Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Josephat Sinkamba Kandege

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalambo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nina kila sababu ya kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema kwa kunijalia afya ili na mimi nisimame mbele yako kuweza kuchangia hoja ambayo imeletwa kwetu leo. Naomba nianze kwa kuunga mkono hoja. Nina kila sababu ya kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri ambayo anaifanya, na sisi wana Rukwa tuna kula sababu ya kumuombea kwa Mwenyezi Mungu ampe afya katika kuendelea kuwatumikia Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tumefanyiwa tukio la kihistoria, kwa mara ya kwanza baada ya kwamba tumepiga kelele kwa muda mrefu Mheshimiwa Mbalawa umeenda kufanya tukio ambalo halitasahahulika, la Kwenda kuweka saini juu ya ujenzi wa uwanja wetu wenye thamani ya bilioni 53. Ni matarajio yetu na matumaini yetu matumaini yetu makubwa kwamba uwanja huu wa ndege utakamilika kwa mujibu wa mkataba ndani ya miezi 18, tumesubiri muda wa kutosha hatutarajii extension hata ya mwezi mmoja maana uwanja huu tulitamani uwe umekamilika tangu zamani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizo naomba niungane na mwenzetu, Mheshimiwa Kiumbe Ng’enda ambaye aliyeelezea juu ya umuhimu wa kuwepo kwa meli katika Ziwa Tanganyika. Maneno haya hayapendezi, hivi leo tunavyoongea hakuna meli ziwa Tanganyika, na ahadi imekuwa ikitolewa na Serikali, mara wanataka kufanya ukarabati wa MV Liemba, mara meli mpya; na ni vizuri tukawaambia Serikali, tusije tukafanya makosa kama walivyofanya wenzetu wa DRC tukajenga meli ambayo tunadhani kwamba itachukua abiria 600 halafu tukawakosa hao. Ni vizuri Serikali mkafikiria wakati mnaenda kuweka mkataba tukafikiria kujengewa meli mbili ili ziwe zinapishana moja ikiwa Kigoma nyingine iwe Kalambo, kulikoni kujenga meli moja na kwa bahati nzuri hatujafikia extent ya kuweka mkataba, kwa hiyo ni vizuri Serikali mkalitazama; kwa sababu itakuwa si busara kwamba eti meli tusubiri itoke Kigoma sisi ambao tuko Kalambo tunasubiri mpaka ije hiyohiyo haitakuwa na msaada. Kwa hiyo namuomba Mheshimiwa Waziri na Serikali kwa ujumla mlifikirie hili kwa mara ya pili kabla hamjaenda kuanza kujenga meli hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nipongeze kazi nzuri, na kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri imeonesha juu ya ukamilikaji wa ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami kutoka Sumbawanga hadi Kasanga Port jumla ya kilometa 107, kazi nzuri sana hongereni. Lakini kazi nzuri hii inakuja inaunganishwa pamoja na ujenzi na upanuzi wa bandari ya Kasanga. Kazi ambayo inafanyika ni kazi nzuri lakini niiombe Serikali, kama tunataka kumaliza mzizi wa fitina ni namna gani Watanzania tunatumia fursa ya kwenda Congo DRC tukiwa tunatoka Tanzania bila kupita nchi Jirani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri leo wapo watu wa TATOA, watu ambao wanaendesha malori, ninaamini wamehakwambia adha ambayo wanalazimika kukutana nayo wakati wanapoenda Congo ya Lubumbashi Kwenda kulazimika kukaa mwezi mzima kwa nchi ambazo si za kwetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na nimkumbushe Mheshimiwa Waziri, uchumi wa kibiashara ni uchumi ambao lazima kwa vyovyote vile tushindane. Mwenyezi Mungu ametujaalia tuna port ambayo mmefanya vizuri, imeebaki kazi moja tu, kuhakikisha namna gani imetoka Kasanga Port Kwenda Congo ya Lubumbashi. Na hili niiombe Serikali, najua kuna maboresho makubwa ambayo mnafanya juu ya Sheria ya Manunuzi, kwamba itatoa fursa kwa PPP ambayo kwa vyovyote vile private sector itaweza kushiriki. Na nimekuwa nikiiomba Serikali muda wote, kwamba si lazima Serikali ndiyo itoe fedha Kwenda kujenga upande wa pili wa Congo, lakini ikiwapendeza mtakuwa mmefanya vizuri zaidi. Wenzetu Uganda wamefanya sisi tunashindwaje ilhali tuna uhakika ni kitu ambacho tunakipata huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi ya asilimia 80 ya copper ambayo inapatikana DRC inapatikana Katanga ambayo ndiyo Lubumbashi na njia ambayo rahisi ni kupita kasanga. Nilishasema mara nyingi na Mheshimiwa Waziri naamini hii itakuwa ni kuchangia kwa mara ya mwisho, ninachotarajia next time tuone utekelezaji. Nimekuwa nikikwambia kwamba Wabelgiji walifanya uchunguzi, kwamba sehemu nzuri kwa ajili ya kuwa na port upande wa DRC ni eneo la Mulilo. Eneo la Mulilo unali–access kiurahisi zaidi ukipitia Kasanga Port. Naamini haya yatakuwa yamesikilizwa.

Mheshimwa Mwenyekiti, na ninaomba nimuombe Mheshimiwa Waziri jambo lingine la pili; ni juu ya reli yetu ya TAZARA. Ni kuweli usiopingika, na kamati imesema kwamba mkataba ulivyo hautoi fursa kwa ajili ya sisi ambao tunataka kuwekeza na kipande cha upande wetu kiwe kizuri. Mkautazame mkataba ili tuanze kujenga kutoka Tunduma Kwenda Kasanga na nchi hii yote itakuwa na network ya kuwa na reli, huku iko SGR huku TAZARA. Itakuwa imesaidia sana kwa ajili ya kuhakikisha kwamba Tanzania yote inakuwa networked.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba mkautazame mkataba, yafanyike maboresho ili eneo la kwetu tufanye uwekezaji, wenzetu kama hawakao tayari kwa speed ambayo tunaenda nayo ni vizuri sisi ambao ni wanufaika tukahakikisha eneo hili linaenda kufanyiwa kazi. Na ukitazama tangu zamani inaonesha kwamba reli hii inatakiwa iende mpaka Mbamba Bay ikaunganishe na kule Kyela, mkatizame study ziko kwenye ofisi zenu, ili jambo hili liweze kukamilika mara moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nipongeze; kuna ujenzi wa barabara kutoka Matai kwenda Kasesha border ambayo ni kilometa 50. Jambo kubwa limefanyika na tayari katika mkataba ule unaonesha kwamba ndani ya miezi 18 kipande hicho kitakuwa kimekamilika na hakika kwa utendaji mzuri wa Wizara hii natarajia kazi hii itakamilika kwa wakati ili wnanchi wa Kalambo, Rukwa na wananchi wanaotoka Tabora, wanaotoka Mwanza wanaotaka Kwenda Zambia iwe ni rahisi Kwenda kule bila kulazimika Kwenda mpaka Mbeya, na ndiyo namna pekee ya kuweza kuifungua nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, itoshe katika hayo ambayo nimeyasema ili yachukuliwe kwa uzito mkubwa zaidi kuliko nikitoa mengi akakosa muda wa kuyafanyia kazi. Akayafanyie kazi haya tukija bajeti nyingine tuwe na uhakika meli ziko si moja, meli mbili ndogondogo badala ya kuwa na meli moja kubwa haiutatusaidia. Tuhakikishe kwamba tuna–access Congo DRC kupitia Kasanga Kwenda Lubumbashi ili hayo matunda ambayo unahitaji kuchuma bila hata kutafuta ngazi tuanze kuyachuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja, ahsante sana.