Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Miraji Jumanne Mtaturu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia hoja iliyoko mbele yetu ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kutujalia uzima na kuweza kukutana asubuhi ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nichukue nafasi hii kumshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayoifanya ikiwemo kuridhia fedha nyingi ambazo zinakuja kwenye Wizara hii ambayo ni Wizara inayoendesha na kusukuma uchumi wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yetu ya Ujenzi na Uchukuzi ndiyo imebeba daraja la uchumi wa nchi yetu. Kwa hiyo, Wizara hii ndiyo imebeba mabadiliko ya uchumi ambao tunautarajia. Nachukua nafasi hii kwa kweli kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya katika kujenga barabara, kujenga miundombinu, tunajenga reli, tunanunua meli, tunanunua ndege na kadhalika. Kazi hii inafanyika vizuri na kwa hakika ataendelea kuandikwa kwenye kitabu cha dhahabu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nachukua nafasi hii kumshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Profesa Makame Mnyaa Mbarawa pamoja na wasaidizi wake, Manaibu Waziri, ndugu yangu Kasekenya pamoja na Atupele ambao wanafanya kazi nzuri sana ya kumsaidia Mheshimiwa Waziri; Katibu Mkuu pamoja na Manaibu Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi kubwa; na bahati sisi wengine ni Wajumbe wa Kamati ya Miundombuni, tunaona kazi nzuri inayofanyika katika Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi na shukurani hizo, nichukue nafasi hii kwa hakika nianze kuchangia maeneo kama matatu kama nitapata muda. Nianze na kuchangia upande wa TANROADS ambayo ndiyo imepewa dhamana ya kusimamia ujengaji wa barabara kuu na barabara zinazounganisha wilaya na wilaya katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, TANROADS wanafanya kazi nzuri sana Wizara hii chini ya Eng. Mativila na wenzake wote. Wanawasimamia wakandarasi katika maeneo mbalimbali kujenga barabara, kujenga madaraja makubwa na madogo na kusimamia miundombinu mbalimbali katika eneo letu. Kazi hii ni nzuri na tumesikia kwenye taarifa yetu ya Kamati pamoja na Waziri mwenyewe ameeleza vizuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo hili nipongeze, kwa mujibu wa utaratibu wao tuliojiwekea ni kuhakikisha kwamba tunaunganisha barabara za mikoa na mikoa. Hii ni pamoja na kazi kubwa ambayo imefanyika na imeelezwa. Napongeza sana utaratibu mpya ambao umeanzishwa wa kujenga barabara kwa mfumo mpya wa EPC + F. Mfumo huu utaenda kuwa ni jibu ya barabara ambazo zilikuwa hazijakamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Waziri ametueleza hapa, tunaenda kusaini barabara zenye urefu wa kilomita 2,035. Barabara hizi ambazo zimejengwa pamoja na Barabara ya Handeni – Kiberashi – Kwa Mtoro – Kiteto mpaka Singida, barabara ya kilomita 460. Barabara hii ikikamilika itaenda kubadilisha kabisa uchumi wa eneo hili. Leo hii Bandari ya Tanga ambayo tunaiboresha, itaenda kuwa na majibu kupitia barabara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana mkandarasi apatikane mapema, tumeambiwa mwezi wa Sita mkataba utasainiwa. Namwomba Mheshimiwa Waziri kwa heshima kabisa, tuhakikishe barabara inasainiwa mapema ili Wabunge wa maeneo ya kutoka pale Handeni, ndugu yangu Mheshimiwa Omari Kigua; ndugu yangu wa Kiteto, Mheshimiwa Olelekaita; ndugu yangu Mohamed Monni pamoja na mimi tuweze kufarijika na wananchi wetu waendelee kupata raha kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikimaliza hapo, Mheshimiwa Waziri nilikuomba barabara. Mlinipa barabara ya kilomita moja ndani ya wilaya yangu. Naomba sana mniongezee kilomita 10 kwa barabara ya kutoka Ikungi – Londoni kwenda Kilimatinde (Solya) kwa ndugu yangu Mheshimiwa Dkt. Chaya ili barabara ile ijengwe kwa kiwango cha lami kwa sababu tuna mwekezaji mkubwa wa madini pale ambaye yuko maeneo ya Mang’onyi. Ikiwepo barabara hii itaongeza thamani ya mradi ule ambao tumeuweka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni wenzetu wa ATCL kwa maana ya Shirika letu la Ndege. Kwa muda mrefu tumeendelea kudogolesha Shirika letu na kwenye Kamati imeelezwa vizuri. Katika eneo hili nitaongea maneno mawili. Ili uweze kukuza uchumi wa nchi hii, ukiboresha Shirika la Ndege utaenda kuongeza thamani ya utalii. Watalii wengi watakuja. Biashara zinazofanyika kwenye maeneo mbalimbali duniani, ukiwa na ndege yako mwenyewe utakuwa na uhakika wa biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunategemea kupata ndege hivi karibuni ile ya Cargo ambayo itakuja kubeba mazao ya mboga mboga na maua kwenda nchi za Ulaya na Asia ambapo huko wanahitaji sana bidhaa hizo. Naomba sana shirika hili liangaliwe na Serikali, liendelee kuwezeshwa ili kuhakikisha kwamba linapata faida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo hili, pamoja na changamoto nyingine, kumekuwa na changamoto za madeni la shirika hili. Kwenye taarifa yetu tumepata sisi kwenye Kamati, wao walikuwa wanadaiwa karibia Shilingi bilioni 236 ambazo ni fedha walizokuwa wanadaiwa wakati hili shirika halifanyi kazi, lakini wamejitahidi kulipa karibia Shilingi bilioni 136, wamebakiwa na Shilingi bilioni 100. Serikali iangalie namna ya kumaliza deni hili ili tuweze kuweka mizania sawa ya hesabu za shirika hili, kuondokana na hasara ambayo inaweza kujitokeza na kulifanya shirika letu lifanye kazi vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ni kuondoa matatizo ya kukamatwa ndege katika nchi nyingine ambazo zinaidai Tanzania. Ndege hizi zimekuwa zinashikwa, siyo ATCL inadaiwa, inadaiwa Serikali, lakini kwa sababu Shirika la Ndege halimiliki zile ndege, hizi ndege zinamilikiwa na Wakala wa Ndege za Serikali, ETGF, maana yake ni kwamba hao ni kama Serikali. Kwa hiyo, deni lolote linaloihusu Serikali, likipatikana eneo lolote, ndege yetu inakamatwa. Maana yake mtiririko wa usafiri unaondoka. Leo hii ATCL ikiondoka ndege moja tu, kama inaenda Mumbai ama nchi nyingine, maana yeke unapunguza mtiririko wa abaria. Maana yake usitegemee kupata faida. Leo hii CAG ataenda kuona kila siku shirika linapata hasara kwa sababu ni mpango ambao tumeuweka wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Serikali iangalie uwezekano wa kurudisha ndege hizi ATCL ili ziweze kumilikiwa na Shirika la Ndege lenyewe ili kuleta faida na kulifanya shirika letu liweze kufanya kazi vizuri. Ambacho ni mzigo mkubwa, leo hii Shirika la Ndege linalipa karibia Shilingi milioni 700 kwa ajili ya kukodisha ndege za Serikali. Hivi Serikali na Serikali zinakodishiana, kuna haja gani? Ndiyo maana shirika letu haliwezi kuendelea kwa sababu linakwazwa na mambo mengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana kwenye hili Mheshimiwa Waziri atakaporudi, atuambie ni mpango gani wa Serikali umefikiwa kwa ajili ya kurudisha ndege hizi ATCL kuondoka kwenye Wakala wa Ndege wa Serikali na changamoto ambazo shirika linapata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu ambalo ni la mwisho ni suala la Bandari. Bandari ni lango kuu la biashara. Bandari yetu kwa maana ya mkao wa kijiografia Bandari yetu ya Dar es Salaam imekaa vizuri sana kistratejia. Bandari hii tukiitumia vizuri, inaweza ikaleta mapato mengi kuliko eneo lolote. Leo hii pamoja na mchango inayotoa lakini bado, haitoi mchango wa kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeboresha sana gati Na. 8 mpaka 11, tumeweza kujitahidi kuongeza masuala ya usalama katika bandari, ni sawa, lakini tumeongeza cranes ambazo bado ni kidogo sana. Cranes mbili zile zinazofanya kazi pale, tukiangalia bandari nyingine ambazo ziko kama Mundra kule India, kule Dubai na nchi nyingi, bandari nyingine zinafanya kazi vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, tumeongeza mapato ya Shilingi bilioni 700 mpaka Shilingi trilioni moja tu, ambayo kimsingi ukiangalia hizi fedha bado ni ndogo kwa bandari yetu ilivyokaa. Nchi nane zinategemea Bandari ya Dar es Salaam, maana yake ni kwamba tukiboresha vizuri, Bandari ya Dar es Salaam itakuwa ni jibu la fedha ambazo hatuzipati katika maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana, pamoja na mambo haya, kuna changamoto chache zinakwaza bandari yetu. La kwanza, bado hatujakuwa na mifumo ya kusomana ambayo inaweza kumsaidia mteja kuvutika kuja kufanya biashara na sisi. Naomba sana tuhakikishe kwamba tunaangalia namna ya kumleta mwekezaji ambaye atashirikiana na Serikali. Siyo jambo la dhambi, PPP imetajwa kwenye sheria za nchi yetu, tusiwe waoga Watanzania tunapotaka kubadilisha maisha ya Watanzania wetu.
Tukiweza kuwekeza vizuri, itasaidia sana…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mtaturu, ahsante sana.

MHE. MIRAJI J. MTATURU: Naam!

Mheshimiwa Mwenyekiti, dakika moja nimalizie, ni-conclude hii hoja.

MWENYEKITI: Mheshimiwa, malizia sekunde thelathini muda wako umeisha.

MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa sekunde thelathini.

Mheshimiwa Mwenhyekiti, naomba sana Watanzania tusiwe waoga kwenye mambo ya msingi ili kuhakikisha kwamba tunaweza kubadilisha na kuongeza uchumi wa nchi yetu, kusaidia Taifa hili tuweze kujenga madarasa, tujenge miundombinu mbalimbali kwa ajili ya maisha ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maneno haya, naunga mkono hoja. Nashukuru sana kwa nafasi. (Makofi)