Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

Hon Munira Mustafa Khatib

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

MHE. MUNIRA MUSTAPHA KHATIB: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuchangia bajeti hii ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum. Kwanza kabisa, napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Wizara kwa ujumla. Tunawapongeza sana, wanafanya kazi kubwa kwa kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo anaendelea kuifanya, kuifungua nchi kiuchumi. Pia nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kuwaamini vijana na kuweza kuwapatia ajira zaidi ya 21,000 kwa kada japo ni tofauti, ikiwepo Ualimu na Udaktari. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais na niseme, sisi vijana tuko pamoja naye. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka nielekeze mchango wangu kuhusu watoto waliofanya makosa, waliopo gerezani. Kiukweli watoto ambao wanahukumiwa na kupatiwa adhabu walioko gerezani wengi wao wanafanya wakiwa na umri mdogo. Wanafanya makosa wakiwa na umri wa kuanzia miaka nane hadi 18. Wengi wao wanakuwa chini ya umri wa miaka kumi na nane.

Mheshimiwa Spika, adhabu zinazotoka kwa watoto hawa ni kali. Adhabu zao zinaanza kwa kufungwa jela kwa miaka thelathini, wengine wanahukumiwa kwa kifungo cha maisha, wengine wanahukumiwa kunyongwa. Tukumbuke mtoto huyu anafanya kosa akiwa na umri wa utoto. Mara nyingi wanafanya makosa ya mauaji, lakini kifungo wanachokitumikia ni cha muda mrefu. Je, Serikali inahakikisha vipi wanapata stahiki zao watoto hawa? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, watoto hawa ambao wako kwenye magereza wanakosa zile haki za Watoto. Kwanza kusoma, hawasomi vizuri; kulala, mazingira yao kama watoto bado wanastahiki kulala sehemu nzuri, lakini wanakosa huduma hii ya kulala sehemu nzuri. Japo Serikali imeonesha ina nia na dhamira ya kuendelea kujenga magereza ya watoto, lakini toka bajeti iliyopita Wizara imeendelea kusema itajenga magereza ya watoto, lakini bado hawajaweka miundombinu na miundo rafiki kwa watoto hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukumbuke adhabu hii kwa watoto wetu ni ngumu sana. Naiomba sana Wizara hii kupitia Bunge lako tukufu, ije na muswada wa kurekebisha sheria hizi ili kuwe na adhabu ya watoto. Kwa mfano, mtoto ameua akiwa na umri wa miaka nane, jifikirieni ninyi Waheshimiwa Wabunge nyote hapa, mkiwa na umri wa miaka nane, mlikuwa mnakumbuka nini? Sidhani kama kuna Mbunge alikuwa anajielewa akiwa ameshafanya makosa haya akiwa na umri wa miaka nane. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, adhabu hizi ni kali, tuangalie, kwa mfano kuna msanii mmoja anaitwa Lulu, alimuua Kanumba, lakini amepatiwa adhabu ambazo ni za kiutoto na ametoka, lakini kuna watoto wengine mpaka leo wako magerezani. Wamefanya kosa lile lile la kuua. Tuangalie, kama leo Kanumba angekuwa hai, leo hii angekuwa naye anahukumiwa kwa kosa la kubaka miaka 30 jela.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naiomba Wizara hii iendelee kuangalia watoto ambao wako magereza, adhabu hizi siyo rafiki kwa watoto. Tuangalieni upya, tulete adhabu za watoto ambazo hata wakitoka jela wanaweza kufanya kazi zao za kiuchumi. Leo unamhukumu mtoto akiwa na miaka mitano, umemhukumu akae jela miaka 30, ametoka jela akiwa na miaka 35. Je, unafikiria umemjengea mazingira gani katika jamii yake? Kusoma hajui, biashara hawezi kufanya, atafanya kitu gani? Tunamfanya aingie tena kwenye makundi ya wizi, kwa sababu kule gerezani hakupatiwa elimu na kuweza kujisaidia yeye mwenyewe ili kipindi akitoka jela aweze kujisaidia. Naiomba sana Wizara iweze kuangalia. watoto wanafanya makosa, ni kweli hatukatai, lakini wanafanya makosa wakiwa na umri wa watoto pasipo kujielewa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niongelee suala la udhibiti wa hizi taasisi zisizokuwa za kiserikali. Hivi karibuni tumeshuhudia shughuli ambazo zinafanywa na taasisi zisizokuwa za kiserikali (NGOs). Ni kweli tunazitaka NGOs kwenye nchi yetu ya Tanzania, lakini zipo nyingine hazina lengo zuri kwa jamii zetu. Taasisi hizi zinapotosha watoto wetu, tukae tuziangalie upya. Tuna shida gani kuzifutia leseni taasisi ambazo tunahisi zinahamasisha ushoga? Tukae, tufikirie. Naiomba Wizara iangalie kwa ukaribu na ifuatilie kwa ukaribu mashirika haya ambayo tunahisi yako kinyume na maadili ya kitanzania yafungiwe kwa haraka, kwa sababu bado yapo yanaendelea na yanaendelea ku-support suala la ushoga. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo tunalalamikia mashoga, lakini hatuangalii chimbuko lake ushoga unatoka wapi? Kama tungekuwa tunaangalia ushoga unatokea wapi, tunadhibiti nini, basi tusingefikia huku kwa sababu hakuna shoga ambaye anaweza kuwa mtu mzima akaibuka kuwa shoga. Ushoga unaanzia utoto. Huwezi kuwa shoga mtu una miaka 30 au 35. Ushoga lazima utaanza ukiwa mtoto na kijana, ili ukifika miaka
30 tayari umekomaa kuwa shoga. Naiomba sana Wizara iendelee kuangalia taasisi hizi ambazo haziitakii nchi yetu mema, na kuzifungia taasisi hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sana katika mitaala yetu ya elimu, tunajua sasa hivi kuna marekebisho ya mitaala ya elimu, lakini tuangalie shule za msingi, watoto wetu waanze kufundishwa somo la ukatili wa kijinsia ili waweze kujitambua na kujikinga na ukatili. Kama tutawafundisha watoto wetu mapema, likiingizwa kama somo, watoto wetu wataelewa unapofanyiwa hivi ni udhalilishaji; na unapofanyiwa mambo haya uripoti wapi. Kama hatujafanya hivyo, hatuwezi kuwalinda watoto wetu. Mtoto hajijui kama hiki ninachofanyiwa ni udhalilishaji, wapi niripoti? Leo tunawaimbisha watoto sawa, ukifanya hapa don’t touch me, ukiguswa hapa don’t touch me, lakini bado hatujawapa uelewa zaidi. Tuendelee kwenye mashule kuweka kama subject ili watoto wetu waweze kujitambua.

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Munira kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Festo Sanga.

TAARIFA

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Spika, anachokiongea Mheshimiwa Mbunge ni sahihi kabisa kwa sababu hotuba ya Mheshimiwa Rais ukurasa wa 30 wanasema wamefungua madawati 1,500 na kitu kwenye shule za msingi, na tunajua walimu wengi wana vipindi. Ni wakati sahihi sasa wa Serikali kuajiri Maafisa Ustawi Wajamii wengi kwa ajili ya kila shule kwa ajili ya kusaidia watoto wetu, kwa sababu walimu ni wachache, hawawezi kufanya hiyo kazi. Kwa hiyo, tukiajiri Maafisa Ustawi wa Jamii, wanaweza kusaidia hili jambo, ahsante. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Munira na muda wako umekwisha. Inapokea taarifa hiyo?

MHE. MUNIRA MUSTAPHA KHATIB: Mheshimiwa Spika, naipokea taarifa hiyo lakini tuzingatie zaidi kuanzisha masomo haya kwenye elimu zetu za awali.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)