba TASAF ipo kwa ajili ya kusaidia ustawi wa maisha ya watu. Mimi ninaomba TASAF ije katika Wizara yako, itoke kule iliko kwa sababu huku kwenye Wizara yako ndiyo sahihi ambako kuna uhitaji kusaidia watu katika ustawi wa maisha yao ya kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimekwisha kusema hayo, lakini bado niendelee kusisitiza masuala ya makuzi ya watoto, kama Taifa lazima tuyapigie kelele. Leo hii mtoto analindwa na wewe mama, analindwa na wewe baba, ukisubiri Serikali ikusaidie, Serikali itakuja baadaye.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo mimi nitoe rai kwa Watanzania wote, tunahitaji kuwalinda watoto kwenye maadili ya kidini, kila mtu ana dini yake amfundishe mtoto toka mdogo, kwa sababu tunaamini mtoto akiwa mdogo kichwa chake kinakua kinapokea vitu vipya. Kwa hiyo sisi tuseme nao, tunapokuwa tumechoka ni kweli tukirudi tukazungumze na watoto na tuwaonye watoto, tusiogope. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi ninaamini katika sheria ya viboko japokuwa ipo, tuifwate hiyo sheria lakini itaweza kusaidia kubadilisha. Wengine tumefika hapa kwa sababu tulichapwa, tulionywa, tulikatazwa vitu vibaya, ndiyo maana leo tumefika mahali hapa. Tusianze kuiga mambo mengine kama Taifa tukaacha watoto wetu wanapotea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, mimi naunga mkono hoja kabisa katika Wizara hii kwa sababu mimi ni Mwanakamati na ninaona mambo mengi magumu ambayo Wizara hii inapitia na hasa tukizungumzia watoto ambao wako jela, tukizungumzia wazee ambao wamekosa makazi na Serikali hii inaamua kuwasimamia. Mimi naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)