Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

Hon. Dr. Dorothy Onesphoro Gwajima

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Spika, nashukuru kupata fursa hii mbele ya Bunge lako Tukufu kuweza kuhitimisha hoja yangu ambayo imepokelewa na kujadiliwa siku ya leo hapa Bungeni kwenye kipindi hiki cha asubuhi.

Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kumshukuru sana Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuniamini kuisimamia Wizara hii na kutupatia miongozo na maelekezo ambayo imetufikisha mpaka hapa ambapo Waheshimiwa Wabunge mmeweza kutoa pongezi zenu, tumezipokea, na kutuasa tuendelee na kazi kadri tunavyozidi kuwezeshwa na jemedari wa kwanza Mheshimiwa Dkt, Samia Suluhu Hassan aliyeiunda hii Wizara ya Maendeleo ya Jamii.

Mheshimiwa Spika, Shukrani zangu ziende kwa Makamu wa Rais Mheshimiwa Isdor Mpango kwa jinsi anavyotusaidia katika miongozo pamoja na maelekezo na kufuatilia masuala ya usawa wa kijinsia. Kila anapokwenda kwenye shughuli zake za utekelezaji tumekuwa tukimskia akiweka mkazo kwenye masuala ya maadili tuweze kudhibiti mmomonyoko wa maadili katika nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, vilevile shukrani kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa (Mb), kwa jinsi ambavyo ametoa uongozi kwa mawaziri pamoja na Wizara yetu katika kuendelea kupambana kuboresha huduma za ustawi wa jamii.

Mheshimiwa Spika, nikushuru wewe mwenyewe kwa jinsi ambavyo umekuwa ukiliongoza Bunge lako pamoja na sisi wenyewe Wizara ya Maendeleo ya Jamii. Kwanza umetuundia Kamati nzuri kabisa ya Huduma na Maendeleo ya Jamii na kutupatia viongozi mahiri kabisa ambao wameendelea kutupatia uongozi na maelekezo ambayo yametufikisha tulipo. Shukrani kwa Kamati yangu chini ya uongozi wa Mheshimiwa Toufiq (Mb), ambaye ndio mwenyekiti wa Kamati hii pamoja na wajumbe wote wa Kamati kwa jinsi wanvyoendelea kutuongoza.

Mheshimiwa Spika, nawashukuru Wabunge wote kwa maswali ambayo mmekuwa mkiuliza na michango ambayo mmekuwa mkitupatia. Hoja mbalimbali ambazo mmekuwa mkizilta zimekuwa chachu ya kutufanya sisi tufikiri zaidi jinsi ya kwenda mbele katika hii Wizara kubwa ambayo leo hapa nimeona ikifananishwa unga wa ngano, na kweli kabisa ni sawa, ina mambo mengi sana kwa sababu jamii na ina mambo mengi sana. Hii ni bahari inayounganisha Wizara zote zingine kwenda kufikia jamii.

Mheshimiwa Spika, nawashukuru Mawaziri wenzangu wote ambao wameendelea kufanya kazi hizi kwa ushirikiano wa kisekta na wameweza kuchangia pakubwa hasa katika suala la ajenda ya jukwaa la usawa wa kijinsia ambayo nimeielezea hapa. Haiwezi kutekelezwa na mtu mmoja, hii inatekelezwa na sekta zote. Ukigusa maji, ukigusa kilimo, ukigusa nishati, sisi wote, biashara tunatekeleza masuala haya ya kwenda kumkomboa mwanamke na kumwezesha kiuchumi.

Mheshimiwa Spika, nimshukuru sana Naibu Waziri wangu Mheshimiwa Mwanaidi Ali Khamisi kwa kazi nzuri anayofanya na kunipa ushirikiano, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu wangu na watendaji wote, kuanzia ngazi ya makao makuu hadi kwenye mikoa, halmashauri na kata zote. Sifa hizi tunazopata si kwa sababu yangu ni kwa sababu wao wanagusa maisha ya wananchi. Niwashukuru wadau wote niliowataja mpaka dakika hii ya sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa maneno haya ya utangulizi niseme kwamba hoja hii ukiacha hoja za Kamati zilizowasilishwa hapa, nakiri kuzipokea hoja hizi na niliahidi Kamati yangu Tukufu kwamba tutazifanyia kazi na kuwasilisha kwa maandishi masuala yote yaliyozungumzwa mle, kuanzia ukarabati wa miundombinu, upatikanaji wa fedha kwa wakati tufuatilie pamoja na kuwezesha upatikanaji wa watumishi ambao ni wachache hasa kundi hili la Maafisa Ustawi wa Jamii. Tutafanya kazi na Wizara za Kisekta kuweza kuona tunafanyaje ili kuendelea kuwezesha upatikanaji wa huduma za maendeleo na ustawi wa jamii.

Mheshimiwa Spika, sitaweza kupita kwenye kila hoja ya mchangiaji mmoja mmoja, kwa heshima na taadhima naomba nikuombe niweze kuyaangalia yale masuala machache ambayo yamechangiwa sana na kuweza kuyatolea ufafanuzi kadri muda utakavyo ruhusu. Nikiri hoja zote tumezichukulia kwa uzito stahiki, tutazifanyia kazi na kuziwasilisha kwa utaratibu wa Bunge kwa maandishi.

Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Mwanaidi Ali Khamis, nami naomba nianze kuongeza kwenye eneo hili la mmomonyoko wa maadili. Mmomonyo wa maadili limekuwa ni janga kubwa kwa sababu kwanza linagusa watoto ambao ni Taifa la kesho na watoto hawa wanajifunza kutoka kwetu sisi watu wazima, ambao tumepewa baraka na Mungu tuwalete watoto duniani na tumepewa dhama ya kuwalea na kuwakuza.

Mheshimiwa Spika, tunayo mikakati mingi eneo hili, lakini niseme kwamba tumejiongeza tumekwenda mbele. Ukiacha masuala haya ya kusema kwamba tuwawezeshe kina mama kiuchumi kwa kuunda majukwaa haya ya uwezeshaji wanawake kiuchumi, ambapo Jukwaa Kuu la Taifa tumelizundua jana, tumehakikisha kwamba tutakuwa na kampeni mbalimbali tukishirikiana na haya majukwaa ya kupeleka sauti ya fursa zilizopo kiuchumi maana tuna benki nyingi, tuna wadau wengi na sisi wenyewe Serikali tuna mifuko mingi ya kuwezesha wanawake kiuchumi ili wasiweze kuingia kwenye ukatili lakini taarifa zinakuwa hazifiki kwa wananchi hasa wale wa vijijini.

Mheshimiwa Spika, nimekuwa nikizunguka kule, unamuuliza mwananchi unafahamu kama kuna mkopo wa asilimia 10 anakwambia nasikia tu labda hii mikopo ni ya huko kwa wafanyakazi pamoja na watu wa halmashauri. Kwa hiyo tunaona kuna gap kule chini kwenye vijiji na kwenye kata. Kwa hiyo kupitia jukwaa hili na kupitia kampeni zetu hizi tumesema ZIFIUKUKI zijuwe fursa, Imarisha Uchumi, Kata Ukatili Kazi Iendelee. Tutahakikisha tunafikisha sauti ya uwepo wa fursa za uwezeshaji kiuchumi mpaka kwenye kata na mpaka kwenye kijiji. Kila mwanamke mmoja mmoja atajua na atajiunga na jukwaa hili ambalo ndio litakuwa platform ya kuwafundisha, kuwajengea uwezo, wataweza kujifunza kutoka kwa wenzao ili tuwakomboe kama mkakati mmoja wa kutokunyanyaswa.

Mheshimiwa Spika, tuna madawati pia ya jinsia ambayo yapo kwenye Jeshi la Polisi karibu madawati 420, yaani Vituo vyote vya Polisi vina haya madawati na pale tu sio madawati tuna msaada wa kisheria tunaoutoa kupitia Sheria Namba moja, Msaada wa Kisheria ya Mwaka 2017. Wasaidizi wa kisheria wako wengi sana lakini bado wananchi pia hawafahamu. Kwa hiyo, kupitia haya majukwaa pia tutapeleka hii elimu na tutafanya haya matamasha tukiwa tunahusisha na hizo huduma kuzipeleka, sio matamasha tu ya hivi ya kukaa kwenye majumba ni kupeleka zile huduma. Kama ni usaidizi wa kisheria huu hapa, kama ni fursa za kiuchumi hizi hapa.

Mheshimiwa Spika, tumezindua hilo tamasha la kwanza Dar es Salaam, mwishoni mwa Aprili ambapo tulileta taasisi zote zenye fursa za kiuchumi ambapo walihudumiwa wananchi takribani 4,040. Kwa hiyo tunataka tuendelee hivyo kwenye mikoa yote tuifungue nchi, kila mtu ajue uwepo wa hizi fursa isije ikawa wachache tu ndio wanazisikia.

Mheshimiwa Spika, tunakuja na mpango wa pili wa MTAKUWA uliofanyiwa maboresho. MTAKUWA ni Mpango kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili kwa Wanawake na Watoto baada ya ule wa kwanza kuwa umeisha Juni 2022. Mle ndani tumeboresha, masuala ya ukatili wahusike na Wakuu wa Wilaya wahusike na Wakuu wa Mikoa, wanapojadili taarifa zao za Kamati ya Ulinzi na Usalama kwenye halmashauri na mikoa, wakajadili majambazi, wakajadili na hali ya usalama, wajadili na masuala yanayotishia unyanyasaji wa kijinsia kwa watoto na wanawake.

Mheshimiwa Spika, tunataka kuzijua hizi data zikitokea mikononi kwao, kwa sababu wanafanya hiyo kazi na wana vyombo vyote. Kwa hiyo taarifa zikifika pale na Afisa Ustawi wetu akawasilisha pale, Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya au Mkuu wa Mkoa ataweza kuviagiza vyombo vichukue hatua kwa wakati badala ya mama huyu kuwa anahangaika pengine yuko mbali kule kijijini, pengine hana hata usafiri, pengine hata Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa hawajui.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tunaikaribisha hii mifumo yote ya ulinzi na usalama ili pia iangalie hili suala la watoto pamoja na wanawake wanaonyanyaswa. Tumekuja na kampeni nyingine ya “Taifa letu, Maadili Yetu”, tumeizindua hapa juzi. Nimemsikia Mheshimiwa Mbunge Mwakagenda akisema tupige sana kelele, sasa tutapiga sana kelele kupitia hii kampeni kwa kipindi cha miezi sita inayokuja na ndio maana tumewaunganisha na vilabu vya mipira, tumewaunganisha na wanahabari, tumeunganisha na jamii yenyewe kupitia wenzetu wa SUMAUJATA, FAGDI na tunapata wito na mwitikio mkubwa sana wa wananchi na kila mtu anasema nataka kwenda mstari wa mbele, hasa kupitia hii kampeni. Tutapiga sana kelele ili kufikisha hii sauti kule, sio tu sauti ya kwamba kuna ukatili bali na fursa za kiuchumi kwamba ziko hivi na fursa za kisheria, misaada ya kisheria ili wananchi wajue. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru utoaji taarifa sasa unaongezeka si kwa sababu pengine matukio yanaongezeka sana. Awali kasi ya kutoa taarifa ilikuwa asilimia 12, sasa tunainyanyua kwa sababu wanapata ujasiri na kuona kwamba Dkt. Samia Suluhu Hassan yupo kwa ajili yao, Wizara ipo kwa ajili yao, Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya wako kwa ajili yao. Tunaamini hawa watu sasa kama ilivyo kwenye nyumba ya mtu mmoja ameweka askari wa asili ambao tunasema wanalinda ile nyumba, wakibweka, mwizi anakimbia. Lazima hawa wakatili wajue kwamba Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan iko kiganjani kwa huyu wanayetaka kumkatili na ndio maana tunatengeneza namba za mawasiliano 116 na Wizara inazindua dawati lake hivi karibuni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niongelee eneo lingine kuhusu masuala ya NGO hizi ambazo zimekuwa zikihusishwa na masuala haya ya kuchochea mmomonyoko wa maadili. Tulipata hivi karibuni taarifa za wanaharakati ambao pia walikuwa wakishirikiana na Mwakyembe ambaye alikuwa ni Waziri mstaafu kusema kwamba kuna hii hali huko kwenye jamii, baadhi ya mashirika yanahusishwa na kuchochea hivi vitendo.

Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imechukua hatua ya kuyaita yale mashirika yote yaliyokuwa yametuhumiwa kule, kupitia Sheria ya Msajili wa haya mashirika wakaambiwa watoe maelezo. Baadhi yao wameshawasilisha maelezo na wengine wanayawasilisha. Sasa kwa sababu suala hili ni la kisheria, tukasubiri hayo maelezo yakamilike ili yaweze kuchanganuliwa na Bodi yetu ya Usajili ili wasilishwe kwa mujibu wa sheria. Kama kutakuwa na mtu ambae anaona ameonewa sheria inasema rufaa iende kwa Waziri. Mimi nitapokea, lakini sasa hivi mchakato unaendelea wa uwasilishaji hayo maelezo kujibu zile tuhuma ambazo wamehusishwa nazo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nisemee kuhusu suala la hela hizi za Machinga ambazo bilioni 22.9 zilipaswa tupewe, lakini hatukuweza kupewa kwa wakati. Kupitia Wizara ya Fedha ambayo tumekuwa tukiwasiliana nayo ilikuwa inafanya uratibu wa Mifuko sio tu huu wa Machinga ili waweze kuweka mifumo vizuri ikiwepo Mfuko wa Maendeleo wa Vijana wa Wanawake, Mfuko wa Taifa wa Watu Wenye Ulemavu na Mfuko huu wa Wamachinga. Sasa taarifa iliyoko ni kwamba hatua zimekamilika na hiyo taarifa itapelekwa kwenye kikao cha kazi cha IMTC kujadiliwa. Baada ya hapo, utolewaji wa hizo fedha utaanza, lakini kupitia kwa Mheshimiwa Waziri wa Fedha atakapo kuwa analeta hotuba yake atakuwa ameweza kutolea mwongozo sambamba na tathmini hii iliyokuwa inafanywa na ofisi yake.

Mheshimiwa Spika, naomba niendelee kwenye suala lingine linalohusu malezi na makuzi, kwa nini tumeweza kufanya mikoa 10 tu, lakini pamoja na WDF huu mkopo tunaoutoa pale Wizarani tumekwenda mikoa minne tu. Hili suala la mikopo hii ya WDF tulipokuwa tumepewa kibali tuendelee kutoa hizi fedha, kulikuwa na maombi tayari yapo pale ofisini ya siku nyingi. Kwa hiyo, ilikuwa mtu aliyeanza kuleta ndio apewe. Tulipoweza kuwachambua wale wapewe ile mikopo ndio ikaangukia hiyo mikoa lakini kwa sababu marejesho yanakwenda vizuri, tumejipanga kuhakikisha kwamba taarifa zinakwenda mikoa yote na halmashauri zote. Hata kama ni milioni ishirini ishirini tunatenga waombaji wajue kuna hilo fungu. Watakaokidhi hivyo vigezo waweze kupatiwa ili hata kama tunampa mmoja mmoja lakini kila mtu aonje uzuri wa hiyo WDF. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maelekezo ya Serikali ni kwamba, mikopo hii sasa yote tuipeleke benki, kwa sababu wengi wamekuwa katika mikopo kwa mfano ya asilimia 10 hawarejeshi na huu tukaona nao tuupeleke benki. Kwa hiyo utakapokuwa umeshafika pale benki, maana kwa sasa hivi tumesitisha kutoa, watapewa taarifa wote watachukua huko. Sisi tuta-regulate kuhakikisha majukwaa ya uwezeshaji wanawake kichumi yanaleta watu waliokidhi kupata hii mikopo kwenye benki za karibu na maeneo yao.

Mheshimiwa Spika, kuhusu masuala ya majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi kwa nini yamepewa mafunzo kwenye mikoa kumi tu. Ndio ilikuwa hivyo kwa sababu mikoa ile ilikuwa imeweza kutekeleza maelekezo mapema ya kwamba yaundwe hayo majukwaa. Kwa hiyo yale yaliyokuwa yameundwa tuliweza kuyapa mafunzo na sasa kwa sababu Jukwaa la Kitaifa limeundwa jana yote hii inakwenda kuingia kwenye kupata mafunzo. Semina kubwa inaandaliwa, wataitwa waweze kupewa ili waweze kuweka mipango ya mikoa yao, kwamba wanataka kuwafikisha wale wanawake katika ngazi ipi ya kimaendeleo.

Mheshimiwa Spika, kuhusu wajane; wajane ni kundi maalum na nashukuru tunao hapa viongozi wa wajane, tumekuwa tukiwasiliana nao. Tatizo la wajane kweli limekuwa kubwa na mwishoni mwa mwezi huu wa Juni tutakuwa na siku ya wajane, Kitaifa tutaifanyia Mkoa wa Mbeya. Tutakusanyika nao pale na baada ya hapo wale viongozi na wenyewe watapewa mafunzo, kisha wataweka mpango ingawa wao ni sehemu ya wanawake, lakini tutayaangalia mahitaji yao kwa utofauti, kwa jicho la hali ile ya maisha yao yalivyo. Hasa masuala ya kisheria, wananyanyaswa sana, wananyang’anywa mali zao baada ya mwanamume kufariki wanapitia kwenye mateso makali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilishaagiza tupewe list yao wote ambao kesi hazisogei ili tuwaunganishe na watoa huduma za msaada wa kisheria. Kwa hiyo ole wao wale waliobeba mali za wajane, wajue kwamba moto unakuja, tumejipanga, baada ya Siku ya Wajane Mbeya, mkikutwa huko mjue kwamba sheria inakuhusu. Lazima tuwaheshimu kwa sababu ujane ni hali ya kutokujichagulia, bali kudra za Mwenyezi Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, utitiri wa mikopo umelalamikiwa sana. Nashukuru sasa kwamba jukwaa hili la uwezeshwaji wanawake kiuchumi limeanza. Wanawake wote wanaolia machozi sasa ya mikopo hii isioeleweka wanakwenda kupona. Wanakwenda kuziona fursa zingine tofauti kabisa za mikopo nafuu kupitia haya majukwaa. Sasa na hawa wanaoitwa mikopo ya makomandoo, sijui mikopo ya pasua kichwa, damu na nini, niwaombe huko mliko majukwaa yameanza mtaniona mpaka kwenye ofisi zenu, mniambie mlisajiliwa na nani, mlipewa kibali na nani katika kuwapatia wanawake hawa mikopo ambayo pengine hata haikidhi hadhi ya utoaji mikopo. Waende wakajisajili kwenye utaratibu sahihi, wapewe miongozo ya utowaji mikopo. Kwa hiyo ukombozi wa wanawake umefika kupitia haya majukwaa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimalizie eneo moja kuhusu vitambulisho vya Wamachinga. Vitambulisho vya Wamachinga sasa vinavyokuja ni vya kidijitali, vinaweza kuwezesha Mmachinga huyu kutoa fedha na kupokea fedha, lakini vimeunganisha na NIDA pamoja na e-GA pamoja na maeneo yote ambayo Machinga atakuwa anapita kwenye mzunguko wake wa kupata fedha. Akikionyesha kile kitambulisho wanamsoma, mifumo inasomana. Kwa hiyo ni kipindi cha mpito hiki Mwaka huu wa Fedha 2022/2023, kama nilivyosema tayari umekamilika, unafanyiwa majaribio, tutaanza na baadhi ya mikoa, kisha tutaenda nchi nzima.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo suala hili litakuwa limeweza kuwanyanyua Wamachinga kuaminika na kupewa mikopo na taasisi zingine zote, kwa kuwa vitambulisho vyao vitakuwa vimekidhi vigezo vyote vinavyohitajika.

Mheshimiwa Spika, kuhusu pension ya wazee; niseme kwamba tumepokea wazee ni tunu ya Taifa, wazee tunawapenda na sisi wote tutazeeka. Tunafanya mapitio ya sera ya mwaka 2003 na mwaka jana tulifanikiwa kuunda Baraza la Taifa la Wazee ambapo tuliongea mambo mengi kuhusu mwelekeo wa kuboresha masuala ya wazee. Sera hii tumeshaiwasilisha, hatua nzuri itafanyiwa mapitio. Kwa hiyo humo ndani yake ndio tutakuja mpaka na Sheria ya Wazee, lakini tutakuja mpaka na masuala haya ya pension ya hawa wazee. Kwa hiyo utaratibu unaendelea na tutaendelea kuwasiliana nao kupitia Baraza la Wazee tunalofanya nalo kazi.

Mheshimiwa Spika, naomba kwa haya machache kwa kibali chako niombe kuwasilisha mengine yote kupitia maandishi, tukizingatia hoja za Wabunge wote ambao wamezitoa hapa siku ya leo.

Mheshimiwa Spika, kwa hayo niliyoyaeleza, naomba kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Spika, naafiki.