Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

Hon. Janeth Elias Mahawanga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

MHE. JANETH E. MAHAWANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika Wizara hii. Kwanza kabisa, nampongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara kwa kazi nzuri wanayoifanya. Kipekee kabisa, nampongeza Mkurugenzi wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalum. Kwa kweli Mkurugenzi huyu amekuwa ni mtu anayetoa ushirikiano sana pale unapokuwa unafuatilia masuala ya wanawake, watoto na watu wenye mahitaji maalum. Ni mtu anapokea simu, anajibu meseji na bado anafuatilia kama umefanikiwa suala lako. Kwa hiyo, nampongeza sana kwa hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia, nampongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ndiye mwanzilishi wa majukwaa ya kuwawezesha wanawake kiuchumi. Leo hii nitazungumzia kuhusu majukwaa ya kuwawezesha wanawake kiuchumi. Mheshimiwa Rais akiwa Makamu wa Rais mwaka 2016, alianzisha majukwaa haya ambapo mwaka 2022 yaliratibiwa rasmi. Lengo kubwa la majukwaa haya lilikuwa ni kuwakutanisha wanawake pamoja, kujadili masuala ya kiuchumi, masuala ya masoko, fursa mbalimbali zinazowazunguka kwenye makazi yao, na kubwa zaidi, kujadili changamoto zao mbalimbali katika shughuli zao za kiuchumi za kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais ambaye nie mwasisi wa majukwaa haya, aliziona changamoto za akina mama wajasiriamali wa Taifa hili, ambazo ni mitaji midogo isiyotosheleza, nyenzo duni, ujuzi mdogo, fursa za masoko, mila kandamizi na kukosa dhamana za kuweza kupata mikopo mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, Wizara hii imekuwa ikifanya vizuri na tumemsikia Mheshimiwa Waziri hapa, ameeleza vizuri kuhusu majukwaa, lakini tuiombe Wizara, elimu kwenye majukwaa haya kama ambavyo Mwongozo wa Uanzishwaji wa Majukwaa haya unavyosema, isishuke tu kwenye ngazi ya viongozi wa mkoa wa jukwaa, iende mpaka ngazi ya Halmashauri, ngazi ya Kata, ngazi ya Vijiji na Mitaa. Kule ndiko kwenye wanawake wajasiriamali wengi, na wanawake wengi bado hawana uelewa wa mwongozo huu. Kwa hiyo, naiomba Wizara ifanye taratibu, mwongozo huu uwafikie wanawake wote mpaka wa kule chini.

Mheshimiwa Spika, nimejaribu kushiriki majukwaa machache ya wanawake kule chini, wengi wao wamehamasika sana. Kwa mfano, Mkoa wa Dar es Salaam, vikundi vilivyo chini ya majukwaa ni vikundi 18,240, ni vikundi vingi sana na ni mwamko kwa wanawake wa Dar es Salaam kuhusu majukwaa haya. Wanawake wengi bado hawajajua lengo mahsusi la haya majukwaa. Wengi wao wamejiunga humo wakiwa tayari wanasubiri fursa za mikopo, lakini lengo mahsusi ni kutoa elimu kwa wanawake wa majukwaa haya. Hivyo naiomba Wizara, ihakikishe kweli majukwaa haya yakafanye vizuri kama ambavyo mwasisi wetu ametamani kuona anainua uchumi wa wanawake wa Tanzania kupitia majukwaa haya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumeona majukwaa haya yako katika ngazi ya Mkoa, ngazi ya Halmashauri, Kata na Vijiji. Naiomba Wizara ishirikiane na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kuhakikisha majukwaa haya yanakuwa yenye tija na yanamsaidia kweli mwanamke wa kitanzania kwa kuratibu utoaji wa mafunzo, upatikanaji wa mitaji, kuwaunganisha na fursa mbalimbali, na kubwa zaidi kuendelea kutafuta wadau watakaowasaidia mitaji, maana kiu kubwa ya wanawake kwenye masuala ya ujasiriamali ni mtaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naiomba zaidi Wizara, ihakikishe kwenye Mwongozo huu wa Uandaaji wa Majukwaa, na kuwasaidia akina mama hawa wajasiriamali, ihakikishe inakwenda kugusa vitu vitatu ambavyo ni muhimu sana kwa mwanamke wa kitanzania ambaye ni mjasiriamali. Vitu hivi ni elimu, mitaji na fursa. Mjasiriamali yeyote ukimgusa kwenye hivi vitu vitatu, unakuwa umemkomboa. Kumpa mtaji peke yake bila elimu wala kuzitambua fursa, bado haisaidii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naiomba Wizara, inapoenda kutoa elimu kwa hawa waratibu, ihakikishe inafika ngazi ya kata na huko kwenye kata ihakikishe Madiwani wa Viti Maalum wanahusishwa. Kwa sababu kwenye majimbo yetu tuna Madiwani wa Viti Maalum. Madiwani hawa wanasaidia vikundi vingi sana vya akina mama kutoa elimu mbalimbali na pia kuwasimamia kwenye mikopo. Kwa hiyo, hata wao wanatakiwa wajue lengo la majukwaa haya ili yakafanye vizuri. Hatutamani tena kuona majukwaa haya yameanza halafu yanakufa, hayaleti tija kwa mwanamke wa Kitanzania.

Mheshimiwa Spika, tunaiomba Wizara ijitahidi pia kutoa uelewa hata kwa Waheshimiwa Wabunge wanawake, kuwahamasisha katika kujua huu Mwongozo wa Majukwaa, kwa sababu pia na Waheshimiwa ni akina mama ambao wanasimamia akina mama huko chini. Mwongozo unaeleza vizuri kabisa, Wizara imeshautoa, ugawanywe kwa Waheshimiwa Wabunge, wahakikishe hata kwenye majimbo yao na mikoa huko iwafikie akina mama wapate uelewa wa kutosha.

Mheshimiwa Spika, pia nawaomba Mabibi Maendeleo wote na waratibu wote wa majukwaa wawasimamie akina mama ipasavyo kwenye vikao vyao, wanapokuwa wanajadili mambo mbalimbali na mafunzo, wahakikishe wanawaunganisha na wadau mbalimbali washiriki kwenye vikao vyao. Kuna wadau kama SIDO, TBS, Taasisi za kifedha BRELA, Maafisa Biashara wa Halmashauri na wataalam wa masoko. Wasijadili fursa hizo peke yao, waletewe na wataalam wa hayo masuala.

Mheshimiwa Spika, ninaamini kabisa kwa kufanya hivi hata mikopo ya Halmashauri ambayo sasa hivi Serikali imeenda kujipanga vizuri ili kuhamasisha hii mikopo iweze kutoka kwa tija, lakini itakaporudi tunataka kuona watakaonufaika wa kwenye majukwaa nao wawe wamojawapo. Kwa sababu kwa muundo huo wa majukwaa na kwa tija ya majukwaa, kama kweli akina mama wataenda kunufaika na majukwaa haya kwa kupata hii elimu, nina uhakika kabisa mikopo ya Halmashauri itakayoanza kutoka itakwenda kuwa na tija na itawasidia sana wanawake, wajasiriamali wa Taifa hili. Pia itasaidia kuwaondoa kwenye masuala manne ambayo yanawaumiza akina mama.

Mheshimiwa Spika, tumeona mikopo ya Halmashauri ilikuwa hairudi, lakini kama majukwaa haya tangu mwaka 2022 yaliporatibiwa yangekwenda kufanya kazi nzuri na kuwaelimisha akina mama hawa, wanufaika wa mikopo wangeweza kurudisha ile mikopo. Haiwezekani unamkopesha mtu, bado hujampa elimu. Mtu anapata fedha kwanza, ndiyo anaanza kuwaza kitu cha kufanya. Kwa lengo la majukwaa haya, tutaiona Halmashauri inakwenda kufanya vizuri kwenye mikopo, sababu wanufaika watakuwa wameshapata fursa za kufahamu ujasiriamali na mambo mbalimbali kupitia majukwaa yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia majukwaa haya yakifanya vizuri, yatakwenda kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja. Kwa sababu mama anayeenda kujifunza kwenye majukwaa anayeenda kupata pale ujuzi, utamsaidia hata katika shughuli zake mwenyewe kama mtu mmoja mmoja. Pia tutashuhudia viwanda vidogo vidogo vya akina mama wajasiriamali kwenye Taifa hili kama tutashirikisha wadau mbalimbali katika kuwainua akina mama. Vilevile tutawakomboa akina mama na mikopo umiza. Tumeona mikopo ya Halmashauri ilikuwa haitoshi, wahitaji ni wengi, vikundi ni vingi. Kwa hiyo, mtu anatamani kufanya biashara, anakwenda kukopa, lakini hajui ile riba itamuumiza kiasi gani?

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nilikuwa naiomba sana Wizara izingatie kwenye hayo mambo manne ambayo yatakwenda kuwasaidia akina mama kupitia majukwaa haya.

Mheshimiwa Spika, mwisho niombe Serikali…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. JANETH E. MAHAWANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)