Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

Hon. Angelina Adam Malembeka

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuchangia mada iliyoko mbele yetu. nichukue nafasi hii pia kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniweka hai hadi leo. Niwashukuru Wabunge Wote, Mheshimiwa Spika na Katibu wa Bunge kwa jinsi ambavyo mliweza kuniliwaza na kunihudumia nikiwa hospitali. Ninaendelea kuwashukuru Madaktari wote walionihudumia. Leo ni mara yangu ya kwanza kuchangia baada ya mwaka mmoja. Namshukuru Mwenyezi Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza waziri kwa uwasilishaji mzuri, nimemsikiliza vizuri nampongeza yeye, Naibu wake na timu yake yote. Pia nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anazozifanya nchini mwetu ambazo zimetuongezea sifa ndani ya nchi na nje ya nchi. Pia wanawake, vijana na watoto tumeona maendeleo ya wazi ambayo kila mtu bila hata ya kumuonesha anaona kwamba nchi imebadilika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nizungumzie suala la ukatili na unyanyasaji. Wengi tumekuwa tukizungumzia watoto,wanawake na wazee. Leo hii ninaomba nizungumzie ukatili na unyanyasaji unaofanyika kwa wafanyakazi wa ndani, wengi huwa hatulioni. Wafanyakazi wa ndani wanaendelea kunyanyaswa na kufanyiwa ukatili. Wafanyakazi wa ndani hawana likizo, wafanyakazi wa ndani hawaumwi, wafanyakzi wa ndani ndio madakatari, wafanyakazi wa ndani ndio ma– nurse, wafanyakazi wa ndani ndio kila kitu lakini bado wanalipwa mshahara mdogo. Nilikuwa naomba Wizara iwapitie na kuangalia jinsi gani wanaweza kulisaidia kundi hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna suala pia la watumishi wa kada hii ya Wizara ya maendeleo ya jamii. Kada hii asilimia kubwa imesahaulika. Ukifika hata ndani ya halmashauri au kwenye ofisi yoyote, ofisi ambayo utaona haina gari itakuwa ni hiyo ya Maendeleo ya jamii, ofisi ambayo haina furniture nzuri ni hiyo ya maendeleo ya jamii, Ofisi ambayo watu wake wanachelewa kwenda kusomeshwa nje ya nchi ni hiyo ya maendeleo ya jamii. Ofisi ambayo yale mambo ya hovyo hovyo yanayotakiwa yawepo pale basi watapewa Wizara ya maendeleo ya jamii. Nilikuwa naomba Mheshimiwa waziri, alifuatilie suala hili na wale pia awatoe. Wale nao wapo kwenye ajira kama walivyo wengine. Wapewe mshahara mzuri, wapewe posjho nzuri na wao pia wasomeshwe ili waweze kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia katika hiyo hiyo maendeleo ya jamii, Vyuo vyao vingi vimechakaa na vilijengwa zamani. Sisi wakati ule ndio tulikuwa tunakwenda tunawafuata mama zetu tunaita wanaenda kwenye community center, huko ndiko walikuwa wanakwenda kujifunza vitu. Majengo yale tunaomba yakarabatiwe ili yawe ya kisasa yapendeze na watu wapate hamu ya kwenda kujifunza kutoka pale. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo nilikuwa naomba bajeti ya wizara hii iongezwe. Wizara hii ina mambo mengi kama unga wa ngano, kwenye chapati, kwenye mandazi, kwenye sambusa, kwenye nini, ndio wizara hii. Sasa iongezewe pesa ili iweze kufanya kazi zake vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wizara hii pia ndio inayoongea na jamii yetu kwa haraka zaidi. Ninaomba wakaongee na wajasiriamali kuhusu suala la mikopo. Mheshimiwa Waziri, kama huna taarifa huko mitaani kuna mikopo inaitwa kichefu chefu, kuna mikopo inaitwa kibangala, kuna mikopo ya rusha roho, kuna mikopo ya komandoo, kuna mikopo ya miyeyusho, kuna mikopo pasua moyo. Haya yote ni mikopo ambayo wakinamama wanahangaika nayo na mingine inawadhalilisha. (Makofi)

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Nani amesimama? Mheshimiwa Felista Njau.

TAARIFA

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Spika, ninataka nimpe taarifa Mama anayechangia kwamba kuna mkopo unaitwa Kausha damu na sasa umesababisha wanawake wengi wameachika kwenye ndoa na kufirisika kabisa. Kwa sababu una riba kubwa na unalipa kila siku. Ahsante sana. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Angelina Malembeka, unapokea taarifa hiyo?

MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Spika, taarifa ya mikopo ya kausha damu ninaipokea. Ninaipokea kwa sababu hiyo ni moja ya ile mikopo ninayosema inawadhalilisha wakinamama. Kuna mikopo ambayo wakinamama unaenda kulipa mwili badala ya pesa. Kuna wanaume wamekaa huko standby wanaitwa mzee wa vikoba. Yaani mama akakope yeye kazi yake kulipa tu lakini analipa mwili, hii inatudhalilisha wanawake. Waziri, pita huko kwenye vikoba, pitia angalia wanakwendaje, tutakwisha magonjwa mengi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nizungumzie pia suala la mabinti mama. Tunao mabinti wetu ambao wamepata watoto wakiwa na umri mdogo. Familia nyingi zimekuwa kwamba akishapata yule mtoto, wanamsusa au wanamtenga badala ya kumuweka karibu, kumwelekeza na kumsaidia. Jinsi wanavyozidi kumtenga ndivyo ambavyo wanatupa watoto, mara utasikia kaokotwa kwenye jalala, mwingine anampelekea bibi yeye mwenyewe aingie mtaani kwenye biashara nyingine.

Mheshimiwa Spika, sasa hivi tuwapunguzie mzigo wakina bibi kulea wajukuu. Basi wale mabinti-mama tukae nao tuongee nao, tuwape elimu ya ujasiriamali, tuwape mikopo wafanye kazi ili walee watoto wao waache kuwapeleka kwa bibi zao lakini pia nao waache kazi hiyo nyingine ya ziada wanayokwenda kuifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nizungumzie pia maeneo ya vitambulisho vya wajasiriamali. Vitambulisho vilitolewa na baadae vikasitishwa wakasema wanaenda kuboresha, waziri atakapokuja naomba aje aniambie hivyo vitambulisho vimeboreshwa nini na vitapewa lini kwa hawa wajasiriamali? Kwa sababu huko mtaani usumbufu uko pale pale, haijulikani aliyepewa kitambulisho wala asiyepewa kitambulisho. Wanasumbuliwa maeneo ya biashara, wanasumbuliwa mara leseni, yaani ili mradi shida. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine kwa hao hao wajasiriamali na wafanyabiashara, ilizungumzwa kwamba watengewe maeneo kwa ajili ya kufanya biashara zao. Kuna halmashauri nyingine maeneo wametenga lakini wametenga tu eneo, vile vitu muhimu vya kupeleka pale havipo ni sawa sawa na hakuna. Unamwambia mtu kafanye biashara pale hakuna wateja, hakuna maji, hakuna usafiri, hakuna choo yaani ili mradi tu kero. Sasa, waziri atakapokuja hapa atwambie wapi ambapo wameandaa vizuri wakashinda? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuwapongeze wa Dodoma. Tumeona pale Dodoma aneo lao la wajasiriamali ni zuri na lina huduma nzuri. Sasa tunaomba na halmashauri nyingine zifuate hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lipo suala lingine la baba lishe na mama lishe. Hawa kila siku mimi nasema unaongea nao, kwa sababu nimekuona maeneo mengi ukiwa unafanya vikao na mama Lishe na baba Lishe na wajasiriamali wadogo wadogo kwenye vikundi. Pamoja na kuwatengea maeneo, je, yale maeneo mnayowatengea kweli yanawateja? Kwa sababu mtaji wao ni mdogo, unapompeleka kwenye eneo akafanye biashara wateja hana unajikuta kwanza hata kile chakula anakula mwenyewe na watoto wake. Kwa hiyo, hafanyi biashara. kwa hiyo, mnapowapangia maeneo ya kufanya biashara muangalie je, hapa wateja wapo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mchango wangu huu wa leo ninaunga mkono hoja. (Makofi)